• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na FAO inaonesha kuwa lengo la kutokomeza njaa linakaribia kufikiwa

    (GMT+08:00) 2015-05-28 11:33:09

    Ripoti kuhusu hali ya usalama wa chakula kwa mwaka huu iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, inaonesha kuwa idadi ya watu wanaokabiliwa na upungufu wa chakula imepungua hadi watu milioni 800 kutoka watu bilioni 1 kati ya mwaka 1990-1992, na kutarajiwa kufikia watu milioni 795 kati ya mwaka 2014-2016. Na idadi ya watu wanaokosa lishe bora duniani imepungua kwa asilimia 45.5 kutoka asilimia 18.6 hadi asilimia 10.9, na kwenye nchi zinazoendelea kutoka asilimia 23.3 hadi asilimia 12.9. Xie Yi anatueleza zaidi kuhusu yaliyomo kwenye ripoti hiyo.

    Takwimu zilizopo kwenye ripoti hiyo iliyotolewa mjini Roma kwenye mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa kwa pamoja na FAO, Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo IFAD na Shirika la Mpango wa Chakula WFP, zimeleta hali ya matumaini kwa maofisa wa Umoja wa Mataifa. Mkurugenzi Mkuu wa FAO Bw Jose Graziano Da Silva amesema kukaribia kutimiza lengo la maendeleo la milenia kwenye kupunguza njaa, kunaonesha kuwa sio tu njaa inaweza kupunguzwa bali inaweza kutokomezwa katika kizazi chetu.

    Katika nchi zilizochunguzwa na FAO imeonekana kuwa ni nchi 72 pekee kati ya nchi 129 zilizoweza kutimiza lengo la kupunguza njaa kwa nusu kama ilivyoagizwa kwenye malengo ya maendeleo ya milenia, kwa nchi zinazoendelea zilishindwa kidogo tu kutimiza lengo hilo.

    Ripoti imezitaja nchi zenye idadi kubwa ya watu, yaani China na India, kuwa zimetoa mchango mkubwa katika kupunguza njaa kati ya nchi zinazoendelea. Mkurugenzi Mkuu msaidizi wa FAO anayeshughulikia mambo ya uchumi na maendeleo ya jamii Bw Jomo Sundaram amesema nchi hizo mbili zimechangia zaidi ya nne ya tano ya kupungua kwa njaa duniani.

    Hata hivyo ripoti hiyo imeonesha kuwa eneo la Afrika kusini mwa Sahara bado linaendelea kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa chakula, kwani watu milioni 220 wanaoishi katika eneo hilo hawapati chakula cha kutosha. Nchi 24 za Afrika kwa sasa zinakabiliwa na msukosuko wa chakula, idadi ambayo ni mara mbili kuliko ya mwaka 1990. Bw Sundaram ameshauri kuwepo kwa sera zinazowawezesha wakulima wadogo kwenye nchi zinazoendelea kuongeza usalama wa chakula.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako