• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Yoga inavyotuliza akili za wanawake wafungwa

    (GMT+08:00) 2015-04-27 08:29:01

    Wengi wetu tunafahamu kuwa mazoezi ni muhimu katika mwili wa binadamu. Katika maisha ya kila siku, kila binaadamu anakula na hiyo ndiyo kawaida ya mzunguko wa maisha. Je tunakumbuka kufanya mazoezi ili kuwa na afya bora, au kutuliza akili zetu jibu linaweza kuwa ndio au hapana na hii pia inategemea na hulka ya maisha ya mtu ya kila siku. Kwa kuwa tunanakula kila siku tunahitaji kukitumia chakula tulichokula kwa kufanya mazoezi ili kuepuka maradhi kama ya moyo, kisukari na kuwa na uzito uliokithiri, huna budi kufanya mazoezi katika maisha yako bila kujali umri na jinsia.

    Haya ni mazoezi ambayo yanasaidia kudhibiti na kuongoza akili na miili yetu. Hivyo ili kuyatumia vizuri mazoezi hayo, kundi la wanawake wafungwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi hivi sasa wanajifunza njia mpya ya kujituliza. Wanawake hao kutoka gereza la Nairobi wanajifunza mazoezi ya yoga kwa kutarajia kuwa yatawasaidia kupata amani katika maisha yao.

    Muongozaji wa mazoezi hayo Bibi Margaret Njeri ameamua kutumia fursa ya kuwatuliza kiakili na kimwili kwa kuwakusanya wafungwa 30 wanawake, ambao wanakutana mara mbili kwa mwezi kufanya yoga katika gereza la wanawake la Langata. Ingawa wengi tunafahamu kuwa gereza ni sehemu ya kutisha kutembelea mwanamke wa kawaida lakini Bibi Njeri hakuona hilo, isipokuwa tu kuwasaidia wanawake wenzake.

    "Hawa watu, wapo hapo, walifanya makosa mbalimbali: kama vile, kuua waume zao, kuiba – hivyo nikafikiria kama ninaweza kupeleka mazoezi ya yoga gerezani litakuwa jambo zuri sana. Na ndio nimefanikiwa, niliuliza kama naweza kufundisha yoga gerezani, na wakasema ndio!"

    Kwa kweli Bi Njeri ni mwanamke wa kupigiwa mfano, kwani hajali ni wanawake wa aina gani anaowasaidia, kwasababu baadhi ya wanawake anaowafundisha yoga wamefanya makosa makubwa na wanasubiri adhabu ya kifo. Lakini wote wanakabiliwa na adhabu tofauti na wote ni waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi. Lakini pia kuna wale ambao siku moja watatoka gerezani na kurudi katika jamii. Yoga inasaidia kuushughulisha mwili kwa njia ya taratibu kwa wanawake kama Mary Mwangi, ambaye mara nyingi anajisikia dhaifu kutokana na kula dawa kali za anti-retroviral na kukosa chakula bora.

    "Nilipoanza mazoezi ya yoga mwaka 2011, nilikuwa dhaifu sana. Lakini nilipoendelea kuja, nikaendelea kuja hapa, mwili wangu ukaanza kupata nguvu zaidi."

    Mazoezi hayo ya taratibu yamemuwezesha kurudisha nguvu zake polepole. Lakini bahati mbaya Bi. Mary Mwangi hivi sasa anasubiri adhabu ya kifo baada ya kupatikana na hatia ya kuiba akitumia silaha, kosa ambalo amekanusha kuwa hajalifanya. Kutokana na adhabu ya kukaa gerezani, pamoja na unyanyapaa wa hali yake ya afya, Mwangi anasema anajisikia wasiwasi kila siku, lakini baada ya kuhudhuria yoga hali hiyo imepotea kabisa.

    "Wala hujisikii tena kutengwa, unapumzika tu. Ndio. Hujihisi chochote, na huiwazii hata hukumu uliyopewa. Unakuwa salama tu."

    Wengi wetu tunafahamu kuwa yoga inatoa hali fulani ya utulivu kwa mtu kama inavyoonesha kwa Bi. Mary Mwangi. Mtu akifanya mazoezi hayo anajisikia vizuri kwa hiyo kwa wafungwa hao hususan wanaoishi na virusi vya Ukimwi ni muhimu kwani wengi hukabiliwa na msongo wa mawazo. Mshauri nasaha wa gerezani Bibi Christabel Abwaku naye kila wiki anajaribu kupanga kundi la kusaidia watu waishio na virusi vya Ukimwi. Na hapa anasema ameona wafungwa hao sio tu wamepata nguvu za mwili bali hata akili zao pia zimetulia kwani sasa wafungwa wengi wanawake wamefikia hatua ya kukubali hali zao ngumu.

    "Angalau inafanya akili yako ishughulike, baadhi ya wakati unapokuwa umekaa tu, unaweza hata kufikiria kwamba 'Nitakufa dakika moja ijayo.' Kwa hiyo angalau wakiwa na haya mazoezi wanakuwa wazuri kimwili na kiakili."

    Na Bibi Njeri yeye mwenyewe pia amekulia katika maisha magumu katika mtaa wa mabanda huko Nairobi, kabla ya kujifunza kuwa mwalimu wa yoga miaka minne iliyopita akiwa na Mradi wa Yoga wa Afrika, mfuko ambao umefadhili mazoezi hayo anayofanya ya gerezani. Bi Njeri anaona mafunzo yamebadilisha maisha yake, lakini pia anatarajia kurithisha mafunzo hayo kwa wanawake wenye akili timamu wa gerezani, hususan wale wote watakaoachiliwa hivi karibuni.

    "Kama naweza kuondoka hapa, na kwenda huko nje, naweza kufanya mambo mazuri sana. Naweza kufanya yoga, au naweza kuja na kusafisha, kama vile kuwa msaidizi wa nyumbani. Ndio? Au unaweza kupata kazi nyepesi. Na watu watakukubali. Ndio maana nafanya mazoezi ya yoga. Kwasababu inakufanya ujitambue."

    Na hilo ndio lengo hasa kama anavyosema Bi Njeri, kwani wafungwa wengi wanapoachiliwa hutazamiwa kubadilika tabia na kubadilisha maisha yao pia, kwa kujaribu kutafuta shughuli ya kufanya ili kuepuka kurejea tena kule walikotoka. Na kwa vile mazoezi hayo yatakuwa yamewasaidia kutuliza akili zao na kubadilisha misimamo yao, wataweza kukaa chini na kutafakari nini wafanye baada ya kuachiliwa huru. Kwani huko huko nje kuna mashirika mengi tu yanayowasaidia wanawake kujiendeleza. Pia wanaweza kutumia ujuzi wa yoga walioupata na kufundisha watu wengine katika jamii ikiwa kama njia ya kujiingizia kipato.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako