• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Dakta. Li Jin, mmoja wa madaktari wa China walio mstari wa mbele katika vita dhidi ya Ebola

    (GMT+08:00) 2015-04-23 15:43:50

    Mwezi Februari mwaka 2014, mlipuko mkubwa wa ugonjwa wa Ebola ulitokea Afrika Magharibi. Ili kukabiliana na msukosuko huo wa kiafya wa kimataifa, serikali na jeshi la China lilichukua hatua mara moja na kupeleka vikundi 10 vya madaktari na wataalamu wa afya zaidi ya 1,000 katika nchi za Afrika Magharibi, hatua ambayo ilisifiwa sana na jumuiya ya kimataifa. Daktari Li Jin alikuwa ni kiongozi wa kikundi cha kwanza cha matibabu kupelekwa na China nchini Sierra Leone katika mapambano hayo dhidi ya Ebola.


    Nchi ya Sierra Leone yenye watu zaidi ya milioni 6 ina madaktari wasiozidi 200 na magari 6 tu ya kubeba wagonjwa. Kila mwaka nchi hiyo inakumbwa na maambukizi ya malaria na kipindupindu, hali ambayo ilimshangaza Dkt. Li Jin ambaye ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufika nchini humo.

    "Tulianza kazi mjini Freetown, ambako hakuna taa za kuongoza magari, wala miundombinu ya maji taka, mazingira ya kimatibabu yalikuwa mabaya. Hospitali ya urafiki kati ya China na Sierra Leone tuliyofanya kazi ilijengwa kwa msaada wa China. Mwezi Julai au Agosti mwaka jana, mgonjwa mmoja wa Ebola alifariki katika hospitali hiyo, wahudumu wote wa afya kwenye hospitali hiyo wakakimbia. Tulipoanza kazi huko, kitu cha kwanza tulichofanya ilikuwa ni kurekebisha vifaa na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya wa Sierra Leone, ambao mwanzoni hata hawakufahamu jinsi ya kuvaa maski na hawakujua njia sahihi ya kunawa mikono kabla ya kuanza kutibu wagonjwa. Mwanzoni tulikumbwa na matatizo mengi tusiyoyatarajia. Wahudumu wa afya wa Sierra Leone tuliofanya kazi nao hawakuwa na ujuzi au ustadi wa jinsi ya kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza."

    Ili kukabiliana na mlipuko wa Ebola ambao ni ugonjwa mbaya zaidi wa kuambukiza katika karne ya 21, tarehe 16 Septemba mwaka jana, hospitali No.302 ya Jeshi la China ilipeleka kikundi cha kwanza cha madakari 30 akiwemo Dkt. Li Jin nchini Sierra Leone. Kabla ya hapo, Shirika la Afya Duniani WHO lilikuwa limetangaza mara nyingi kuwa, maambukizi ya ugonjwa wa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi haswa Sierra Leone yameshindwa kudhibitiwa. Jukumu la kikundi hicho ni kuiokoa nchi hiyo na wananchi wake kutoka kuondokana na tishio la kifo. Dkt. Li Jin anasemaļ¼š

    "Safari ile tulipokwenda Afrika Magharibi, kikundi chetu kilikuwa ni cha kwanza cha madakari kilichotumwa na jeshi la China nje ya nchi, na tulifika nchini Sierra Leone tukiwa tumevaa sare za kijeshi. Nilikwenda nchini Sierra Leone kwa mara ya kwanza kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 8 mwezi Septemba, siku tatu tu baada ya kurudi, tuliwasilisha ripoti katika wizara ya afya na uzazi wa mpango ya China. Alasiri ya siku iliyofuata, tulipokea amri kuwa kikundi chetu chenye watu 30 kinatakiwa kuondoka tena tarehe 16 Septemba, hatukukuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa. Kikundi chetu kina madaktari, wauguzi, wahandisi na wafanyakazi wa ugavi. hospitali nzima ilikuwa na pilikapilika kutusaidia kuandaa vifaa vitakavyotumika katika nusu mwaka unaofuata, kama vile vifaa vya matibabu na vya kujikinga, pia vitu vya kujikimu kimaisha. Pia tulitakiwa kupewa mafunzo kwa kuwa kabla ya hapo hatujawahi kukutana na wagonjwa wa Ebola moja kwa moja."

    Kutokana na mazingira mabaya ya kimatibabu na miundombinu hafifu nchini Sierra Leone, Dkt. Li Jin na wenzake walifanya juhudi kubwa katika kurekebisha vifaa vya hospitali na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya wa nchini humo. Baada ya wiki mbili tu, madakatari hao wa China walianza kupokea wagonjwa, Dkt. Li Jin anasema, katika muda wa siku 40 tu, idadi ya wagonjwa waliopata matibabu katika hospitali yake ilichukua nafasi ya pili miongoni mwa hospitali za nchi hiyo.

    "Sierra Leone ilikuwa kama jukwaa la kimataifa, wahudumu wa afya kutoka nchi nyingi kama vile Marekani, Uingereza, Canada na Afrika Kusini walikuwa wanatoa misaada ya kimatibabu nchini humo. Katika mapambano dhidi ya Ebola, nchi yetu si kama tu ilitoa vifaa, bali pia ilipeleka madakari na wauguzi, na kujenga hospitali, hiyo ni misaada halisi. Nchi za Ulaya na Marekani zilitoa pesa au vifaa tu, lakini hazikupeleka wahudumu wa afya, kwa hiyo hata rais Ernest Koroma wa Sierra Leone alisema, China ni mfano mzuri wa kuigwa katika suala la kutoa misaada barani Afrika. Tulianza kupokea wagonjwa tarehe 1 Oktoba, hadi tarehe 16 Novemba, kwa jumla tulitoa matibabu kwa magonjwa 274, kati yao 145 walithibitishwa kuambukizwa virusi vya Ebola, na 86 miongoni mwao walifariki. Kuanzia siku ya kwanza tuliyoanza kupokea wagonjwa hadi siku tuliyoondoka, hospitali tuliyofanya kazi ilichukua nafasi ya kwanza kwa kupokea idadi kubwa ya wagonjwa kwa siku nchini humo, na katika muda huo mzima, hakukuwa na mhudumu yoyote wa afya kutoka China au Sierra Leone aliyeambukiziwa Ebola."

    Madaktari na wauguzi ndio ni watu wanaokabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa na virusi vya Ebola. Kwa hiyo Dkt. Li aliongozana na wenzake kutoa mafunzo kamili ya kujikinga kwa wafanyakazi wenyeji wa hospitali hiyo.

    Katika kazi iliyodumu kwa miezi miwili nchini humo, si kama tu madaktari wa China hawakuambukizwa Ebola, bali pia hakuna mfanyakazi yeyote mwenyeji wa hospitali hiyo aliyeambukizwa virusi vya ugonjwa huo, mafanikio ambayo hayakupatikana kwa urahisi. Dkt. Li Jin alisema, madakari na wauguzi wanatakiwa kuvaa nguo nzito za kujikinga pamoja na maski, miwani na viatu katika mazingira yenye unyevu na halijoto juu ya digri 30. Baada ya kumaliza kazi, pia wanatakiwa kufuata kwa makini utaratibu wa kujisafisha ili kuzuia hatari ya kuambukizwa. Aidha, madakari walipaswa kuingia zaidi ya mara tatu katika vyumba vya wagonjwa ambavyo vilikuwa vinajaa matapishi ya wagonjwa, na kugusa miili ya wagonjwa waliofariki. Baadhi ya wakati, pia walipaswa kutoka nje kuwatafuta wagonjwa ambao hawakutaka kufuata maelekezo ya madaktari, kuwapimia joto na kuwapatia dawa. Kutokana na kazi hizo walizofanya kwa makini na kwa moyo wa kuwajibika, maisha ya wagonjwa wengi yaliokolewa na kusadia kudhibiti maambukizi ya virusi vya Ebola nchini humo.

    "Nikiwa ni mwanajeshi, sikusita kutekeleza jukumu langu, lakini nikiwa ni kongozi wa kikundi cha madakari, kweli nilikuwa na shinikizo kubwa. Wakati tunaondoka China, viongozi wa hospitali na jamaa zetu walitusindikiza, na wakati huo niliwaahidi kwa dhati kuwa kama daktari hata mmoja wa kikundi changu akiambukizwa Ebola barani Afrika, nitabaki huko huko na sitarudi, inanibidi niwalinde. Ili kuzuia maambukizi, tuliweka kanuni kali, kuanzia hatua za kijikinga hadi jinsi ya kutoa huduma katika vyumba vya wagonjwa, tuliweka kanuni yenye vifungu zaidi ya 200. Pia tulitoa mafunzo muhimu kwa wafanyakazi wenyeji wa Sierra Leone, na waliruhusiwa kuanza kazi tu baada ya kuwa tayari, na walitakiwa kutoa ripoti ya mambo yote wanayofanya nje ya hospitali. Nchini Sierra Leone, mbali na Ebola, pia kuna magonjwa mengine ya kuambukizwa kama vile malaria, ingawa huko kuna joto sana, hatukuruhusiwa kuvaa kaptula tulipotoka nje."

    Kutokana na kazi zao za matibabu zenye ufanisi na kuwajibika, kikundi cha kwanza cha madaktari cha jeshi la China nchini Sierra Leone kilisifiwa sana na watu wa nchi hiyo, na wenzao wa nchi za nje. Kabla ya kurudi nyumbani China, daktari Li Jin na wenzake walitoa mafunzo ya uzoefu waliopata kwa madaktari wa China walikwenda Sierra Leone kuendelea na jukumu hilo la kupambana na Ebola.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako