• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wakulima wanufaika na biashara ya maua ya rapa

    (GMT+08:00) 2015-04-22 16:11:55

     


    Ni mchana wa siku moja katikati ya mwezi Aprili, pilika pilika zinaanza katika mikahawa mbalimbali inayoendeshwa na wakulima wa kijiji cha Dongwang mashariki mwa China. Kuna mikahawa zaidi ya mia moja kwenye kijiji hicho chenye wakazi 4000 hivi, ambao wote ni wakulima. Mkulima Zhang Dehua anayeendesha mkahawa uitwao Chunlan, alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, sasa ni kipindi cha tamasha la maua ya rapa katika mji wa Xinghua ulioko karibu, watalii wengi wanakwenda vijijini kuangalia maua ya rapa, na mkahawa wake hawa unazidiwa kwa kuwapokea watalii wengi, hivyo analazimika kuwaongoza baadhi ya watalii kwenda kwenye mikahawa mingine inayoendeshwa na wakulima wenzake. Anasema kwa furaha kuwa amepata faida kubwa kutokana na idadi kubwa ya watalii wanaovutiwa na maua ya rapa.

    Jina kamili la tamasha la maua ya rapa iliyotajwa na Bw. Zhang Dehua ni "sikukuu ya maua ya rapa ya visiwa vya Xinghua", hii ni hatua ya mji wa Xinghua katika kuendeleza kilimo na utalii kwa kutumia mazingira ya asili. Tamsaha hilo limekuwa likifanyika kila mwaka kuanzia mwaka 2009, , na mwaka huu ni mwaka wa saba. Kila mwezi Aprili ambapo maua ya rapa yanapochanua, watalii wengi kutoka sehemu mbalimbali wa China wanakwenda mjini Xinghua kuyaangalia.

    Mkurugenzi wa eneo hilo la utalii wa maua ya rapa Bw. Yan Zhonghe alisema, tofauti na maua ya rapa yanayopandwa kwenye mashamba ya nchi kavu ya vijiji vingine, maua ya rapa ya Xinghua yanapandwa kwenye visiwa vidogo vidogo vya eneo la maziwa. Anasema,

    "Miaka 800 hadi 1000 iliyopita, sehemu hii ilikuwa kinamasi, kutokana na mahitaji ya kimaisha mababu zetu walichimba udongo kutoka kwenye maji na kuukusanya, baadaye udongo huo uliokusanywa ulikuwa kama visiwa vidogo vidogo, na mababu zetu walikuwa wanapanda chakula kwenye mashamba ya visiwa hivyo."

    Kila ifikapo mwezi Aprili, maua ya rapa yenye rangi ya dhahabu yanachanua sana kwenye visiwa vidogo vidogo, hali hiyo inajulikana kama "bahari ya dhahabu ya maua ya rapa". Hivi sasa tamasha la maua ya rapa limekuwa ni alama ya mji wa Xinghua, mji mdogo uliopo kaskazini mwa mkoa wa Jiangsu, ambao unawavutia watalii kutoka sehemu mbalimbali za China.

    "Sisi tunatoka mkoani Shanxi, maua ya rapa ya hapa yana umaalum mkubwa, tunaburudishwa na mandhari nzuri ya maua tukiwa tunakaa kwenye mashua.Ni sawa na tunasafiri miongoni mwa maua ya rapa."

    Bw. Yan Zhonghe amesema, kabla ya kuanzishwa kwa tamasha la maua ya rapa, wakulima walikuwa wanapanda maua ya rapa wao wenyewe, na eneo la maua ya rapa halikuwa kubwa kama la hivi sasa. Wakati wa majira ya mchipuko ya mwaka 2006, baadhi ya wapiga picha walikwenda Xinghua kupiga picha za maua ya rapa, na waliweka picha hizo kwenye mtandao wa Internet. Picha hizo ziliwavutia watu wengi, wakisifu maua ya rapa ya Xinghua kuwa ni maua mazuri zaidi ya rapa nchini China. Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii, na kuendelea kujulikana kwa maua ya rapa ya visiwa vingi, serikali ya mji wa Xinghua ilitambua kuwa hii ni fursa nzuri. Hivyo ilianzisha kampuni ya utalii, na kupanga upya eneo la utalii la maua ya rapa. Serikali ya huko inataka kuweka vizuri uwiano kati ya juhudi za kuendeleza uchumi na uhifadhi wa mazingira ya asili, ili kuendeleza shughuli za kilimo na utalii kwa wakati mmoja. Zaidi ya kuwa moja ya mazao ya kilimo, serikali ya huko inajitahidi kuyafanya maua ya rapa kuwa injini mpya ya kuleta ongezeko la uchumi.

    "Eneo letu la utalii la maua ya rapa lina hekta 667, kampuni ya utalii imekodisha hekta 87 za mashamba zilizoko kiini cha eneo hilo kutoka kwa wakulima, na inashughulikia upandaji wa maua ya rapa kwenye sehemu hiyo, na wakulima wanashughulikia mashamba mengine. Lakini serikali inatoa ruzuku kwa wakulima wanaopanda maua ya rapa, ambao wanaweza kupata ruzuku ya yuan 200 kwa kila hekta 0.07 ya shamba. "

    Pesa hizo ni sawa na dola za kimarekani 34. Kutokana na umbali mfupi kati ya kijiji cha Dongwang na eneo la utalii la maua ya rapa ya visiwa vingi, wakulima wa kijiji cha Dongwang wameanza kushughulikia biashara za huduma za utalii katika miaka kadhaa iliyopita. Zhang Dehua mwenye umri wa miaka 61 anasifiwa na wakulima wengine kuwa mtu mwenye akili. Hapo awali serikali ya huko iliwatuma wafanyakazi kwenye kijiji cha Dongwang na kuwahimiza kuendesha mikahawa ya vijijini. Wakati ule wakulima wengi walikuwa hawaamini kama maua ya rapa yanaweza kuwaletea faida nyingine. Lakini kutokana na hali ya miundo mbinu iliyopo karibu na kijiji inavyoboreshwa na idadi ya watalii inavyozidi kuongezeka siku hadi siku, Bw Zhang Dehua ameona imani ya serikali katika kuendeleza eneo la utalii na fursa ya biashara, hivyo mwaka 2011 alianza kuendesha mkahawa wa kwanza kijijini.

    "Wakati ule serikali ilitushawishi kuendesha mikahawa ya vijijini, na wanakijiji wengine walikuwa hawapendi kufanya hivyo. Baadaye walipoona napata faida kubwa, walianza kuanzisha mkahawa mmoja baada ya mwingine. Eneo la utalii la maua ya rapa limeleta faida kubwa kwa kijiji chetu. Serikali imewekeza fedha nyingi, imejenga barabara na vifaa mbalimbali, na kuweka eneo la utalii. Hivi sasa sisi wanakijiji tunaendesha mikahwa na hoteli, na kuuza mboga na matunda, na sote tunanufaika na eneo la utalii. "

    Baada ya maendeleo ya miaka kadhaa, ukubwa wa mkahawa wa Chunlan unaoendeshwa na Zhang Dehua unaongezeka hatua kwa hatua, hivi sasa mkahawa huu unaweza kuandaa chakula cha watu 300, na kutoa malazi kwa watu 50. Ili kuwavutia watalii wengi kula chakula halisi cha kijijini, Zhang Dehua pia amepanda mboga karibu na nyumba zake, na amefuga kuku zaidi ya elfu moja.

    Uchumi wa maua ya rapa pia unachochea hamasa ya wakulima kupata nafasi za ajira na kufanya biashara kwenye maskani zao. Hapo awali wanakijiji walipendelea kwenda mijini kutafuta ajira, lakini hivi sasa wameona fursa kubwa zinaletwa na maua ya rapa nyumbani kwao, hivyo vijana wengi wameanza kuendesha mikahawa, na baadhi ya wazee wameajiriwa kwenye mikahawa ya kijijini kama mkahawa wa Chunlan, na wengine wamepata ajira kwenye eneo la utalii la maua ya rapa, ambao wanafanya kazi ya kuendesha mashua, usafi na ulinzi.

    Bibi Jiang wenye umri wa miaka 60 hivi sasa ameajiriwa katika eneo la utalii, akiwa mwendesha mashua. Amesema eneo la utalii linamlipia kutokana na idadi ya watalii wanaopanda kwenye mashua yake, na anaweza kupata yuan moja kwa kila mtalii. Kwa kawaida kila mwendesha mashua anaweza kupata yuan 100 hadi 150 kwa siku. Katika kipindi cha mwezi moja cha tamasha la maua ya rapa, mwendesha mashua anaweza kupata yuan 3000 hadi 4000, sawa na dola za kimarekani 500 hadi 667.

    "Kila siku ninaweza kuwasafirisha watalii 80 hivi, lakini mashua ylangu ni ndogo sana, kila mara nawasafirisha watalii watano hadi sita, wenzangu wana mashua kubwa zinazoweza kuwasafirisha watu 10."

    Bw. Yan Zhonghe amesema baadhi ya wanakijiji wanaofanya kazi katika miji hurudi nyumbani wakati wa tamasha la maua ya rapa, na wanafanya biashara au kuwasaidia jamaa zao katika kipindi hicho. Baada ya kumalizika kwa tamasha hilo wanarudi mijini kuendelea na kazi zao. Bw. Yan amesema mapato ya wanavijiji yameongezeka sana kutokana na tamasha la maua ya rapa.

    "Kabla ya kuanza kwa tamasha la maua ya rapa, mapato ya wastani ya kila mkulima wa hapa kwa mwaka ni yuan elfu 5, lakini hivi sasa mapato hayo yamefikia yuan elfu 15. Sasa maisha ya wakulima wa hapa ni mazuri. Kila familia ina nyumba kubwa. Na karibu wakulima wote wanaoishi karibu na eneo la utalii la maua ya rapa wanaendesha mikahawa na hoteli za kuwapokea watalii. Hata baadhi ya familia inaweza kupata faida za yuan laki 1 katika kipindi cha mwezi mmoja cha tamasha la maua ya rapa."

    Ingawa uchumi wa maua ya rapa unaotekelezwa na serikali ya mji wa Xinghua umeleta faida kubwa kwa wakulima wa huko, lakini maua ya rapa yanachanua kwa muda wa mwezi mmoja tu, je, wakati mwingine eneo la utalii linaweza kuwavutia vipi watalii? Zhang Dehua hana wasiwasi hata kidogo kuhusu suala hilo,. Amemwambia mwandishi wetu wa habari kuwa mwaka huu ataendelea kupanua ukubwa wa mkahawa wake, ataongeza vyumba kumi ili kuwapokea watalii wengi zaidi. Amesema mpango wa serikali ya huko umemletea imani. Ameelekea upande wa bango la matangazo lililowekwa na serikali kando ya barabara, ambapo mpango wa kuendeleza eneo la utalii unaonesha kuwa, eneo la utalii litawavutia watalii kwa mandhari tofauti ya aina mbalimbali za maua yanayochanua katika majira tofauti, yaani maua ya rapa wakati wa mchipuko, mayunguyingi siku za joto, chrysanthemum majira ya mpukutiko, na matete siku za baridi.

    Bw. Yan zhonghe amesema serikali ya huko na eneo la utalii wanatafuta njia endelevu ya utalii wa kiviumbe. Kutokana na mpango uliowekwa, tamasha la maua ya rapa bado ni mwanzo tu, baadaye wataendelea kuongeza uwekezaji, na kujenga mandhari tofauti kutokana na mabadiliko ya majira. Lengo lao ni kuhimiza matumizi na uchumi wa huko, pia kutoharibu mazingira ya asili, na muhimu zaidi ni kuwanufaisha wakulima wa huko.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako