• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Uvumbuzi wa teknolojia ya mawasiliano wasukuma mbele kilimo barani Afrika

    (GMT+08:00) 2015-02-11 09:26:23

    Tovuti ya AgInvest Africa imezinduliwa hivi karibuni, na inatoa data mbalimbali kuhusu miradi ya kilimo ya nchi za Afrika mashariki, kati na kusini, na kuwawezesha wakulima, wawekezaji, wateja na watunga sera kuwasiliana, na kusaidia miradi ya kilimo itekelezwe kwenye msingi mzuri wa upangaji wa rasilimali, ugawaji wa kazi na ushirikiano. Kuanzishwa kwa tovuti hii ni hatua mpya muhimu ya nchi za Afrika katika kuendeleza kilimo kwa kutumia uvumbuzi wa teknolojia ya mawasiliano.

    Kilimo ni mhimili wa uchumi wa nchi nyingi za Afrika, na kinachangia theluthi moja ya pato la taifa la nchi za Afrika, pia kinatoa asilimia 60 ya nafasi za ajira. Kilimo kinahusiana na masuala mbalimbali yakiwemo usalama wa chakula, umilikaji wa ardhi, migogoro ya makabila, ukosefu wa ajira na umaskini. Kuendeleza kilimo ni msingi wa kutatua masuala mbalimbali barani Afrika.

    Ili kuondoa vikwazo mbalimbali na kuharakisha maendeleo ya kilimo, mwaka 2003 viongozi wa Afrika walisaini taarifa ya Maputo nchini Msumbiji, ambayo inasema nchi za Afrika zitatumia zaidi ya asilimia 10 ya bajeti kwenye sekta ya kilimo, ili kuhakikisha ongezeko la kilimo linafikia asilimia 6 kwa mwaka. Kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita, utekelezaji wa taarifa hii hauridhishi, lakini bado umepata mafanikio kadhaa, hasa katika kuhimiza maendeleo ya kilimo kwa teknolojia za mawasiliano.

    Kenya imepata umaarufu kutokana na M-pesa, teknolojia hiyo ya kuhamisha fedha kupitia simu za mkononi imewanufaisha mamilioni ya watu wasioweza kupata huduma kutoka benki. Sasa Kenya pia inaongoza katika kuendeleza kilimo kwa uvumbuzi wa teknolojia. Hivi karibuni nchi hiyo ilitoa software ya simu ya mkononi iitwayo iCow. Wafugaji wa ng'ombe wa maziwa wakijisajili kwenye software hii, wanapata taarifa mbalimbali kuhusu ufugaji, uzazi na matibabu ya ng'ombe, pia wanaweza kujua bei ya bidhaa za maziwa sokoni. Software hii inapendwa sana na wafugaji wa ng'ombe nchini Kenya, Uganda na Tanzania. Kampuni iliyobuni software hii pia imepata maombi ya kujisajili ya wateja wa Malaysia, Russia na China.

    Katika miaka ya karibuni, software zilizobuniwa na makampuni ya nchi za Afrika zimeweza kutoa huduma za aina nyingi kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, uzalishaji na bei za mazao ya kilimo, biashara kupitia Internet, na utaalam wa kilimo. Miongoni mwa software zinazojulikana, ni pamoja na Esoko iliyobuniwa na kampuni ya Ghana, Agro-Hub ya Cameroon, M-Farm na Kilimo Salama za Kenya. Ripoti iliyotolewa na Shirika la watoa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi duniani GSMA inaonesha kuwa zaidi ya vituo 50 vya uvumbuzi wa teknolojia vimeanzishwa barani Afrika, vikiwemo kituo cha Hive Colab nchini Uganda, Limbe Labs nchini Cameroon na iHub mjini Nairobi Kenya. Vituo hivi vikiungwa mkono na makampuni makubwa ya mawasiliano ikiwemo Google, vinasukuma mbele maendeleo ya sekta mbalimbali ikiwemo kilimo barani Afrika kwa uvumbuzi wao wa teknolojia za mawasiliano.

    Wachambuzi wamesema, uvumbuzi wa teknolojia unachangia maendeleo ya kilimo barani Afrika katika mambo matatu. Kwanza, teknolojia za mawasiliano zimeinua uwezo wa uzalishaji wa kilimo. Wataalam wa kilimo wanaweza kutoa mafunzo moja kwa moja kwa wakulima kupitia software za simu ya mkononi, ya mbinu za kukinga na kuua wadudu, na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, na kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji. Takwimu zinaonesha kuwa software ya iCow iliwasaidia wafugaji wa ng'ombe wa maziwa nchini Kenya kuongeza uzalishaji kwa asilimia 50 na mapato yao kwa asilimia 42. Pili, teknolojia za mawasiliano zinaweza kuondoa tatizo la miundo mbinu duni ambalo linaathiri uchukuzi wa mazao ya kilimo katika nchi nyingi za Afrika. Takwimu zinaonesha kuwa, gharama ya uchukuzi inachukua asilimia 40 ya bei ya mbolea ya kemikali barani Afrika. Kubadilishana taarifa na kufanya biashara kupitia Internet kumerahisisha mauzo ya bidhaa za kilimo, na kupunguza gharama ya uchukuzi. Tatu, teknolojia zimewasaidia wakulima kutoa maoni yao katika utungaji wa sera za kilimo. Wakulima wengi wako vijijini na ni vigumu kwao kushiriki kwenye utungaji wa sera za kilimo unaofanyika mijini, hivyo sera nyingi haziendani na hali halisi ya vijijini, na utekelezaji wake unakuwa ni mgumu. Teknolojia za mawasiliano si kama tu zinaweza kuwafahamisha wakulima moja kwa moja habari mbalimbali zikiwemo sera, huduma, utaalam na bei, bali pia zinakusanya data mbalimbali zikiwemo mahitaji ya wakulima, eneo la mashamba, uzalishaji na mauzo, ambazo ni msingi wa kutunga sera za kilimo.

    Licha ya hayo, teknolojia za mawasiliano pia zimezisaidia serikali za nchi mbalimbali barani Afrika kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa miradi ya kilimo kwa urahisi zaidi, kusukuma mbele utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya kilimo barani Afrika katika pande zote CAADP, na kuhimiza maendeleo ya kasi ya kilimo hata uchumi wa jumla.

    Kuna software nyingi za simu za mkononi au kompyuta zinazoweza kuwasaidia wakulima barani Afrika kuboresha kazi zao kilimo, na kuongeza mauzo ya mazao yao. Kwenye mkutano wa 2013 wa ICT4AG, shirika linalohimiza kilimo kwa mbinu za upashanaji habari, mawasiliano na teknolojia, wadau waliungana na wavumbuzi na wabunifu wa software kujadili maswala ya teknolojia zinazolenga wakulima. Zifuatazo ni software kadhaa bora zinazohusu kilimo.

    *Rural eMarket

    Hii ni software inayohusu soko la mazao ya kilimo. Software hii ni njia rahisi na yenye ufanisi mkubwa katika kuwasilisha habari kuhusu masoko kwa kutumia simu au kompyuta. Inaweza kutumiwa kwa lugha nyingi, ni rahisi kujifunza namna inavyofanya kazi, na pia watu wengi wanaweza kumudu gharama zake. Kutumia software kama hii kunaweza kusaidia kuwepo kwa uwazi na upatikanaji wa masoko, na hivyo kuboresha maisha ya wakazi wa vijijini.

    *mFisheries

    Kuna software nyingine inayowasaidia wavuvi, mFisheries ndiyo moja inayofaa wafuga samaki wadogo wadogo. Software hii ilitengenezwa na chuo kikuu cha West Indies kwa msaada wa Kituo cha kimataifa cha utafiti wa maendeleo IDRC. Wafuga samaki wanaweza kutumia software hiyo kufahamu bei ya samaki. Pia ina sehemu ya kuwakutanisha wauzaji na wateja, na biashara inaweza kufanyika papo kwa hapo. Wafugaji pia wanaweza kuuza samaki kwenye maduka au kwenye soko la samaki kwa kutumia software hii. Ina vifaa kama vile dira, mfumo wa GPS wa kuonesha muuzaji alipo na mafunzo ya kiufundi yakiwemo masomo mafupi kuhusu huduma ya kwanza.

    *M-Shamba

    M-shamba inatumiwa na wakulima wengi nchini Kenya. Software hii inawasaidia wakulima kutumia teknolojia za kisasa za kilimo cha mpunga, na inatoa habari za maeneo maalum kuhusu utunzaji wa mifugo na mimea. Wakulima pia wanaweza kubadilishana habari kuhusu maswala mbalimbali ya kilimo. Huduma zinazotolewa kupitia M-shamba pia ni pamoja na uvunaji, masoko, mikopo na hali ya hewa. Software hii inawawezesha wakulima kupata habari kwa kutumia simu zao za mkononi.

    *AgroSim

    AgroSim inatoa huduma kupitia kompyuta au simu za mkononi. Software hii inawasaidia wakulima kufanya uamuzi kuhusu miradi ya kilimo. Data zinazotolewa kwa wakulima kupitia huduma hii zinakusanywa kutoka kwenye mtandao wa internet na inahusu viwango mbalimbali vya ukuaji wa mimea. Data hizo pia zinaeleza wakulima kiwango na ubora wa mavuno watakayopata kwa kuzingatia aina ya mbegu, udongo, hali ya hewa, eneo na hali ya kiuchumi ya jumla ya eneo fulani.

    *Farming Instructor

    Farming Instructor ni software ya simu ya mkononi inayotoa habari za kilimo kwa wakulima na jamii kupitia kwa ujumbe mfupi na picha. Software hii inalenga kuwashawishi vijana na watu wengine katika jamii kuwa na hamasa ya kujihusisha na shughuli za kilimo kama njia moja ya kujiajiri. Kwa kutumia huduma hii wakulima ama walaji wanaweza kupata habari zote zinazohusu kilimo na kubadilishana ushauri na mawazo kuhusu sekta ya kilimo.

    *Mobile Agribiz

    Mobile Agribiz ni software nyingine iliyobuniwa na kampuni ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Huduma za software hii zinaweza kupatikana kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi au tovuti yake ya Mogribu.com. Inasaidia wakulima kupanga muda wa kupanda, kuchagua mimea inayofaa eneo lao kwa kutumia habari kuhusu hali ya hewa, na pia inatoa habari kuhusu masoko. Wakulima wanaunganishwa na wateja wa bidhaa zao, na wanashauriwa kuhusu bei na njia bora za upandaji na matumizi ya mbolea. Kwa kutumia simu zao za mkononi wakulima wanaweza kutuma ujumbe unaoonesha mazao walio nayo, ubora wake na bei zake. Data hiyo inawekwa kwenye mtandao wa internet na kusambazwa kwa wateja ili kuwaunganisha na wakulima.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako