• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Shinikizo la mama ni kubwa zaidi au la baba?

    (GMT+08:00) 2015-05-11 09:32:46

    Jana dunia nzima iliadhimisha siku ya mama. Tunafahamu kuwa mama ni kiungo muhimu sana cha familia, na kuonesha thamani yake kumekuwa na misemo mbalimbali inayoashiria kuwa mama ni mtu muhimu zaidi katika familia na hata katika jamii, miongoni mwa misemo hiyo ni nani kama mama, hakuna kama mama, hakuna mtakatifu au mtukufu hapa duniani asiyezaliwa na mama na mingineyo. Tunafahamu kuwa kwa nchi za Afrika mama ndiye anayeibeba familia nzima katika masuala mengi tu ikiwemo kulea watoto, kupika, kusafisha nyumba, kumtimizia mume mahitaji yake n.k. Ingawa katika nchi nyingine za nje ya Afrika wanaume wamekuwa wakisaidia kidogo shughuli hizo za ndani.

    Ingawa tunasema mama ana kazi nyingi za nyumbani, baba naye kwa upande wake sio kama hana shughuli, la hasha, kwani naye anawajibu wa kuhakikisha familia yake ama watoto wake wanasoma, wanakula wanavaa vizuri n.k. Ndio maana hutokana na hayo kila upande umekuwa ukihisi shinikizo kubwa. Na ili kujua nani mwenye shinikizo kubwa zaidi, hapa tunaye Bwana Qian anayetuelezea mtazamo wake kuhusu swali hilo ni mama au baba:

    "Naona sote tuna shinikizo, lakini upande wa shinikizo letu ni tofauti. Shinikizo langu linatoka kazini, napaswa kushughulikia mambo mbalimbali ya kikazi. Vilevile mama wana shinikizo lao, kwa mfano wanahitajika kushughulikia vizuri uhusiano kati yao na mama wakwe zao, na kuweka nguvu nyingi zaidi katika kuwaelimisha watoto. Naona malalamiko makubwa zaidi kati ya baba na mama ni kuhusu suala la kuwaelimisha watoto. Kwani wakati fulani maoni yao yanatofautiana, hadi watoto wakashindwa kujua nini la kufanya."

    Ni kweli katika familia pande zote mbili zina shinikizo kama anavyoeleza bwana Qian, kwani kuna majukumu mengi ambayo yanapaswa kutekelezwa kwa pamoja. Lakini tunajua kuwa hakuna mtu hata mmoja awezaye kutimiza mahitaji maalumu ya mume na watoto kama sio mama. Ndio maana mama anajihisi kuwa ana mzigo mkubwa sana katika familia na hususan anapomuona mwenzake hatumii muda mwingi sana nyumbani bali anathamini kazi zaidi kuliko familia. Hivyo akina mama wengi hujiona wapweke na kuhisi kama jukumu la familia wameachiliwa kulitekeleza wao wenyewe tu bila msaada wa mume. Bibi Zhao akiwa kama mwanamke amekuwa akisikia malalmiko mengi ya wanandoa kila siku na hapa anaeleza jambo kubwa linalowafanya walalamike:

    "Ninacholalamika zaidi? Naona ni kuhusu wakati, yaani nani anatarajiwa kukaa pamoja na watoto? Suala hilo huleta mgongano. Kwa sababu tukiwa kama wazazi, hususan wazazi wenye kazi zao, nani anaweza kutumia muda mwingi zaidi kukaa pamoja na watoto, wanalalamika kupita kiasi. Mfano leo sisi sote tuna mambo mengi ya kufanya, lakini watoto wanalazimika kutunzwa, kucheza nao pamoja, au kusimamiwa wanapofanya kazi za shule. Hivyo nani anaweza kujitolea kufanya mambo kama hayo na watoto wao? Inabidi kujitolea muda wako."

    Watu husema wanaume na wanawake wanatoka dunia tofauti. Utafiti mpya unaonesha kuwa, wanaume na wanawake wanatofautiana sana katika kutunza watoto. Na ingawa muundo wa ubongo wa wanaume na wanawake uko sawa, lakini kuna tofauti katika ukubwa na unene wa ubongo wao. Kwa kawaida, upande wa kulia wa ubongo wa wanaume unaendelezwa zaidi, huku upande wa kushoto wa ubongo wa wanawake ndio unaoendelezwa zaidi. Pande hizo mbili zinadhibiti kazi tofauti za ubongo. Vizuizi vilivyopo kati ya baba na mama katika kuwatunza watoto zinatokana na tofauti hiyo. Lakini kuna njia mbili za kutatua vizuizi hivyo, ya kwanza ni kuwapa baba kazi zinazofaa kwao zaidi, na ya pili ni kuwa na uvumilivu na ufahamu.

    Tunapozungumzia kazi anazopaswa kupewa baba kwa vile wengi wao wanapenda sana kuona watoto wao wakitabasamu, na kuwa na nyuso zenye furaha hivyo hali hiyo inawachangamsha zaidi kina baba, pia hali hiyo inasaidia kutolewa kwa kitu kiitwacho dopamine katika ubongo wao, na kuwafanya baba kuwa na shauku, hivyo kazi kama za kucheza michezo mbalimbali na watoto wao pamoja na kuogelea, zinapaswa kwenda kwa baba. Watoto wakiwa na furaha zaidi, akina baba nao wanachangamka zaidi, na kupenda zaidi kuwatunza watoto wao. Lakini kwa upande mwingine akina baba hawapendi shughuli zisizo na maana kubwa yaani zile za kawaida za kila siku.

    Hapa tunaposema shughuli zisizo na maana hatukusudii kusema kazi anazofanya mama kwa mtoto wake hazina maana. Lengo kubwa hapa ni kuona baba anamshughulikia mtoto ama kucheza naye kwa njia za uchangamfu zaidi, kwani homoni zao zinawafanya watafute mambo yaliyochangamka zaidi pamoja na mabadiliko. Lakini wakati huohuo hawana uwezo mkubwa katika mambo madogo madogo kama vile kubadilisha nepi au kumbembeleza mtoto alale kwani wanaona ni mambo yanayochosha.

    Ni kweli kwa vile dunia sasa imebadilika hata wanaume nao pia wanapaswa kufanya kazi kama zile wanazozipenda kufanya akina mama. Kwani wanawake wengi siku hizi sio tu wanakaa nyumbani bali wanatoka na kwenda kazini, na wakirudi nyumbani pia majukumu ya kutunza familia yanawasubiri. Tunafahamu kuwa kina mama wengi wanapenda zaidi kuwagusa watoto wao, kwa mfano kuwabeba na kwenda kuwalaza. Hivyo kuna homoni moja iitwayo Oxytocin au homoni ya upendo inaweza kuwafanya akinamama wawasiliane zaidi na watoto kimwili, na kumpa mama hisia nzuri kwa watoto.

    Lakini pia tunaona ni vigumu sana kwa mama, kuwa mbali na watoto wao, kwani wanakuwa na wasiwasi hata wakitengana nao kwa muda mfupi. Tukimzungumzia baba yeye watoto kwake ni kama wenzi au washindani katika michezo wanayocheza, lakini kwa mama watoto ni malaika wao wanaohitaji upendo. Lakini pia kina mama wanapenda kuonesha upendo wao kwa watoto wao kupitia kuwagusa, ndio maana wanapenda sana kuwashika na kuwabeba.

    Kwa hiyo kwa ujumla akina mama wengi huwa wanaumizwa sana wakiona akina baba hawatoi kipaumbele cha kuwa karibu na watoto wao, au kujishughulisha nyumbani, kwa mfano baba kama hambadilishi nepi mtoto, basi kwao wanamchukulia kuwa sio baba mzuri. Mama pia wanafutilia kila hatua ya ukuaji wa watoto. Mama huwa wanapanga vizuri kila kitu, hawataki kukosa hatua yoyote ile ya ukuaji wa watoto. Lakini kama mipango yao waliyoweka haitekelezwi kama wanavyotarajiwa, wanakuwa na wasiwasi na kuumia sana moyoni.

    Sasa tuangalie malalmiko makubwa matano kati ya mama na baba. Na tunaanza malalamiko ya baba kwa mama huwa wanawaambia:

    1) Usiongee ongee mambo kuhusu watoto

    2) Wewe hunihurumii hata kidogo

    3) Kwa nini unakasirika bila sababu

    4) Kwa nini huwezi kufahamu shinikizo langu la kikazi

    5) Hivi ninavyosaidia kufanya kazi za nyumbani na kuwatunza watoto unaona jambo dogo tu.

    Naye Mama humlalamikia baba:

    1) Hufahamu juhudi yangu kubwa ya kuwatunza watoto

    2) Unajifikiria wewe tu kwanza wakati wote

    3) Hunisikilizi

    4) Huwatunzi watoto hata kidogo

    5) Upendo wako kwa watoto hautoshi

     

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako