• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Duka la vitabu la Sanlian linalofunguliwa saa 24 kwa siku

    (GMT+08:00) 2015-05-22 09:21:20

    Kuna mikahawa na maduka mengi yanayofunguliwa saa 24 kila siku katika sehemu mbalimbali duniani, lakini maduka ya vitabu ya saa 24 sio mengi sana. Mwezi Aprili mwaka jana, duka la vitabu la Sanlian Taofen la Beijing lilianza kufunguliwa saa 24 kwa siku, na limekuwa duka la vitabu la kwanza linalokuwa wazi siku nzima jijini Beijing. Baada ya mwaka mmoja, duka hilo limefungua tawi lake katika eneo lenye vyuo vikuu vingi jijini Beijing, ambalo pia liko wazi saa 24. Kutokana na mafanikio ya duka hilo, maduka mengine mawili pia yameamua kujiunga na kundi la maduka ya vitabu ya saa 24. Je, ama kweli watu wanakwenda duka la vitabu usiku wa manane? Na baada ya mwaka mmoja, uendeshaji wa duka la vitabu la Sanlian linalofunguliwa saa 24 inakuwaje? Wasomaji wana maoni gani kuhusu duka hilo?

    Duka la vitabu la Sanlian Taofen liko katika sehemu ya Dongcheng jijini Beijing, na linajulikana sana hapa Beijing. Duka hilo lina historia ya zaidi ya miaka 80 ambalo liliundwa na maduka matatu ya vitabu, kwa hiyo kwenye jina lake la Kichina Sanlian Taofen, San kwa Kichina ni tatu na Lian ni muungano, jina hilo ndilo ni kumbukumbu ya muungano wa maduka matatu ya vitabu. Na duka hilo pia lilipewa jina la Taofen ili kumkumbuka mchapishaji maarufu wa China Marehemu Zou Taofen. Mwaka 1949 ofisi kuu ya uendeshaji ya duka hilo ililihamishia jijini Bejing kutoka Hong Kong, kisha likaingia katika maisha ya wakazi wa Beijing. Kuanzia mwaka jana, duka hilo lilianza aina mpya kabisa ya biashara, yaani liko wazi saa 24 siku 7 kwa wiki. Mwandishi wetu anawafuatana na wasomaji wengi kuingia katika duka hilo.

    Sasa imezidi saa tatu usiku, maduka mengi ya vitabu yanakuwa yamefungwa hapa Beijing. Sasa niko ndani ya duka hilo la Sanlian Taofen, , naona bado kuna wasomaji wengi wanasubiri kwa mstari kulipia vitabu vyao, na idadi ya wateja haipungui sana ikilingnishwa na machana, pia kuna wasomaji wengi wanasoma na kuchagua vitabu. Katika eneo la vitabu vya watoto, Bibi Li na mtoto wake wanachagua vitabu, anasema kwa sababu maduka mengi yanafungwa mapema sana, hivyo hawezi kununua vitabu vya watoto baada ya kazi, lakini sasa duka hilo la saa 24 linampa nafasi yeye na mtoto wake waweze kuchagua vitabu.

    "Nafurahi sana, labda hali hii itakuwa sehemu ya utamaduni wa Beijing, hatua kwa hatua maduka yote ya vitabu yatafunguliwa saa 24 siku 7 kwa wiki. Watu wengi wanaweza kuja kusoma vitabu, sio kutazama televisheni nyumbani, wana muda mwingi zaidi kutafuta vitabu wanavyopenda dukani. Hilo ni jambo zuri kwa wapenzi wa vitabu na wapenzi wa maduka ya vitabu."Maduka mengi ya vitabu hapa Beijing yanafungwa saa tatu usiku, na mikahawa inayofunguliwa saa 24 inatoa mahali pa kusoma kwa wasomaji, lakini haiuzi vitabu. Kwenye duka hilo la vitabu la Sanlian la saa 24 naona mbali na safu za vitabu, pia kuna meza, viti na taa za mezani kwa wateja, na mkahawa ulioko ghorofa ya pili ya jengo la duka hilo pia unafunguliwa saa 24 kutoa huduma kwa wateja hao. Wateja wengi wanaosoma vitabu hapa dukani wameeleza jinsi wanavyolipenda.

    "Naweza kupumzika hapa dukani, vitabu ni vizuri, kwa kawaida nakuja kukaa na kusoma kwa saa kadhaa. Niliwahi kusoma vitabu hapa usiku kucha."

    "Mchana nafanya kazi, hivyo ni manufaa kwangu duka likifunguliwa saa 24."

    "Nakuja mara kwa mara, mazingira ni mazuri, na yananifanya niwe na kiu ya kusoma vitabu."

    Naibu mkuu wa shirika la uchapishaji la China Bw. Li Yan anasema, duka la vitabu linalofunguliwa saa 24 ni jaribio ambalo limefanikiwa kwani limeunganisha huduma za kununua vitabu, kusoma, na kupumzika.

    "Huu ni muungano mpya, watu sio tu wanachagua na kusoma vitabu, bali pia wanajisikia raha, wanapumzika. Haya ni mafanikio ya jaribio la kubadilisha mtindo wa uendeshaji."

    Kwa kweli, mbali na mtindo wa biashara, duka la vitabu linalofunguliwa saa 24 pia ni mtindo wa maisha kwa watu wa sasa. Naibu meneja wa duka la vitabu la Sanlian, Bibi Wang Yu amesema,

    "Tumefanya mabadiliko. Kufungua saa 24 ni mtindo mpya kwa duka la vitabu la Sanlian, na unakidhi mahitaji ya baadhi ya watu wanaopenda kukesha. Aidha, kabla au baada ya kufanya kazi ya usiku, unaweza kuja kusoma vitabu. Naona tumetoa mtindo wa maisha, usiku mbali na kwenda kuimba karaoke au kula chakula, watu pia wanaweza kuja duka la vitabu."

    Naonalicha ya vijana, wazee na watoto pia wanakuja hapa kusoma vitabu usiku, watu wenye umri tofauti wanafahamu duka hilo kwa njia gani? Niliongea na baadhi yao.

    "Kutoka televisheni na tovuti za mtandao wa Internet, nilipata habari ya watu kusoma vitabu usiku kucha katika duka la vitabu la Sanlian."

    "Kupitia simu za mkononi, marafiki walinitumia habari hiyo, nataka kusoma usiku kucha leo."

    "Nilisoma habari kwenye tovuti ya Internet, nitasoma vitabu hadi saa kumi na moja au kumi na mbili. Mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu, kesho asubuhi nitaenda darasani moja kwa moja."

    Kutokana na kuongea na wateja hao, naona wengi wanapata habari kuhusu duka hilo la vitabu kufunguliwa saa 24 kupitia Internet, inamaanisha kuwa vijana wanaozoea kupata habari kupitia Internet bado wana mahitaji ya kusoma vitabu vya karatasi. Katika enzi ya Internet kubadili mtindo wa kusoma vitabu na njia ya kununua kitu, duka la vitabu pia linakabiliwa na changamoto kubwa. Naibu meneja wa duka hilo Bibi Wang aliniambia kuwa, katika kipindi kigumu zaidi, duka hilo la vitabu lilikuwa na faida ya dola elfu 7 tu za kimarekani kwa mwaka. Na sasa kuwa wazi kwa saa 24 kumechochea kiu ya wasomaji ya kusoma vitabu, pia kunaongeza mauzo ya vitabu. Mwaka jana, thamani ya biashara ya duka hilo iliongezeka hadi kufikia dola milioni 3.2 hivi za kimarekani, na kuleta ongezeko kubwa la faida. Bibi Wang anasema,

    "Tunatakiwa kuchukua msimamo wenye uvumilivu kwa wasomaji, ili kuwavutia wasomaji wengi zaidi. Kwangu mimi, hali ya duka la vitabu haitakuwa duni, itakuwa na nguvu zaidi."

    Aprili 23 mwaka huu, duka la vitabu la Sanlian lilifungua tawi katika sehemu ya Haidian ambayo ni maarufu kwa kuwa na vyuo vikuu vingi jijini Beijing.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako