• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Rais Kenyatta akagua ujenzi wa reli

    (GMT+08:00) 2015-05-27 11:09:47

    Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta jana alasiri alikagua ujenzi wa mradi wa reli ya geji ya wastani katika eneo la mbuga ya wanyama ya Tsavo,mjini Voi,katika kaunti ya Taita Taveta.

    Katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Balozi wa China nchini Kenya Bw.Liu Xianfa ,Rais Kenyatta aliandamana na Naibu wake William Ruto ambapo walionyeshwa jinsi ujenzi huo unavyoendelea,huku wakandarasi wa ujenzi huo ambao ni kampuni ya China ya CRBC ikiwa inaendelea kujenga daraja refu lenye umbali wa mita 1987.69 katika mbuga ya wanyama ya Tsavo ambapo treni itapitia ili kurahisisha uvukaji huru wa wanyama mbugani.

    Mwandishi wetu Khamis Darwesh ametuandalia ripoti ifuatayo kutoka mji wa Voi nchini Kenya

    Akizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi katika daraja la Tsavo,Rais Uhuru Kenyatta amesema ujenzi wa reli hii utafungua fursa nyingi kwa nchi ya Kenya na nchi jirani.

    Kenyatta amesema mradi huu hautanufaisha tu wale wanaoishi maeneo ambayo mradi huo unapitia bali kila sehemu ya nchi.

    "Tunaamini ya kwamba huu mradi utakuwa wa manufaa kwa wakenya wote.Huu mradi utatusaidia sisi kama wakenya kupunguza bei za bidhaa mbalimbali kwa sababu tutapunguza gharama za usafirishaji.Mradi huu utawezesha maeneo kama hapa Taita Taveta ambako kuna madini kuweza kusafirisha madini kwa kutumia treni"

    Aidha Rais Kenyatta aliwapongeza viongozi wote pamoja na serikali ya China kwa kuwaunga mkono katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi ya reli.

    Wakati huohuo Naibu Rais William Ruto alisema reli inayojengwa sasa na kampuni ya China ya CRBC itaongeza wepesi wa kubeba mizigo na watu kwa asilimia 50.

    Naibu Rais William Ruto aidha alisema kufikia mwaka 2017 ujenzi wa reli hiyo utamalizika na treni kuanza kubeba abiria na mizigo.

    Ruto alisema reli hii itasaidia pakubwa katika kuongeza mapato na kupanua biashara na uchumi wa nchi ya Kenya.

    "Itawawezesha wakenya kulipa gharama ya chini ya usafirishaji wa mizigo pamoja na abiria.Hiyo itachangia pakubwa kuhakikisha ya kwamba mali inayotoka nje ya Kenya na zile tunazokuza humu nchini ambazo zinasafirishwa kwenda nchi nyingine tutalipa gharama ya chini,tutangeza mapato kwa wakulima wetu,na biashara itapanuka pamoja na uchumi wa taifa letu la Kenya"

    Balozi wa China nchini Kenya Bw.Liu Xianfa amesema China iko mstari wa mbele katika kuimarisha uhusiano wake na nchi ya Kenya.

    Alisema mbali na ujenzi wa reli hii unaotekelezwa na kampuni ya China ya CRBC wenyeji wa Kenya wananufaika kwa nafasi za ajira na pia kupata fursa ya mafunzo kuhusu utaalamu wa uhandisi hasa kuhusu ujenzi wa reli kutoka kwa wahandisi wa China wanaojenga reli hiyo.

    "Nahisi faraja sana kwamba kila wakati tunaona wakenya wengi zaidi hasa vijana na wanawake wakihusika katika ujenzi wa reli hii.Kuna vijana wengi na wanawake ambao wanafanya kazi na wahandisi wa China na kufunzwa kuhusu teknolojia za ujenzi wa reli.Naamini ushirikiano wa aina sio tu kwamba utaimarisha mradi huu bali pia utachukua fursa nzuri katika kuimarisha taaluma ya wakenya na waafrika katika teknolojia ya ujenzi wa reli na kukuza uchumi wa Kenya na Afrika"

    Bw Xianfa alisema wajenzi wa China wanajali sana mazingira na uhifadhi wa wanyamapori ndiposa wakajenga daraja kubwa na refu ili kurahisisha uvukaji huru wa wanyama mbugani,bila kujali gharama kubwa za ujenzi wa daraja hilo.

    Kwa upande wake Rais wa kampuni ya CRBC Bw Lu Shan amesema kampuni ya CRBC inatilia maanani ubora katika ujenzi wa mradi huo.

    "Kampuni ya CRBC inajali sana kuhusu ubora.Tuna mifumo mitatu ya uangalizi wa ubora,tuna kituo kikuu cha uhandisi na vingine 17 vidogo. Tunakagua ubora wa mradi huu mara kwa mara ili kuhakikisha ubora unaohitajika bila matatizo yoyote"

    Tangu kuanza kwa ujenzi wa mradi huu,wakenya wengi wamepata fursa za ajira.Kufikia sasa wakenya 10,889 wanahusika moja kwa moja katika ujenzi wa mradi huu,huku wengine 4,000 wakihusika japo sio moja kwa moja kama vile maajenti wa usafirishaji.

    Kampuni ya CRBC ina mipango ya kuwapatia mafunzo wafanyakazi wa kikenya kuhusu teknolojia ya reli na uendeshaji ambao watasaidia wakati wa ujenzi na pia reli hiyo itakapoanza shughuli.

    Mradi huu utakapokamilika,treni za abiria zitaenda kwa kasi ya kilomita 120 kwa saa huku treni za mizigo zikienda kwa kasi ya kilomita 80 kwa saa.Hii itapunguza muda wa kusafiri kati ya Mombasa na Nairobi hadi masaa manne na nusu kwa treni za abiria na masaa manane kwa treni za mizigo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako