• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Muuguzi Wang Jinhua aliyetoa huduma nchini Cambodia

    (GMT+08:00) 2015-04-23 15:43:04

    Kwa muda mrefu, hali duni ya huduma ya afya nchini Cambodia iliwafanya watu wa nchi hiyo wamiminikie nchi jirani kutafutia huduma hiyo. Tangu mwaka 2007, kutokana na ombi la Cambodia, wizara ya ulinzi ya China ilianza kupeleka wahudumu wa afya wa kijeshi kushiriki kwenye shughuli za Hospitali ya Preah Ket Mealea ambayo ni hospitali kuu ya jeshi la Cambodia. Madaktari hao wachina wamekuwa wakiwatibu wagonjwa na kutoa mafunzo kwa madaktari wazawa. Muuguzi Wang Jinhua ni mmoja kati yao. Alipelekwa nchini Cambodia mwaka 2012 na kwa mwaka mmoja uliofuata, yeye pamoja na madaktari wengine wa China walifanya kila wawezalo kusaidia wenzao wa Cambodia katika kutibu na kuendesha hospitali kiasi kwamba ujuzi wao bado unatumika mpaka leo baada ya wao kuondoka nchini humo.


    Kwa watu wengi, mwezi Februari mwaka 2012 ulikuwa ni mwezi wa kawaida kama ilivyo miezi mingine maishani mwao, lakini haukuwa wa kawaida kwa Bibi Wang Jinhua. Muuguzi huyo akiwa na umri wa miaka 56 alipata habari kwamba hospitali aliyofanya kazi ilipokea jukumu la kutuma kikundi cha madaktari nchini Cambodia. Muuguzi Wang akatoa ombi la kushiriki kwenye kikundi hicho.

    "Niliambiwa muda wa kutekeleza jukumu hilo ni mwingi, utakuwa mwaka mmoja. Nikasema hamna shida. Tangu nianze kufanya kazi, sijawahi kusema hapana hata mara moja, bila kujali nimepewa kazi ya namna gani."

    Muuguzi Wang alianza kazi miaka 40 iliyopita katika hospitali ya Changzheng ya Chuo Kikuu cha Pili cha Udaktari cha Kijeshi iliyopo mjini Shanghai China. Katika miaka iliyopita, akiwa mhudumu wa afya wa kijeshi, alipewa kazi mbalimbali ikiwemo uokoaji baada ya tetemeko la ardhi kutokea na kwenye uwanja wa vita. Lakini jukumu alilopewa safari hii, ni tofauti.

    "Mama yangu alikuwa amelazwa kwa zaidi ya mwaka mmoja kwenye hospitali ninayofanya kazi kutokana na tatizo la ubongo lililosababishwa na shida ya mzunguko wa damu kwenye mishipa ya ubongo, na baba yangu mwenye umri wa miaka zaidi ya 90, na hali yake ya afya haikuwa nzuri. Nilikuwa na wasiwasi nao. Kama kitu chochote kingewatokea, nisingeweza kuwawahi."

    Mwezi Machi mwaka 2012 muuguzi Wang akiongozana na kikundi cha madaktari cha China waliwasili mjini Phnom Penh, mji mkuu wa Cambodia, na kuanza kufanya kazi katika hospitali ya kijeshi ya Preah Ket Mealea, ambayo inatoa huduma kwa wanajeshi na raia wa kawaida. Kutokana na msaada wa China, kiwango cha huduma zilizotolewa na hospitali hiyo kimeinuka kiasi, lakini bado kulikuwa na changamoto nyingi zitakazowakabili madaktari hao watakaofanya kazi kwenye hospitali hiyo katika mwaka mmoja uliofuata. Kwa mfano, hospitali hiyo haikuwa na utaratibu wala kanuni za kazi katika utawala wake, matibabu au uuguzi. Kilichowashangaza zaidi madaktari hao wachina ni kwamba, usafi kwenye hospitali hiyo haukuweza kuhakikishwa. Daktari Deng Houbin alikuwa mmoja wa madaktari kutoka China. Akikumbuka anasema:

    "Wafanyakazi wa hospitali hiyo hawakufahamu mazingira yanayotakikana wakati wa upasuaji, na hawakujua kabisa kuhusu kunyunyiza dawa za kuua vijidudu. Muuguzi mkuu Wang Jinhua mwenye uzoefu mkubwa wa kazi alituongoza kufanya usafi katika hospitali nzima, kunyunyiza dawa kwenye chumba cha upasuaji, na kurekebisha vifaa mbalimbali kwenye chumba hicho, kama vile meza ya upasuaji na taa ya upasuaji. Kazi hizi zilihakikisha mafanikio ya upasuaji wetu wa kwanza."

    Madaktari wazawa wa hospitali hiyo pia walishirikishwa sio tu katika maandalizi kabla ya upasuaji, bali pia upasuaji wenyewe. Bibi Wang aliweka utaratibu wa "Saini Tatu" ambao unataka saini za wahusika wakuu watatu wa upasuaji, wakiwemo daktari anayefanya upasuaji, daktari wa China anayesimamia upasuaji, na mkuu wa kikundi cha madaktari cha China. Utaratibu huo uliobainisha majukumu na wajibu wa moja kwa moja wa kila mhusika wa upasuaji. Mbali na utaratibu wa upasuaji, muuguzi mkuu Wang Jinhua alisaidia karibu kila idara ya hospitali hiyo kuanzisha au kukamilisha utaratibu wa kazi waliokuwa nao. Hata mpaka leo, miaka miwili baada ya Bibi Wang kuondoka nchini Cambodia, taratibu hizi bado zinafuatwa na kufanya kazi kwenye hospitali hiyo.

    Daktari Tony ni daktari mzawa wa hospitali hiyo. Akikumbusha mafunzo aliyopewa pamoja na operesheni alizofanya chini ya usimamizi na msaada wa madaktari wa China anasema:

    "Bibi Wang alipokuwa hospitalini kwetu, alituonesha jinsi usafi unavyotakiwa kufanywa katika chumba cha upasuaji kwa kunyunyiza dawa, alisaidia kukamilisha taratibu na kanuni za kazi, na kufanya kazi nyingi katika idara yetu ya upasuaji ya Neva (neurosurgery). Alitusaidia kwa moyo, na kuwa mfano wa kuigwa"

    Katika muda wa mwaka zaidi ya mmoja kilipokuwa katika hospitali hiyo ya Cambodia, kikundi kilichoongozwa na muuguzi mkuu Wang Jinhua, kiliwatibu wagonjwa karibu elfu 10, kufanya operesheni karibu 200, zikiwemo operesheni ngumu kama vile majeraha ya ubongo, kuondoa uvimbe, na kuunganisha mifupa iliyovunjika.

    Nje ya kazi, Bibi Wang Jinhua alionekana zaidi kama Balozi Asiye wa Kiserikali. Aliongoza kikundi cha madaktari wa China kutoa msaada wa dawa na vifaa vya tiba kwa idara mbalimbali nchini Cambodia, kuwapatia matibabu bure watoto yatima, kuwatembelea watoto ambao wazazi wao walifariki kutokana na UKIMWI, na kutunga, kuchapisha na kusambaza vipeperushi vya ujuzi wa kujikinga na magonjwa yanayotokea mara kwa mara nchini Cambodia.

    Kutokana na michango hiyo inayosifika, wizara ya ulinzi ya Cambodia ilitoa nishani ya amani na nishani ya urafiki kati ya Cambodia na China kwa Bibi Wang Jinhua. Akizungumzia urafiki huo kutokana na uzeofu wake wa kazi nchini Cambodia, muuguzi huyo anasema huo ni urafiki wa kivitendo, ambao unaonekana, unaguswa na kuhisiwa.

    "Nilikwenda nchi nyingine iliyo tofauti na China, lakini niliichukua nchi hiyo kama nyumbani kwangu, nilifanya kazi kwa moyo, kwa hiyo nikapata urafiki mkubwa ambao ninakumbuka mara kwa mara."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako