• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mkulima anavyoanzisha biashara yake ya chai

    (GMT+08:00) 2015-05-26 14:06:25

    Wilaya ya Shitai iko katika sehemu ya kusini mwa mkoa wa Anhui, mashariki mwa China. Eneo kubwa la wilaya hiyo ni la milima, na misitu imechukua asilimia 80 ya ardhi yote. Hali ya kijiografia inayobadilika badilika kwenye milima mingi imeweka mazingira ya kuwepo kwa maliasili za aina mbalimbali, lakini kwa kiasi imekwamisha maendeleo ya kilimo, kwa hiyo Shitai imeorodheshwa kuwa wilaya maskini ya ngazi ya taifa nchini China. Chanzo kikuu cha mapato ya wakulima wa Shitai ni kilimo cha chai, na wakulima wengi wanalima au kuuza chai walizolima na kutengeneza, ama kuuza majani ya chai kwa viwanda vya chai.

    Chen Weiwu alikuwa mkulima wa chai, ana moyo wa ujasiri, haogopi taabu. Kutokana na bidii zake alianzisha kampuni ya chai ya Xihuangshan baada ya kulima na kutengeneza chai kwa miaka mingi. Kampuni yake pia imetoa fursa kwa wakulima wengine wa chai wa wilaya hiyo kuongeza pato lao. Kutokana na fikra ya uvumbuzi na msimamo wa kuendesha biashara kwa uaminifu na bidii, kampuni ya Xihuangshan imejulikana sana miongoni mwa viwanda zaidi ya elfu moja wilayani Shitai.

    Jina la Kampuni ya Xihuangshan linatokana na mlima wenye mandhari nzuri wa Guniujiang ambao zamani uliitwa Xihuangshan. Mlima Guniujiang upo katika eneo la mpaka kati ya wilaya ya Shitai na Qimen, ni mmoja kati ya milima mitatu iliyopo kusini mwa mkoa wa Anhui, na pia ni msitu wa asili unaohifadhiwa vizuri katika mikoa ya Anhui, Jiangxi, Zhejiang na Jiangsu ambayo ipo mashariki mwa China. Wastani wa urefu wa eneo la mlima Guniujiang ni mkubwa, na tofauti ya halijoto kati ya usiku na mchana ni kubwa, hii imetoa mazingira mazuri kwa ajili ya ukuaji mzuri wa majani ya chai. Chai zilizotengenezwa na Kampuni ya Xihuangshan zote zilitoka katika eneo hilo. Akieleza sababu ya kuchagua majani ya chai yanayokulia katika eneo hilo, Chen Weiwu anasema,

    "Anhui ni mkoa unaojulikana kwa chai bora, na kati ya chai maarufu kumi za jadi nchini China, nne zinatoka mkoani humo. Chai maarufu na mazingira ya kijiografia ya Anhui vinahusiana sana. Watu wanasema chai bora inapatikana katika mlima. Chai ya Shitai ni maarufu kati ya chai mkoani Anhui. Mbali na hali nzuri ya asili, Guniujiang iko katika digrii 30 kaskazini ya Ikweta. Vilevile, Shitai ni eneo pekee lenye utajiri mkubwa wa Selenium mkoani Anhui, na chai ya hapa ina Selenium ya asili. Hii ni sifa pekee ya majani ya chai ya Shitai yakilinganishwa na majani ya chai ya sehemu nyingine."

    Maliasili za kimaumbele za kipekee zilizopo Guniujiang zimeongeza thamani ya chai, lakini katika nyanda za juu wakulima wanakabiliana na ugumu katika kupanda miche ya chai katika eneo kubwa. Tofauti na mashamba makubwa ya chai katika sehemu nyingine, miti ya chai inaonekana katika miteremko mikubwa na midogo wilayani Shitai. Mbali na miti ya chai inayopandwa na wakulima, pia kuna chai nyingi inayomea porini. Ni nadra kuona mashamba makubwa ya chai katika wilaya ya Shitai. Kwa muda mrefu, familia zinazoishi Shitai zinachuma, kutengeneza, na kuuza chai wao wenyewe. Chen Weiwu aliyekuwa mkulima wa chai alisimulia kazi za kuvuja jasho alizofanya katika uzalishaji na uuzaji wa chai kabla ya kuanzisha kampuni ya chai.

    "Katika miaka ya 70, wakati China ilipoanza kufanya mageuzi na kufungua mlango nje, nilibeba kikapu na kuuza chai. Kila siku, wazazi na dada walienda kuchuma majani ya chai na kutengeneza, na siku inayofuata, asubuhi nilipanda baiskeli na kuuza chai katikati ya wilaya. Wakati ule, wakulima wa chai walimimilika katika mitaa yote kuuza chai zao. Katika wilaya ya Shitai, kuna wakulima karibu elfu 80 wa chai, na kila siku walienda katikati ya wilaya yetu na kila familia ilibeba kilo moja au mbili za chai."

    Mtindo wa kuuza chai wao wenyewe baada ya kutengeneza uliwalazimisha wakulima wa chai kufanya kazi kwa kufuata utaratibu mzima, tangu kuchuma, kutengeneza na hadi kuuza chai. Hii sio tu inahitaji muda na jasho lao, lakini kipato pia hakilingani na malipo. Chen Weiwu aligundua dosari ya mtindo huo, na kuanza kutafuta ufumbuzi. Alianzisha kampuni ya Xihuangshan, na kuunda mtindo mpya wa biashara wa kuunganisha nguvu za kampuni, mashamba ya chai na wakulima, ambao umewakomboa wakulima wa huko kutoka kazi kubwa za kutengeneza chai, na kuongeza kipato chao kwa kiasi kikubwa. Afisa wa idara ya utangazaji ya wilaya ya Shitai Chen Chao anasema,

    "Zamani wakulima walipata kipato kidogo kwa kutengeneza na kuuza chai wao wenyewe. Lakini kwa kufanya ushirikiano na kampuni hiyo, kipato chao kimeongezeka, huku kazi wanazofanya zikiwa zinapungua kwa kuwa thamani ya chai imeongezeka kupitia mauzo ya jumla."

    Wakulima wanaweza kusaini mkataba na kampuni ya Xihuangshan, na kujiunga na mashamba makubwa ya chai kwa njia ya ushirika wa kilimo. Mashamba ya chai yanapaswa kufuata kwa makini kanuni za kampuni katika kupanda miche ya chai na kuchuma majani ya chai, ili kuhakikisha ubora wa chai. Kazi zinazofanywa kila siku na wakulima wa chai ni kusafirisha majani ya chai wanayochuma kwenye kituo maalumu cha manunuzi cha kampuni hiyo. Mbali na kipato kinachotokana na uuzaji wa majani ya chai, ifikapo mwishoni mwa kila mwaka, wakulima wa chai wanaofanya ushirikiano na kampuni pia wanaweza kupata faida ya ziada kutoka kampuni hiyo kwa mujibu wa kiasi cha majani ya chai wanayochuma katika mwaka mzima na ukubwa wa mashamba ya chai waliyo nayo. Katika siku zilizopita kulikuwa na wakulima elfu 2 waliouza chai waliyolima katika tarafa ya Dayan, wilaya ya Shitai, lakini sasa karibu wakulima hao wote wamejiunga na kampuni hiyo, na wakulima wengine 30 wanaendelea na mtindo wa jadi wa kufanya biashara. Hivi sasa eneo mashamba ya chai ya kampuni ya Xihuangshan limefikia hekta zaidi ya 350.

    Hata hivyo ongezeko la wakulima wanaotaka kujiunga na eneo la chai limeipa kampuni ya Xihuangshan changamoto kubwa. Tofauti na kampuni nyingine zinazojitahidi kupanua biashara zao, Chen Weiwu ana msimamo wake wa kuendesha biashara ambao unatilia maanani hatua madhubuti katika kuendeleza mashamba ya chai.

    "Tunaendeleza biashara yetu kwa hatua madhubuti. Tunapenda kufanya vizuri mashamba ya chai tuliyo nayo, na hatutarajii kupanua ukubwa kwa kasi. Tunafuatilia njia za usambazaji na ujenzi wa chapa, bado kuna safari ndefu."

    Mtindo mpya wa kununua chai kutoka kwa wakulima wa chai umeongeza utoaji wa majani mabichi ya chai. Ili kufanya utengenezaji ulingane na kasi hiyo, Chen Weiwu alitumia Yuan milioni mbili kununua mashine mbalimbali za kisasa za kutengeneza chai, na kuongeza ufanisi wa uzalishaji wa chai.

    Matumizi ya mashine yamesababisha njia za jadi za kutengeneza chai kusahauliwa na watu. Chen Weiwu alitoa mtindo mpya wa utengeneza wa chai na kufanya biashara, na ameunganisha mbinu za jadi na za kisasa za kutengeneza chai. Kampuni ya Xihuangshan inaendeleza kwa pamoja mashamba ya chai, utengenezaji wa chai na shughuli za burudani. Watalii wanaposafiri katika wilaya ya Shitai wanaweza kutembelea mashamba hayo huku wakijifunza mbinu za jadi za kuchuma majani ya chai na kutengeneza chai.

    "Utamaduni wa jadi wa chai wa China na mbinu za zamani za kutengeneza chai vina umaalumu wake. Mambo mazuri ya zamani yanapaswa kuhifadhiwa. Tunafanya juhudi kuunganisha shughuli za utalii na utengenezaji wa chai, watalii wenyewe wanaweza kuchuma majani ya chai na kutengenezaji chai, mbinu zote za jadi zinarejeshwa, isipokuwa ugumu wa kazi hiyo umepungua, kwani zamani ilikuwa ni kazi nguvu sana inayohitaji nguvukazi kubwa na jasho jingi."

    Mbali na mashine ya kisasa, kampuni ya Xihuangshan inayoongozwa na Chen Weiwu inaongoza katika teknolojia ya habari ya kilimo kuliko kampuni nyingine za chai wilayani humo. Vifaa vya CCTV vya kulinda usalama kwa njia ya video vimewekwa katika mashamba ya chai na viwanda vya kutengeneza chai, na wasimamizi wanaweza kufuatilia ukuaji wa majani ya chai na utengenezaji katika viwanda vya chai kwa njia ya kompyuta na simu za mkononi.

    Akizungumzia matarajio yake kuhusu kampuni yake katika siku za baadaye, Chen Weiwu anasema

    "Baada ya chapa ya chai yetu kujulikana na njia za usambazaji kupanuliwa, natarajia kufanya ushirikiano na viwanda vidogo vidogo vya chai katika wilaya ya Shitai, ambavyo utengezaji wao ni mzuri."

    Hivi sasa, kampuni ya Xihuangshan imefungua maduka yake nje ya wilaya ya Shitai, na pia kuuza chai yao kwenye mtandao wa internet. Ingawa biashara ya kampuni hiyo inaongezeka siku hadi siku, lakini tabasamu ya dhati aliyoonesha Chen Weiwu bado haijabadilika. Lengo lake la siku za baadaye ni kufanya kampuni yake kuwa chapa maarufu ya chai ya Anhui, nchini China, na kuwawezesha wakulima wenzake kutajirika, na kufanya harufu nzuri ya chai ya Guniujiang isikike sehemu zote nchini China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako