• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mji wa Tacheng waweka mkazo katika kuendeleza sekta yake ya ufugaji

    (GMT+08:00) 2015-07-28 17:36:24


    Mji wa Tacheng ni mji maarufu wa kihistoria ulioko kwenye Njia ya Hariri ya kaskazini, na ndipo ilipo forodha ya Baktu, ambayo ilifunguliwa mapema zaidi mkoani Xinjiang. Katika miaka ya karibuni, mji wa Tacheng umeiga uzoefu na ufundi wa kisasa kukuza sekta ya ufugaji kwa njia ya kufungua mlango kwa nje, na kupata mafaniko makubwa.

    Kwenye eneo la malisho la Woygayileo, mwandishi wetu wa habari ameona kuwa eneo hilo limegawanywa kwa kila hekta 33. Naibu mkurugenzi wa malisho hayo Bw. Jens Jumash amesema, baada ya kuiga uzoefu kutoka Australia, utaratibu huo umeanza kutekeleza njia mpya ya malisho kwa mifugo, kwani mifugo inapokuwa kwenye eneo moja, maeneo mengine yanafungwa. Bw. Jumash amesema utaratibu huo umewanufaisha wafugaji. Anasema,

    "Tangu mwaka 2013 tulipotekeleza utaratibu huu mpya wa ufugaji, wafugaji wetu wamenufaika sana. Kwanza, utaratibu huu unaweza kuzuia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza ya mifugo. Pili, majani ya malisho yanaweza kuhifadhiwa. Ya tatu, utaratibu huu umepunguza nguvu kazi, wafugaji wanaweza kushughulika na mambo mengine, mfano kufanya biashara."

    Bw. Nurtay Tolieohaz na familia yake wamehamia mjini hapo hivi karibuni, pamoja na kupeleka mifugo yake kwenye eneo la malisho, vilevile anatoa huduma zenye umaalumu kwa watalii. Anasema, utaratibu wa kufuga kwa zamu unaweza kutunza maeneo ya malisho, pia wafugaji wanaweza kupata faida kubwa zaidi kutokana na shughuli za utalii. Anasema,

    "Tuna mwezi mmoja tu toka tuhamie hapa, hivi sasa kipato chetu kinafikia yuan elfu 20 kila mwezi. Utaratibu wa ufugaji kwa zamu una manufaa gani? Majani yanahifadhiwa vizuri, na hii inasaidia mifugo yetu. Awali tulipoishi kwenye sehemu nyingine, tulipata yuan elfu 5 hadi 6 tu kila mwezi. Hivi sasa sera za serikali ni nzuri, na zimetunufaisha sana. Serikali imetujengea nyumba, na kuweka sehemu za kufuga kwa zamu. Hasa hivi sasa watalii wengi wanakuja hapa."

    Ili kuinua sifa ya mazao ya mifugo katika mji huo, Tacheng pia umejenga kituo cha msingi cha ufugaji wa kondoo aina ya Dorper. Maneja mkuu wa kampuni ya teknolojia ya mifugo ya Datang Shenghui Bi. Zhu Hongran amesema, wakati kampuni hiyo inapowasaidia wafugaji kuongeza kipato na kutajirika kupitia aina bora za mifugo, kampuni yake pia inafanya juhudi kuendeleza soko kwenye nchi za Asia ya Kati na Russia. Anasema,

    "Tuna mpango mmoja wa miaka 5, tutawekeza yuan milioni 200. na kila mwaka tunaweza kuuza kondoo 3,000. Kwanza tutakidhi mahitaji ya soko la Xinjiang, halafu tutapanua soko nchi nzima na hata nchi jirani. Kwa nini tumechagua mji wa Tacheng? Mji huo uko karibu na Kazakhstan na Russia, na tunaweza kufanya ushirikiano na nchi hizo mbili."

    Katibu wa kamati ya chama cha Kikomunisti cha China ya mji wa Tacheng Bw. Zhang Yan amesema, pendekezo la China kuhusu Ukanda Mmoja na Njia Moja limeleta fursa ya maendeleo kwa utamaduni, biashara na ushirikiano wa kimataifa kwa mji huo. Serikali ya huko itaimarisha ujenzi wa miundo mbinu ikiwemo mpaka wa Baktu, reli na uwanja wa ndege, ili kuweka mazingira mazuri kwa maendeleo ya sekta ufugaji inayolenga masoko ya nchi za nje. Anasema,

    "Tunafanya juhudi kuinua ufanisi wa forodha, tumeanza kujenga reli, tunaongeza uwezo wa uchukuzi wa barabara, pia tumeanza kupanua ujenzi wa uwanja wa ndege. Katika mpango wa 13 wa miaka 5, thamani ya uwekezaji kwenye uwanja wa ndege, forodha na reli itafikia yuan bilioni 7. Mazao ya mifugo yana umaalumu wa kipekee wa Mji wa Tacheng ulio kwenye Njia ya Hariri, hivi sasa tunafanya juhudi kuifanya forodha hiyo iwe njia ya uagizaji na usafirishaji wa mifugo na mazao ya mifugo."

    *********************

    Tunapoitaja Khorgos, watu wengi wanajua ni forodha muhimu ya nchi kavu ya China kwa Asia ya Kati, lakini hawafahamu kuwa Khorgos ina raslimali nyingi za utalii. Ili kukuza sekta ya utalii ya huko, mwaka huu Khorgos imeandaa shughuli mbalimbali za kuimarisha sekta hiyo, kama vile kuzindua ujenzi wa eneo la utalii la mlango wa taifa, kuandaa sikukuu ya utalii ya barafu na theluji kati ya China na Kazakhstan, na sikukuu ya kwanza ya utalii ya kimataifa ya maua ya peach, shughuli ambazo zimewafanya watalii kutoka ndani na nje ya nchi wafurahie utalii pamoja na manunuzi ya zawadi.

    Mwezi Julai, safari za treni za kimataifa zinazotoka Urumqi hadi Khorgos na Alma-ata nchini Kazakhstan zimezinduliwa, sera ya viza baada ya kuwasili imeanza kutekelezwa mwezi huu, na kampuni nyingi za utalii zimegundua fursa hii na kufanya maandalizi. Msaidizi wa maneja mkuu wa kampuni ya utalii ya Huayu ya Xinjiang Bw. Zhang Ziqin amesema,

    "Wakati tulipoambiwa kuwa Khorgos itatekeleza sera ya viza baada ya kuwasili, tulifanya juhudi kuwasiliana na baadhi ya mashirika ya kimataifa mjini Urumqi. Mara sera hiyo itakapotekelezwa, hakika watalii wanaopitia Khorgos wataongezeka sana. "

    Bw. Zhang Ziqin anaona kuwa Khorgos ina vivutio vingi vya watalii kutoka Kazakhstan, hasa mandhari ya kimaumbile na utamaduni wa makabila. Anasema,

    "Jimbo la Yili lina vivutio vingi vya watalii, kwa mfano malisho ya Narat, eneo la utalii la mlango wa taifa la Khorgos, malisho ya Kekedala, na ziwa la Sayram. Utamaduni na historia ya China pia zinawavutia sana, kwa mfano utamaduni wa kabila la Uygur, kabila la Kazakhstan na kabila la Sibe."

    Mjini Khorgos kuna wakazakhstan wengi wanaokwenda kununua bidhaa. Wanapendelea nguo, skafu na bidhaa za mahitaji ya maisha. Kwa sababu Kazakhstan bado haijafungua mlango kwa wachina walio na visa binafsi ya utalii, si rahisi kwa watalii wa China kwenda Kazakhstan. Lakini eneo la utalii la mlango wa taifa la Khorgos, soko la biashara la kimataifa la Yiwu lililoko kwenye kituo cha ushirikiano kati ya China na Kazakhstan, na maduka yasiyotozwa ushuru bado vinawavutia watalii kutoka sehemu mbalimbali nchini China.

    Akijulisha umaalum wa utalii wa huko, naibu mkurugenzi wa ofisi ya idara ya utalii ya Khorgos Bi. Ma Huanhuan anasema,

    "Kituo cha ushirikiano kati ya China na Kazakhstan ni cha pekee duniani kinachotumika na nchi mbili. Kuja kwenye kituo chetu ni kama kwenda nchi za nje, huu ndio utalii wa mpakani. Kwa kupitia kituo hicho, tumeandaa shughuli nyingi za utalii wa mpakani pamoja na Kazakhstan."

    Hivi sasa wakazakhstan walio na pasipoti na wachina walio na kitambulisho wanaruhusiwa kuingia kwenye kituo cha ushirikiano kati ya China na Kazakhstan. Bidhaa za Chocolate, manukato, na asali zinapendwa sana na watalii wa China. Kuanzia mwezi Januari hadi Mei mwaka huu, idadi ya watu waliokwenda kituo hicho imefikia milioni 1.1, ambayo ni ongezeko la asilimia 138 kuliko mwaka jana wakati kama huo.

    Hivi sasa Khorgos inafanya juhudi ili kukamilisha mapema iwezekanavyo utaratibu wa msamaha wa visa kwa utalii wa siku moja hadi saba kwa wachina wanaokwenda Kazakhstan. Naibu mkurugenzi wa eneo la uchumi la Khorgos Bw. Guo Jianbing ana imani kubwa kwa mustakabali wa utalii wa huko. Anasema,

    "Mpaka kufikia mwaka 2016 au 2017, sekta ya utalii ya Khorgos itapata maendeleo makubwa. Utalii wa vijijini, utalii wa utamaduni, utalii wa maeneo ya kihistoria, utalii wa forodha ya eneo la biashara huria, na utalii wa ununuzi kwenye maduka yasiyotozwa ushuru, vitasukuma mbele kwa pamoja ujenzi wa bonde la utalii la kimataifa lenye umaalumu."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako