• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Vitoweo kula kiafya

    (GMT+08:00) 2015-07-28 14:25:04

    Mwezi uliopita tuliwaelezea upishi wa kitoweo cha "Gongbaojiding" ambapo tuliwapasha faida mbalimbali ya viungo vinavyotumika kwenye kitoweo hicho. Katika kipindi cha leo tutaanza kuzungumzia chakula kingine ambacho ni maarufu sana hapa China kiitwacho Jiaozi. Wasikilizaji wetu wengi sana watakuwa wanaifahamu japo kwa kuisikia kwani ni chakula ambacho tumekuwa tukikielezea sana kwenye sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China.

    Leo tutapika Jiaozi. Jiaozi ambayo ni kama sambusa zilizochemshwa katika maji, ni chakula cha jadi kinachopendwa sana na watu wa China, watu wana utamaduni wa kula jiaozi katika siku maalumu kwa kalenda ya kilimo ya China. Hapa nchini China kuna msemo mmoja, "hakuna chakula kingine, ambacho ni chakula kitamu zaidi kuliko jiaozi", msemo huu unaonesha umuhimu wa jiaozi kati ya vyakula vya kichina. Jiaozi ni chakula kinachopikwa kwa kutumia unga, nyama na mboga, kwa hiyo ni chakula chenye lishe nyingi. Vitu vinavyoweza kutiwa ndani ya jiaozi ni vingi sana, hivyo imetimiza matakwa ya watu ya kuwa na lishe za aina mbalimbali.

    Kitu muhimu zaidi katika mapishi ya jiaozi ni vitu vinavyotiwa ndani yake, vitu hivyo ni vingi sana, ikiwa ni pamoja na nyama za aina mbalimbali zikiwemo ya nguruwe, ng'ombe, kondoo, au nyama ya kaa wa baharini, kamba kavu, nyama ya chaza, mboga kadhaa zinazoweza kupatikana kwa urahisi, vyote hivyo vinaweza kuwa vitu vinavyotiwa ndani ya jiaozi.

    Kila inapofika sikukuu ya Spring, ambapo vitu vinavyotiwa katika jiaozi, huwa vinachaguliwa kwa makini. Matamshi ya mboga ya qincai (figili) yanafanana na matamshi ya maneno "bidii ya kazi" na "mali, na ni kama tumaini la kupata mali nyingi na mara kwa mara, hususan huwa ni pongezi kwa bidii ya kazi na kupiga hatua halisi.

    Jiucai (chives ya kichina), ambayo ni matamshi ya mboga hiyo pia yanafanana na matamshi ya maneno yenye maana ya mali na muda mrefu, hivyo ni tarajio la kuwa na mali nyingi kwa muda mrefu; na matamshi ya mboga ya baicai (kabichi ya kichina), nayo pia yanafanana na matamshi ya maneno mia na mali, na ni matarajio ya kuwa na mali za aina mia moja. Jambo lingine linalostaajabisha watu ni ustadi wa utengenezaji wa jiaozi. Hivyo basi nampisha mwenzangu Pili aingie jikoni na kukuelezeeni taratibu zote za mapishi haya halafu tutaangalia faida zake mwilini kumbuka tule kwa afya.

    Kwa vile vifaa vya mapishi ya chakula hiki tayari tumeshaavielezea hivyo utengenezaji wa kimsingi kabisa ni kuweka mboga na nyama kwenye kipande chembamba cha unga cha duara, unga unakuwa kama wa sambusa ila mkato wake unakuwa duara kama unavyopika meatroll. Baada ya kutia vijazo vyako ambavyo tumesema unaweza kutia nyama za aina mbalimbali ukichanganya na mboga, unazifunga katika umbo la yuanbao, ambalo ni umbo maalumu la kipande cha madini ya dhahabu au fedha nchini China, mbali na hayo kuna watu wengine wanaopenda kutia nakshi za kupendeza kwenye jiaozi wakati wa kuzitengeneza. Kwa ujumla, jiaozi inaonesha matarajio mbalimbali ya watu juu ya maisha mazuri, vitu vinavyotiwa ndani jiaozi ni vitamu, tena vinaonesha kitu muhimu cha utamaduni wa China, kwa hiyo machoni mwa wageni kutoka nchi za nje, jiaozi ni chakula kinachoweza zaidi kuiwakilisha China. Kwa hiyo baada ya kuifunga unazipika kwa kuzichemsha huku ukiongeza maji kidogo kidogo. Ukimaliza hapo Jiaozi zako zinakuwa tayari. Na mimi huwa napenda zaidi kutoelea kwa siki, kwani ladha ya Jiaozi ukichanganya na uchachu wa siki unapata ladha nzuri zaidi na tamu.

    Msikilizaji natumai utakuwa umekwenda sambamba na mwenzangu Pili hapa katika kufuatilia hatua moja moja za upishi huu wa Jiaozi. Mimi nimeshawahi kuonja mara nyingi sana, na kwa kweli ni tamu sana kama anavyopenda Pili na mimi pia napenda kula kwa siki. Sasa wacha tuangalie upande wa pili wa mapishi haya kama tulivyosema mwanzo upishi huu au chakula hiki kina lishe sana kutokana na vifaa vinavyotumika kupikia Jiaozi. Hebu tuangalie mbogamboga ambazo zinaweza kutiwa kwenye chakula hiki. Wengi tunafahamu kuwa mboga nyingi zina manufaa makubwa mwilini. Ni chanzo cha vitamin C. halafu kwa wale wanaopenda kupunguza uzito ni vizuri sana wakila Jiaozi za mboga na mayai.

    Kuna mboga ambazo tumezitaja zikiwemo figili, kabichi la kichina, na nyenginezo. Mboga pia ni chanzo cha alkaline mwilini, wataalamu wanatushauri katika mlo wetu basi tuhakikishe lazima zinakuwepo mboga. Na kwa wale wasio fahamu miongoni mwa mboga ambazo zina alkaline nyingi mwilini ni kabichi. Hivyo wenye matatizo ya gesi au asidi nyingi tumboni basi kabichi au mbogamboga nyingi huwa zinasaidia kupunguza tatizo, bila kusahau kunywa maji mengi sana.

    Mbali na hayo kabichi ni mboga ambayo ina kalori kidogo sana, pia ina kitu kiitwacho anthocyanins ambacho kinasaidia mwili wako kupambana na saratani, ina folate ambayo inasaidia watoto kuwalinda wasizaliwe na kasoro.

    Na kwa vile tunazungumzia mboga ya kabichi iliyomo kwenye mapishi yetu ya leo ya Jiaozi, hebu tuiangalie mboga hiyo jinsi inavyochukuliwa katika nchi za Afrika hususan Tanzania. Kabichi ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya magonjwa mbalimbali licha ya kuchukuliwa kama ni mboga ya kimaskini na ambayo huliwa kwa shida zaidi kuliko kimanufaa ya kiafya. Ingawa inaonekana kuwa kabichi ni miongoni mwa mboga za majani zinazolimwa kwa wingi na kusambazwa kwenye masoko mengi ya Tanzania, hasa katika miji mikubwa, lakini ni watu wachache sana wanaopenda kula mboga hii.

    Katika miji mikubwa, kabichi inatumika zadi kwa walaji wa chips. Hata hivyo hawaitumia ipasavyo kwa sababu huwa inapikwa na kukaangwa kwa mafuta kwa muda mrefu na hivyo kupoteza baadhi ya virutubisho vyake muhimu. Miongoni mwa faida nyingi zinazopatikana kwa kula kabichi (nyeupe na nyekundu), inayoongoza ni ile ya kutoa kinga dhidi ya ugonjwa hatari wa saratani. Kwani inaelezwa kuwa zaidi ya tafiti 475 zimefanyika kuhusu virutubisho vinavyopatikana kwenye kabichi na kuthibitisha kuwa vina uwezo wa kuzuia ugonjwa wa saratani na wakati mwingine kutibu.

    Kabichi imeonekana kuwa na uwezo wa kipekee katika kupambana na ugonjwa huu kutokana na kuwa na kiasi kikubwa cha aina tatu muhimu za virutubisho; 'Antioxidant', 'Anti-inflammatory' na 'Glucosinolates,' ambazo zina uwezo wa kudhibiti magonjwa nyemelezi kadhaa ambayo husababisha saratani za aina mbalimbali mwilini. Kwa kuzingatia madhara na mateso yatokanayo na ugonjwa wa saratani, na kwa kuzingatia upatikanaji wa kabichi usiokuwa na gharama, huna sababu ya kupuuzia ulaji wake.

    Laiti kama watu wote tungejua sawasawa faida za kabichi, bila shaka mboga hii ingekuwa ghali kuliko hata samaki. Mbali ya kuwa na uwezo wa kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa saratani, Utafiti mwingine uliofanyika kuhusu kabichi umeonesha kuwa mboga hii huimarisha mfumo mzima wa moyo kwa kudhibiti utengenezwaji wa lehemu (cholesterol) mbaya mwilini ambayo inapozidi mwilini, husababisha matatizo ya moyo.

    Ndani ya kabichi, kuna kiwango cha kutosha cha aina mbalimbali za vitamin, hususan Vitamin K, Vitamin B1, Vitamin B2, Vitamin A na Vitamin C. Aidha, kabichi ina kiasi kingi cha kambalishe (fiber) Manganizi (Manganese), Potashiamu (Potassium) na Fatty-3 acids. Vyote hivi ni kinga ya mwili dhidi ya magonjwa nyemelezi. Ili kupata faida za kabichi na kujenga kinga imara dhidi ya magonjwa ya saratani, weka mazoea ya kula kabichi mara kwa mara, angalau mara tatu kwa wiki, kwa namna ambayo utaona mwenyewe inafaa, iwe kama mboga au kachumbari au kuchanhanya kijazo cha Jiaozi kama tulivyochanganya sisi kwenye mapishi yetu ya leo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako