• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kipindi maalum cha Siku ya Wapendanao

    (GMT+08:00) 2015-02-16 11:03:37

    P. Katika kipindi cha leo tutazungumzia Siku ya wapendanao yaani Valentine's Day iliyokuwa jumamosi iliyopita. Siku hiyo inaonekana kama ni sikukuu ya vijana, na zawadi kama vile chokoleti na maua ya waridi zinazowakilisha mapenzi zinaonekana kila mahali wakati wa sikukuu hiyo. Watu wengi wanasherehekea sikukuu hiyo kwa namna tofauti. Lakini sikukuu hii chimbuko lake ni nini hasa?

    C. Katika upekuzi wangu nimekuta kuwa, siku hii ya Valentine's Day ilibuniwa na kiongozi mmoja wa dini ya kikristo miaka kadhaa iliyopita aliyeitwa Valentino ikiwa na maana upendo zaidi katika maisha ya mwanadamu na familia yake, ila jinsi miaka inavyokwenda siku hii imekuwa ikiadhimishwa tofauti na malengo yake. Siku ya wapendano yaani Valentine's Day huwa ni February 14 ya kila mwaka, na inapendwa sana na wale walio kwenye mahusiano ya kimapenzi, kuliko yale ya kifamilia.

    P. Sikukuu hii si kama imeanza hivi karibuni, ilikuwepo kwa miaka mingi sana, ila kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2000 siku hii imekuwa na shamrashamra sana katika nchi mbalimbali hasa za Afrika. Ni wazi kuwa sikukuu hiyo kwenye nchi zetu sio rasmi, lakini kutokana na tamaduni za kimagharibi kuingia sana barani Afrika na kuigwa hasa na watu wa kizazi kipya, kutokana na ukuaji wa teknolojia hasa internet, simu za mkononi, TV hata vituo vya radio ambavyo vimeingiza kwa kasi kubwa tamaduni za kimagharibi katika nchi hizo.

    C. Siku hiyo inapambwa zaidi na mavazi ya rangi nyekundu na maua mekundu ya waridi, kila kona na kila utakayekutana nae siku hiyo hasa vijana basi atakuwa amevaa nguo nyekundu au hata kuwa na kitu kidogo tu chenye rangi nyekundu ambayo wengi wanadai kuwa ni rangi ya upendo. Nchini China ni tofauti kidogo na nchi nyingine, siku hii haina nafasi sana kwao kwa maana wao Wachina, wanajali sana tamaduni zao ingawa hivi sasa baadhi ya vijana wa kizazi hiki cha sasa wanaihusudu siku hiyo. Sasa kuhusu siku ya wapendanao ya mwaka huu, Bw. Zhang kutoka mkoa wa Fujian ana mpango wake maalum.

    "Siku ya wapendanao ya mwaka huu ni karibu na Sikukuu ya Spring, kwa hivyo nina mpango wa kuomba likizo mapema ili kurudi kwetu kusherehekea pamoja na mchumba wangu. Labda nitanunua zawadi, kama vile maua, na pia tutakwenda kula pamoja, hii bila shaka haikosekani. Labda siku hiyo hiyo tutakwenda kutembelea sehemu za burudani, au tutakwenda madukani, au kwenda kitongoji."

    C. Huo ndio mpango wa Bw. Zhang ambaye ana miaka zaidi ya 30. Pili, nadhani si Zhang tu mwenye mpango kama huo. Naona hapa China, vijana wengi, haswa wanaoishi mijini wanajua siku ya wapendanao, lakini wavulana na wasichana wanaipokea kwa maoni tofauti. Hebu tusikilize maoni ya kijana huyo Zhang.

    "Naona maneno yanayowakilisha siku hiyo kwanza ni 'kula', na lingine ni 'furaha'. Binafsi sifuatilii sana siku ya wapendanao, lakini mchumba wangu anafuatilia sana, hivyo nitafanya anachopenda."

    P. Ni kweli kuwa sio wanaume wengi wanaofuatilia siku ya wapendanao, bali wasichana na wanawake wanaipenda sana na wanapenda kuonyeshwa mapenzi kutoka kwa waume, wachumba, au marafiki zao wa kiume. Bi Zhang kutoka mkoa wa Heilongjiang, kaskazini mashariki mwa China amesema, awali alikuwa anafuatilia sana siku hiyo, na alikuwa anafanya maandalizi mapema sana. Alipendelea kwenda kwenye migahawa au baa zenye mandhari ya kimapenzi, au kwenda migahawa inayozunguka iliyo na mandhari nzuri nyakati za usiku. Hata hivyo, sasa Bi Zhang anaona kuwa haina haja kupoteza pesa kwenye mikahawa au baa ambazo zinaweza kuwa na msongamano, na anapenda zaidi zawadi inatolewa kwa moyo uliojaa upendo kuliko maua na chokoleti.

    "Bila kujali wapenzi wamekuwa pamoja kwa muda gani, bado wana matumaini ya kupata zawadi ndogo, haihitaji kuwa na gharama kubwa, hasa sitaki mchumba wangu aninunulie maua ya waridi siku hii. Anaweza kunizawadia herein au cheni, ambazo si za bei kubwa au za chapa maarufu, lakini zionyeshe tu upendo wake halisi kwangu. Aidha, nilisikia kuwa baadhi ya wenzangu wanatengeneza 3D printer, inayoweza kutengeneza chokoleti maalum ya siku ya wapendanao kwa ajili yao. Naona hii pia ni nzuri, kama ikiwezekana, ningependa kujaribu."

    C. Unajua Pili watu wengi wameweka umuhimu mkubwa kwenye zawadi katika siku hii, lakini kwa mtazamo wangu, naona hata kama huna zawadi, kuwa pamoja na mpenzi wako ni muhimu zaidi. Kama huna zawadi, mnaweza kuandaa chakula pamoja kisha mnakula pamoja, au hata mnaweza kuangalia tamthilia mnazopenda kwa pamoja. Cha muhimu zaidi, ni kuwa na yule umpendaye na kufanya yale mnayoyapenda katika siku hizi.

    P. Ni kweli kabisa Carol, kwani unatakiwa kumwonyesha mapenzi mwenza wako siku 365 za mwaka, sio siku moja tu. Hebu sasa tuangalie kule nchini Kenya ili kufahamu siku hii ilisherehekewaje?

    P. Haya, ni maoni ya watu kuhusu Valentine's Day. Kuna wanaosema kuwa siku hiyo ni gharama tu, kwani ukizingatia hali ya maisha ni ngumu, hivyo kununua maua na mavazi ya rangi nyekundu ni kupoteza tu pesa! Lakini pia kuna wanaosema kuwa, siku hiyo ni siku ya kuonyeshana upendo bila kujali imani za kidini, bali kwa pamoja watu waonyeshane upendo wa kweli kutoka moyoni.

    C. Haya msikilizaji, mpaka hapo ndio tumekamilisha kipindi hiki cha Sauti ya Wanawake ambapo kwa siku ya leo tulikuwa tunazungumzia siku ya Valentine iliyosherehekewa mwishoni mwa wiki iliyopita. Hadi wiki ijayo, kwa niaba ya mtangazaji mwenzangu Pili Mwinyi, mimi ni Caroline Nassoro, asante, na kwa heri.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako