• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ukatili dhidi ya wanawake na watoto majumbani

    (GMT+08:00) 2015-03-23 14:40:49

    Ukatili majumbani umeendelea kuwa tatizo kubwa ambalo hadi leo halijaweza kutokomezwa moja kwa moja na wanaume wameendelea kuwa vichwa na viongozi wa familia. Mfumo dume unaendelea kushika hatamu na utamu katika katika jamii nyingi duniani. Wanawake wengi wamekuwa wakidhalilishwa kwa kupigwa na kama haitoshi baadhi ya wakati hata watoto nao pia huingia katika mkumbo huo wa kupigwa majumbani.

    Mama anayelia kwa uchungu na kumtaka mtoto wake ni bibi Wang. Mara baada ya mwandishi wa habari kuingia nyumbani kwake akasikia kilio cha mama huyu, na baada ya kumuangalia aliona kovu nyingi usoni mwake, je ni masaibu gani yaliyomtokea mama huyu? Shemeji yake bibi Wang alimwambia mwandishi wa habari kuwa, usiku wa tarehe 15 Januari mwaka huu, mume wa bibi Wang aitwae Bw. Gu, alitumia shoka kumkata bibi Wang mara 17 usoni na kichwani mwake, kama hiyo haitishi alimkata pia mtoto wa bibi Wang mwenye umri wa miaka minane tu, lakini bahati nzuri tu bibi Wang na mtoto wake wote wamenusurika.

    Kwa kweli inasikitisha sana kwani hicho kitoto hakina hatia yoyote lakini kimeingizwa kwenye ukatili huo. Bibi Wang na Bw. Gu hii ni ndoa yao ya pili, na mtoto huyo ni mtoto wa bibi Wang aliyempata kwa mume wake wa zamani. Bibi Wang aliolewa na Bw. Gu akiwa na mtoto wake baada ya kufahamishwa na rafiki yake na kuwa pamoja kwa miezi miwili tu.

    "Tulipooana tulikubaliana kuwa tuishi vizuri, lakini haikuwa hivyo. Siku chache tu baada ya kuoana, alianza kumpiga mtoto wangu. Mtoto ni mdogo namna hii, nasikitika sana moyoni mwangu."

    Kama tulivyoweza kumsikia bibi Wang ni kwamba wiki moja tu baada ya ndoa, mume wake Bw. Gu alianza kumpiga mtoto, jambo ambalo linamfanya bibi Wang asikitike sana. Taratibu, bibi Wang akagundua kuwa, tabia ya mume kumbe ni mbaya sana. Hivyo kabla hata mwaka mmoja kumalizika, bibi Wang alitaka kutalikiana kwa mara ya kwanza, lakini mume wake alimrubuni kwa kutaka kumpa bibi Wang Yuan elfu 10.

    Bibi Wang hana kazi, na anaishi kwa kutegemea kilimo. Yeye na mtoto wake wanategemea msaada wanaoupata kutoka kijiji kwao Yuan 9,000 kila mwaka. Hivyo bibi Wang alikataa matakwa ya mumewe, na masuala ya talaka pia yalikwisha kwa muda. Lakini mwezi mmoja baadaye, Bibi Wang alipokuwa amelala aliamshwa usingizini na Bw Gu na kuanza kuongelea tena suala la kumpa fedha, hata hivyo bibi Wang alikataa tena. Na baada ya kumkatalia mumewe, bibi Wang akaendelea kulala. Lakini hapo sasa jambo labaya na ukatili likatokea.

    "Nilikuwa nimepitiwa na lepe la usingizi, mara nikashtuka alipoanza kunifinya, na kunipiga kwa nguvu kubwa, baadaye sikufahamu lolote lile."

    Hayo ni maneno ya kuhuzunisha kutoka kwenye kinywa cha mwanamke aliyefanyiwa kitendo cha ukatili nyumbani pamoja na mtoto wake. Baada ya Bw. Gu kumpiga bibi Wang, hakuishia hapo, akaamua kuchukua shoka na kuanza kuwakata bibi Wang na mtoto wake aliyekuwa amelala kando yake. Kwa kuwa alijeruhiwa vibaya, bibi Wang akashindwa kujihudumia, kwa hiyo akawa anahudumiwa na dada yake pamoja na shemeji yake wenye umri wa miaka zaidi ya 60.

    Hapa tunaweza kujifunza kutokana na ukatili huu, kwa mfano namna ya kugundua kama mchumba wako ana tabia za ukatili ikiwemo kupiga na hasira za kupindukia au la kabla ya ndoa? Namna ya kumfahamu mchumba wako kwa kikamilifu? Pia, baada ya kubishana, utajikingaje na mtu huyo mwenye hasira za kupindukia na apendaye kupiga?

    Sasa mtaalam wa kisaikolojia wa kampuni ya utoaji ushauri wa kisaikolojia ya Chenhui Beijing Bw. Lei Ming anasema, tunapokabiliana na vitendo vya ukatili nyumbani, mara ya kwanza ni muhimu sana kulishughulikia vizuri suala hilo. Kama mwanamke atavumilia anapokabiliwa na vitendo vya ukatili nyumbani kwa mara ya kwanza, na kuamua kumsamehe anayefanya vitendo hivyo, ni sawa na kumfumbia macho kwa makusudi anayefanya ukatili huo kisaikolojia na kivitendo. Naye Mwanasheria wa Ofisi ya sheria ya Zhaotianqing Bw. Yuan Tao pia alitoa shauri na hapa anasema,

    "Mhanga wa vitendo vya ukatili nyumbani lazima aseme Hapana kwa vitendo hivyo! Akiwa kila mara anavumilia itachochea kuongezeka kwa vitendo vya ukatili nyumbani."

    Mbali na hayo Bw. Yuan pia amesema, baada ya kutokea kwa vitendo vya ukatili nyumbani kwa mara ya kwanza, mhanga anaweza kulinda haki na maslahi yake kupitia idara ya kulinda usalama wa umma au idara ya sheria na hapa anaeleza zaidi

    "Baada ya kufanyiwa ukatili kwa kupigwa nyumbani, kwanza lazima uwe na ushahidi husika, kwa mfano vipimo vya hospitali, ikiwa ni pamoja na risiti za gharama za matibabu, picha inayoonesha ulivyoshambuliwa tena iwe ya wakati ule ule, baadaye utoe ripoti katika idara ya polisi, au kwenda mahakamani moja kwa moja kumshitaki Yule aliyefanya ukatili dhidi yako, na kumtaka atoe fidia, au kutoa shataka katika mahakama inayohusiana na makosa ya uhalifu."

    Na katika kuonesha unyeti wa suala hili katika kipindi cha Mikutano miwili ya China ya mwaka huu iliyomalizika hivi karibuni, waraka wa kwanza nchini China wa kuelekeza sheria ya kupambana na vitendo vya kukatili nyumbani umetolewa, na kuonesha kuwa sheria ya kupambana na vitendo hivyo inafuatiliwa tena. Sheria hiyo inaonesha kuwa taifa linafuatalia watu dhaifu, pia inaonesha maendeleo ya jamii ya China na ukamilishaji wa utaratibu, ambapo pia inasaidia kulinda hadhi ya wanawake kwenye jamii na maslahi yao.

    Kila siku huwa tunasema kwamba watu dhaifu wanaokumbwa na vitendo vya ukatili nyumbani, basi wengi ni wanawake na watoto, na wanfanyaji wa vitendo hivyo wengi wao ni wanaume. Uchunguzi uliofanywa na Shirika la wanawake la China umeonesha kuwa, idadi ya wanawake waliowahi kutukanwa, kupigwa, kunyimwa uhuru na fedha na waume zao ama kukabiliwa na vitendo vingine vya kikatili nyumbani inakaribia asilimia 25. Kati yao, idadi ya wanawake walio olewa ambao walieleza dhahiri kupigwa na waume zao imefikia asilimia 5.5, ambapo idadi hiyo ya vijijini ni asilimia 7.8 na mijini ni asilimia 3.1.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako