• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kipindi maalum cha pili kuhusu Siku ya Albino ya Kimataifa--Familia maalum katika mji wa kale nchini China

    (GMT+08:00) 2015-07-24 11:04:53


    Wiki iliyopita tulikuletea sehemu ya kwanza ya mfululizo wa vipindi vitatu kuhusu Siku ya Kimataifa ya Albino, na tulizungumzia zaidi changamoto wanazokumbana nazo Albino barani Afrika, hususan nchini Tanzania na Kenya. Leo hii tunaendelea na sehemu ya pili, na kama tulivyowaahidi, tutazungumzia changamoto wanazokutana nazo Albino hapa China. Tulitembelea familia za albino na shirika lisilo la kiserikali linaloitwa "familia ya watoto wa mwezi" katika mji wa kale wa China, Xi'an, tukaelewa hali ya maisha, kazi na masomo yao. Na tunakuletea sehemu ya kwanza ambayo tunaiita "familia maalum katika mji wa kale nchini China".

    Ugonjwa wa albino sio mgeni kwa watu wengi nchini China, kwani vitabu vya baiolojia katika shule za sekondari vinafahamisha ugonjwa huo wa kurithi. Lakini watu wengi wana elimu husika kutokana na vitabu hivyo vya masomo tu, hawana elimu ya kina zaidi.

    "Albino sio wengi, naona mmoja wawili tu. Nasikia mababu zao walikuwa ni watu wa asili katika sehemu zao."

    "Sina ufahamu mwingi juu ya albino. Najua uko kwenye ukoo. Sijui ni sawa au la."

    "Wana nywele nyeupe, hawawezi kuvumilia mwanga, ila huu sio ugonjwa na hauambukizwi, bali ni tatizo la kurithi. Tukiwaona albino, haifai kuwaepuka. Nilipowaona watu hao, niliwahurumia sana"

    Albino sio ugonjwa, bali ni tatizo la kurithi, hakuna rangi ya asili katika retina zao, mboni za macho yao ni rangi ya pinki isiyokolea, wanaogopa mwanga mkali wa jua. Ngozi, nyusi, na nywele zao zinaonekana rangi ya nyeupe au manjani yenye mchanganyiko na nyeupe. Albino sio ugonjwa hivyo hautibiki. Takwimu zinaonesha kuwa, kati ya watu elfu 20, mmoja ni albino. Kutokana na kiwango hiki, kuna albino kati ya elfu 60 hadi 70 nchini China.

    "Familia ya watoto wa mwezi" ilianzishwa mwaka 2008 katika mji wa kale wa Xi'an mkoani Shangxi, ili kutoa habari na ushauri husika kwa albino pamoja na familia zao, na kuwasadia wawe na imani, kujitahidi kuweka mazingira yenye usawa katika jamii kwa watu hao kwa kupitia matangazo kwa jamii,. Wengi wa waanzilishi ni familia hiyo ni albino. Shirikishi hilo ni moja ya mashirikisho makubwa zaidi na yaliyoanzishwa mapema yanayolenga kuwasaidia albino nchini China. Sasa, hadithi yetu inaanzia kwa mwanzilishi wake Guan Lu. Guan vilevile ni albino, ana miaka 35 sasa, alipozungumzia masomo na maisha ya utotoni, anaona hakuna tofauti kubwa kati yake na watoto wengine.

    "Kila mara nilikuwa wa mwisho kwenye matukio. Nakumbuka nilipokuwa mtoto nilikuwa huru, bila wasiwasi wowote, sina maoni mengine. Labda nilijua kila mtu ameumbwa tofauti. Kama vile wimbo unavyoimba, watoto wana rangi tofauti za ngozi duniani. Pia nilikua hali ya kila mtu inatofautiana. Mimi ni mweupe zaidi, nahitaji kuvaa miwani ya jua"

    Familia ya Guan Lu ina watu watatu, ni familia ya kawaida na yenye furaha. Mke wake, Liu Ying sio albino, na anaunga mkono sana kazi ya mume wake katika "familia ya watoto wa mwezi". Lakini ndoa yake na Guan Lu ilikumbwa na vizuizi. Anatuambia maisha mazuri ya baraka ndiyo anayojitahidi kujipatia.

    "Tulijuana kama nusu mwaka hivi. Anadhani, usiku kucha anapata ndoto za kutisha – kuchelewa kufunga ndoa kunaweza kuleta matatizo, akataka tuoane. Lakini tulipozungumzia jambo hilo, baba yangu hakufurahi, kwa nini, baba yangu alisema 'haoni vizuri'. Lakini hakupinga uamuzi wetu, mama yangu alipinga na kusema sana, majirani na marafki zake wote walisema, msichana mzuri namna hii, anaweza kuolewa na mtu yoyote anayempenda. Lakini nilimwambia mama yangu, maisha yangu hayatafuata maneno ya wengine, bali nitaishi mimi mwenyewe."

    Liu Ying anasema, machoni mwake Guan Lu hana tofauti kubwa na wengine, yeye ni mtu wa kawaida kabisa.

    "Sasa hivi tulipotembelea barabarani alisema, 'ona, zamani ulinitunza, lakini sasa umeniacha.' Namwonea kama mtu wa kawaida, unaweza kuona au hauwezi, sijali, ufanye unalotakiwa kufanya."

    Bi. Liu pia alizungumzia dhana potofu na ubaguzi kutoka kwa watu wengine. Anasema mwanzoni hakuweza kuvumilia, lakini sasa anaweza kukabiliana na jambo hilo kirahisi.

    "Tulipooana, mwanzoni tulipata taabu sana. Wengine walisema, 'familia ya Guan ni tajiri sana. Unaolewa naye kwa ajili ya pesa?' nilisikitika sana. Mbali na hayo, tulipokwenda bustani, wengine hutupiga picha. Mume wangu haoni vizuri, hafahamu hili. Lakini niligeuka na kuona hilo. Wengine wanatupiga picha, na wengine wanatuzungumzia. Lakini baadaye nilizoea hali hiyo, ingawa mwanzoni nilisikitika."

    Lakini, ndoa ni hatua ya kwanza tu inayochunguza upendo wao, marafaki zao wengi wanawashawishi wafikiri mara mbili kabla ya kupata mtoto. Kwa sababu ingawa kuna uwezekano mkubwa mtoto wao atakuwa wa kawaida, lakini ataishi na jeni za albino. Bila kujali hali hiyo, Liu Ying ana uamuzi wake:

    "Mimi, niliona kuwa, 'bila kujali nini kitatokea, nitazaa mtoto.' Kwani mtoto wangu bila shaka ataishi na gene ya albino, na mtoto wake unapaswa kumwambia vilevile. Wenzangu waliniuliza kwa nini? Sikufikiri sana. Baba wa mtoto alisema, 'itakuwaje kama mtoto wetu ni albino?' Nilimjibu, 'hata kama ni albino, ni mtoto wangu, nitamtunza."

    Guan Lu alituambia lengo lake la mwanzo la kuanzisha "familia ya watoto wa mwezi", ambalo ni kuwafanya watu waweze kufahamu, kuelewa na kuwakubali albino kwa kupitia matangazo na mwongozo mwafaka, na vilevile kuinua hadhi ya Albino pamoja na familia zao katika jamii. Ili kufanikisha hilo, iliwabidi kuanzisha familia ya watu wa albino. Msichana Ma Longyan mwenye umri wa miaka 7 ni mwanachama mtoto katika "familia ya watoto wa mwezi". Baba yake anamona kama lulu kwenye kiganja cha mkono. Anakumbuka vizuri binti yake alivyozaliwa.

    "Alipozaliwa, nilikuwa na umri wa miaka 37, 38. Nilipenda sana kupata mtoto wa kike. Nilisubiri nje ya chumba cha kujifungua, mama yake alikuwa wa kwanza kuingia chumba hicho, lakini alikuwa humo ndani kwa muda mrefu. Baadaye muuguzi alitoka na kusema, 'mtoto wako ni wa kawaida, isipokuwa nywele zake ni nyeupe kidogo.'"

    Kuzaliwa kwa Longyan hakukuleta furaha kwa familia Ma, alipofikiri kwanza anatakiwa kukubali mwenyewe matokeo, kisha kuwaeleza ndugu zake, hapo kweli kichwa kilimuuma.

    "Sikujua nifanye nini. Nilikuwa nimekubaliana na mke wangu, mtoto wetu akifikia mwezi mmoja, tutawashukuru marafiki, viongozi na jamaa. Lakini katika mwezi wa kwanza baada ya kuzaliwa kwake, mama yake alilia mwezi mzima. Haikuwa rahisi kwetu kukubali hali hiyo, licha ya kuwaambia wengine. Na kwa wazazi wangu, sikujua niwaambie nini, ilikuwa ngumu kutumia maneno mwafaka. Mwisho nilimwambia mama yangu kuwa, 'ni mzuri sana, isipokuwa nywele zake sio nyeusi.' Wakati ule, hakujua maana ya 'sio nyeusi'."

    Lakini hali halisi haikuwa mbaya kama Ma alivyofikiri. Ma aliguswa sana na upendo wa bibi na babu kwa Longyan. Zaidi ya hayo, wazee hao wanafahamu kidogo kuhusu Albino:

    "Mama yangu ana upendo sana. Alipojua hali halisi alisema, 'hakuna shida, tuliwahi kuona Albino tulipokuwa wadogo. Maisha yake ya baadaye yatakuwa mazuri, na atakuwa mwalimu.' Ni wakarimu sana, hata wanakubali hali hiyo haraka zaidi kuliko sisi wazazi, na wanatufariji."

    Kuelewa na kuungwa mkono na familia, hii ndiyo inawafanya albino na watu wanaojitolea katika "familia ya watoto wa mwezi" kujisikia vizuri. Lakini bado watu wanawachukulia kama kituko, na watoto wengi albino mara kwa mara wanazuiwa kuingia shule, hali hii pia imemtokea Longyan.

    "Binti yangu alipokwenda chekechea, tulipata wakati mgumu sana. Kwanza tulijimwaandikisha katika likizo ya majira ya joto, lakini mpaka hadi masomo yanakaribia kuanza, hatukupewa taarifa yoyote. Nikaenda kwenye hiyo chekechea. Walimu walisema, nafasi zimejaa. Lakini ukweli ni kuwa, walifahamu hali ya binti wangu, na hawajawahi kupokea moto albino kabla ya hapo."

    Lakini mbingu hazikosi mlango wa kutokea. kwenye shule ya pili ya chekechea, Ma alikutana na mtu mwenye roho ya huruma.

    "Mkuu wa chekechea ya pili alikuwa na upendo sana. Aliwaambia walimu, wazazi na watoto hali yetu. Na mwishowe alimwandikisha mtoto wangu, na kumtunza vizuri. Alimbeba na kutembea naye katika madarasa mengine, na kumtambulisha kwa watoto wengine. Hivyo matangazo kuhusu watoto Albino kwa jamii kweli ni muhimu."

    Nchini China, ingawa albino sio kama wenzao barani Afrika, hawana wasiwasi juu ya usalama wao, lakini kutokana na uwezo mdogo wa kuona na sababu nyingine, wengi wao wanakosa fursa ya kupata elimu, hata wakiwa hawana elimu au wana elimu ndogo, inawabidi kufanya kazi kubwa zinazotumia nguvu nyingi. Na wale waliomaliza masomo yao wanakabiliwa na ubaguzi kazini, hawana nafasi ya kupanda daraja. Mwanzilishi wa "familia ya watoto wa mwezi" Guan Lu ana wasiwasi juu ya hali hiyo:

    "Sasa naona kwa upande wa Albino, taabu kubwa zaidi ni kupata ajira, yaani kuna ubaguzi maofisini. Kwa mfano ukiwa na shahada sawa na wengine na uwezo sawa na wengine, kampuni husika hatikuajiri"

    Kutokana na hali hiyo, "familia ya watoto wa mwezi" inatoa mwito kwa jamii nzima nchini China: kama familia yako au familia ya marafiki zako ina "mtoto wa mwezi" aliyezaliwa hivi karibuni, usimtenge wala kujali itakuwaje, wanaamini kuwa atakuwa na mustakabali mzuri. Kama ukikuta "mtoto wa mwezi" barabarani, tafadhali usimshangae, pia usimwogope, wana ngozi na nywele zenye rangi tofauti na wengine tu. Kama unashughulikia ajira katika kampuni, tafadhali usiwaache nje, wakikubwaliwa na kuaminiwa, wataleta mafanikio makubwa kwa matendo yao halisi. Tafadhali uonesha upendo wako, kuwapa anga yenye usawa na uhuru, kuweka mazingira yenye kujali na kuwamini, wao watatimiza thamani yao, kutoa mchango wao kwa jamii, na kuwa na maisha mazuri. Tunaamini, baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuamua tarehe 13 Juni kuwa Siku ya Kimataifa ya Albino, watu wengi zaidi watatoa elimu kwa jamii kuhusu albino, na "watoto wa mwezi" watapewa misaada mingi zaidi.

    Katika kipindi kijacho tutafuatilia kwa pamoja ustawi na maendeleo ya "watoto wa mwezi" wa China na Afrika, usikose. Msikilizaji mwisho tungependa kuwashukuru wasikilizaji wetu wote kwa kutusikiliza. Vilevile tungependa kupokea maoni yenu kuhusu kipindi hiki cha leo, na mnaweza kutuma maoni hayo kwa njia ya facebook anuani yetu ni www.facebook.com/kiswahilicri, au kwa njia ya simu namba yetu ni +8615611015572, pia unaweza kukutumia kwenye tovuti yetu, tunathamini michango na maoni yako. Ahsante na kwaheri.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako