• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Umuhimu wa kunyonyesha watoto wachanga

    (GMT+08:00) 2015-05-18 14:30:17

    Katika kipindi cha leo tutazungumzia umuhimu wa maziwa ya mama, au unyonyeshaji na manufaa yake kwa mama na mtoto pia. Kuna baadhi ya kina mama huwa hawanyonyeshi watoto wao kwa hofu kuwa matiti yao yatalala au saa 12 jioni. Jambo hili linasikitisha sana kwani kunyonyesha ni njia mojawapo muhimu inayomuunganisha mama na mtoto, sasa kama mtoto hatanyonya, hata ule ukaribu na mama pia hautakuwepo. Kwa miongo kadhaa sasa, manufaa ya kiafya kutokana na unyonyeshaji na mapendekezo ya jambo hilo yameendelea kuongezeka. Shirika la Afya Duniani WHO linaweza kusema kwa uhakika kuwa unyonyeshaji unapunguza vifo vya watoto wachanga na una manufaa yanaendelea hadi umri wa utu uzima. Inapendekezwa kuwa watoto wanyonye maziwa ya mama kwa muda wa miezi sita ya mwanzo, na baada ya hapo, wanaweza kupata vyakula vingine vinavyopendekezwa lakini huku wakiendelea kunyonya.

    Shirika la Afya Duniani WHO na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF vinapendekeza mtoto aanze kunyonya maziwa ya mama saa moja baada ya kuzaliwa, na kama ulivyosema Pili, mtoto anatakiwa anyonye maziwa ya mama pekee bila ya chakula wala kimininika chochote cha ziada, hata maji ya kunywa. Wataalam wanasema kuwa, maziwa ya mama ni chakula halisi cha kwanza kwa watoto, na yanawapatia watoto virutubisho vyote vinavyohitajika katika miezi ya mwanzo ya maisha yao.

    Wanawake wanachukulia kitendo cha kunyonyesha kama cha kawaida, lakini mwanamke anaweza kujifunza tabia ya kunyonyesha. Utafiti uliofanywa na kundi la wataalam umegundua kuwa, wakina mama na watoa huduma wengine wanahitaji kuungwa mkono ili kuanza na kudumisha utamaduni unaofaa wa kunyonyesha. Maana kuna kina mama wengine wanaweza kuona aibu kuwanyonyesha watoto wao mbele ya hadhara. Lakini sehemu kama hiyo, mama anaweza kumfunika mtoto na kitambaa maalum na kumyonyesha bila matatizo yoyote. Lakini kwa hapa China je, hali ikoje?

    Kwa hapa China kuna msisitizo mkubwa wa kuwanyonyesha watoto, kwani kama tulivyosema hapo awali, maziwa ya mama ni muhimu sana kwa makuzi ya mtoto. Mkurugenzi wa shirikisho maalum la vyakula vya watoto la China Bw. Xie Hong ana haya ya kusema:

    "Virutubisho vinavyopatikana kwenye maziwa ya mama, mchanganyiko wake ni wa asili zaidi, ni nzuri zaidi. Kwa kuwa yanayotolewa kiasili, hayana gharama yoyote, na ni salama zaidi. Yanaletea manufaa ya kisaikolojia vilevile, yanasaidia kujenga uhusiano mzuri kati ya mama na mtoto mchanga. Mbali na hayo, yanamsaidia mama kurejea afya njema ya mwili baada ya kujifungua."

    Huyo ni mkurugenzi wa shirikisho maalum la vyakula vya watoto la China Bw. Xie Hong. Lakini kwa upande wa kina mama je, wao wana maoni gani kuhusu kunyonyesha? Mama Lin anasema:

    "Nikiwa kama mama, naunga mkono kunyonyesha watoto wachanga. Nina binti mwenye umri wa miaka 6 kwa sasa. Nilimnyonyesha kwa miezi 11 hivi. Baadaye nilirudi kazini, nikapunguza muda wa kumnyonyesha. Naona manufaa ya kunyonyesha ni dhahiri. Kwanza ni maziwa masafi na ninaokoa pesa. Zaidi, kutokana na kusoma vitabu, najua kuwa, kunyonyesha kunaweza kupunguza hatari ya kuwa na saratani ya maziwa. Lakini muhimu zaidi ni kuwa, kunyonyesha ni njia ya moja kwa moja inayoimarisha uhusiano kati ya mama na mtoto, na ni njia yenye ufanisi zaidi. Nakumbuka vizuri jinsi alivyoniangalia nilipombeba mtoto wangu nikimnyonyesha."

    Mama Lin anasema kunyonyesha kuna manufaa ya kiafya kwa mama lakini pia kunajenga uhusiano wa karibu kati ya mama na mtoto. Mama Liu je anasemaje?

    "Mtoto wetu ana umri wa miaka zaidi ya mitatu. Baada ya kuzaliwa, alinyonya mpaka alipofikisha mwaka mmoja na miezi miwili. Naona maziwa ya mama yanasaidia kujenga afya nzuri ya mtoto, na kuwaongezea kinga ya asili dhidi ya maradhi mbalimbali. Pia naona yana umuhimu mkubwa katika kuimarisha uhusiano kati ya mama na mtoto."

    Wakina mama hao wote wanasema ni muhimu kumyonyesha mtoto kwani unamjenga kiafya na kisaikolojia pia. Kwa wale wanawake wanaowakamulia watoto maziwa na kuweka kwenye chupa kisha kupasha moto na kuwapa baada ya muda fulani, tukumbuke kuwa, pamoja na kusafisha vizuri vyombo vya mtoto, bacteria wanaweza kuingia kwa urahisi na kusababisha madhara kwa mtoto. Tuwanyonyeshe watoto wetu kwa manufaa yao na wetu pia.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako