• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tanzania yatarajia makampuni ya China kushiriki kwenye uendelezaji wa eneo maalum la kiuchumi Bagamoyo

    (GMT+08:00) 2015-04-10 21:57:17

     


    Miaka 35 iliyopita, mji wa Shenzhen ulipokuwa kijiji kidogo cha uvuvi kusini mwa China, hakuna watu walioweza kufikiria ungekuwa na sura uliyo nayo sasa, na kubadilika kuwa mji wa wenye pato la serikali zaidi ya dola za kimarekani elfu 24 kwa kila mtu kwa mwaka. Mabadiliko hayo yalianzia uanzishwaji wa eneo maalumu la kwanza la kiuchumi huko Shenzhen. Mbali na kuwa mfano wa kuigwa na miji mingi nchini China, mtindo wa maendeleo ya Shenzhen pia umezivutia nchi nyingi ikiwemo Tanzania.

    Bagamoyo ni mji muhimu wa bandari nchini Tanzania, na hali yake ya kijiografia inafanana na Shenzhen. Mwaka 2013, rais Xi Jinping wa China alipofanya ziara nchini Tanzania, alikubaliana na mwenzake wa Tanzania rais Jakaya Kikwete kuendeleza kwa pamoja eneo maalumu la kiuchumi la Bagamoyo pamoja na bandari yake. Hivi sasa, eneo la ardhi na mpango wa jumla vimepatikana. Ijumaa iliyopita, mkurugenzi wa idara ya uhamasishaji na urahisishaji wa uwekezaji katika Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje ya Tanzania EPZA Bibi Zawadia Nanyaro na wajumbe wengine sita kutoka serikali na kampuni ya Tanzania walikwenda mjini Changzhou, mashariki mwa China kuhudhuria mkutano wa kuhimiza uwekezaji nchini Tanzania ambao uliwakutanisha maofisa wa serikali ya Changzhou na wajumbe kutoka makampuni zaidi ya 40 ya mji huo.

    Katika hotuba yake, bibi Zawadia alisema anatarajia wachina wengi zaidi watashiriki katika uendelezaji wa eneo maalumu la kiuchumi la Bagamoyo.

    "Nazungumzia moja kwa moja mradi muhimu unaotekelezwa na EPZA wa eneo maalum la kiuchumi la Bagamoyo. Ukubwa wake ni hekta elfu tisa, na litajengwa kuwa mji wa viwanda na biashara. Eneo hilo liko kilomita 50 tu kaskazini mwa Dar es Salaamu, mji muhimu wa biashara nchini Tanzania. Pia eneo hilo liko katika ukanda wa pwani, na tunatarajia kujenga bandari moja mpya itakayokuwa kitovu cha uchukuzi wa bidhaa cha nchi yetu na nchi nyingine nane zinazopakana na Tanzania. Naweza kusema wazi kwamba eneo maalumu la kiuchumi la Bagamoyo litaiga kwa asilimia mia moja mtindo wa maendeleo wa Shenzhen na miji mingine ya China, na makampuni ya China ni wenzi wetu muhimu wa ushirikiano wa kimkakati."

    Kuanzia mwaka 2009, Tanzania ilianza ujenzi wa maeneo maalumu ya uzalishaji kwa mauzo ya nje EPZs ili kufikia malengo ya kuvutia mitaji ya kigeni, kupanua mauzo ya nje, kuongeza nafasi za ajira, na kuinua kiwango cha teknolojia ya uzalishaji na uendeshaji wa uchumi nchini Tanzania. Hivi sasa, makampuni 117 yamejiunga na utaratibu wa EPZs nchini Tanzania, kati yao kuna makampuni 12 kutoka China. Bibi Zawadia Tanzania inapenda kuona wawekezaji zaidi kutoka China wakifungua viwanda katika maeneo hayo.

    "Serikali za Tanzania na China zote zinatarajia wachina zaidi kuanzisha viwanda vyao nchini Tanzania, haswa katika mradi mkubwa tunaofanya kwa bidii, yaani eneo maalumu la kiuchumi la Bagamoyo. Eneo hilo na bandari mpya itakayojengwa ndani yake vitajengwa kwa ubia na nchi zetu mbili. Kinachofurahisha ni kwamba makampuni mengi ya China yana hamu ya kuanzisha viwanda vyao katika eneo hilo. Kwa hiyo makampuni 12 ya China tuliyo nayo sasa ni mwanzo tu, na baada ya kukamilika kwa mradi wa eneo maalumu la Bagamoyo, tutahitaji ushiriki wa makampuni mengi zaidi kutoka China."

    Kwa mujibu wa Bibi Zawadia, nguo zinazotengenezwa kwenye viwanda vya China vilivyopo ndani ya utaratibu wa EPZs zimeingia soko la Marekani, na makampuni mengine ya China pia yamejenga viwanda vya kutengeneza pamba na ngozi, shughuli ambazo zinaongeza kwa kiasi kikubwa thamani ya bidhaa hizo ghafi.

    Akiulizwa kwa nini makampuni ya China yanachagua kuanzisha viwanda vyao katika EPZs nchini Tanzania, Bibi Zawadia alijibu kwa imani na kusema kuwa serikali ya Tanzania na mamlaka yake zimetoa sera nyingi zenye unafuu, ambazo zinavutia sana.

    "Kwanza watapata unafuu wa kodi, na sheria ya EPZs na sheria ya SPZ itatoa vivutio mbalimbali. Kwa mfano wanapojenga viwanda, watapata msamaha wa ushuru wa kuingiza vitu kutoka nje na kodi ya nyongeza VAT. Wanapoanza kuzalisha watasamehewa kodi ya mapato katika miaka kumi ya kwanza. Pili, tutakuwa na miundo mbinu mizuri ili kuhakikisha uzalishaji wao na kupunguza gharama zao; tatu, Tanzania ina bandari nyingi, ambazo zinaweza kusaidia kupanua soko lao katika nchi nyingine za Afrika mashariki. Nne, ikilinganishwa na hali ya China, mshahara wa wafanyakazi wa Tanzania sio mkubwa, hili ni jambo linalovutia zaidi makampuni ya China. Aidha, Tanzania na China zimekuwa na ushirikiano mzuri na wa muda mrefu, nataka kutumia vizuri jambo hilo kuwavutia wawekezaji kutoka China."

    Hivi sasa, kati ya kampuni 12 za China zilizopo katika EPZs, nne zinatoka Changzhou. Kampuni ya nguo ya Dong'ao ya Changzhou ni mojawapo. Meneja wa idara ya udhibiti wa ndani wa kampuni hiyo He Yuwen anasema utaratibu wa EPZs unaweza kusaidia kampuni za nchi za nje kuingia kwa urahisi na haraka kwenye soko la Tanzania.

    "Kwanza, kampuni zinazotumia mitaji kutoka nchi za nje zilizopo katika EPZs hakika zinaendesha biashara yao kwa ufanisi zaidi kuliko zile zilizopo nje, kwani EPZA inaweza kutoa huduma zote, hatuna haja ya kuwasiliana na idara mbalimbali za nchi hiyo. Pili, EPZA pia imetoa huduma kama mlezi wa mtoto, kwa mfano tunapopata matatizo katika kusafirisha nje bidhaa, wanaweza kutusaidia kutatua. EPZA ni kama daraja kati yetu na idara za serikali ya Tanzania, na inaweza kuongeza ufanisi."

    Hata hivyo, He Yuwen pia amekiri kuwa kampuni za China zinakabiliwa na matatizo kadhaa katika kuwekeza nchini Tanzania. Kwanza ni kuwa China na Tanzania ziko mbali, na inachukua muda mrefu kwa mizigo kufika Tanzania kutoka China, ambao huwa ni mwezi mmoja, hali hii itaongeza muda wa uzalishaji wa kiwanda. Pili ni kuwa hali duni ya miundombinu bado ni sababu kuu inayokwamisha maendeleo ya Tanzania, na gharama ya kuegesha meli bandarini ni kubwa mno ikilinganishwa na nchi nyingi zilizopo kusini mashariki mwa Asia."

    Kuhusu wasiwasi hiyo, Zawadia amesema mazingira ya uwekezaji ni jambo linaloamua kama nchi inaweza kufanikiwa kuwavutia wawekezaji kutoka nje au la, na miundombinu ni sehemu muhimu ya mazingira ya uwekezaji. Kwa muda mrefu sasa, maeneo ya EPZs ni madogo, na miundombinu pia ilikuwa mibovu, lakini hali hiyo itabadilika kufuatia maendeleo ya eneo maalumu la kiuchumi la Bagamoyo. Bibi Zawadia ameeleza kuwa EPZA ilipata mkopo kutoka Benki ya Uwekezaji ya Tanzania TIB, ambao ulitumiwa kununua ardhi, kuandaa mpango wa jumla, na pia utatumiwa kujenga miundombinu. Zaidi ya hayo, ujenzi wa miundombinu pia umepata uwekezaji kutoka kampuni za Shenzhen na Hong Kong China pamoja na kampuni kutoka Oman.

    "Ujenzi wa miundimbinu hiyo ni kwa ajili ya kulipatia eneo hilo umeme wa uhakika na barabara. Na ili kuongeza mawasiliano, tutajenga reli na barabara zinazounganisha eneo hilo la Bagamoyo na Dar es Salaam, cha muhimu ni kuwa kutakuwa na bandari kubwa ya kisasa."

    Mwanzoni mwa mwaka huu, mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma na naibu waziri wa mambo ya nje wa China Zhang Ming walisaini kumbukumbu ya ushirikiano itakayodumu miaka 48 na kujumuisha karibu maeneo yote ya Afrika. Ushirikiano huo utajikita kwenye miundo mbinu ya reli ya mwendo kasi, barabara kuu na usafiri wa ndege. Wachambuzi wanaona kuwa mpango huo unamaanisha kuwa pendekezo lililotolewa na China la ujenzi wa "Ukanda wa Kiuchumi wa Njia ya Hariri na Njia ya Hariri Baharini ya Karne 21", yaani kwa ufupi "Ukanda Mmoja Njia Moja" litalifikia pia bara la Afrika.

    Akizungumzia "Ukanda Mmoja Njia Moja", Bw. He Yuwen alisema Tanzania ni moja ya nchi zinazohusishwa kwenye pendekezo hilo linalolenga kuimarisha ushirikiano na kupata maendeleo kwa pamoja, kwani Njia Kongwe ya Hariri iliyowahi kuunganisha China na sehemu nyingine duniani katika siku za kale ilifikia Afrika mashariki. Ana imani kuwa kutokana na jukwaa la EPZs na mkakati wa "Ukanda Mmoja Njia Moja", kampuni yake itapata fursa zaidi za kujiendeleza nchini Tanzania.

    "Nina imani kuwa serikali ya China itaongeza uwekezaji katika miradi ya ujenzi wa miundo mbinu katika nchi zilizopo kwenye 'Ukanda Mmoja Njia Moja", hii itasaidia kuboresha mazingira ya uwekezaji ya Tanzania na kupunguza gharama zetu za uendeshaji."

    Kabla ya kuamua kuanzisha eneo maalumu la kiuchumi la Bagamoyo, Bibi Zawadia aliwahi kutembelea Shanzhen mara nyingi kujifunza uzoefu ulio nao mji huo. Hivi sasa, ardhi ipo, mpango wa jumla ipo, lakini je, Bagamoyo itaweza kupata mafanikio kama Shenzhen?

    "Mafanikio ya Shenzhen yamevutia sana, ndiyo ninataka Bagamoyo nayo iwe kama Shenzhen. Nina imani kuwa Bagamoyo inaweza kuwa hivyo, na pia tutafanikiwa."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako