• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mwitikio wa wananchi wa China kuhusu sera ya kuwa na watoto wawili

    (GMT+08:00) 2015-04-09 19:57:19

    P. Ni mwaka mmoja sasa tangu sera ya kuwaruhusu wanandoa kuwa na mtoto wa pili kama mmoja kati yao ni mtoto wa pekee katika familia ianze kutekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini China. Lakini hali halisi ni kuwa, ombi la kuzaa mtoto wa pili halikuongezeka kwa kiasi kikubwa kama wachina walivyotarajia.

    C. Pili unajua kila kitu kinakwenda kwa mpangilio. Sasa huenda maombi hayajaongezeka kwa kuwa watu bado wanajiandaa na kujipanga kama kweli wanaweza kuwa na mtoto wa pili na kumtimizia mahitaji yote yanayotakiwa. Kuna mambo mengi ya kuangalia kabla ya kupata mtoto, hata mmoja. Unatakiwa ujipange kuhakikisha mtoto wako atapata elimu nzuri, atakula vizuri, atapata haki zote ambazo mtoto anastahili kuzipata, na si kukurupuka tu na kusema unataka mtoto wa pili!

    P. Sasa wakati serikali imetoa sera inayowaruhusu wanandoa kuwa na watoto wawili, kuna baadhi yao ndio kwanza wanajipanga kupata mtoto wa kwanza. Bibi Yan ambaye ameolewa kwa miaka mitatu sasa ni kati ya hao wanaojipanga kuwa na mtoto wa kwanza, lakini ana wasiwasi wake.

    "Mwaka huu ni mwaka wa mbuzi katika kalenda ya kichina, ambao wachina wanaona watoto wanaozaliwa mwaka huu hawatakuwa na hatma nzuri. Huu ni msemo wa jadi nchini China. Kwa hivyo mimi kama marafiki zangu wengi, natumai kuwa na mtoto atakayezaliwa mwaka ujao. Hivyo napanga kupata mimba katika nusu ya pili ya mwaka huu."

    C. Ingawa Bibi Yan sio mtoto wa pekee katika familia yake, lakini mume wake ni mtoto wa pekee, hivyo wanandoa hao wanaruhusiwa kuzaa watoto wawili. Kuhusu suala la kutaka kuwa na mtoto mmoja tu au watoto wawili, Yan anaona

    "Kama tuna uwezo, nataka kuzaa watoto wawili. Hili ni jambo zuri kwa ukuaji wa watoto. Wataandamana pamoja. Na vilevile naona wazazi, babu na bibi wanafuatilia sana mtoto kama ni mmoja, hivyo tukiwa na watoto wawili, watagawanya ufuatiliaji wao kwa watoto hao wawili."

    P. Bi Yan anatambua changamoto za kutekeleza kihalisi mpango wa kuwa na watoto wawili. Anasema hivi sasa nchini China kuwalea vizuri watoto, na kuwapatia elimu nzuri na kuwaandalia maisha mazuri ya baadaye, msingi imara wa kiuchumi unahitajika. Zaidi ya hayo, shinikizo la ajira pia ni changamoto ambayo kinamama hawawezi kuiepuka. Hii inatokana na kuwa, mama ndio mlezi mkubwa wa familia, hatukatai mwanamume ni kichwa cha familia, lakini tunaweza kusema kuwa mama ni waziri mkuu wa familia. Hivyo mama anatakiwa ajipange vizuri kuendeleza kazi yake na wakati huohuo kuwa mlezi mzuri wa familia yake.

    "Kwa sisi wanawake, tunatakiwa kuwa na mpango wetu wa kazi. Kwa sababu ulipozaa mtoto wa kwanza, ulisimamisha shughuli zako kwa muda, kisha ukaendelea tena na kazi. Sasa utakapozaa mtoto wa pili, itakubidi usimamishe tena shughuli zako kwa mara nyingine tena. Basi nitaangalia na kuamua nifanye nini."

    C. Sio tu Bi. Yan ambaye ana tahadhari juu ya kuzaa watoto wawili, mama Chen mwenye mtoto wa kiume wa mwaka mmoja na nusu, anaona kuwa, katika familia yake nyumba sio kubwa ya kutosha, fedha kwa ajili ya kumpatia mtoto mmoja elimu bora haitoshi, na hata yeye mwenyewe binafsi anaona hana nguvu za kuwa na mtoto wa pili. Anasema yeye na mume wake watamtunza mtoto huyo pekee ndani ya miaka minne ijayo, na labda baada ya muda huo, anaweza kuzaa mtoto wa pili kama wengi wa wazazi waliozaliwa katika miaka ya 80 karne iliyopita.

    "Umeniuliza swali zuri, leo ni maadhimisho ya miaka minne tangu nifunge ndoa. Naona kama hutafuata mweleko wa kuwa na mtoto wa pili, basi mtoto wangu anaweza kuuliza 'Baba, kwa nini sina kaka au dada? Nataka sana kuwa na kaka ama dada.' Ukiwa na mtoto mwingine, wataweza kucheza pamoja. Na jambo lingne ni kuwa, baada ya kuwa na mtoto wa kiume, nataka kuwa na mtoto wa kike. Labda watu wengi tuna hamu ya "kuwa na mtoto wa kiume pamoja na mtoto wa kike."

    P. Na ni kweli, maana wengi wenye watoto wa kiume wanapenda kupata watoto wa kike, na wenye watoto wa kike wanapenda kupata watoto wa kiume. Hivi sasa nchini China kuna familia nyingi zenye mtoto mmoja tu, na kutokana na mzingira ya maisha, baadhi ya watoto hao wamekuwa na desturi za kuwa wabinafsi sana. Na watu wana wasiwasi kuwa watoto hao wanakosa msimamo, yaani wanakuwa vigeugeu, wana kiburi, na kuwategemea wengine kupita kiasi. Chen ana haya ya kusema ili kuwawekea mazingira mauri watoto hao:

    "Katika mchakato wa kukua kwa watoto kwa uhuru na kuwa na msimamo, ni lazima ajue kushirikiana na wenzake na marafiki. Kama ukiwa na kaka au dada, utafanyaje? Tunaweza kuwaweka pamoja na kuwafundisha."

    C. Tangu sera ya kuwa na watoto wawili ipitishwe, kwa hapa Beijing, zaidi ya wanandoa elfu 30 wamejiandikisha kwa ajili ya kupata mtoto wa pili. Na maombi ya watu 28,778 yamekubaliwa, idadi ambayo ni ndogo kuliko iliyokadiriwa awali ambayo ilikuwa ni elfu 50. Wanandoa wengi ambao wanaweza kuwa na mtoto wa pili wameamua kutofanya hivyo mwaka huu, lakini hii haimaanishi kuwa hawataki, bali labda hawakao tayari kwa mtoto wa pili.

    P. Unajua kila kitu kina sababu. Sasa baadhi ya wale wasiotaka mtoto wa pili wana sababu zao, wengine wanasema hali ya kiuchumi haiwaruhusu, wengine wanadai kuwa na mtoto wa pili kutawapotezea muda wao, na wengine wanasema, mtoto mmoja anatosha. Kila mtu ana sababu yake ambayo binafsi anaona inafaa. Hata hivyo mji wa Beijing unaendelea kujiandaa kupata watoto elfu 50 kila mwaka, na vitanda 1000 vya ziada vitaongezwa katika hospitali za mji huu ili kukabiliana na ongezeko hilo.

    C. Naam msikilizaji mpaka hapo ndio tumekamilisha kipindi hiki cha Sauti ya Wanawake. Kwa niaba ya mtangazaji mwenzangu Pili Mwinyi, mimi ni Caroline Nassoro. Kwa heri.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako