• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Siku ya Baba Duniani

    (GMT+08:00) 2015-06-22 08:39:28

    Tarehe 8 Machi ni Siku ya Wanawake Duniani, na May 10 ilikuwa ni siku ya Mama. Sasa kina baba bao hawako nyuma, kwani tarehe 21 June ni Siku ya Baba. Kina baba nao wameona wasibaki nyuma bali wenyewe wawe na siku yao inayotambulika rasmi! Katika kipindi cha leo, tutazungumzia siku ya Baba, lakini kwa mtazamo wa tamthilia ya kichina ambayo imepata umaarufu mkubwa sana. Tamthilia hiyo inaitwa, 'Baba, tunaenda wapi?' Katika tamthilia hiyo, wakina baba ambao ni maarufu, wanaenda na watoto wao nje ya mji kwa muda wa siku tatu na kuwahudumia watoto hao peke yao, bila ya mama wa watoto kuwepo. Tamthilia hiyo inachekesha lakini pia kuna sehemu zinazosikitisha.

    Ni wazi kuwa kina baba wengi wanashughulikia kazi zao na hivyo kuwa na muda mchache wa kucheza na watoto wao, hivyo kupitia tamthilia hii, baba hao wanapata fursa ya kuwa na watoto kwa muda mrefu, na muda huo wanaoutumia pamoja si rahisi kusahau. Utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Maryland kitivo cha madawa umegundua kuwa, watoto ambao wanaishi na baba zao wanasoma vizuri, wanajistahi, na wanaonyesha dalili chache za msongo wa mawazo kuliko watoto wasioishi na baba zao. Pia utafiti huo umegundua kuwa, watoto wanaodhani kuwa baba zao wanawaunga mkono wanahisi kukubalika zaidi katika jamii.

    Baba anapojihusisha na maisha ya mtoto inaleta tofauti kubwa katika maeneo mbalimbali, iwe ni kwenye maendeleo ya kiakili, uhusiano wa kimapenzi, au maendeleo ya kisaikolojia. Hivyo ni wazi kuwa, baba ana nafasi kubwa zaidi katika maisha ya watoto wao. Watu wa ngazi mbalimbali za maisha waliohojiwa kuhusu suala hili walikuwa na mambo tofauti ya kusema, ila ukweli unabaki palepale kwamba, baba ni sehemu muhimu katika makuzi na malezi ya mtoto.

    Baba anachukua nafasi ya kiongozi wa dini katika nyumba. Vitabu vyote vya dini vinampa baba nafsi muhimu sana ya makuzi ya kiroho ya familia, anatakiwa kuiongoza familia yake katika masuala yote muhimu ya kiroho. Baba pia ni mlinzi wa familia. Baba anatakiwa kufuatilia kwa makini na kwa uhakika kila kitu kuhusiana na usalama wa familia yake. Baba anatakiwa kuwalinda watoto wake sio tu kutoka kwenye hatari zozote za kimwili, bali pia zile za kisikolojia na kiimani. Utafiti umeonyesha kuwa, matatizo mengi katika jamii ya sasa, ikiwemo kushindwa kusoma, kiakili, tabia, na kisaikolojia yanayosababisha uhalifu kwa watoto, kujamiina kabla ya ndoa, matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu, yote yanatokana na mtoto anapokua bila ya mzami kutokana na kuvunjika kwa ndoa.

    Pamoja na hayo, baba pia ana nafasi muhimu ya kutimiza kikamilifu mahitaji ya familia yake. Moja ya ahadi ambazo mwanamume anatoa wakati wa kufunga ndoa ni kutimiza mahitaji ya familia yake, na nafasi yake hii haibadiliki kamwe. Baba sio tu anatimiza mahitaji ya kiroho ya familia, bali pia mahitaji ya kimwili na pia mahitaji ya kiakili. Kwa kushirikiana na mke wake, baba anatakiwa kuwafundisha watoto kuishi ndani ya uwezo wao, na hilo analifanya kwa kuwa mfano kwao. Baba anatakiwa kuwafundisha watoto kuwa na matumizi yanayoendana na kipato chao, na hivyo kuwa huru.

    Baba pia ni mwalimu. Baba anafungua macho ya mtoto wake kwa dunia, kupitia yeye, watoto wake wanapata uzoefu wa maisha na jinsi ya kuishi. Baba anatakiwa kuwa sambamba na watoto wake, kama wanajifunza masomo ya shule au michezo mbalimbali, baba ni vizuri akishiriki nao. Kwa njia hii, baba anakuwa na fursa nzuri ya kucheza na watoto wake. Kuna michezo ambayo watoto wa kiune wanacheza na baba zao kama vile mpira wa miguu. Muhimu zaidi, baba anapaswa atenge muda maalum kuwa na familia/watoto wake.

    Ndio huwa kizungumkuti, maana baba atakwambia nikae na watoto watakula nini? Lakini naamini kinachosemwa hapa ni kuwa, baba anatakiwa kuwa na wakati maalum wa kukaa na kuongea na watoto wake, pia asikose siku muhimu kwa watoto kama vile siku ya kuzaliwa, kama kuna maonyesho shuleni ambayo watoto wanashiriki, michezo, mikutano ya walimu, wazazi, na watoto, na mambo mengine ambayo ni muhimu kwa watoto wao. Halafu ikumbukwe kuwa, baba haishi kuwa baba baada ya watoto wao kuwa na familia zao, bado anatakiwa kuwasaidia watoto na wajukuu.

    Baba pia anatakiwa kukuza vipaji vya watoto. Hapa baba anapaswa kuwa makini kuangalia kitu ambacho mtoto wake anapendelea, na kuhakikisha anamsaidia kukuza kipaji alicho nacho, na sio kumlazimisha kufanya kitu ambacho mtoto hakipendi. Kuna baadhi ya wazazi wanapenda kuwachagulia watoto wao marafiki, kazi gani anatakiwa afanye, wanasahau kuwa watoto pia wana utashi wao, cha muhimu ni kumfuatilia mtoto wako kwa makini na kujua anapendelea nini, na umsaidie kuendeleza kipaji chake.

    Jukumu lingine la baba ni kuwa mtumishi. Pamoja na kuwa baba ni kichwa cha familia, lakini vilevile ni mtumishi. Ni mtumishi kwa kuwa yale anayofundisha kwa watoto wake anapaswa kuyafanya. Awe mwalimu sio wa maneno tu, bali pia matendo.

    Kuna baadhi ya baba ni maarufu sana kwa kusema, lakini inapofikia kutenda kile wanachosema inakuwa ni tatizo. Baba, hakikisha unakuwa karibu na familia yako, hususan watoto, uwasaidie kwenye majukumu yao, iwe ni homework, au ushauri, maana ukimwacha mtoto, kuna wengine watakaomfundisha kwa njia ambayo sio nzuri. Kwa upande wa China, kuna mtazamo gani kuhusu nafasi ya baba kwenye familia?

    Kwa kweli mtazamo sio tofauti na sehemu nyingine duniani. Baba ana nafasi muhimu sana katika malezi na makuzi ya mtoto, kama anavyosema Bibi Liu

    "Naona baba anayeweza kutumia muda mrefu kukaa pamoja na watoto ni baba mzuri. Wanachohitaji watoto ni kuwa pamoja na wazazi. Kama baba anaweza kutimiza uwiano mzuri kati ya ufuatiliaji wa familia na kazi, na kutumia muda mrefu zaidi kwa watoto na familia, hakika ni baba mzuri."

    Baba mzuri, kwa mtazamo wa Bi. Liu, ni yule anayetumia muda mwingi zaidi na familia. Lakini Bw. Fang naye ana mtazamo wake.

    "Baba wa namna gani ni baba mzuri? Naona baba anayemfundisha watoto imani nzuri ni baba mzuri. Baba anapaswa kuwa mfano mzuri mbele ya watoto wake, anapaswa kufikiria kwa kina kabla ya kusema chochote, ni lazima awe na athari nzuri kwa watoto, na kuwafanya waone uzuri wa maisha, mazingira, familia, watoto wenzao na walimu."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako