• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maelezo kuhusu "hali mpya ya kawaida" ya uchumi wa China

    (GMT+08:00) 2015-03-24 20:13:56

     

    "Hali Mpya ya Kawaida" ni maneno yanayotajwa mara kwa mara wachina wanapozungumzia uchumi wa nchi hiyo, kuhusu ukuaji na mageuzi ya uchumi wa China. Lakini maneno hayo yanamaanisha nini haswa?

    Katika mkutano wa Bunge la Umma la China uliokamilika wiki iliyopita, serikali ya China ilitangaza lengo la ukuaji wa uchumi wa China wa asilimia 7 kwa mwaka 2015.

    Mwaka jana, uchumi wa China ulikua kwa asilimia 7.4, ikiwa ni chini kidogo ya lengo la asilimia 7.5 lililowekwa mwanzoni mwa mwaka huo, na pia ilikuwa ni kasi mdogo zaidi ya ongezeko la uchumi wa China katika miaka 24 iliyopita. Na mwaka huu, China ilizidi kupunguza lengo hilo kuwa asilimia 7, huku uchumi wa China ukiingia kwenye "hali mpya ya kawaida". Hali hiyo inazungumzia mabadiliko kutoka ukuaji wa kasi kubwa hadi kasi yenye kiwango cha kati. Pia inaonesha mabadiliko kutoka kufuatilia ukubwa na kasi hadi ubora na ufanisi kwenye mfumo wa ukuaji. Kuzoea "hali mpya ya kawaida" ni chaguo la kimkakati kwa serikali ya China ili kusaidia uchumi wake ukue kwa utulivu na kupata maendeleo mazuri japokuwa kasi ya ukuaji inashuka kidogo.

    Chen Fang ni mjumbe wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China ambalo ni chombo cha ngazi ya juu cha kutoa ushauri wa kisiasa nchini humo.

    "Hii ni fikra na chaguo la kimkakati kwa ajili ya ukuaji wa uchumi. Inaelezwa kwa maneno mawili: 'mpya' na 'kawaida'. Maana ya 'mpya' ni kuwa tunapaswa kuwa na wazo tofauti la maendeleo ikilinganishwa na la zamani, huku 'kawaida' ikimaanisha kuwa uchumi unapaswa kupata ukuaji endelevu, wa utulivu na mzuri."

    "Hali mpya ya kawaida" ambayo inasisitiza mpangilio mpya wa uchumi itaweka msingi endelevu kwa maendeleo ya uchumi wa China.

    Akizungumza na Shirika la Habari la China, Xinhua, mwanauchumi wa kampuni ya ukaguzi wa hesabu na ushauri ya Deloitte tawi la Ufaransa Jean-Paul Betbeze amesema "hali mpya ya kawaida" ya uchumi wa China inamaanisha kuwa, China inapaswa kutilia mkazo zaidi nguvu ya matumizi ya wananchi na mahitaji ya ndani ya nchi, na ukuaji wa uchumi unapaswa kuzingatia zaidi ubora, ulinzi wa mazingira na wajibu wa jamii.

    Naye mwakilishi wa Bunge la Umma la China Liu Yonghao anakubaliana na Betbeze na kusema,

    "Tunatakiwa kuacha mtindo wa kupata ukuaji unaotegemea kuwekeza kama kipofu, matumizi ovyo ya rasilimali, na kupuuza ulinzi wa mazingira. Biashara zetu, uwekezaji na maendeleo vinatakiwa kutilia maanani zaidi ulinzi wa mazingira na matumizi sahihi ya rasilimali, na pia kufuatilia athari za maendeleo ya biashara na uchumi kwenye jamii."

    Kama alivyosema Liu Yonghao, katika miongo mitatu iliyopita, serikali kuu na za mitaa nchini China zilitoa kipaumbele kwa maendeleo ya uchumi kuliko uhifadhi wa mazingira, maliasili na rasilimali, kutokana na kwamba wakati ule tatizo kubwa la njaa ndilo la kwanza lililopaswa kushughulikiwa. Lakini sasa, baada ya uchumi wake kukua kwa kasi mno kwa miongo mitatu, China inashika nafasi ya pili kwa ukubwa wa uchumi wake, kwa hiyo imeamua kuachana na ukuaji usio na uwiano wa uchumi, na watunga sera wamesisitiza kuwa, ulinzi wa mazingira utakuwa kipaumbele cha serikali ya China kwa mwaka huu. Msisitizo kuhusu ulinzi wa mazingira kutoka kwa serikali na jamii nzima inaonesha kuwa, China inatafuta njia bora na endelevu kwa maendeleo. Sheria mpya ya mazingira iliyotolewa mwezi Januari inayojulikana nchini China kama sheria kali zaidi ya uhifadhi wa mazingira imeongeza adhabu kwa vitendo vinavyochafua mazingira na kuweka wazi kwamba mashirika yanayotetea maslahi ya umma yana haki ya kutoa mashtaka kuhusiana na mazingira.

    Baadhi ya watu wana wasiwasi kama kweli China itapunguza kasi ya ukuaji kwa ajili ya kulinda mazingira. Lakini hali halisi ni kuwa, ulinzi wa mazingira na ukuaji wa uchumi havikinzani, na "hali mpya ya kawaida" pia haimaanishi kuwa uchumi wa China utakwama au hata kurudi nyuma. Lengo la kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi lililo chini ya "hali mpya ya kawaida" na msisitizo kuhusu ulinzi wa mazingira vitatoa mzunguko mzuri kutokana na kwamba kupungua kwa uwekezaji wa mali zisizohamishika kutapunguza shinikizo kwa mazingira, na kuongeza ukali wa sheria za mazingira kutalazimisha sekta zilizo nyuma kuondolewa.

    Hivi majuzi waziri mkuu wa China Li Keqiang alisema serikali itatunga sera kabambe ili kuhakikisha uchumi unakua kwa kiwango kinachofaa mwaka huu. Anasema

    "Kama kasi ya ukuaji wa uchumi ikifikia mstari wa chini wa kiwango kinachofaa kwenye mchakato wa uendeshaji wa uchumi na kuathiri sekta ya ajira na mapato ya watu, tuko tayari kuchukua taratibu za uchumi wa jumla ili kuongeza imani ya sasa katika soko, na pia kudumisha mfululizo wa sera za uchumi wa jumla ili kutuliza imani ya soko kwa muda mrefu."

    Li Keqiang alikiri kuwa uchumi wa China unakabiliwa na shinikizo na hatari zinazotokana na kupungua kwa kasi ya ukuaji, lakini alisisitiza kuwa serikali ina nafasi kubwa kwa mabadiliko ya sera.

    "Jambo zuri ni kuwa, katika miaka kadhaa iliyopita, hatukuchukua hatua nyingi za kuchochea uchumi. Hali hii inatuwezesha kuchukua hatua mbalimbali za kujaribu sera za uchumi wa jumla, pia tuna njia nyingi za kisera zilizohifadhiwa ambazo zinaweza kutumiwa."

    Wakati uchumi wa China unapoingia kwenye "hali mpya ya kawaida", wataalamu wa kiuchumi pia wameeleza ufuatiliaji wao na kutoa tahadhari. Naibu mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge la Umma la China Yin Zhongqing anasema, China inatakiwa kuwa macho kutokana na hatari za aina sita ambazo ni pamoja na uzalishaji wa kupita kiasi, mfumuko wa bei katika soko la nyumba, madeni ya serikali za mitaa, mashirika ya kifedha yaliyo nje ya utaratibu wa kusimamia sekta ya benki, shinikizo la muundo kwenye kilimo na punguzo la fedha kwenye mazunguko.

    Ili kukabiliana na masuala hayo, aliyekuwa mwanauchumi mkuu na makamu mwandamizi wa rais wa Benki ya Dunia Bw. Justin Yifu Lin anasema, China inaweza kuwa na manufaa katika maeneo kadhaa. Anasema katika utengenezaji wa vifaa, China inaweza kutilia maanani sekta ya elektroniki, malighafi na vyombo vya kisayansi, na mtandao wa internet nchini China pia ni eneo jingine jipya ambalo nguvu zake hazijatumiwa ipasavyo. Pia ametoa mapendekezo kuhusiana na uzalishaji wa kupita kiasi.

    "Ingawa kuna uzalishaji wa kupita kiasi, kama vile katika saruji, chuma cha pua na aluminiamu, lakini kutokana na uwekezaji katika ujenzi wa miundo mbinu kama vile mpango wa "Ukanda Mmoja na Njia Moja", vitu hivyo vitakuwa na soko kubwa"

    Bw. Justin Yifu Liu ameeleza imani yake kubwa na uchumi wa China, na kusema kuwa una nguvu ya kukua kwa asilimia 8 katika miaka 20 ijayo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako