• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tamasha la tiara la kimataifa lafanyika Beijing

    (GMT+08:00) 2015-04-16 13:53:09

    Baada ya majira ya baridi kumalizika, China kwa sasa imeingia katika majira ya mchipuko, ambayo ni mazuri kwa watu kutoka nje na kuwa katika mazingira ya kijani huku wakijiburudisha na tiara. Katika kipindi cha leo, tutazungumzia Tiara na historia yake.

    Tiara ni kitu cha jadi cha kuchezea kinachotengenezwa kwa kutumia vipande vyembamba vya mwanzi na karatasi au vitambaa, halafu kufungwa na nyuzi, na kinaweza kuruka kwa kufuata nguvu ya upepo. Tiara ina mashabiki wengi hapa China, na huenda kila mchina aliwahi kuchezea tiara akiwa utotoni, na hata kwenye baadhi ya shule za msingi kuna masomo yanayofundisha namna ya kutengeneza tiara.

    Mpaka leo, tiara iliyovumbuliwa hapa China imekuwa na historia ya zaidi ya miaka 2000. Nyaraka za kihistoria zinasema, tiara ya kwanza ilivumbuliwa na mwanafikra mashuhuri wa China anayeitwa Mo Di, historia inasema Bw. Mo Di alifanya utafiti kwa miaka mitatu kabla ya kufanikiwa kutengeneza tiara kwa kutumia mbao, lakini bahati mbaya tiara hiyo iliharibika baada ya kuruka kwa siku moja tu. Inaaminika kuwa hii ilikuwa ni tiara ya kwanza duniani.

    Mwanafunzi wa Bw. Mo Di anayeitwa Lu Ban alirithi ndoto ya mwalimu wake ya kuboresha utengenezaji wa tiara, katika usanifu wa mwanzo, Bw. Lu Ban alibadilisha vifaa na kujaribu kutumia vipande vyembamba vya mwanzi badala ya mbao, na kuvichoma kidogo ili kuweza kuvipinda, halafu akatengeneza tiara yenye umbo la ndege. Historia inasema, tiara hiyo iliyoitwa 'ndege ya mbao' ilifanikiwa kuruka kwa siku tatu angani.

    Mwanzoni tiara ikiwa ni uvumbuzi muhimu, ilitumika zaidi katika mambo ya kijeshi, kama vile kupashana habari, kufanya upelelezi, kupima umbali na kuvuka sehemu ambazo farasi na meli haziwezi kupita. Miaka 1400 iliyopita, kutokana na maendeleo ya teknolojia ya kutengeneza karatasi, tiara ilianza kutengenezwa kwa karatasi, na karne ya 11 tiara ilianza kuwa kitu cha burudani kilichopendwa na watu wengi. Kumbukumbu ya historia ya wakati huo huo ilionesha watu wakitoka nje kurusha tiara wakati wa majira ya mchipuko, pia kuna michoro mingi maarufu ya enzi hiyo iliyoonesha watu wakichezea tiara.

    Kuanzia karne ya 10, tiara ilienezwa hadi eneo la peninsula ya Korea na baadaye Japan, na iliingia barani Ulaya katika karne ya 13 hadi karne ya 14. Hivi sasa nchini China tiara bado inatoa mchango muhimu katika kuhimiza mawasiliano ya kiutamaduni na nje, kuimarisha urafiki na watu wa nchi mbalimbali na kukuza sekta za uchumi na utalii. Tiara za kichina zinahifadhiwa katika majumba ya makumbusho ya nchi mbalimbali, kama vile kwenye jumba la makumbusho la taifa la Marekani, kuna tangazo lililoandikwa wazi kuwa 'Vyombo vya asili vinavyoweza kuruka angani duniani ni tiara na roketi za China", na pia jumba la makumbusho la Uingereza linaitaja tiara kuwa "Uvumbuzi wa tano wa China" uliochangia ustaarabu wa binadamu, ikiwa ni pamoja na uvumbuzi wa utengenezaji wa karatasi, dira, baruti na teknolojia ya uchapishaji.

    Kwa wachina, ukitaja Tiara, mji wa kwanza unaokuja akilini huenda ukawa ni Weifang mkoani Shandong, mashariki mwa China, kwa kuwa mji huo ni maarufu sana kwa tiara yake na kusifiwa kuwa ni Mji wa Tiara duniani. Mji wa Weifang ulikuwa ndio asili ya utengenezaji wa tiara, na kuanzia miaka 650 iliyopita, walijitokeza wasanii wengi wa kutengeneza tiara. Baadaye mila ya kurusha tiara ilienea sana na usanii wa tiara pia ulifikia kilele. Hadi mwishoni mwa karne ya 19, mji huo ulikuwa na masoko mengi ya tiara, na wafanya biashara kutoka sehemu mbalimbali za China walikwenda Weifang kununua tiara, ili kuvutia wateja, wasanii wa tiara walionesha ustadi wao mkubwa wa kutengeneza tiara zenye maumbo mbalimbali na ukubwa mbalimbali, na kati ya hizo, aina ya tiara ndefu yenye umbo la nyoka inajulikana zaidi. Hivi sasa kuna aina nyingi zaidi za tiara, ile iliyo ndogo zaidi ukubwa wake ni kama mkono tu, na tiara kubwa zaidi inaweza kuwa mita mia kadhaa, tiara hizi za kisasa zina maumbo mbalimbali na kutiwa mapambo na rangi mbalimbali, kama vile zile zenye umbo la ndege za kivita, zenye mapambo ya rangi mbalimbali, zinazotoa milio ya upepo, na hata kuna tiara zinazotiwa mapambo ya taa na kuweza kuwaka usiku.

    Kuanzia mwaka 1984, tamasha kubwa la tiara hufanyika kila mwaka mjini Weifang kuanzia tarehe 20 hadi 25 Aprili, na kuvutia wataalamu na mashabiki wengi wa tiara kutoka sehemu mbalimbali duniani.

    Mbali na tamasha la Weifang, pia kuna matamasha mengine ya tiara yanayofanyika kila mwaka katika miji tofauti nchini China. Tarehe 4 mwezi huu, lilifanyika tamasha la tiara la Wulong la mji wa Chongqing, kusini magharibi mwa China, kwenye tamasha hilo, tiara moja yenye urefu wa mita 6000 iliyovunja rekodi ya Guinnes ya mita 5000 na kuwa tiara ndefu kabisa duniani, ilirushwa kwa mafanikio, na kutokana na urefu wake wa ajabu, ilichukua muda wa saa 6 hadi 8 kumaliza kurusha sehemu zake zote angani.

    Jumamosi iliyopita, tamasha la tiara la kimataifa ilifanyika kwenye bustani ya Garden Expo, hapa Beijing. Mashabiki zaidi ya 120 kutoka nchini na nchi 22 za nje zikiwemo India, Japan, Marekani, Uingereza na Pakistan walishiriki kwenye tamasha hilo, kuonesha ustadi wao wa kutengeneza na kurusha tiara za aina mbalimbali.

    Mkaazi wa mjini Beijing kwa jina bwana Cheng anajitayarisha kurusha tiara alioitengeneza yenye umbo la baiskeli wakati wa tamasha za urushaji wa tiara. Kwenye tamasha za mwaka huu kulikuwa na zaidi ya warushaji na watengenezaji tiara 120.

    Ron kutoka Marekani na mke wake kutoka Thailand waonyesha tiara yao yenye picha zao. Wanasema kurusha tiara ni hafla ya kifamilia, wanafanya kazi pamoja, kucheza pamoja na kurusha tiara pamoja

    Tiara nyekundu yenye umbo la taa inaelea angani ikiwa na maandishi ya kichina yenye maana kupaa angani kwa ndoto, afya na furaha. Maudhui tamasha za tiara za mwaka huu yalikuwa ni kuweka juu matumaini na kuiunga mkono Beijing kwenye kutunukiwa uandaaji wa michezo ya olimpiki mwaka wa 2022.

    Mzee Luo Huanwen mwenye umri wa miaka 70 ni msanii hodari wa sanaa za kijadi wa China. Alipenda kutengeneza tiara tangu utotoni. Tiara kwa kawaida hutengenezwa kwa kutumia kitambaa chepesi, ngundi na vijiti.

    Tiara zilizotundikwa ukutani wakati wa tamasha za tiara za mwaka 2014 mjini Beijing. Utamaduni wa kurusha tiara kulingana na kumbukumbu za maandishi ulianza mwaka wa 200 K.K nchini China.

    Bwana Edo kutoka Italia akiwa na tiara yenye umbo kubwa na la kipekee inayofanana na parashuti. Amekuwa akirusha tiara kwa miaka 30.

    Grem Rakuct kutoka Uingereza mrushaji tiara kwa zaidi ya miaka 20 ni stadi sana wa sanaa hii. Hata hivyo anasema anahitaji eneo lililo wazi zaidi na nafasi kubwa ili aweze kurusha tiara tatu kwa wakati mmoja akiambatanisha na muziki.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako