• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  •  China na Afrika zasaidiana kiuchumi

    (GMT+08:00) 2015-06-17 17:01:04

     

    Mkutano wa Afrika wa baraza la uchumi duniani umefanyika tarehe 3 hadi tarehe 5 mwezi huu huko Cape Town, Afrika Kusini, ambapo wajumbe 1,250 kutoka sekta za biashara, siasa, taaluma na vyombo ya habari kutoka nchi 75 wamejadili fursa na changamoto zinazoukabili uchumi wa Afrika kwenye kipindi kipya. Ingawa mkutano huo ulihudhuriwa na waafrika ambao wamejadili masuala kuhusu Afrika, lakini pia umevutia wachina wengi, na baadhi yao wametoa hotuba kwenye mkutano huo. Kutokana na ongezeko la uchumi wa Afrika, kampuni nyingi zaidi za China zimeanzisha matawi yao barani Afrika, na soko kubwa la Afrika pia limetoa fursa mpya kwa uchumi wa China.

    Naibu mkurugenzi wa kampuni ya Huawei ya China Bw. Ding Shaohua alihutubia mkutano wa baraza la uchumi duniani kuhusu teknolojia za mawasiliano ya simu za mkononi barani Afrika. Kwenye hotuba hiyo, amependekeza kuwa kutokana na mazingira halisi ya sekta ya upashanaji habari na mawasiliano barani Afrika, nchi za Afrika zinapaswa kuongeza fedha kwenye ujenzi wa miundombinu husika, hasa broadband. Anasema,

    "Broadband inayounganisha mtandao wa Internet kwa kasi inaweza kuzisaidia serikali za nchi hizo kupata raslimali zinazohitajika, hivyo kufanikisha maendeleo na ustawi. Kwa kweli, matokeo ya uchunguzi uliofanywa na kampuni yetu ya Huawei yanaonesha kuwa, kila nyongeza ya asilimia 20 katika ujenzi wa miundombinu ya teknolojia za upashanaji wa habari na mawasiliano, pato la taifa litaongezeka kwa asilimia 1."

    Katika mwongo uliopita toka Huawei iingie kwenye soko la Afrika, kampuni hiyo imejenga zaidi ya nusu ya vituo vya wireless barani Afrika. Kutokana na hatua hii, gharama za mawasiliano ya simu zimepungua kwenye baadhi ya sehemu, na watu wa Afrika wamepata huduma nzuri za mawasiliano ya simu za mkononi.

    Mbali na ujenzi wa miundombinu ya upashanaji habari na mawasiliano, Afrika pia inahitaji sana kuboresha miundombinu inayohusika na maisha ya wananchi, kama vile reli, barabara, madaraja, na uzalishaji umeme kwa nguvu ya maji. Serikali na kampuni za China zimetoa fedha nyingi na nguvukazi kubwa katika mwongo uliopita katika miradi mbalimbali barani Afrika. Mjumbe maalumu wa serikali ya China kwenye mambo ya Afrika Bw. Zhong Jianhua amesema, utoaji mkubwa wa China katika ujenzi wa miundombinu barani Afrika ni umuhimu maalumu unaofanywa na China katika maendeleo ya Afrika. Amesema,

    "Uhusiano wa kiuchumi kati yetu na Afrika ni tofauti na uhusiano wa kiuchumi kati ya wakoloni na Afrika katika enzi za ukoloni, sisi tunafanya juhudi kubwa zaidi ili Afrika itimize utandawazi wa viwanda, pia tumetoa fedha nyingi zaidi ili Afrika iwe na miundombinu inayohitajika katika kipindi cha utandawazi wa viwanda."

    Umuhimu wa China kwa maendeleo ya Afrika unajulikana duniani. Mkurugenzi wa Mfuko wa Bill & Melinda Gates kuhusu miradi ya dunia Bw. Mark Suzman amesifu sana mchango uliotolewa na China kwa maendeleo ya kilimo barani Afrika. Anasema,

    "Nadhani katika miongo kadhaa iliyopita, China imekuwa ni mwenzi muhimu wa ushirikiano wa Afrika. China na Afrika zimefanya ushirikiano kwa pande nyingi, hasa kwenye sekta ya kilimo. Kwa kupitia vituo vya mfano vya kilimo, China imetoa ufundi wa kilimo cha kisasa na kuwaandaa watu wenye ujuzi kwa nchi za Afrika. Kampuni za China zimefanya utafiti na kutengeneza chanjo ya kuku nchini Ethiopia, na kueneza utaalam wa kilimo cha mpunga nchini Kenya, ujuzi wa kilimo wa China una mustakabali mzuri barani Afrika. China ni mfano wa mageuzi ya nguvu ya uzalishaji duniani, mageuzi ya kilimo nchini China yamehimiza ongezeko la uchumi, hii imetoa uzoefu kwa Afrika."

    Kwa mujibu wa Baraza la uchumi la dunia, katika miaka 25 iliyopita, kasi ya ongezeko la uchumi wa Afrika imezidi kiwango cha wastani cha ongezeko la uchumi wa dunia. Shirika la Fedha la Kimataifa IMF limekadiri kuwa, kati ya nchi kumi zilizo na kasi zaidi ya ongezeko la uchumi duniani mwaka 2015, nchi saba zitatoka barani Afrika, kusini mwa Sahara, na kasi ya ongezeko la uchumi wa kanda hiyo ni mara mbili kuliko kasi ya wastani ya ongezeko la uchumi wa dunia. Uchumi wa Afrika wenye ongezeko la kasi vilevile umetoa soko kubwa kwa kampuni za China. Maneja wa kampuni ya Huawei anayeshughulikia uhusiano wa umma kanda ya Afrika Kusini Mashariki Bw. Wang Shunli amesema, katika siku za baadaye soko la Afrika litakuwa muhimu zaidi kwa kampuni ya Huawei. Anasema,

    "Bara la Afrika lina watu zaidi ya bilioni moja. Kama uchumi wake unaongezeka kwa asilmia 4 hadi 5, baada ya miaka kumi, ukubwa wa uchumi wake utaongezeka zaidi, na idadi ya wateja itaongezeka zaidi, pia soko litaongezeka zaidi."

    Kampuni nyingi zaidi za China zimegundua soko kubwa barani Afrika, hivyo nazo zimetuma wawakilishi wao kwenye mkutano wa Afrika wa Baraza la uchumi la dunia, ambao wanataka kuelewa uchumi wa dunia na kutafuta wenzi wa ushirikiano. Mkurugenzi wa kampuni ya sayansi na teknolojia ya Phoenix Bw. Li Fan anayeshughulikia uuzaji wa dawa za kichina Magharibi mwa Afrika amehudhuria mkutano huo kwa miaka mitatu mfululizo. Amesema msimamo wa maofisa na wafanyabiashara aliokutana nao kwenye mkutano umeongeza imani yake ya kuwekeza barani Afrika. Anasema,

    "Tuko hapa, tunafanya biashara barani Afrika. Kama hatuelewi umaalumu wa siasa na uchumi hapa, hatuwezi kujua mwelekeo wetu katika siku za baadaye. Baada ya kuhudhuria mkutano huo mwezi Mei mwaka jana, tuliamua kuongeza uwekezaji wetu nchini Nigeria. Tatizo la maambukizi ya Ebola na uchaguzi mkuu wa Nigeria vimepita salama, na uamuzi wetu wa uwekezaji ni sahihi, tumepata ongezeko mara tatu hadi nne."

    Katika siku za baadae, huenda Afrika itachukua nafasi ya China na kuwa nguvu mpya ya kuhimiza ongezeko la uchumi wa dunia. Mjumbe maalumu wa serikali ya China kwenye mambo ya Afrika Bw. Zhong Jianhua amesema, kutokana na maendeleo ya kasi ya Afrika, katika siku za baadaye msaada utakaotolewa na Afrika kwa China utazidi msaada utakaotolewa na China kwa Afrika, na China inapaswa kutambua mwelekeo mpya wa maendeleo ya uhusiano kati ya pande hizo mbili. Anasema,

    "Kundi lolote la uchumi lina mahitaji makubwa zaidi katika mchakato wa maendeleo kutoka hali duni ya kimaendeleo hadi hali ya maendeleo ya katikati. Kutokana na kuongezeka kwa uchumi wa Afrika, ushirikiano wa uchumi kati ya China na Afrika utaimarishwa siku hadi siku. Zamani tuliisaidia Afrika, baadaye pande hizo mbili zimefanya ushirikiano wa usawa na kusaidiana, na katika siku za baadaye huenda Afrika itatoa msaada mkubwa zaidi kwa China. Labda mwelekeo huu utaonekana wazi baada ya miaka 40 au 50, lakini hautazuiliwa. Kama tukiweza kukubali mwelekeo huo, tutazoea na kurekebisha vizuri msimamo wetu kwa Afrika, halafu tutarekebisha sera na hatua kwa Afrika, hivyo tutatimiza hali ya kunufaishana na kupata maendeleo ya pamoja kama walivyopendekeza viongozi wetu."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako