• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Vichochoro ya Hutong ni alama ya kiutamaduni kwa wenyeji wa Beijing

    (GMT+08:00) 2015-07-07 16:57:21

    Hutong, ni vichochoro au mitaa miembamba inayozunguka kasri la kifalme yaani the Forbbiden City, ambavyo vinaunganisha makazi ya watu wa kawaida. Hutong imekuwa na historia ndefu, na tunaweza kusema ni moja ya sehemu muhimu zinazohifadhi utamaduni wa Beijing ya kale.

    Hutong za Beijing zilijengwa katika enzi ya Yuan katika karne ya 13, na zina historia ya zaidi ya miaka mia saba. Kwa wenyeji wa hapa Beijing, hizo Hutong si kama tu ni sehemu muhimu ya mji, bali pia ni mahali muhimu kwa maisha ya kila siku ya wakazi wa Beijing.

    Hutong zote ziko karibu na sehemu ya kibiashara yenye maduka mengi, ukiwa huko pia unaweza kusikia kelele za mji, lakini ndani ya Hutong hakuna msongamano wa magari, wala hakuna kelele za watu, unaona tu majirani wanaishi vizuri kwa pamoja. Uhusiano wa kijirani kama huo si rahisi kuuona kwenye maeneo ya majengo yenye ghorofa nyingi. Inayoonekana kwenye Hutong ni hali halisi ya maisha ya wenyeji wa Beijing, na uhusiano mzuri kati ya majirani pia ni sehemu muhimu ya maisha yao.

    Wasikilizaji wa Tanzania wanaweza kuelewa zaidi kuhusu hali hii, maana yake ni sawa na kuishi kwenye familia kubwa, au kuishi kwenye mtaa au eneo lenye nyumba ambazo watu wanaoishi hapo wanafahamiana na kuonana kila siku. Labda kwa Tanzania huenda isiwe sawa kabisa na Hutong, lakini hali ya maisha inafanana na ya Hutong.

    Mfano mzuri ni baadhi ya sehemu za maeneo ya mkoa wa Tanga Tanzania, au Mji Mkongwe Zanzibar, huko kuna vichochoro vingi sana, na mazingira ya maisha yanafanana na Hutong za hapa Beijing.

    Ingawa zinafanana, lakini pia kuna tofauti kubwa. Kwanza, Hutong za Beijing zote zinaenda sambamba na kuelekea moja kwa moja kaskazini-kusini au mashariki-magharibi, kama ukiwa kwenye ndege na ukiangalia chini, utaona Hutong zinaungana na kuonekana kuwa umbo la mraba. Lakini kwenye mji mkongwe, vichochoro haviendi moja kwa moja na vinazungukazunguka. Ya pili ni kwamba Hutong ziko nyingi zaidi na zinafunika eneo kubwa zaidi kuliko vichochoro vya Mji Mkongwe.

    Hapa Beijing kuna msemo kwamba kuna Hutong zenye majina zaidi ya elfu tatu, na zile zisizo na majina ni nyingi kama manyoya ya kuku. Kweli mjini Beijing kuna Hutong, yaani vichochoro vingi sana. Takwimu zinasema hapa Beijing kuna zaidi ya Hutong elfu saba, na nyingi kati ya hizo ni zile zinazozunguka kasri la kifalme. Takwimu nyingine zinaonesha kuwa, kichochoro kirefu kabisa kina kilomita 6.5, na kifupi kabisa ni mita kadhaa tu, na kichochoro chembamba kabisa upana wake ni mita 0.7 tu.

    Wenyeji wa Beijing wana hisia maalumu kuhusu Hutong, baadhi ya wakazi wenyeji wameishi ndani ya Hutong hizo kwa miongo kadhaa na hata vizazi kadhaa. Kwa watu hao Hutong si kama tu ni njia ya kuingia na kutoka nyumbani, bali ni kama majumba ya makumbusho, karibu kila mahali kuna alama ya maisha na historia.

    Kuna utamaduni na mila nyingi zinazohusiana na Hutong za Beijing, lakini kama Hutong hizo zikichukuliwa kuwa ni sehemu ya kihistoria, mbali na umaalumu wa kiujenzi, pia kuna undani wake maalumu wa kiutamaduni. Kuna baadhi ya wasomi walijaribu kujumuisha kwamba utamaduni wa Hutong ni "utamaduni uliofungwa", "kiini cha utamaduni huo ni kuvumilia na kufuata utaratibu uliowekwa", tunaweza kusema utamaduni wa Hutong una mambo mengi mazuri yanayostahili kuenezwa, lakini pia una mambo mengine yaliyopitwa na wakati yanayotakiwa kuachwa.

    Utamaduni wa Hutong unaonesha maisha ya wakazi wenyeji wa Beijing ya zamani. Lakini kutokana na maendeleo ya uchumi na jamii, baadhi ya mila na desturi pia zimeanza kutoweka, kwa mfano sauti za wachuuzi wa bidhaa mbalimbali zamani zilikuwa zinasikika sana kwenye Hutong mjini Beijing, lakini kwa sasa hazisikiki tena, zinasikika tu kwenye maonesho au filamu.

    Hiyo ni sauti ya mchuuzi wa Beijing ambayo ilijulikana sana, mtu huyo anatangaza huduma ya "kunoa visu na mikasi". Hivi sasa sauti kama hizo hizisikiki kabisa, na hata biashara hiyo si rahisi kuiona tena. Kwa sasa sauti hiyo imekuwa kama sanaa ya kiutamaduni ambayo imetoweka kabisa kwenye Hutong, au tuseme kwenye maisha halisi.

    Tunaweza kufikiri kwamba zamani kwenye vichochoro vya hapa Beijing, wachuuzi walifanya biashara kwa mtindo kama wanavyofanya sasa wamachinga kule Tanzania au jua kali kule Kenya, sauti za wachuuzi kweli zinavutia sana. Na hata maneno yanayosemwa pia yanavutia.

    Kwa mfano wachuuzi wa tikitimaji walikuwa wanauza matunda hayo kando ya njia au vichochoro, wakitangaza biashara yao kwa sauti kubwa kuvutia wateja, ingawa walitia chumvi kidogo, lakini wachuuzi hao walivutia kweli. Wachuuzi hao walikuwa wa aina mbili, aina ya kwanza walikuwa na sauti ya kuvutia watu, na aina ya pili walipiga sauti ikiendana na sauti ya ala fulani, kama kitu kinachogongwa na kusikika mbali sana.

    Kweli sauti hizo zinavutia sana, lakini inasikitisha kuwa sasa zimetoweka kabisa kwenye maisha yetu, zinasikika tu kwenye maonesho ya utamaduni au filamu. Lakini uzuri ni kwamba serikali ya mji wa Beijing imetoa ombi kwa Umoja wa Mataifa kuziweka sauti za wachuuzi wa aina mbalimbali mjini Beijing katika siku za zamani kuwa urithi usioonekana wa utamaduni wa dunia.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako