• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Maneno sita ya kuelezea madhumuni makuu ya mpango wa "Imetengenezwa China Mwaka 2025"

    (GMT+08:00) 2015-06-23 10:54:19


    Katika kipindi cha wiki iliyopita, tulizungumzia mpango uliotolewa hivi karibuni na serikali ya China wa "Imetengenezwa China Mwaka 2025", ukiwa ni hatua ya kuhimiza kwa pande zote mkakati wa kujenga China kuwa nchi yenye nguvu kubwa ya utengenezaji. Na katika kipindi cha leo cha uchumi na maendeleo, tutatumia maneno sita kuelezea kwa kina madhumuni makuu ya mpango wa "Imetengenezwa China Mwaka 2025".

    Nchi yenye nguvu kubwa ya utengenezaji:

    Kama tukifafanua kwa urahisi maana ya "Imetengenezwa China Mwaka 2025", jibu lililotolewa na Waziri wa Viwanda na Teknolojia ya Habari wa China Miao Wei ni "kutoka nchi kubwa ya utengenezaji hadi nchi yenye nguvu kubwa ya utengenezaji". Baada ya maendeleo ya miaka 30 tangu China ianze kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, nchi hiyo imekuwa na mfumo unaokamilika wa sekta ya viwanda, na ukubwa wa sekta hiyo umechukua asilimia 20 ya dunia nzima. Lakini uwezo wa uvumbuzi wa kujitegemea katika sekta ya utengenezaji hautoshi, teknolojia muhimu zinategemea nchi za nje, chapa ya kichina haina ushawishi, na muundo wa sekta ya viwanda bado unahitaji kufanywa mageuzi, mambo hayo yanaonesha kuwa China bado ni nchi kubwa ya utengenezaji badala ya nchi yenye nguvu kubwa ya utengenezaji.

    Miao Wei amesema serikali ya China imetoa mkakati wa "hatua tatu", na inatarajia kufanya juhudi katika miaka 30 kujenga China kuwa nchi yenye nguvu kubwa ya utengenezaji duniani ifikapo mwaka 2049 wakati itakapotimia miaka 100 ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China. Mpango wa "Imetengenezwa China Mwaka 2025" ni hatua ya kwanza katika mkakati wa "hatua tatu", na pia ni mara ya kwanza kwa China kutoa mwongozo wa kujenga nchi yenye nguvu kubwa ya utengenezaji.

    Naibu mkurugenzi wa idara ya mipango katika Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari ya China Li Beiguang anaona kuwa hivi sasa nchi nyingi zilizoendelea zinapanga kustawisha sekta ya utengenezaji kwa lengo la kuongeza nafasi za ajira na uwezo wa uvumbuzi wa taifa.

    Akizungumzia jinsi ya kujenga taifa lenye nguvu kubwa ya utengenezaji, waziri wa viwanda na teknolojia ya habari wa China Miao Wei amesema teknolojia ya habari inapaswa kuchangia maendeleo ya sekta ya utengenezaji na kuhimiza uwezo wa ubunifu wa China katika sekta hiyo, na pia kusukuma mbele utengenezaji unaotumia teknolojia ya hali ya juu, usiochafua mazingira, na kuhimiza maendeleo ya sekta inayotoa huduma kwa ajili ya kuhakikisha mchakato wa utengenezaji, na kuinua kiwango na ushindani wa sekta ya utengenezaji.

    Imebuniwa China:

    Katika mpango wa "Imetengenezwa China Mwaka 2025", mabadiliko yanayotakiwa kufanywa ni kutoka "imetengenezwa China" hadi "imebuniwa China", na kwamba ni lazima kuweka kipaumbele kwenye kazi za kuendeleza uvumbuzi kwa ajili ya kupata maendeleo ya sekta ya utengenezaji. Naibu waziri wa viwanda na teknolojia ya habari wa China Mao Weiming anasema mazingira ya ndani na nje ya maendeleo ya uchumi yanabadilika kwa kiasi kikubwa, na kupungua kwa nguvu za jadi na ushindani wa kimataifa unaozidi kuwa mkali vimetaka mabadiliko ya haraka ya kutoka "imetengenezwa China" hadi "imebuniwa China".

    "Imebuniwa China" inaonekana zaidi kupitia uvumbuzi wa teknolojia. Maendeleo na uvumbuzi wa teknolojia sio tu vinaweza kuinua kiwango cha uzalishaji na ubora wa bidhaa katika maeneo ya jadi ya utengenezaji, bali pia vinaweza kusababisha kuibuka kwa nyenzo mpya, nishati mpya, bidhaa mpya za biolojia na vifaa vipya.

    Katika miaka ya hivi karibuni, China imezingatia sana shughuli za utafiti na maendeleo. Mwaka 2013, fedha zilizotengwa na jamii nzima kwa ajili ya shughuli hizo zilikuwa dola za kimarekani bilioni 190, kiasi ambacho kilichukua asilimia mbili ya pato la taifa la mwaka huo. Hata hivyo, ikilinganishwa na nchi zenye nguvu duniani, uwezo wa uvumbuzi bado ni mdogo.

    Takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha China cha kutegemea teknolojia za nje ni zaidi ya asilimia 50, na vifaa vingi venye teknolojia ya hali ya juu vinaagizwa kutoka nje. Naibu mkurugenzi wa idara ya mipango katika Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari ya China Li Beiguang amesema ni lazima kuweka kipaumbele kwenye kazi ya kuongeza uwezo wa uvumbuzi, na pia kuendeleza teknolojia muhimu, kuharakisha mchakato wa kutumia teknolojia mpya viwandani, kuongeza uwezo wa uvumbuzi katika hatua na maeneo muhimu, na kufuata njia ya kujiendeleza kwa kupitia uvumbuzi.

    Utengenezaji unaotumia teknolojia ya hali ya juu:

    Katika mpango wa "Imetengenezwa China Mwaka 2025", utengenezaji unaotumia teknolojia ya hali ya juu umeamuliwa kuwa jambo muhimu linalotiliwa mkazo katika utengenezaji wa China. Waziri wa viwanda na teknolojia ya habari wa China Miao Wei anaona kuwa utengenezaji unaotumia teknolojia ya hali ya juu utafanikishwa kama mbinu na vifaa vipya vya utengenezaji vinatumiwa na pia kufanya teknolojia ya mawasiliano ya habari inayoendelezwa kwa kasi kutumiwa katika sekta ya utengenezaji ili kubadilisha kabisa njia za utengenezaji na uhusiano kati ya watu, na kuleta mabadiliko na uvumbuzi katika njia za utengenezaji na mtindo wa kibiashara.

    Mtaalamu wa uhandisi wa China Profesa Zhou Ji amesema duru mpya ya mapinduzi ya teknolojia na mageuzi ya kiviwanda inaibuka, na teknolojia katika habari, baiolojia, nyenzo mpya na nishati mpya zinaenezwa, na zimeleta mapinduzi ya kiteknolojia kwa nyanja karibu zote, muhimu zaidi katika mchakato huo ni utengezaji unaotumia teknolojia ya hali ya juu."

    Naibu mkurugenzi wa idara ya vifaa katika Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari ya China Li Dong amesema utengenezaji unaotumia teknolojia ya hali ya juu utaongeza kwa kiasi kikubwa ufanisi katika uzalishaji na matumizi ya rasilimali, na wakati huohuo, utapunguza muda wa utafiti na uzalishaji, gharama za uendeshaji na asilimia ya bidhaa zisizofikia viwango vinavyokubalika.

    Utengenezaji usiochafua mazingira:

    Mpango wa "Imetengenezwa China Mwaka 2025" umetaja mara nyingi neno la "kutochafua mazingira", kama vile kutekeleza kwa pande zote utengenezaji usiochafua mazingira; kufanya mageuzi yanayolenga kuondoa uchafuzi wa sekta za jadi za utengezaji za chuma cha pua na medali isiyo ya chuma, kutekeleza mpango wa kuinua kiwango cha utengenezaji usiochafua mazingira katika maeneo, mabonde na sekta muhimu; na kupanga vigezo na kufanya tathmini kuhusiana na uchafuzi wa mazingira kwa bidhaa, viwanda, maeneo ya kiviwanda na makampuni,.

    Naibu waziri wa viwanda na teknolojia ya habari wa China Mao Weiming amesema utengenezaji usiochafua mazingira ni chaguo la lazima katika kutimiza maendeleo endelevu ya sekta ya utengenezaji, na sekta ya utengenezaji ya China bado haijaondokana na mtindo wa kujiendeleza kwa kutumia fedha na raslimali nyingi na kutoa uchafuzi mwingi.

    Njia pekee ya kushughulikia vizuri uhusiano kati ya maendeleo na maliasili na mazingira ni maendeleo yasiyochafua mazingira, na kwamba kuharakisha kuhimiza mageuzi ya sekta za jadi za utengenezaji, kuongeza ufanisi wa maendeleo ya sekta ya viwanda, na pia kujenga utaratibu wa utengenezaji usiochafua mazingira wenye ufanisi, safi, kiwango cha chini cha utoaji wa carbon na matumizi endelevu.

    Mkurugenzi wa idara ya uhifadhi wa nishati na matumizi ya jumla katika Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari ya China Gao Yunhu amesema wizara hiyo itajenga utaratibu wa utengenezaji usiochafua mazingira, ikiwa ni pamoja na kujenga viwanda visivyochafua mazingira, kufanya utengenezaji usiochafua mazingira, kuongeza kiwango cha matumizi endelevu na manunuzi yasiyochafua mazingira, na pia kutoa vigezo vya hali ya juu na kufanya tathmini kwa makini, na kama makampuni yasipofanya utengenezaji usiochafua mazingira, yatawekwa kwenye "orodha nyeusi".

    Ubora wa China:

    "Imetengenezwa China mwaka 2025" imesema ubora ni jambo linaloweza kuamua kama lengo la kujenga China kuwa nchi yenye nguvu kubwa ya utengenezaji linaweza kutimizwa, na imesisitiza majukumu ya makampuni katika kusimamia ubora, kuongeza nguvu ya teknolojia katika kuongeza ubora, kutunga sheria, kanuni na taratibu, mfumo wa kusimamia ubora, utamaduni wa kisasa wa ubora, na kuweka mazingira ya soko yenye uaminifu, na kupata maendeleo kwa kupitia ubora mzuri.

    Ubora mzuri ni alama muhimu ya utengenezaji wenye nguvu kubwa, na pia unaweza kuonesha nguvu ya jumla ya nchi moja katika upeo wa ushindani wa sokoni. Unaweza kuonesha ushindani wa makampuni na sekta ya kiviwanda, na ni ishara ya kiwango cha ustaarabu wa taifa. Pia unaweza kuonesha kiwango cha uvumbuzi wa teknolojia, uwezo wa uongozi na sifa ya wafanyakazi, pamoja na mazingira ya utawala wa sheria, elimu ya kitamaduni na ujenzi wa uaminifu.

    Naibu mkurugenzi wa idara ya teknolojia katika Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari ya China Sha Nansheng anasema ubora wa bidhaa za China haujafikia kiwango cha kuridhisha watu katika baadhi ya nyenzo muhimu, vipuri na mifumo muhimu, na kwa muda mrefu inahitaji kuagiza vitu hivyo kutoka nje. Kuongeza ubora kunaweza kubadilisha hali ya kiwango cha chini na thamani ndogo ya nyongeza ya bidhaa.

    Kwa miaka zaidi ya kumi, kiwango cha ubora wa sekta ya utengenezaji ya China kinaongezeka, na kuhakikisha ongezeko tulivu la manunuzi na maendeleo endelevu ya uchumi. Kutokana na mabadiliko katika mahitaji ya manunuzi, mahitaji ya watu kwa ubora yanaongezeka siku hadi siku, katika sekta ya manunuzi ya vitu vya kila siku, ubora unazingatiwa zaidi badala ya idadi.

    Mkuu wa Shirika la Ubora la China Jia Fuxing anasema ubora ni jambo muhimu katika kipindi kipya cha maendeleo ya uchumi, ni mada inayofuatiliwa na kushirikishwa kwa pamoja na serikali, jumuiya za kijamii, makampuni na wateja, nguvu zote za jamii zinapaswa kushiriki kwenye kazi za kuinua ubora wa bidhaa.

    Chapa ya kichina:

    Kutimiza mabadiliko kutoka bidhaa zinazotengenezwa nchini China hadi chapa ya China ni lengo jingine muhimu lililotajwa kwenye mpango wa "Imetengenezwa China mwaka 2025"

    Hivi sasa, China imeshika nafasi ya pili duniani kwa ukubwa wa sekta ya utengenezaji, lakini bado ni nchi kubwa inayotengeneza bidhaa kwa mujibu wa oda za makampuni ya nchi nyingine, wala siyo nchi yenye chapa nyingi maarufu duniani. Asilimia 90 za bidhaa zilizouzwa nje ya China ni za chapa za nchi nyingine.

    Tofauti kati ya kutengeneza bidhaa kwa nchi za nje na kuwa na chapa yenyewe inaonekana moja kwa moja katika mapato. Barbie doll moja katika soko la Marekani inauzwa kwa bei ya dola za kimarekani 10, bei inayouzwa kwa Marekani baada ya kutengeneza ni dola za kimarekani 2, mapato yanayopata makampuni ya China yanayotengeneza ni dola za kimarekani 0.35 tu. Ukosefu wa chapa maarufu umesababisha makampuni ya China yawe katika sehemu ya chini katika mzunguko wa sekta ya kiviwanda duniani, na mapato mengi yanaelekea kwa makampuni ya nchi za nje.

    "Imetengenezwa China" inasisitiza umuhimu wa kutokea kwa chapa maarufu ya kimataifa ya China. Na kutokana na makampuni mengi zaidi kwenda katika nchi za nje, chapa nyingi za kichina zimeibuka katika jukwaa la kimataifa. Kati ya chapa 500 zenye nguvu kubwa duniani, 29 ni chapa kutoka China bara.

    Kutoka nchi kubwa ya utengenezaji hadi nchi yenye nguvu kubwa ya utengenezaji, kutoka nchi kubwa inayotengeneza bidhaa za chapa za nchi za nje hadi nchi zenye chapa maarufu duniani, inatazamiwa kuwa kutakuwa na chapa nyingi zaidi za kichina zinazojulikana duniani.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako