• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mambo maarufu yanayowahusu wachina

    (GMT+08:00) 2015-02-26 15:49:07
    Kama kawaida tuko hapa kuwafahamisha yale tunayoyaona tunapoishi na kufanya kazi hapa China. Leo tunazungumzia mambo yanayotajwa kuwa ni mambo maarufu yanayowahusu wachina.

    Pili: La kwanza kabisa ukitaja mchina kwanza watu huwa wanakumbuka Bruce Lee au Jackie Chan. Ingawa hawa jamaa walitengeneza filamu zao miaka mingi sana iliyopita, bado wamekaa akilini mwa watu wengi. Lakini siku hizi watu wameanza kuwa na maoni mengine kuhusu China, na leo tutawafahamisha wasikilizaji China ni hodari kwa kitu gani, pia tutasikia maoni mbalimbali kutoka kwa wasikilizaji kuhusu China.

    Fadhili: Pili labda kwanza ni vizuri tukianza na maoni ya wasikilizaji wakisema wanawaona vipi wachina, na baadaye tuwaeleze hali halisi iliyopo hapa China. Tuanze na kumsikiliza Bw Godilizen wa Tanzania

    "Kwetu Tanzania, wachina wanajulikana kama wafanyabiashara wakubwa wa kuuza vitu mbalimbali duniani."

    Fadhili: Pili maoni hayo ya Bw Godilizen sio ya watanzania tu, watu wengi duniani wanajua kuwa wachina ni hodari kwenye biashara. Lakini kwa sisi tulioko hapa China, nadhani tunaweza kusema si wachina wote ambao ni hodari kwa biashara. NI kama kwetu Tanzania ukitaja wafanyabiashara, basi mara nyingi unazungumzia wapemba na wachaga, hapa China pia kuna baadhi ya watu ambao ni hodari kwa biashara.

    Pili: Ni kweli kuzungumzia biashara kwa hapa China mara nyingi ni kwamba tunazungumzia watu wa mikoa ya kusini, kama vile Jiangsu, Zhejiang, Guangdong na mingine ya huko, lakini bahati mbaya ni kuwa watu Afrika wakiona mchina wanajua ni mchina tu hata hawajui kabila lake au anatoka wapi.

    Fadhili: Nadhani hali hiyo ni sawa na kwa sisi waafrika, ukiwa hapa China watu wanafikiri ukiwa mwafrika unaweza kucheza muziki vizuri, unaweza kuimba unaweza kukimbia kama wanariadha wa Kenya au Ethiopia

    Pili: Ni kweli hii ndio hali tunayokumbana nayo waafrika hapa China, wakati mwingine wachina wanadhani waafrika wote wanajua Kiingereza au kifaransa. Ukipita baadhi ya sehemu kama vile sehemu za biashara utakuta watu wanakuongelesha kifaransa au Kiingereza.

    Fadhili; Kuna msikilizaji wetu mwingine ambaye anatueleza kule Bujumbura watu wanafikiri nini wakiwaona wachina, maana sasa kama nilivyosema picha ya China imeanza kubadilika kutoka ile ya kina Bruce Lee na Jackie Chan na kuwa na picha nyingine

    "Hapa Bujumbura, wachina wanaotambua kwa viwanda vya mbalimbali kama simu, radio, tv, hata vingine vingi. "

    Pili: Huyo ni msikilizaji wetu Eric kutoka Bujumbura, nadhani imani yake na watu wa Bujumbura kama alivyosema labda haiko mbali sana na ukweli. Ni kweli hapa China kuna viwanda vingi vya simu, Radio na TV. Lakini bidhaa hizi zenye nembo ya "made in China" zinafanya baadhi ya watu wafikiri kuwa China ni nchi ya viwanda tu, ukweli ni kuwa bado sehemu kubwa zaidi ya wachina ni wakulima, na kuna shughuli nyingi sana za kilimo hapa China mbali na shughuli za viwanda.

    Fadhili: Njia rahisi ya kutaja hilo ni kuwa China ni nchi yenye watu zaidi ya bilioni 1.3, na watu hao wanakula kila siku, kwa hiyo unaweza ukipiga mahesabu kuhusu uzalishaji wa chakula hapa China. Ni si kila mtu ana simu, si kila mtu ana radio na si kila mtu ana televisheni, wakati mwingine familia ya watu watatu ina radio moja au haina kabisa radio, TV moja au haina TV kabisa, lakini chakula kila mtu anakula bila kujali yeye ni tajiri au maskini.

    Pili: kuna msikilizaji wetu mwingine Juma Ochora kutoka Kenya, yeye pia amesema wachina ni hodari kwa viwanda, biashara, lakini ametaja lingine muhimu, michezo. Anasema kila mara anaona wachina ni hodari kwenye michezo ya gymnastic.

    Fadhili: NI kweli, pamoja na kuwa kwa sasa Marekani ndio inaongoza kwenye michezo hiyo, China kimsingi ina nafasi kubwa ya kuipiku Marekani. China ni nchi hodari zaidi kwenye michezo ya ndani, na ina viwanja vingi sana vya michezo ya ndani. Lakini tatizo moja kubwa kwenye michezo ya China ni kuwa bado sio hodari kwenye soka, na uhodari wa wachina uko kwenye michezo ya mchezaji mmoja mmoja, ile michezo ya vikundi iko nyuma.

    Pili: Lakini kwenye michezo ya makundi ya wanawake, wachina wanajitahidi sana na wanafanya vizuri kuliko wanaume. Nadhani tunakumbuka kuwa timu ya soka ya wanawake ya China imepiga hatua kubwa na kutoa changamoto kwa timu kubwa kama Marekani au hata Ujerumani. Kwenye michezo ya olimpiki wanawake huwa wanavuna sana medali.

    Fadhili: Kuna wengine vile vile wana imani za jumla kuhusu China, nyingine labda zinatokana na ufahamu wa China kupitia vyombo vya habari. Nimemuuliza Bw Exaud Mayao wa Tanzania yeye alikuwa na maoni yafuatayo ya jumla kuhusu China

    "Ninapoona mchina au kusikia jina la mchina, kuna vitu vitatu vinakuja kwa haraka katika akili yangu. Jambo la kwanza namona mchina kuna ni mbunifu, tumesikia vitu vingi sana ambavyo bidhaa nyingi zinakuwepo duniani kwa sababu ya ubunifu wa wachina. kwa hiyo nikiona mchina, naona mbunifu. Jambo la pili, nimesikia kwamba China hakuna masuala ya rushwa, kwa hiyo nikiona mchina, ninaona mtu msafi asiyekula rushwa, asiyeingia katika masuala ya siku hizi kama tunavyosema ya ufisadi. Na jambo la tatu, nikimwona mchina, ninaona mtu ambaye ni mchapakazi. Mara nyingi nimeona wacina wako spidi sana, hawafanya kazi kwa taratibu, wanafanya kazi kwa haraka sana. hata lugha wanavyoongea wachina, anaongea naweza kufikiri anagombana na wenzake. wanakimbizana na muda, hawana muad wa kupoteza. "

    Pili: Naona Bw Makyao ameeleza mengi na kwa ujumla sana kuhusu wachina. La ubunifu ni kweli kwa kuwa tunaona mengi sana ambayo tungependa yawepo kwenye nchi zetu, na la kuchapa kazi ni kweli kwani hata matokeo yake huko kwenye nchi zetu yanaonekana, kwanza kwa bidhaa wanazotengeneza wachina na pili ama alivyosema Bw Makyao kuwa wakiwa kwenye maeneo ya kazi wanaonekana kufanya kazi sana. Lakini kuhusu ufisadi, nadhani si kweli kama hakuna ufisadi hapa China. Upo, labda tofauti kubwa iliyopo kati yetu na wenzetu ni kuwa hawacheki na ufisadi

    Fadhili: kwa sasa hapa China kuna kampeni kali ya kupambana na ufisadi, Rais wa China Xi Jinping amesema kuwa serikali itakamata "chui na nzi". Kule nyumbani tunasema "mapapa na vidagaa". Hapa China ukweli ni kuwa tunaona mapapa wanakamatwa, sio kauli tu za kuwafurahisha wananchi au hadithi kwenye vyombo vya habari.

    Pili: Lakini kuna mambo mengine mengi sana yamebadilika, lakini bado watu wanaendelea kuamini kuwa bado yapo. Na baadhi ya mambo naona yamebaki Afrika na hapa China hata huwezi kuyaona, kwa mfano hapa China sikumbuki kama nimewahi kuona mtu amevaa suti ya Zhou Enlai, kama ukiona mtu amevaa suti ya namna hiyo basi ujue kuwa ni mwanasiasa aliyekuja kutoka Afrika anayekumbuka enzi zile za kina mwenyekiti Mao na Zhou Enlai. Pia hakuna watu wanaovaa sare za bluu kama tulivyokuwa tunaona kwenye filamu za zamani za China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako