• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Vitoweo kula kiafya

    (GMT+08:00) 2015-06-29 13:20:42

    Karibu msikilizaji kwenye kipindi hiki cha sauti ya wanawake, kumbuka ndani ya kipindi tunapata fursa ya kuangalia mambo mbalimbali kuhusu wanawake na watoto, lakini kuanzia kila Jumatatu ya mwisho wa mwezi tukianzia na mwezi huu wa sita tutakuwa tunawaletea sehemu maalumu ya tule kwa afya.



    Kama ulivyosema kwamba tutakuwa tunaleta sehemu maalumu ya tule kwa afya katika kipindi hiki cha sauti wa wanawake, kwasababu siku zote tunasema afya ni bora kuliko kitu chochote kile. Tunajua kuwa afya bora inaanzia kwenye utaratibu wetu wa chakula tunachokula kila siku, ila kwa maisha ya sasa tunavyo ishi, basi ulaji wetu umekuwa mbovu sana. Shirika la Afya Duniani WHO limeweka mpango maalum wa kula vizuri ili binadamu aweze kuwa na afya bora.



    Kwa kuzingatia umuhimu huo tutajaribu kuwaletea vyakula mbalimbali na manufaa yake mwilini. Na leo hii tunaanza kwa kuwaelezea vitoweo vyenye afya bora na namna vinavyopikwa na wachina bila ya kuondoa ubora wake au manufaa yake mwilini. China ni nchi inayochukua nafasi za mbele katika mapishi, ni nchi yenye utamaduni mkubwa wa chakula ulioanza zamani sana, na inasifiwa sana duniani. Wachina wanapopika ama kula wanazingatia sana lishe, milo mitatu inayoliwa kila siku haipo kwa ajili ya kuondoa njaa na kiu tu, bali Wachina wanafuatilia lishe ya chakula, maumbo ya kupendeza, hisia za upendo na adabu. Miongoni mwa vyakula vingi vya aina mbalimbali, vyakula vyepesi ambavyo ni maarufu hapa China, vinapendwa zaidi na wageni waliotoka nchi za nje.



    Tuanze na Kitoweo kiitwacho "Gongbaojiding". Hiki ni kitoweo maarufu cha jadi hapa China, vitu vilivyoko katika kitoweo hiki ni pamoja na vipande vidogo vidogo vya nyama ya kuku, pilipili kavu pamoja na karanga, ambavyo vinakaagwa kwa mafuta. Kitoweo hiki kinapendwa sana na watu kutokana na kuwa nyama yake ni laini, tamu na yenye ladha kali ya pilipili, ambayo inachanganywa na ladha tamu ya karanga. Hususan hivi sasa katika nchi za magharibi, kitoweo hiki cha "Gongbaojiding" ni maarufu sana, hali ambayo imefanya karibu iwe ndio jina la vitoweo vya China.



    Kwa upande wa namna ya kupika "Gongbaojiding" kwanza Unachukua nyama ya kuku sehemu ya kidari na kuikata katika vipande vidogovidogo, halafu unavichanganya pamoja na chumvi, sosi ya soya na wanga uliotiwa maji, halafu unavikoroga mpaka vichanganyike vizuri; baada ya hapo unakaanga karanga katika sufuria yenye mafuta yanayochemka, ondoa magamba laini baada karanga kupoa kabisa, halafu kata pilipili vipande vidogovidogo; Baada ya hapo unatayarisha mchanganyiko wa viungo kwa kuweka sukari kidogo, siki, sosi ya soya, maji ya moto, sosi ya nyama na wanga uliotiwa maji na kuwa rojorojo.



    Safisha sufuria na kuweka mafuta kidogo, baada ya mafuta kupata moto weka kidogo huajiao yaani (mbegu za prickly ash za China), (zimekaa kama pilipili mtama) ambazo zinaondolewa wakati inaposikika harufu yake, weka pilipili ndani ya sufuria, wakati pilipili zinapobadilika rangi na kuwa ya kahawia iliyokoza, unaweka nyama ya kuku ndani ya sufuria, baadaye unachanganya na mvinyo, kisha weka vipande vidogovidogo vya tangawizi, vitungu saumu na vitungu vya kijani, hadi inaposikika harufu nzuri ya kitoweo, mchanganyiko wa viungo uwekwe haraka katika sufuria, wakati sosi ya viungo inapochemka, karanga ziwekwe ndani ya sufuria, baada ya kukorogwa vizuri, kitoweo kinaweza kupakuliwa.



    Kama tulivyosema hiki ni kitoweo cha China ambacho ni maarufu sana. Ndani ya mapishi haya kuna mboga mbalimbali ambazo zina manufaa sana mwilini. Tukianza na kuku kwenye kitoweo hiki ambaye ni kidari, wengi tunafahamu kuwa kuku kidari ni mzuri zaidi kuliko sehemu nyingine ya kuku mzima, kwani sehemu hii haina mafuta. Kwa wale ambao wapo kwenye utaratibu wa kuangalia uzito wao au hawapendi kunenepa wanashauriwa kula kidari cha kuku kuliko sehemu nyingine zote za kuku. Kuku ana protini mwilini, na kama tunavyoshauriwa katika milo yetu, lazima tuweke na protini.



    Katika mboga hiyo pia kuna Tangawizi ambayo inakatwa vipande vidogo vidogo. Tunajua kuwa Tangawizi inasaidia sana mwili. Na hapa wacha tukutajie miongoni mwa faida nyingi sana za tangawizi kwa mwili wa mwanadamu mbazo ni Kusaidia kusaga chakula tumboni, Kutibu tatizo la gesi tumboni, Kuondoa tatizo la msokoto wa tumbo (bila kuharisha) Husaidia kuzuia kutapika, Mshtuko/Mkazo wa ghafula (wa msuli), Maumivu ya tumbo na Kibofu cha mkojo ikiambatana na Homa, Mafua, Kukohoa na Pumu.



    Pia kwa upande wa kitunguu thomu nacho kina faida kubwa mwili. Kitunguu thomu kimetajwa kwenye vitabu mbalimbali vya dini vikielezea faida zake katika kutibu maradhi mbalimbali yasababishwayo na bakteria, matatizo katika mapafu, matatizo katika mfumo wa umen'genyaji chakula, na matatizo ya kuishiwa nguvu. Historia inaonesha kuwa, vitunguu thomu vilianza kutumika China mwaka 510 K.K na pia vilitumiwa na wanajeshi wa Ugiriki na Roma. Vitunguu thomu vinasaidia kutibu saratani ikiwemo saratani ya tumbo na utumbo mkubwa. Tafiti zinaonesha idadi ndogo ya wagonjwa wa saratani katika nchi ambazo wakazi wake wana utamaduni wa kutumia vitunguu thomu kwa wingi. Pia husaidia kudhibiti kiwango cha sukari katika damu. Husaidia ufyozwaji wa thiamin, hivyo kusaidia kuepusha mwili na ugonjwa wa beriberi. Ina kiasi kikubwa cha vitamini C ambayo husaidia kuzuia ugonjwa wa kiseyeye. Pia Hutumika kutibu magonjwa nyemelezi kama toxoplasmosis, hasa kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini.



    Mwisho tunaangalia kiungo cha upishi huu wa "Gongbaojiding" ambacho ni kitunguu cha kijani. Hiki ni tofauti na kitunguu maji. Aina hii ya vitunguu inakuwa kama majani marefu. Ingawa harufu yake inakaribiana na kitunguu maji, lakini ni tofauti na kitunguu maji. Kitunguu cha kijani ni kizuri mwilini kwani mboga zote zenye asili ya ukijani zina vitamini C, nacho pia kinasaidia kuongeza vitamin C mwilini na kuongeza kina ya mwili.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako