• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Adhabu ya viboko kwa watoto

    (GMT+08:00) 2015-07-20 10:36:53

    Kuna jambo moja ambalo bado linajadiliwa katika nchi mbalimbali duniani, nalo ni adhabu ya viboko kwa watoto. Kuna baadhi ya nchi adhabu hiyo imefutwa, lakini kuna sehemu ambazo adhabu hiyo bado inatumika, hususan mashuleni na hata majumbani. Kwa mffano nchini Tanzania, adhabu hiyo ilifutwa mashuleni, lakini kutokana na mtokeo mabaya ya wanafunzi, serikali inafikiria kurudisha adhabu hiyo.

    Lakini, kwani matokeo mabaya yanatokana na viboko au ufundishaji? Binafsi nadhani ni njia za ufundishaji zinazotumiwa na walimu. Wakati mwingine unapomchapa mtoto kutokana na kosa lolote ndivyo unavyomjenga kuwa sugu, maana anajua kuwa akifanya kosa hilo atachapwa na mambo yanaishia hapo. Lakini kama ukibadili njia, na kumkalisha kitako kumweleza kwa ufasaha kosa lake na madhara yake, anaweza kuelewa na kutorudia tena kosa hilo. Nakubali kuwa kuna wakati viboko ni lazima vitumike, lakini sio katika kuwalazimisha watoto kufanya mambo ambayo kwanza hawajayaelewa, na pili wanaona kama wanaonewa.

    Licha ya shuleni, adhabu ya viboko pia hupendwa na baadhi ya wazazi pindi watoto wanapofanya makosa. Hilo linakubalika, lakini sio kwa kupitiliza kiwango. Unakuta mama au baba anamchapa mtoto mpaka anamtoa vidonda, akiulizwa, eti anamfundisha adabu. Ongea na mtoto wako kwa utaratibu, tafuta mbinu za kujua sababu iliyomfanya kutenda kosa hilo, na umweleze njia sahihi ya kufuata. Viboko hujenga usugu kwa mtoto. Ndio maana mwaka 1998, siku maalum ya kupinga adhabu ya viboko ilianzishwa na Shirikisho la kupinga adhabu hiyo. Lengo hasa la siku hiyo ni kutoa elimu zaidi kuhusu haki za watoto ambayo inapinga adhabu ya viboko.

    Adhabu ya viboko ilikuwepo sana enzi zetu. Sasa hebu kwanza tuangalie kwa hapa China. Kwa vijana wa sasa, ambao wamezaliwa miaka ya 80, wanachukuliaje njia hii ya kuwaelimisha watoto kwa viboko? Na watoto ambao wana uelewa wa haki zao, wanafikiri nini kuhusu adhabu hii? Kutokana na elimu ya siku hizi, vijana hao ambao nao kwa sasa wamekuwa wazazi, wanasema hawapendi kuwachapa watoto wao. Lakini pia kuna wakati wanashindwa kuvumilia na hivyo kujikuta wakiwaadhibu watoto kwa viboko, ingawa moyoni wanasikitika. Hebu tuwasikie baadhi yao

    "Baadhi ya wakati siwezi kuvumilia na hivyo namchapa mtoto wangu, lakini pia najuta baada ya kumchapa."

    "Baadhi ya wakati mtoto wangu ni mtundu sana, lakini kila baada ya kumchapa ninajuta."

    Wazazi hao wanajisikia vibaya wanapowaadhibu watoto wao kwa viboko. Lakini kwa yule ambaye anachapwa, ana lipi la kusema? Kuna baadhi wanasema mtoto huchapwa kwa sababu ya utundu wake. Hebu tuwasikilize watoto hawa

    "Nilichukua bastola ya maji ya mtoto mwingine kuchezea, bahati

    mbaya ikaharibika, baba yangu akanichapa."

    "Sikuchapwa sana, nilichapwa pindi nilipofanya makosa, nilipokuwa na mwaka mmoja mpaka miwili, walinipiga vibao usoni, nililia sana, kwa sababu nimepigwa."

    Walimu wenye uzoefu wa miaka mingi wa utoaji elimu wamesema, kufanya makosa kwa watoto ni hali ya kawaida. Yanayotakiwa kufanywa na wazazi na walimu ni kuwaambia kwa njia sahihi nini ni makosa. Kama kutumia viboko, ambayo ni njia ya kimabavu, watoto si kama tu hawajui nini ni makosa na nini ni jambo sahihi, bali watakuwa na moyo wa kupinga na hata chuki.

    Kule nchini Kenya hususan jijini Nairobi, Mark Muli alipata fursa ya kuhojiana na Kaserekea Kumbi, ambaye ni mzazi, kuhusiana na adhabu ya viboko kwa watoto. Bwana Kumbi anasema, mtoto anapokosea, ni lazima aadhibiwe, hata kwa viboko, lakini sio achapwe mpaka apate majeraha.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako