• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Sanaa ya michoro ya Tingatinga yahitaji kutangazwa zaidi ili kupanua soko lake duniani

    (GMT+08:00) 2015-06-03 14:14:18

    Michoro ya tingatinga ni sanaa iliyoanzishwa nchini Tanzania ambayo inajulikana kwa mitindo yake maalumu ya kiafrika. Jina la sanaa ya 'Tingatinga' linatokana na mwanzilishi wake Bw. Tingatinga Edward Saidi. Msanii huyo kutoka kabila la Wamakua aliyeishi mkoani Tanga, Tanzania aliwahi kuwa mfanyakazi wa kukata mkonge, kwa sababu hakuridhika na kazi hii ya sulubu na yenye mshahara mdogo, katika miaka ya 60 ya karne iliyopita, aliondoka maskani yake na kwenda Dar es Salaam ambako aliajiriwa na kuwa mlinzi wa nyumba. Na kuanzia hapo, alianza kujifunza kuchora mwenyewe kwa kutumia mafuta ya kawaida, na polepole aliendeleza mtindo wake maalumu. Baada ya kufariki katika ajali, wachoraji wengi wa kizazi baada ya kizazi walirithi mtindo wake na baadaye kuufanya kuwa sanaa ya kipekee inayojulikana sasa kama Tingatinga.

    Michoro ya Tingatinga huchorwa kwa kutumia rangi mbalimbali ang'avu zinazovutia macho, kutokana na wasanii wa Afrika kuwa na upendeleo huo maalumu wa rangi, Tingatinga inachukuliwa kuwa ni moja ya sanaa zinazowakilisha mitindo ya uchoraji ya kiafrika.

    Mwanzoni michoro ya tingatinga ilichorwa kwenye ubao mwepesi au gamba gumu, vifaa hivyo vinaweza kukaa kwa muda mrefu sana bila kupoteza rangi zake. Katika miaka ya hivi karibuni baadhi ya wasanii wameanza kuchora kwenye vitambaa.

    Bw. Mohamed Said Chiramboni na Bw. Suedi Thabiti Mchisa ni wasanii wa Tingatinga walieleza kuhusu sanaa ya Tingatinga na maendeleo yake ya sasa.

    Tingatinga ni sanaa ambayo sio maarufu sana kwa wachina. Mwaka 2012 maonesho ya Tingatinga yalifanyika katika miji kadhaa nchini China, na yalikuwa ni miongoni mwa fursa chache kwa Wachina kufahamu kwa karibu sanaa hiyo kutoka bara la Afrika.

    Pro. Jiang Fu ambaye ni mtazamaji wa maonesho hayo alisema anavutiwa sana na picha za Tingatinga. Yeye aliwahi kufanya kazi katika TAZARA na kuishi nchini Tanzania kwa miaka 5.

    Ni mara ya kwanza kwa watazamaji wengi wa China kupata fursa ya kutazama michoro ya Tingatinga kwenye jumba la maonyesho ya sanaa, ufahamu wao wa awali kuhusu sanaa hiyo unatokana na vyombo vya habari au mtandao wa Internet.

    Lakini ni kitu gani kilichomo katika michora ya Tingatinga ambacho kinawavutia zaidi watazamaji wa China? Watazamaji wanasema ni mtindo maalumu wa sanaa hiyo. Wachoraji wa Tingatinga hutumia rangi mbalimbali nzito zinazong'aa. Bw. Yue Longshan alisema amevutiwa.

    Michoro ya Tingatinga ya Tanzania ina tofauti gani na michoro ya mtindo wa kichina? Bw. Mohamed Said Chiramboni anasema, tofauti ya kwanza ni rangi, michoro ya Tingtinga ya Tanzania huchorwa kwa kutumia rangi za mafuta, huku michiro ya kichina ikichorwa kwa kutumia rangi za maji.

    Ingawa watu wa China wanapenda michoro ya Tingatinga, lakini soko la sanaa hiyo nchini China bado halijastawi. Katika maduka ya vitu vya sanaa za Afrika tuliyotembelea mjini Beijing hatukuona duka hata moja linalouza michoro ya Tingatinga. Lakini kwenye mtandao wa Internet, tuliona duka moja linalouza vitu kutoka Afrika, moja ya vitu hivyo ni michoro ya Tingatinga. Tulipowasiliana na mwenye duka hilo, alisema kuna wateja wengi wanaonunua vinyago, lakini walionunua michoro ya Tingatinga bado ni wachache.

    Hali hiyo haiko hapa China tu, hata katika nchi za Ulaya, Marekani na Japan, hali ya soko la michoro ya Tingatinga ni sawa sawa na hapa China. Bw. Mohamed Said Chiramboni alisema bado hakujawa na soko la uhakika.

    Hata nchini Tanzania, michoro ya Tingatinga inapendwa na watu, lakini wenyeji wengi hawanunui michoro hiyo kutokana na kuuzwa kwa bei kubwa.

    Thamani ya michoro ya Tingatinga bado haijatambuliwa duniani kwa kuwa sanaa hiyo ina historia fupi, ambayo ilianzishwa miaka 50 tu iliyopita. Ili kustawisha soko la sanaa hiyo duniani, ni lazima michoro hiyo itangazwe zaidi.

    Ni kweli kwamba juhudi kubwa zaidi zinatakiwa kufanywa kuitangaza sanaa ya Tingatinga na kupanua soko lake duniani, na kuandaa maonesho ya michoro ni njia moja nzuri ya kuitangaza sanaa hiyo. Jumanne wiki hii, maonesho ya sanaa ya Tingatinga yalifunguliwa huko Dar es Salaam, mwandishi wetu wa habari alikwenda kwenye maonesho hayo, na sasa tusikilize ripoti aliyotuandalia kuhusu maonesho hayo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako