• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Hali ya masikilizano ya kidini nchini China

    (GMT+08:00) 2015-02-05 14:15:49

    Wiki hii ni wiki ya masikilizano ya kidini duniani, wiki iliyotajwa na Umoja wa Mataifa kuwa ya wiki ya kuhimiza watu duniani kuishi kwa masikilizano bila kujali tofauti za kidini, na kukumbuka madhara yaliyotokea na yanayoweza kutokea kutokana watu kutowavumilia wenzao kwa dini au imani tofauti. China ni nchi yenye makabila 56, dini zaidi ya tano, na makundi mengine mbalimbali yenye imani za jadi, lakini ni nchi yenye kiwango cha juu cha masikilizano. Tutawafahamisha ni vipi wenzetu wanaweza kuwa na masikilizano katika hali ya kuwa na idadi kubwa ya watu, makabila mengi na dini mbalimbali.

    Pili: wasikilizaji wetu watakuwa wanafahamu kuwa China ni nchi yenye watu zaidi ya bilioni 1.3, makabila 56, kabila kubwa zaidi likiwa ni la wahan, pia ina watu wanaoamini dini za jadi kama vile dini ya kidao na imani nyingine, kuna wakristo, waislamu na waumini wa dini ya kibuddha. Ukiangalia mchanganyiko wa namna hii unaweza kudhani basi watu wanao jamii ya China wanaishi kwa mikwaruzano, lakini sisi tunaoishi hapa China tunaona wachina wanaishi kwa utulivu na masikilizano, licha ya tofauti hizo.

    Fadhili: Ni rahisi kusema China ni nchi yenye masikilizano, lakini ni vigumu kutaja sababu moja inayofanya iwe nchi yenye utulivu na masikilizano. Ingawa tukisoma kuhusu historia ya China huko nyuma kuna habari kuhusu mapambano mengi kati ya madola, lakini jamii ya sasa ni tofauti sana na jamii za kale, ni jamii yenye utulivu na masikilizano.

    Pili: Kwanza tukiwaangalia wachina wenyewe, walio wengi ni watu watulivu. Japo kuwa kuna baadhi ni wakorofi, hao ni wachache sana. Upole na utulivu wao kwanza unatokana na mafunzo ya maadili ya jadi ya kuheshimu wengine, haya yanatolewa katika familia na shuleni na wanakua nayo.

    Fadhili: Lakini hata tukiangalia mawazo ya wachina walio wengi, unaweza kuona kuwa wana akili ya kuangalia maslahi ya walio wengi na maslahi ya taifa. Hata mchina wa kawaida mtaani anajua na kuthamini chini yake kwanza, anajua historia ya enzi mbalimbali za China, ana hali ya kupenda taifa na hata kujua umuhimu wa masikilizano kwa maendeleo yake binafsi au hata maendeleo ya nchi, hii ni tofauti kidogo na kwenye baadhi ya nchi zetu Afrika, mtu anatambua kwanza dini yake, kabila lake halafu baadaye ndio nchi yake.

    Pili: Tusieleweke vibaya kuwa hapa China hakuna malalamiko au ni nchi ambayo kama paradiso. Mbali na kuwa na makabila mengi, na dini mbalimbali, China ni moja ya nchi zenye pengo kubwa sana kati ya matajiri na maskini. Kuna mabilionea, matajiri wa kati na maskini ambao hata vigumu kwao kupata chakula kizuri. Pia kuna pengo kubwa la maendeleo kati ya sehemu ya mashariki na magharibi, watu huwa wanalalamika kuhusu mambo hayo, kwa hiyo malalamiko yapo. Lakini licha ya hayo bado kuna masikilizano na maelewano ya kijamii.

    Fadhili: Uzuri ni kwamba serikali ya China huwa inafuatilia malalamiko na kuyafanyia kazi. Kwa mfano kuna sera ambazo zinalenga kuwaendeleza watu maskini, kuna baadhi sera zinatekelezwa kulenga kuwanufaisha watu wa makabila madogo, na hata kutoa fursa kwa wale wanaotaka kujiendeleza. Kwa hiyo kwa upande mmoja tunaona kuwa watu wanatoa malalamiko yao kwa njia za kistaarabu, na serikali inasikiliza na kuyafanyia kazi.

    Pili: Hali kama hii ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu katika jamii, kutokana na tofauti za kidini, kikabila, imani za kisiasa zinafanya hali ya masikilizano katika jamii mbalimbali kupotea, hasa watu wanapokuwa na hali mbaya kiuchumi. Wasikilizaji wetu Kiza Mustafa kutoka Bujumbura Burundi, Abdalah kutoka Zanzibar, Hassan Ali kutoka Lamu Kenya na Bw Samwel Ombati pia kutoka Kenya, wamekuwa na maoni kuhusu masikilizano katika jamii zao na namna jinsi matatizo hayo yanavyoweza kutatuliwa.

    Fadhili: Moja kubwa ambalo limezungumzwa na wasikilizaji wetu ni siasa. Mashabiki wa kundi moja la kisiasa wanapambana na wa kundi lingine, au wa chama kimoja wanapambana na wa kundi lingine, tofauti zao zinaonekana kuwa na maana zaidi kuliko nchi zao. Msikilizaji wetu kutoka Kenya Samwel Ombati anaeleza baadhi ya mambo anayoona yanachochewa kutokuwepo kwa masikilizano ya kijamii.

    Fadhili: Bw OMbati amezungumza jambo moja kuwa watu wa pwani wanalalamika kuwa wabara wanakwenda kwenye miji ya Pwani kuchukua ajira, na wenyeji wanakosa ajira. Mimi ni mbara na wewe mpwani lakini bahati nzuri tuko China, hatuwezi kushutumiana. Hapa China tukiangalia tunaweza kuona watu kutoka mkoa mmoja, mji mmoja wanakwenda kufanya kazi katika sehemu nyingine bila tatizo lolote. Kuna baadhi ya wafanyakazi wenzetu ni wapwani wanafanya kazi hapa, na nina marafiki pia kutoka hapa Beijing wanafanya kazi katika miji ya pwani.

    Pili: Wenzetu naweza kusema wanajali zaidi elimu, ujuzi na uzoefu wa kazi, sio mtu unatoka wapi. Uzuri ni kwamba wenzetu wana taratibu za ukazi, na utaratibu mzuri wa kusimamia soko la ajira. Wachina wana utaratibu wa "Hu Kou" ambao unasaidia kupanga hadhi ya ukazi wa watu na hata ajira, lakini hali hii haipo kwenye nchi zetu kwa kuwa nchi zetu ni ndogo hazina changamoto ya shinikizo la idadi kubwa ya watu

    Fadhili: Jambo hili limezungumzwa pia na msikilizaji wetu wa Zanzibar Abdalah, yeye amezungumzia changamoto inayowakabili vijana wa Zanzibar kwenye sekta ya utalii. Anaona kutokuwepo kwa vijana wenyeji wa kutosha kwenye sekta ya utalii kufanya wawe na malalamiko, na anaona malalamiko haya yanafanya kuwe na chuki kati ya wenyeji na watu kutoka sehemu nyingine za nchiā€¦.(Sauti ya Abdalah wa Zanzibar)

    Pili: Bw Abdalah amezungumzia usawa. Yeye anaona kuna ubaguzi, lakini tukiangalia kwa undani tunaona kuwa ajira huwa zinatolewa kutokana na elimu, ujuzi na uzoefu wa kazi, kwa baadhi ya watu wanaweza kuona kuwa huo ni ubaguzi. Lakini hali kama hiyo ipo hata hapa China, lakini kuulaumu upande mmoja wakati kuna na tatizo la ajira si busara au sio kisingizio cha kuvuruga masikilizano.

    Pili: Msikilizaji wetu wa Lamu Kenya Bw Hassan Ali, yeye anaona tunatakiwa tuweke tofauti zetu pembeni na kuheshimu watu tofauti. Anatoa pendekezo moja zuri kuwa, kwa kawaida kila mtu anaona yeye yuko sahihi lakini mwingine hayuko sahihi. Yeye ametoa mfano kwa dini kuwa si lazima kuwa fikra zako ni sahihi na zangu si sahihi inawezekana si sahihi, yeye anasisitiza kuheshimiana.

    Pili: Wanayosema wasikilizaji wetu ni ya kweli. Mambo ya udini, ukabila, tofauti za kisiasa zisiwe kisingizio cha kuvuruga masikilizano ya watu, tunatakiwa kukumbukuka kuwa umoja na utulivu ndio msingi. Burundi ni nchi ambayo ilikumbwa na vurugu zilizosababisha kutokuwepo kwa masikilizano, lakini msikilizaji wetu Kiza Mustafa wa Bujumbura anasema warundi sasa wameamka wanatahimi zaidi nchi yao kuliko makabila yao.

    Fadhili: Wasikilizaji wetu wote waliochangia anasema uvumilivu na kuheshimiana ni jambo muhimu, vile vile kama kuna kutokuelewana na pande mbili kujadiliana na kusikilizana. Na haya ni mambo tunayoona yanafanya China iwe nchi yenye utulivu na masikilizano.

    Kufikia hapa ndio kwa leo tunakamilisha kipindi cha China Machoni mwetu, usikose kuwa nasi alhamisi ijayo kwenye kipindi kingine cha China Machoni mwetu

    Kabla ya kukamilisha kipindi hiki tunapenda kuwashukuru wasikilizaji wetu mnaotusikiliza kupitia masafa ya 89.2 FM mjini Bujumbura, 99.7 FM mjini Zanzibar, 91.9FM Nairobi, na 103.9 FM Mombasa, na wasikilizaji wetu mnaosikiliza kupitia KBC na masafa mafupi kwa michango yenu, bila kuwasahau mnaoendelea kutuma maoni yenu kwa njia ya whatasapp. Ningependa kuwataja Bw Kiza Mustafa wa Bujumbura Burundi, Hassan Ali na Samwel Ombati wa Kenya, na Abdalah wa ZNZ kwa maoni yetu. Kumbuka nambari yetu ni +8615611015572 tafadhari taja jina lako na mahali ulipo, utashiriki kwenye mada zetu

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako