• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Juhudi za kupambana na ugonjwa wa fistula

    (GMT+08:00) 2015-05-25 09:10:41

    Kwa lugha ya kitalaamu ugonjwa huu hujulikana kama Peri-anal fistula. Ni tatizo la kuwapo kwa tundu au matundu karibu na njia ya haja kubwa. Tundu hilo huwa na mfereji unaojitokeza katika njia ya haja kubwa kwa ndani na hupitisha choo kikubwa bila ya mgonjwa kujitambua au kufahamu. Tatizo hili linatokea wakati mwanamke anapojifungua na linakuwa katika misuli kati ya uke na kibofu cha mkojo au kati ya uke na njia ya haja kubwa au vyote viwili. Ingawa huwakumba zaidi wanawake lakini badhi ya wakati hata wanaume pia nao huugua.

    Kutokana na kukithiri kwa ugonjwa huu tarehe 23 Mei imepangwa kuwa ni siku ya kimataifa ya kutokomeza fistula. Wanawake wengi wanatakiwa kufahamu kuwa huu ni ugonjwa unaotibika hivyo hakuna haja tena ya wanawake kuona dunia imewaelemea endapo watasumbuliwa na ugonjwa huu, ama kujihisi aibu katika jamii. Pia fistula siyo tatizo pekee miongoni mwa kinamama wanaojifungua wakiwa na umri mdogo, bali pia kwa akina mama wenye umri zaidi ya miaka 40, na mara nyingi familia maskini zinaathirika zaidi kutokana na ukosefu wa lishe bora, huduma za afya na taarifa muhimu za afya.

    Kwa mujibu wa takwimu wanawake wapatao milioni 2 hadi 3.5 wanaugua ugonjwa huu katika nchi zinazoendelea, kila mwaka kesi mpya zipatazo elfu 50 hadi laki mwaka zinaripotiwa kwa mwaka. Kwa vile wanawake wa nchi nyingi zinazoendelea ndio wanaosumbuliwa zaidi na ugonjwa huu, shirika la UNFPA pamoja na washirika wake walianzisha kampeni ya kutokomeza fistula mwaka 2003, na sasa kampeni hiyo ipo katika nchi za 50 duniani zikiwemo za Afrika, Asia na za Kiarabu.

    Kama tulivyosema kuwa nchi zinazoendelea ndio waathirika wakubwa wa ugonjwa huu, kule nchini Kenya pia hali sio nzuri kwa kina mama wengi hasa wakati wanapojifungua na hapa tunaye Daktari wa Fistula kutoka Hospitali ya Kenyatta Bibi Nelly Bosire alisema kina mama wengi wanaamua kukaa kimya na kutozungumzia ugonjwa huo kwani wengi wao wanajihisi wanabaguliwa, kudharauliwa na hata kulaumiwa na jamii kutokana na harufu mbaya inayotoka kwenye mkojo na kinyesi chao.

    Hata hivyo mara nyingi sana tumekuwa tukisisitiza kuwa kama kuna tatizo lolote katika jamii iwe kwa mwanamke au mwanamme ni lazima lizungumziwe kwani tuna msemo usemao mficha maradhi kifo humuumbua. Kwa hiyo ingawa wanawake wanaona haya au wanaona tabu kuyazungumzia haya maradhi kwa watu kutokana na uhalisia wa ugonjwa wenyewe ni vyema sasa wanawake wakabadilisha mawazo na kuanza kuelimishana kwani tukiendelea kukaa kimya ndio tatizo litakapokuwa kubwa zaidi katika jamii.

    Kama tulivyosema awali kuwa huu ni ugonjwa unaotibika kabisa. Kupatwa na fistula haimaanishi ndiyo kuteseka maisha yote, fistula inaweza kutibiwa kwa upasuaji, hata ikiwa miezi au miaka kadhaa baada ya kutokea na dalili nyingi au zote zinaweza kuondolewa na mama kurejea katika hali yake ya kawaida. Lakini tatizo hili kama likikaa muda mrefu linaleta athari gani kwa mama.

    Haya wanawake wenzetu mmewasikia wanawake mbalimbali waliokuwa wakitoa ushuhuda kuhusu ugonjwa huu wa Fistula na wengi wao walikuwa ni wagonjwa wa muda mrefu na sasa wameshapona. Hivyo wale wenye mawazo kuwa haya ni maradhi yasiyotibika waondoe kabisa mawazo hayo na waende hospitali kuonana na madaktari.


    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako