• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Sanaa ya kuchorachora na zentangle

    (GMT+08:00) 2015-07-06 09:56:56

    Leo hii katika kipindi hiki tutakuelezea kuhusu sanaa ya kuchorachora ambayo inapendwa na watu wengi zaidi. Watu wengi wanapenda kuchorachora wakati wanapoongea na simu, kukaa kwenye mkutano au kusikiliza wanachofundishwa darasani. Hivi sasa kuchorachora kunachukuliwa kama mtindo wa sanaa unaopendwa na watu wengi.


    Katika kituo cha sanaa katika mtaa mmoja uliopo kitongoji kusini mwa mji wa Cape Town, Afrika Kusini mchoro wa kupendeza wenye utata ndio unaendelea kuchorwa. Akitumia maudhui ya herufi alizochagua kuchora kwa siku hii, Kari Longman anachora muundo wa ukoo. Longman anasema kuchukua muda kuchorachora kuna manufaa mengi haswa kwa watu wanaoishi maisha yenye shughuli nyingi mjini.

    "Naweza kujiita mtu mwenye ubunifu, lakini kwa ujumla wakati wa mchana ninakuwa na kazi isiyo na ubunifu. Hivyo kwangu mimi kuwa na mahali ambako ninaweza kukaa kimya na kujiwezesha kupata muda wa kutafakari, ingawa kunakuwa na sauti zinazosikika. Hii ni njia nzuri ya kuponya na kupoza hisia zilizochemka, na ndiyo maana ninaipenda. Nafikiri kuchorachora wakati nikiwa nje ya familia yangu kunasaidia, kwa sababu nyumbani mara nyingi huwa nazungukwa na watoto wangu watatu wanaopenda kupiga kelele. "

    Kutokana na uchunguzi uliofanywa na chuo kikuu cha Plymouth mwaka 2009, kuchorachora kunasaidia kuboresha kumbukumbu ya watu, kwa sababu kunawazuia watu kufikiria mambo yasiyowezekana, jambo ambalo linatumia nguvu nyingi za akili.

    Mhadhiri wa sanaa Kelly van der Watt anafundisha katka chuo cha sanaa cha Ruth Prowse, huko Cape Town.

    "Kuchorachora ni njia ya kuchora picha isiyo na muundo. Kuchorachora hakuhitaji kufanywa kwenye karatasi au vifaa maalumu, kitu chochote kinaweza kutumiwa katika kuchorachora. Kuchorachora pia hufanywa na watu bila kujitambua, kitu ambacho unakifanya wakati unapokuwa na pilika kama vile unapotayarisha orodha ya vitu au unapoongea na simu huwa unachora. Na kawaida huwa hufahamu unachora nini, lakini unachorachora, unatengeneza vitu. Kuchorachora hakuhitaji upate mafunzo yoyote maalumu, hivyo hilo ni jambo ambalo mtu yeyote anaweza kufanya."

    Tukirudi tena kwenye kituo cha sanaa cha Frank Joubert, mtaalamu wa elimu ya Sanaa Gabby van Heerden anafundisha mafunzo yaitwayo "Kuchorachora kwa raha" darasani. Lengo la mafunzo hayo ni kutengeneza maumbo yenye ubunifu.

    Van Heerden alichora umbo lake lililotokana na kuchorachora kwake kwa asili. Alisisitiza thamani ya kutafakari ya kuchorachora.

    "Unachofanya ni kuzingatia kuweka umbo moja kwenye karatasi kwa wakati mmoja, bila kuwa na mawazo mengine, unafuata mwelekeo huohuo, wa umbo unalolichora, na kwa kweli inaweka mawazo yako kwenye hali ya utulivu na amani. Ni kama njia fulani ya kutafakari, ambayo inaleta matokeo yaleyale na vitendo vilevile sahihi vya ubongo kama wakati unapokaa na kutafakari. Kwa watu wengi, mtindo huu wa kutafakari huwa ni rahisi zaidi, kama unafanya kazi kwa kalamu, unatengeneza maumbo, unachorachora, hii ni njia rahisi zaidi kwa watu kutafakari kuliko kutulia tuli."

    Kwenye kitovu cha mji wa Cape Town, darasa lingine la kuchorachora linaendelea, na hili ni la kimataifa. Darasa la kuchorachora ni sehemu ya Michoro 1000 iliyoanzishwa mwaka 2007, ikiwa ni kama njia ya kuchangisha fedha kwa shirika lisilo la kiserikali ambalo linasaidia watu wasio na makazi.

    Tamasha la Usiku wa Michoro 1000 limeenea katika sehemu nyingine za dunia, ikiwemo Canada, Uholanzi, Dubai, Italia na Ujerumani.

    Shani Judes ni mwandaaji wa shughuli hiyo.

    "Mwaka jana tulifanikiwa kukusanya michoro 8,500 kutoka madarasa yote ya kuchorachora. Tulichorachora kileleni mwa mlima, ufukweni, kwenye mapaa, kwenye magofu ya bustani, shuleni, yaani watoto wote wa shule walichorachora. Na kila mmoja aliyechorachora alifahamu kuwa mchoro anaouchora utapelekwa kwenye maonesha, na mtu fulani atakuja na kuuchagua na kulipa Rand 100 au dola 10 au kiasi chochote kile. Watachagua na kulipa kwa ajili ya mchoro, na hizo pesa ni muhimu sana, kwa sababu tunazitumia kusaidia chochote tunachokifanya katika kipindi hicho."

    Pesa zilizopatikana kwenye tamasha la Usiku wa Michoro 1000 la mwaka 2014 zilitolewa kwa ajili ya shule ya watoto kutoka familia zenye hali duni kiuchumi huko Cape Town. Tamasha jingine la Michoro 1000 ya Cape Town, ambalo litajumuisha michoro hii litafanyika mwaka 2016.

    Kate Julien Eriksen ambaye ni mwanafunzi wa sanaa anakamilisha kuchorachora kwake.

    "Ninajifunza vyombo vipya vya habari, ambavyo ni somo la wa ubunifu wa michoro, vifaa vya kampyuta kama vile Photoshop, Illustrator. Siku zote ninakaa na kampyuta, hivyo hii ni njia nzuri ya kurudi kwenye hatua za msingi, kuchora kwa kutumia kalamu za rangi, penseli na vitu vingine, ni nzuri sana."

    Zentangle ni aina ya sanaa ya uchoraji inayofuata wazo la zen la dini ya Kibudhaa. Studio moja iliyoko katika maeneo ya katikati ya Beijing imefungua darasa la kufundisha uchoraji wa Zentangle. Uchoraji huu unaweza kuwafanya watu wanaochora watafakari na kujipumzisha. Caroline Nassoro ana maelezo zaidi.

    Katika studio moja, darasa la kufundisha uchoraji linaendelea.

    Mwalimu mwenye umri wa miaka 27 Bw. Wang Yifan aliwahi kujifunza ubunifu wa sanaa, miaka miwili iliyopita alifahamu uchoraji wa Zentangle kupitia tovuti ya mtandao wa Internet. Bw. Wang aliyejifunza sanaa ya uchoraji wa dini ya Kibudhaa alipoanza tu uchoraji huo, akaupenda sana. Bw. Wang anasema, uchoraji wa Zentangle ni tofauti sana na uchoraji wa aina nyingine, ambao una uzuri wake wa kipekee.

    "Zentangle ni uchoraji unaozingatia mstari, ambayo ni tofauti na michoro katika maisha yetu na ustadi wake ni mgumu zaidi. Zen katika zentangle inamaanisha kuzingatia mstari mmoja bila kufikiri mambo mengine."

    Ingawa Zentangle ni mtindo wa sanaa ulioibuka katika miaka ya hivi karibuni, lakini chimbuko lake linatokana na sanaa ya dini ya Kibudhaa. Katika mchakato wa maendeleo ya historia ya dini ya Kibudhaa, uchoraji wa Budhaa wa nyakati tofauti na sehemu mbalimbali unaounda sanaa ya dini ya Kibudhaa, na Zentangle ni sanaa inayotokana na sanaa ya dini ya Kibudhaa, ambayo inawafaa watu wa sasa. Katika mchakato wa uchoraji, wachoraji hawatakiwi kuwa na ufundi mwingi wa kuchora, hawatakiwi kufikiri sana, wanachotakiwa kufanya ni kuzingatia katika mstari mmoja tu. Uchoraji huo rahisi unaweza kuwafanya wachoraji kujisikia raha.

    "Darasani tunapata furaha, na tunapashana furaha , kati ya walimu na wanafunzi. Sio tu unatazama michoro, bali pia unaweza kuchora. Hatuna lengo maalumu, tunaufanya uchoraji uwe jambo la kawaida, naweza kujipumzisha kupitia sanaa hiyo."

    Wang anasema, asilimia 60 ya wanafunzi wanaojifunza zentangle walijisikia raha akilini na kupunguza shinikizo katika kazi na maisha. Kwa kawaida, kila mwanafunzi anaweza kumaliza mchoro mmoja ndani ya saa 3, na kupata ustadi wa msingi. Katika miezi minne tangu studio hiyo ianzishe darasa la zentangle, watu zaidi ya 60 wamekwenda na kujifunza uchoraji huo.

    Bw. Li pia ni mmoja kati ya wanafunzi wanaojifunza zentangle. Bw. Li anafanya kazi katika saluni, kila siku anafanya kazi zaidi ya saa 10, ambayo inamchosha sana. Anaona kuwa zentangle inamfanya ajipumzishe na kujipunguzia shinikizo linalotokana na kazi.

    "Zentangle inanifanya nijisikie vizuri, unachora huku ukisikiliza muziki laini, ni kimya sana. Unaondokana na kelele za mjini, unaweza kujisikia uhai kutokana na kuchora."

    Bw. Li anasema, kama vijana wengine, alipokabiliwa na shinikizo alikuwa anapenda kwenda baa, kutazama sinema au kuimba karaoke, lakini sasa baada ya kuanza kujifunza uchoraji, anapendelea shughuli zenye maana za starehe.

    "Nataka kufanya jambo lenye maana zaidi. Ingawa nakuja kwenye studio hiii wakati wa kupumzika tu kila mwezi. Kama nikienda baa au kwenda kuimba karaoke, nahisi kama napoteza muda, sitapata chochote. Lakini kama nikija hapa kuchora, kila mara nitapata mchoro wangu, ambao unanifanya nijisikie fahari."

    Studio hiyo inayoitwa Muye imekuwa na historia ya miaka mitano. Mzinduzi wake ambaye pia ni mchoraji huru Bw. Ge Muye alisema, wakati studio hiyo inaanzishwa, aligundua kuwa kuna watu wazima wengi wanaotaka kujifunza uchoraji, lakini hawakuwa na njia. Ili kutoa mahali ambako watu wangeweza kujifunza uchoraji na kuchora, alizindua studio ya Muye.

    "Wanaokuja kujifunza uchoraji wanapenda kuchora. Kutokana na kupenda kwao kuchora, wana ndoto ya kuchora moyoni mwao, hivyo wakipata nafasi wanakuja kujifunza. Utaratibu ndio unakuwa hivyo."

    Baada ya maendeleo ya miaka mitano, studio ya Muye imekuwa na walimu watano na msaidizi mmoja ambao wanafundisha uchoraji wa kimagharibi na wa kichina kwa watu wazima. Katika miaka mitano iliyopita, watu zaidi ya elfu moja wenye umri wa miaka 18 hadi 76 walikwenda kujifunza. Bw. Ge anasema, kufuatia kuboreshwa kwa mazingira ya kiutamaduni ya China, mambo yanayopendwa na watu pia yanabadilika, huku mambo yanayofanywa wakati wa mapumziko pia yakibadilika, watu wengi zaidi wanataka kupata mapumziko na kujiinua katika sanaa.

    "Katika miaka mitano iliyopita, ilikuwa sio rahisi kwa watu wazima kutafuta sehemu ya kufundisha uchoraji. Wazee waliweza kwenda shule ya wazee, watoto na vijana walikuwa na madarasa mengi ya kujifunza uchoraji. Baada ya studio yetu kuanzishwa, mashirika yanayofundisha watu wazima kuchora sasa yanaongezeka sana. Hasa katika miaka miwili iliyopita, idadi imeongezeka kwa kasi sana."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako