wh0501.m4a
|
Tamasha la filamu la kimataifa la Beijing lilifanyika kwa mafanikio kuanzia tarehe 16 hadi 23 mwezi Aprili, katika kipindi hiki, tutazungumzia tamasha hilo kubwa la filamu.
Tamasha hili la filamu la kimataifa la Beijing ni la awamu ya tano. Katika miaka mitano iliyopita toka lianzishwe, tamasha hilo limepevuka na kuimarisha nafasi yake kama soko la kwanza la filamu barani Asia, na limekuwa jukwaa muhimu la mawasiliano kati ya wadau wa setka za filamu za China na za nchi za nje.
Mwaka huu tamasha hilo lilivutia na kuhudhuriwa na wanafilamu zaidi ya elfu 14 kutoka nchi na sehemu zaidi ya 50, pamoja na mashirika zaidi ya 340 ya filamu ya China na ya nchi za nje. Wachezaji nyota wa filamu wapatao 800 walihudhuiia shughuli mbalimbali za tamasha hilo, filamu 930 kutoka nchi na sehemu 90 ziliandikishwa kugombea tuzo ya Tiantan ya tamasha hilo, na filamu 1524 kutoka nchi na sehemu 13 zilioneshwa kwenye tamasha hilo. Mashabiki wa filamu zaidi ya milioni moja walihudhuria tamasha hilo.
Kwenye ufunguzi wa tamasha hilo, mwongozaji mashuhuri wa filamu wa Ufaransa ambaye alikuwa mwenyekiti wa jopo la majaji Bw. Luc Besson alisema, amehisi nguvu kubwa ya uhai kwenye tamasha hilo, na anaamini kuwa litaendelea kupiga hatua zaidi.
"Miaka 5 ni kidogo sana, ni kama mtoto, lakini sijawahi kuona mtoto mwenye akili kiasi hiki, akili ya wazee wa busara wa kichina. Majaji wote wanatoka nchi na sehemu tofauti duniani, tuna hisia tofauti, na hii ni njia bora ya kujaji filamu kwa kuwa jopo letu ni mfano mzuri wa mchanganyiko wa tamaduni na hisia mbalimbali. Filamu ni kama zawadi kutoka kwa watu kwenda kwa watu, tujiburudishe kwa pamoja mamia ya filamu yatakayooneshwa kwenye tamasha hilo. Nalitakia maisha marefu tamasha la filamu la kimataifa la Beijing!"
Bw. Luc Besson alipozungumzia ufahamu wake kuhusu China, alisema filamu ya kwanza ya China aliyotazama ni filamu ya Bruce Lee alipokuwa na umri wa miaka 10 hivi. Alisema, wakati huo aliishi kijijini Ufaransa, ambako kulikuwa hakuna televisheni au mtandao wa Internet, njia yake ya pekee ya kufahamu dunia ilikuwa kwenda kutazama filamu kwenye jumba la sinema lililoko umbali wa kilomita 15 kutoka nyumbani kwao. Bw. Luc Besson alisema, baada ya kutazama aina mbalimbali za filamu za kichina, akafahamu zaidi maisha ya wachina na kutaka kuitembelea China. Anaona kuwa sekta ya filamu ya China imepiga hatua kwa kasi na ina mustakbali mkubwa.
Msikilizaji mpendwa, uliosikia ni wimbo wa kauli mbiu wa tamasha la tano la filamu la kimataifa la Beijing. Sasa tuendelee na kipindi chetu.
Kwenye awamu hii ya tamasha la filamu la kimataifa la Beijing, mbali na shughuli zinazofanywa katika matamasha yote ya filamu kama vile utoaji wa tuzo, maonesho ya filamu bora na biashara ya filamu, pia kuna shughuli mbili mpya. Naibu katibu mkuu wa kamati ya maandalizi ya tamasha la filamu la kimataifa la Beijing Bw. Zhao Zhiyong anasema:
"Moja ni shughuli inayoitwa "tupia macho siku zijazo", ikiwa ni mpya katika tamasha la mwaka huu, inalenga kugundua wachezaji chipukizi na waongozaji vijana hodari wa filamu. Kwa upande wa filamu zilizopendekezwa na maoni ya majaji, mwaka huu zimejitokeza kazi hodari, na idadi kubwa ya waongozaji na wahusika na filamu hizo wamehudhuria tamasha hilo. Shughuli nyingine zinahusu filamu za documentary, lengo lake ni kuinua na kupanua kwa pande zote ushirikiano katika fani ya filamu za documentary, kwa njia ya mawasiliano na biashara za filamu hizo."
Jambo lingine linalovutia kwenye tamasha hilo ni kuwa lilijihusisha zaidi na mtandao wa Internet. Mwaka jana ulikuwa ni mwaka ambao kampuni za Internet zilijiingiza kwa wingi kwenye sekta ya filamu nchini China, zikiwekeza kwenye utengenezaji wa filamu. Mwaka huo, idadi ya watazamaji wa filamu nchini China ilifikia milioni 830, ongezeko ambalo pia linatokana na mchango mkubwa uliotolewa na sekta ya mtandao wa Internet.
Kwa watazamaji wa kawaida, jambo la kuvutia zaidi kwenye tamasha hilo la filamu ni maonesho ya filamu bora za China na za nje, zikiwemo filamu zilizopata tuzo ye Oscar kama vile Birdman, Gone Girl na The God Father, filamu za mchezaji mashuhuri wa Uingereza Audrey Hepburn, na filamu za mwongozaji mashuhuri wa Ufaransa Luc Besson. Filamu hizo zinapendwa sana na watazamaji wa China, na tangu tarehe 9 April tiketi zilipoanza kuuzwa ilikuwa vigumu sana kuzipata.
"Nilitaka sana kununua tiketi za filamu zilizopata tuzo ya Oscar ya mwaka huu, lakini ofisi ya tiketi iliniambia kuwa zimeisha, kwa hiyo basi."
"Nataka kutazama Once Upon a Time in America, lakini sijapata tiketi. Nilienda jana nikakuta tiketi zote zimeisha. Mwenzangu aliniambia kuwa tiketi ziliisha mapema sana."
Naibu katibu mkuu wa kamati ya maandalizi ya tamasha la filamu la kimataifa la Beijing Bw. Zhao Zhiyong amesema, hakutarajia kuwa tiketi za filamu zilizooneshwa kwenye tamasha hilo zitamalizika haraka namna hiyo.
"Tulianza kuuza tiketi tarehe 9 Aprili, siku hiyo tu, tiketi zaidi ya elfu 10 ziliuzwa ndani ya dakika 15. Sasa tiketi za filamu maarufu zote zimeisha, hata zile zisizojulikana sana, asilimia 40 hadi 50 ya tiketi pia zimeuzwa. Ni filamu 50 tu ambazo zaidi ya nusu ya tiketi bado hazijauzwa."
Mbali na maonesho ya filamu yanayopendwa sana mashabiki wa filamu, jambo jingine muhimu linalofuatiliwa zaidi na wanafilamu kutoka nchi na sehemu mbalimbali kwenye tamasha hilo ni uchaguzi wa tuzo ya Tiantan.
Filamu kutoka Mexico inayoitwa The Beginning of Time, ilipata kura nyingi miongoni mwa filamu 15 zilizopendekezwa na kuchukua tuzo ya filamu bora.
Filamu hiyo inazungumzia hadithi ya nchi ambayo wanandoa wa muda mrefu wenye umri wa miaka zaidi ya 90 Bw. Antonio na Bi. Bertha ilitokea msukosuko mkubwa wa kijamii na kiuchumi, hali ambayo ilisababisha serikali kusimamisha kutoa pensheni kwa wazee hao na kukwamisha maisha yao. Lakini mtoto wa wazee hao alitoweka kwa miaka mingi, ili kuendelea na maisha, wazee hao walilazimika kuuza mali za nyumbani na kuanza biashara ndogo mtaani. Jambo lisilotarajiwa ni kuwa siku moja mtoto wao alirudi nyumbani pamoja mjukuu wao…
Mhusika wa filamu hiyo anasema, maisha si rahisi nchini Mexico, haswa kwa wazee. Amesema, bila kujali ni katika filamu au maisha ya kweli, ameguswa sana na wazee hao wawili, na kuwa na upendo na huruma kubwa kwao. Filamu hiyo imemfanya azingatie upya maana ya familia. Mwongozaji wa filamu hiyo Bernardo Arellano amesema anapenda kueleza hadithi kuhusu ubinadamu, na kutumai kupitia filamu hiyo kufafanua mawazo yake kuhusu familia, kazi, kifo na upweke, na kuonesha heshima kwa watu wenye imani na wanaoheshimu maisha. Bw. Arellano pia anaona, filamu hiyo inafaa kwa wote, na anatarajia kuwa itaweza kuoneshwa kwenye sinema nchini China katika siku za baadae.
Kwenye tamasha hilo, filamu ya China Wolf Totem ilinyakua tuzo mbili za mwongozaji bora wa filamu na Vionjo bora vya picha(Best Visual Effects). Meneja mkuu wa kampuni ya filamu ya China iliyotengeneza filamu hiyo Bw. La Peikang alipokabidhiwa tuzo ya Vionjo bora vya picha anasema:
"Sikutarajia kuwa filamu yetu ya Wolf Totem itapata tuzo ya kwanza ya tamasha ya filamu ya kimataifa ya Beijing, na hii pia ni tuzo ya kwanza tuliyopata tangu filamu hiyo ianze kuoneshwa kwenye sinema. Filamu hiyo ina picha zaidi ya 2000 zilizotengenezwa kwa kompyuta, na zote zimetengenezwa hapa China, tuzo hiyo inaonesha kuwa kiwango cha utengenezaji wa picha kwa kompyuta nchini China kimefikia cha kimataifa."
Filamu nyingine zilizopewa tuzo ya Tiantan ni pamoja na filamu za Russia Battle for Sevastopol na A White, White Night, Filamu ya Czech Deti, filamu ya China The Taking of Tiger Mountain, na filamu ya Austria Gruber Geht.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |