• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Chai ni kinywaji kisichokosekana katika maisha ya kila siku ya Wachina

    (GMT+08:00) 2015-03-26 14:49:25

    China ni maskani ya miti ya chai duniani. Wachina wamekuwa na historia ya miaka elfu nne ya kunywa chai. Chai ni kinywaji ambacho hakiwezi kukosekana katika maisha ya kila siku ya Wachina. Wageni wanapofika nyumbani kwa mchina, hukaribishwa kwa chai, na kuongea na mwenyeji wao huku wakinywa chai pamoja.

    Awali chai ilitumiwa na Wachina kama chakula na dawa, baadaye walianza kunywa chai kama kinywaji. Hadi kufikia karne ya 7, desturi ya kunywa chai ilikuwa imetia mizizi katika jamii ya Wachina, na kubadilika kuwa sehemu ya utadamuni wa China.

    Inasemekana kwamba desturi ya kunywa chai inahusiana na kuenea kwa dini ya Kibuddha nchini China. Watawa wa dini ya Kibuddha waliokuwa wakisoma vitabu vya dini kwa muda mrefu waliisikia usingizi, hivyo walikunywa chai kuondoa usingizi. Pia kwa vile waumini wa dini ya Kibudha walikuwa hawanywi pombe, chai ikawa kinywaji kinachofaa.

    Katika karne ya 8, mchina aliyeitwa Lu Yu aliandika kitabu maarufu cha 'Cha Jing' akijumuisha ujuzi mbalimbali kuhusu chai , kama vile namna ya kulima miti ya chai, kutengeneza majani na sifa za aina mbalimbali za chai. Zaidi ya hayo alitaja kwenye kitabu hicho maadili ya kunywa chai, namna ya kunywa chai ili mnywaji aburudike zaidi kiroho. Kitabu hicho ni cha kwanza cha kitaaluma kuhusu chai duniani. Na kuanzia karne ya 10 wafalme wa China walianzisha desturi ya kuwakaribisha wageni kwa chai.

    Nchini China kunywa chai ni sehemu muhimu ya utamaduni. Tokea enzi na dahari hadi leo mikahawa ya chai inapatikana kila mahali nchini China, na katika sehemu ya kusini kama vile mkoa wa Sichuan pia kuna vibanda vya chai. Watu wanapenda kunywa chai huku wakipumzika na kuburudika na michezo ya sanaa.

    Wachina kutoka sehemu tofauti wanapendelea chai tofauti. Watu wa sehemu ya kaskazini hupenda kunywa chai ya maua kama vile chai ya Jasmine, watu wa kusini hupenda chai ya kijani na baadhi ya watu wanapenda kunywa chai nyeusi.

    Namna ya kunywa chai pia ni tofauti katika sehemu tofauti. Watu wa sehemu ya mashariki ya China wanapenda kutumia bilauri kubwa na kutia majani ya chai ndani yake kisha kumimina maji ya moto kiasi ndani ya glasi. Na watu wa sehemu ya kusini wanafuata utaratibu tofauti, wakipenda kumimina maji ya moto kabla ya kutia majani ndani ya glasi. Maadili ya unywaji wa chai pia yanatofautiana kulingana na sehemu. Mjini Beijing, mwenyeji akileta glasi ya chai, mgeni husimama kuipokea kwa mikono miwili kwa kuonesha heshima na kusema "ahsante". Katika sehemu ya kusini mwenyeji akileta glasi ya chai, mgeni hugonga meza mara tatu kwa kidole kuonesha shukrani.

    China ni chimbuko ya miti ya chai, na pia ni nchi inayozalisha majani ya chai kwa wingi duniani. Nchini China kuna majani ya chai ya aina nyingi, miti ya chai inapandwa katika mikoa 20 ya China. Majani ya chai yakivunwa yanatengenezwa kwa njia mbalimbali za kuyasokota, kuumua, kukausha na kuchoma, na kutokana na njia tofauti za utengenezaji, aina mbalimbali za majani ya chai zinapatikana ikiwa ni pamoja na majani ya chai ya kijani, chai nyeusi, na chai ya maua na kadhalika, aina tofauti za majani zina virutubisho mbalimbali vya kusaidia afya ya watu.

    Kila ifikapo mwanzoni mwa mwezi Aprili katika majira ya Mchipuko, ndipo majani mapya ya chai yanapoanza kuuzwa sokoni, wakati huo watu huburudika kwa chai nzuri bila kuchelewa, haswa aina ya chai ya kijani. Kwani katika majira ya Mchipuko mvua zinakuwa nyingi na halijoto ni ya kufaa, hivyo majani yanayochipuka huwa manene na laini yenye virutubisho vingi kutokana na kuwa miti yenyewe imehifadhi lishe nyingi baada ya kupumzika muda mrefu katika majira ya baridi. Kwa hiyo majani ya chai katika majira ya Mchipuko ni bora zaidi. ndiyo maana majani maarufu ya chai yote yanapatikana katika msimu huo wa mwezi Aprili.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako