• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tatizo la wanafunzi kulazimishwa kuacha masomo shuleni kutokana na kupata ujauzito

    (GMT+08:00) 2015-07-13 16:38:50

    Mimba za umri mdogo ambazo zinapelekea wanafunzi kukatisha masomo yao bado ni tatizo kubwa katika bara la Afrika. Matukio ya mimba kwa wanafunzi mbali na kuwakatisha masomo lakini pia yamekuwa yakitishia afya zao. Nchini Afrika Kusini, kuna shule maalum, ambayo wanafunzi wote ni wasichana waja wazito. Lengo la kuanzishwa kwa shule hiyo maalum ni kuwasaidia wasichana waja wazito wasisimamishwe masomo yao, na kutengwa na jamii. Ingawa serikali ya Afrika Kusini imetoa amri kwamba shule yoyote isiwafukuze wanafunzi wasichana wakiwa waja wazito, lakini bado kuna wasichana wengi wanaofukuzwa shule au kuacha masomo kutokana na shinikizo kutoka kwenye jamii, hali ambayo inaleta athari kubwa na mbaya kwa maisha yao ya baadaye.

    Shule hiyo ipo Mjini Pretoria, na imejengwa maalum kwa ajili ya wasichana hao, wanafunzi wake ni wasichana wajawazito wenye umri wa kati ya miaka 13 na 20. Wakiwa shuleni hapo wanatunzwa vizuri, na wanaweza kuendelea na masomo yao huku wakiwa na ujauzito. Mwanafunzi mmoja wa shule hiyo alisema, baada ya kwenda shuleni hapo, akakuta wenzake wote ni wasichana kama yeye, hivyo hakujihisi kwamba wengine watamchukulia kama mgeni, kwani wote wanafanana, hivyo akaona kwenda shuleni hapo ni jambo zuri. Lakini hivi sasa kuna wanafunzi zaidi ya 100 katika shule hiyo. Na Afrika Kusini nzima, kuna maelfu ya wasichana wajawazito ambao hawawezi kunufaika na maisha hayo ya shuleni.

    Imefahamika kuwa nchini Afrika Kusini watoto wapatao elfu 20 wa shule ya msingi na sekondari, walipata ujauzito mwaka jana. Afrika Kusini kupitia Idara ya Elimu ya msingi imeweka mikakati ya kuhakikisha idara hiyo inashughulikia sera ya kupunguza ujauzito kwa wanafunzi, lakini inaonekana sera hiyo bado haijazaa matunda. Miongoni mwa mambo muhimu yanayotakiwa kutekelezwa kwenye mikakati hiyo ni kutoa huduma za uzazi wa mpango, kuwapa motisha ya kumaliza shule kabla ya kupata ujauzito, na program za elimu ya umma ambayo inakataza ngono isiyo salam na ya watu wa rika mbalimbali.

    Lakini jambo la kusitisha ni kuwa juu ya kuwepo kwa mikakati yote hiyo, idadi ya wasichana wanaorejea shule baada ya kujifungua bado haijajulikana. Sote tunafahamu kuwa elimu ni ufunguo wa maisha, na bila elimu, hawa wasichana hawatakuwa na nafasi ya kupata maisha mazuri. Hivi karibuni rais wa nchi hiyo Jackob Zuma alisema wasichana wa shule wanaopata ujauzito wanyang'anywe watoto wao halafu wafukuzwe na kupelekwa Kisiwa cha Robben, kwa kweli kauli hiyo inarudisha nyuma juhudi zote zinazofanywa katika kuhakikisha watoto hawa wanakuwa salama hawapati ujauzito na hata kama wakipata ujauzito wanaendelea kupata haki yao ya msingi ambayo ni elimu pia kauli hii haitasaidia chochote katika kukabiliana na mimba za utotoni.

    Badala ya kuwakufuza bora wangeiachia Idara ya Elimu ya Msingi iendelee na utekelezaji wake wa kushughulikia na kuhakikisha watoto hawa wanamaliza masomo yao. Kwani sera hiyo inatoa muongozo hatua kwa hatua kwa shule mbalimbali juu ya namna ya kushughulikia mimba za wanafunzi pamoja na kazi na majukumu ya kila mhusika, wakiwemo wanafunzi, wazazi wa wanafunzi waliopata ujauzito, baba aliyempa mimba mwanafunzi, kama baba naye pia ni mwanafunzi, pamoja na shule. Na kwa mujibu wa mipango Idara hiyo itakuwa inawapatia msaada muafaka ikiwemo fursa ya ushauri nasaha, afya zao pamoja na maendeleo ya jamii .

    Lakini mbali na Afrika Kusini, nchini Namibia pia kuna tatizo kama hilo. Kuna shule moja ya mchanganyiko iitwayo Ontoko ambayo ipo katika mkoa wa Omusuti, ina rikodi ya kesi tisa za wanafunzi wanaoacha shule kutokana na ujauzito tena hata miezi mitatu haijafika baada ya shule kufunguliwa kwa mwaka wa masomo wa 2015. Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 800, kesi nyingi zilizoripotiwa za wanafunzi waliopata ujauzito ni wale wa madarasa ya chini. Mwalimu mkuu wa shule hiyo amethibitisha hali hiyo lakini hakutaka kueleza kwa kina na kukataa hata kutaja jina lake kwa madai kwamba haruhusiwi kuongea na vyombo vya habari.

    Kwa kweli hali inasikitisha sana maana kawaida huwa tunashauriwa kukemea na masuala ambayo hayafai katika jamii na sio kunyamaza kimya au kuficha, kwani kufanya hivyo kutapelekea tatizo kuwa kubwa zaidi siku hadi siku. Ndio maana kuna baadhi ya watu katika shule hiyohiyo wamekuwa na wasiwasi kuhusu kiwango cha wasichana wanaopata ujauzito, na kusema tatizo hilo linaweza kuathiri vibaya utendaji wa kielimu pamoja na masomo kwa wanafunzi. Watu hao wanapatwa na hofu kubwa kwani kwa mujibu wa kauli zao mwaka jana pekee kulikuwa na wanafunzi tisa walioacha shule kwa tatizo la ujauzito, na kwa sasa ndani ya miezi mitatu wanawafunzi wengine tisa wajawazito.

    Shule hiyo ikiwa imekata tamaa, hivi karibuni iliwaelekeza wanafunzi wote wasichana kunyoa nywele kwa sababu inaonekana kwamba mitindo ya nywele ndio inayopelekea wanafunzi kujali zaidi mambo ya mitindo na kuwavutia wanafunzi wavulana. Na ingawa shule hiyo ni ya wanafunzi wenye mchanganyiko wa tamaduni mbalimbali, asilimia 90 ya wasichana wameshakata au kunyoa kabisa nywele zao. Hivi sasa wengi wao tayari wana watoto, na wengine wana watoto hadi wawili wakiwa katika darasa la sita.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako