• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • AIIB: Kutilia mkazo bara la Asia, kuvutia nguvu ya dunia

    (GMT+08:00) 2015-04-23 18:41:37


    Mwaka 2013, Oktoba, rais Xi Jinping wa China alipokutana na aliyekuwa rais wa Indonesia Susilo Bambang Yudhoyono, alipendekeza kuanzishwa kwa Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia AIIB, ambayo itaziunga mkono kifedha nchi zinazoendelea za Asia. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa AIIB kuripotiwa kwenye vyombo vya habari. Siku chache baadaye, akihutubia kwenye mkutano wa wakuu wa viwanda na biashara wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Asia na Pasifiki APEC uliofanyika kisiwani Bali, rais Xi Jinping, kwa mara nyingine tena, alizungumzia pendekezo la kuanzisha AIIB.

    Katika siku zilizofuata, waziri mkuu wa China Li Keqiang pia alitumia ziara zake nje ya nchi kurudia tena pendekezo hilo. Hatua hizo za viongozi wa China zimetoa ishara wazi kuwa: China itachukua hatua halisi kutimiza pendekezo la kuanzisha AIIB.

    ********************************

    Je, pendekezo la kuanzisha AIIB linatokana na nini? Kwanza, hivi sasa kuna pengo kubwa kati ya mahitaji ya nchi mbalimbali za Asia kwa ujenzi wa miundombinu na uwekezaji. Benki ya Maendeleo ya Asia inakadiria kuwa, kuanzia mwaka 2010 hadi 2020, dola za kimarekani trilioni 8 zitahitajika katika ujenzi wa miundombinu ya makundi mbalimbali ya kiuchumi ya Asia ili ifikie kiwango cha wastani cha dunia. Kwa upande mwingine, China ina akiba ya fedha za kigeni karibu dola za kimarekani trilioni 4, na ujenzi wa miundo mbinu umefanya kazi muhimu katika kuhimili maendeleo ya kasi ya China katika miaka 30 iliyopita tangu nchi hii ianze kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango.

    Katika hafla ya kusaini kumbukumbu ya kuanzishwa kwa AIIB iliyofanyika baada ya mwaka mmoja, rais Xi Jinping alieleza falsafa iliyopo nyuma ya pendekezo la kuanzishwa kwa AIIB kwa sentensi mbili rahisi zenye ushawishi, "Ukitaka kutajirika, kwanza ujenge barabara" na "Watu wakishirikiana kwa kuwa na lengo moja, wanaweza kuhamisha mlima".

    Kuanzia mwezi Januari hadi Septemba mwaka 2014, mikutano kuhusu kuanzishwa kwa AIIB iliitishwa mara kwa mara, na pia mawaziri wa nchi mbalimbali zenye nia ya kujiunga na AIIB walikutana kwa chakula cha jioni kujadili suala hilo. Washiriki wa mikutano hiyo waliongezeka na kufikia 21 kutoka 10 wa mwanzo, na walifanya mazungumzo ya kina juu ya lengo, uongozi, makao makuu, na mgao wa hisa za AIIB.

    Tarehe 24, Oktoba, mwaka jana, mawaziri wa fedha na wajumbe kutoka wanachama waanzilishi 21 wa awamu ya kwanza wanaotarajia kujiunga na AIIB ikiwemo China, Singapore, Qatar na Thailand walisaini kumbukumbu ya makubaliano hapa Beijing, ikiwa ni hatua ya kwanza katika kuanzisha AIIB, kutoka wazo na kugeuka kuwa kitu kinaonekana. Mwezi mmoja baadaye, Indonesia ilikuwa mwanachama mwanzilishi wa 23 ikionyesha nia ya kujiunga na AIIB. Sura ya AIIB ilianza kuwa wazi, na kwamba itakuwa shirika la maendeleo la pande nyingi kati ya serikali barani Asia. Benki hiyo inatarajiwa kuanzishwa rasmi mwishoni mwa mwaka huu, na makao makuu yake yatakuwa hapa Beijing.

    Mwezi Novemba mwaka jana, wajumbe kutoka wanachama waanzilishi wanaotarajia kujiunga na AIIB walikutana kwa mara ya kwanza mkoani Yunnan, China kujadili utaratibu na kanuni za kupokea wanachama wapya waanzilishi. Duru ya kwanza ya kuomba kujiunga na AIIB ilifikia kilele chake mwaka mpya, ambapo Maldives, New Zealand, Tajikistan, Saudi Arabia na Jordan ziliwasilisha maombi yao.

    Mwezi Januari mwaka huu, wajumbe kutoka wanachama waanzilishi wa AIIB walikutana kwa mara ya pili mjini Mumbai nchini India, na kufanya raundi ya kwanza ya majadiliano kuhusu muswada wa kanuni za AIIB. Mkutano huo uliamua kuwa, tarehe ya mwisho kwa nchi mbalimbali kutoa maombi ya kujiunga na AIIB itakuwa Machi, 31. Uamuzi huo ulizifanya nchi nyingi haswa zile za Magharibi zilizokuwa hazijafanya uamuzi, kutoa maombi ya kujiunga na AIIB mwezi Machi. Tarehe 12, Uingereza ilikuwa nchi kubwa ya kwanza ya Magharibi kutoa ombi la kujiunga na AIIB. Baadaye, "athari ya domino" ilizifanya Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uswisi na nyinginezo kuwasilisha maombi yao.

    Katibu mkuu wa Sekretarieti ya muda ya pande nyingi ya AIIB inayoshughulikia kazi ya uundaji Jin Liqun amesema, maendeleo ya uchumi wa Asia yataziletea nchi zisizo za bara hilo fursa nzuri za kujiendeleza, kuzipatia soko kubwa, kuongeza mahitaji ya uwekezaji na kufufua uchumi wa nchi hizo.

    Katika majira haya ya mchipuko, AIIB imekuwa ajenda moto kwa dunia nzima, na watu wengi wanajiuliza nani atafuata kuwasilisha ombi la kujiunga na Benki hiyo.

    Katika mkutano wa mwaka wa Baraza la Boao la Asia uliofanyika kuanzia tarehe 26 hadi 29 mwezi uliopita, nchi mbalimbali ziliwasilisha maombi ya kujiunga na AIIB. Tarehe 26, Uturuki ilitoa ombi la kujiunga, ikifuatiwa na Korea Kusini na Austria tarehe 27. Tarehe 28, wakati akihutubia mkutano wa Baraza la Boao la Asia, rais Xi Jinping alizungumzia tena AIIB, na naibu waziri mkuu wa Russia Igor Shuvalov alisema kuwa Russia inaomba kujiunga na AIIB. Siku hiyohiyo, Uholanzi, Brazil, Georgia, na Denmark zilitoa maombi rasmi. Tarehe 29 na 30 ni Australia, Misri na Finland. Tarehe 31, Kyrgyzstan na Sweden ziliwahi "gari la mwisho".

    Hadi kufikia sasa, idadi ya nchi na sehemu zinazotarajia kujiunga na AIIB imefikia 56, ambazo zinatoka kwenye mabara matano duniani. Kwa mujibu wa kanuni, wanachama rasmi waanzilishi watajulikana leo.

    Marekani na Japani hazikutoa maombi ya kujiunga na AIIB. Hata hivyo, waziri wa fedha wa Marekani Jacob Lew alipokuwa ziarani hapa China tarehe 30 na 31 mwezi uliopita, alisema Marekani inapenda kufanya ushirikiano na AIIB katika kukuza sekta ya miundombinu kwa kupitia utaratibu wa Mazungumzo ya Mkakati na Uchumi kati ya China na Marekani, ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na AIIB pamoja na hatua nyingine zinazoungwa mkono na pande zote mbili. Balozi wa Japani nchini China Masato Kitera aliwahi kusema Japani itafikiria kujiunga na AIIB, lakini baadaye kauli yake ilikanushwa na maofisa wengi waandamizi wa Japan.

    Baada ya kujulikana kwa wanachama rasmi waanzilishi wa AIIB, jukumu la kwanza kwa pande mbalimbali ni kukamilisha mazungumzo na kusaini kanuni za Benki hiyo kabla ya mwezi Juni mwaka huu, kukamilisha utaratibu wa kanuni hizo mwishoni mwa mwaka huu, na AIIB kuanza rasmi kazi. 

    ************************************

    Je, AIIB na benki nyingine za maendeleo zilizopo hivi sasa duniani zina uhusiano gani, na China ina nafasi gani katika AIIB ambayo ilipendekeza ianzishwe? Kuhusu uhusiano kati ya AIIB na benki za maendeleo ya pande nyingi zilizopo ni wa kusaidiana wala si kushindana. Waziri wa fedha wa China Lou Jiwei amesema AIIB inatilia mkazo zaidi ujenzi wa miundombinu, huku Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Asia zikisisitiza kazi ya kupunguza umaskini.

    "Malengo ya kazi zetu ni tofauti, AIIB inalenga kufanya kazi ambazo hazifanywi na Benki nyingine. AIIB hailengi kupunguza umaskini, bali ni kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya miundombinu. China siku zote imehimiza kuanzisha shirika la kifedha la pande nyingi na kuongeza utoaji wa mkopo, kwani ujenzi wa miundombinu duniani umekwama kwa sasa, ili uchumi wa dunia ufufuke unahitaji mkopo na uwekezaji, lakini uwezo wa nchi moja moja ni mdogo, hivyo shirika la pande nyingi linapaswa kufanya kazi zaidi. Pendekezo letu limeungwa mkono na mashirika hayo ya kimataifa, mwaka jana na mwaka huu, uwekezaji wao umendelea kuongezeka, lakini hautoshi, haswa katika bara la Asia, ujenzi wa miundombinu unakosekana, na AIIB inaweza kuziba pengo hilo. Katika sekta hiyo, tunaweza kusaidiana na kufanya ushirikiano ili kutoa mchango kwa pamoja."

    Wataalamu wanasema AIIB inapaswa kuwa jukwaa la kukusanya mitaji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, kuhimiza mageuzi ya utaratibu wa ukusanyaji wa mitaji, kuhamasisha sekta binafsi kufanya uwekezaji, kukabiliana kwa pamoja na hatari, na kupata mapato kwa pamoja kupitia njia ya ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.

    Bw. Jin Liqun amesisitiza kuwa, AIIB ni chombo chenye ufanisi mkubwa, na nafasi za ajira zitatolewa kote duniani, na kwamba Benki hiyo inapinga kuwepo kwa wafanyakazi wengi, na pia haitavumilia hata kidogo vitendo vya ufisadi.

    "AIIB itashika msimamo wa kufanya kazi kwa ufanisi, kupinga ufisadi na kutochafua mazingira. Tutajenga utaratibu wa kuzuia vitendo vya ufisadi. AIIB itahimiza maendeleo ya uchumi yasiyochafua mazingira na kutoa kiasi kidogo cha carbon, ili kutimiza masikilizano kati ya binadamu na mazingira ya asili."

    Hivi sasa, China ina hisa kubwa zaidi za AIIB. Bw. Jin anasema hii inatokana na ukubwa wa uchumi wa China barani Asia. Kabla ya Marekani na Japan kujiunga na AIIB, China imesema inaweza kuwekeza asilimia 50 ya fedha za kuanzishwa kwa AIIB ili kuhakikisha Benki hiyo inaanzishwa na kuendeshwa kuendana na mpango. Hata hivyo, kadri nchi nyingi zinavyojiunga, ndivyo China itakavyopunguza hisa zake katika AIIB.

    "Nafasi ya kwanza kwa umiliki wa hisa si mamlaka maalumu, bali ni wajibu. China itafuata kanuni zinazotekelezwa kimataifa, na haitajitetea kama mkuu wa AIIB. Ili kufikia ufumbuzi unaoridhisha pande zote, matatizo yanapaswa kutatuliwa kwa njia ya mashauriano, wala sio upigaji kura."

    Imefahamika kuwa AIIB itatenganisha wanachama wake kwa mujibu wa Asia au nje ya Asia. Kadri idadi ya wanachama inavyoongezeka, ndivyo hisa ya kila mwanachama itakavyopungua.

    *******************************

    Je, wataalamu wa China na wa nje ya nchi wanaonaje pendekezo la kuanzishwa kwa AIIB?

    Tukiangalia historia ya binadamu kuhusu mchakato wa kukuza sekta ya viwanda, tunaweza kugundua kuwa mchakato huo nchini Uingereza ulishirikisha mamilioni ya watu, mchakato huo nchini Marekani na Shirikisho la Soviet ulishirikisha mamilioni ya watu, na katika makundi ya kiuchumi yanayoibuka hivi karibuni, kama vile China na India, mchakato huo ulishirikisha mabilioni ya watu. Wachambuzi wanaona kuwa AIIB itatumia uwekezaji wa ujenzi wa miundombinu barani Asia kufanya nchi nyingi kujiunga na mchakato wa kukuza sekta ya viwanda badala ya nchi moja moja na kuunganisha mchakato huo na makumi ya mabilioni ya watu. Pia wanaona China ilitoa pendekezo hilo katika wakati na hali mwafaka, na itabadilisha muundo wa kisiasa duniani kwa kutumia sekta ya uchumi, jambo ambalo linaweza kutarajiwa.

    Naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mambo ya Nje cha China Wang Fan amesema, hii inaonesha kuwa China inafanya kazi kwa bidii na kwa ufanisi zaidi katika mambo ya nje, uwezo wake wa kuweka ajenda ya kimataifa unaongezeka, na wazo la diplomasia linalotetea kusaidiana na kunufaishana badala ya kuangalia thamani ya vitu linazidi kukubaliwa duniani.

    Naye mkuu wa Benki ya Dunia Jim Yong Kim amesema Benki hiyo inakaribisha kuanzishwa kwa AIIB, na iko tayari kubadilishana uzoefu wa maendeleo na benki hiyo. Akizungumza katika mkutano wa majira ya mchipuko wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani uliofanyika katika Kituo cha Mkakati wa Jopo la Washauri na Utafiti wa Masuala ya Kimataifa nchini Marekani, Bw. Jim Yong Kim alisema fedha zinazokosekana katika ujenzi wa miundombinu kila mwaka duniani zinafikia dola za kimarekani trilioni 1.5, na benki mpya ya maendeleo ya pande nyingi inayoendeshwa katika kiwango sahihi cha mazingira, ajira na manunuzi ya bidhaa, inatarajiwa kuwa nguvu muhimu ya kuchangia kazi za kupunguza umaskini. Bw. Jim Yong Kim amesema majadiliano kuhusu kuanzishwa kwa AIIB bado yapo katika kipindi cha mwanzo, Benki ya Dunia inapenda kuongeza ushirikiano na AIIB, haswa katika sekta ya kuzisaidia nchi maskini na dhaifu kujiendeleza. Anatarajia kuwa AIIB itajiunga na Mpango wa Ujenzi wa Miundombinu Duniani uliopendekezwa na Benki ya Dunia ili kuhimiza ushirikiano na kukusanya mtaji kutoka serikali na sekta binasi.

    Mchambuzi mkuu wa masuala ya uchumi katika Gazeti la Financial Times la Uingereza Martin Wolf amesema Uingereza ilifanya uamuzi sahihi unaozingatia hali halisi kwa kuwa nchi ya kwanza kutoka Ulaya kutangaza kujiunga na AIIB. Amesema AIIB italeta manufaa makubwa kwa bara la Asia na dunia nzima, na Uingereza haina sababu yoyote ya kukataa, na pia dunia haipaswi kuangalia jambo hilo kwa kutumia wazo la Mashariki na Magharibi lililotetewa kwenye Vita Baridi.

    Mkuu wa tovuti ya kuchunguza sera za China ya Hispania Xulio Rios amesema Hispania kujiunga na AIIB kunaweza kutoa nafasi mpya za kibiashara kwa kampuni za nchi hiyo. Amesema China ilisema itabeba wajibu mkubwa na wa wazi katika mambo ya fedha, hii inatarajiwa kutoa athari kubwa kwa bara la Asia, na kuibuka kwa AIIB ni injini mpya ya maendeleo kwa Asia. Naye mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Sera cha Ulaya Daniel Gros amesema nchi nyingi za Ulaya ziliamua kujiunga na AIIB baada ya kutambua ushawishi wa kikanda wa China, na kwamba inaweza kuhakikisha uwekezaji wao barani Asia, ili kulinda fedha zao. Hii inaonesha China inachukua nafasi ya kuunganisha Ulaya na Asia katika ushirikiano wa kikanda.

    Kuanzishwa kwa Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia AIIB, hakika ni tukio linalostahili kukumbukwa duniani kwa mwaka 2015.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako