• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Umoja wa Mataifa waanzisha kampeni ya "Okoa Maisha ya Mtoto" ili kuimarisha usalama barabarani kwa watoto

    (GMT+08:00) 2015-08-03 10:45:05

    Wanawake na watoto mara nyingi wamekuwa wahanga wa majanga mbalimbali ya kimaumbile kama vile machafuko, vita, njaa, na majanga mengine kama hayo. Lakini watoto wanakabiliwa na hatari nyingine kubwa, nayo ni ajali za barabarani. Shirika la Afya Duniani, WHO limesema uhai wa watoto uko mashakani kila uchao kutokana na ajali za barabarani. Shirika hilo limesema, kila siku watoto 500 hufariki dunia ilhali wengine wengi hujeruhiwa kutokana na ajali za barabarani, huku ajali hizo zikiwa chanzo kikubwa cha vifo kwa vijana barubaru hususan wavulana.

    Licha ya vifo hivyo, maelfu ya watoto hujeruhiwa, na jambo la kusikitisha zaidi, hali inazidi kuwa mbaya. Kutokana na hali hiyo, WHO imeamua kuangalia madhila ya watoto barabarani na kuchukua hatua kuhakikisha usalama wao. Shirika hilo linasema, kila dakika nne, mtoto mmoja anakufa kutokana na ajali za barabarani, moja ya tatu ya vifo hivyo ni watoto walio ndani ya magari, na theluthi mbili ni wanaotembea kwa miguu.

    Cha kusikitisha zaidi ni kwamba, nchi zinazoongoza kwa idadi ya watoto wanaofariki kutokana na ajali hizo ni zile zinazoendelea katika bara la Afrika, Asia Kusini, Latin Amerika na Ukanda wa Mediterania Mashariki, ambako idadi ya magari inaongezeka kwa kasi na ujenzi wa barabara kupamba moto, lakini kanuni za kuhakikisha usalama barabarani zinapuuzwa. WHO inasema vifo vya watoto kutokana na ajali za barabarani ni changamoto kubwa ambayo haijalishi uwezo au kipato kwa nchi husika. Dr. Etienne Krug, ambaye ni mkurugenzi wa idara ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, ulemavu, uhalifu, na majeraha anasema, miundombinu ya usafiri inapaswa kupangiliwa katika njia ambayo watoto watakuwa salama wanapoenda shule, wanapoenda bustanini kucheza, na hata wanapokwenda kuwatembelea marafiki zao.

    Ni kweli kabisa Carol maana mtoto wako anapokuaga kuwa anakwenda kwa rafiki yake unabaki roho juu mpaka atakaporudi. Dr. Krug amesema sawa, miundombinu ya usafiri inapaswa kuwa rafiki kwa ajili ya watoto. Kwa upande mwingine, wataalam wanatoa wito kwa umma kusimamia usalama wa watoto katika magari hapa nchini China. Utafiti uliofanyika hivi karibuni umegundua kuwa, chini ya asilimia 1 ya familia nchini China inatumia viti maalum vya watoto kwenye magari wakati wakienda matembezi na watoto wao.

    Ukiangalia idadi ya watu nchini China ambayo ni bilioni 3, na unaposikia kuwa chini ya asilimia moja ndio wanatumia viti vya watoto wanapokwenda matembezi, inatisha kwa kweli. Mama mmoja alipoulizwa kwa nini hatumii kiti maalum cha watoto kwenye gari anapokwenda matembezi na mwanae, alikuwa na haya ya kusema

    "Nadhani inategemea wapi tunakwenda. Kama ni safari itakayotufanya tupite barabara kuu, hapo nitamweka mtoto kwenye kiti chake katika siti ya nyuma. Lakini kama nampeleka chekechea tu, situmii kiti chake."

    Mtazamo huu ni wa wengi, kwa dhana kuwa, shule ni karibu na hakuna lolote linaloweza kutokea. Hii si kweli, waswahili husema ajali haina kinga, na bora kinga kuliko tiba. Gazeti la People's Daily la China limeripoti kuwa, katika miaka ya karibuni, zaidi ya watoto 18,000 walio chini ya miaka 14 wanafariki katika ajali za barabarani kila mwaka, na kwamba ajali hizo ni chanzo kikubwa cha vifo vya watoto wa umri huo.

    Ji Yuan ni polisi wa usalama barabarani katika mji wa Shenyang hapa China. Anasema sababu nyingine ambayo wazazi wanatumia ili kutotumia viti maalum vya watoto kwenye magari ni kwamba wana uhakika na uwezo wao wa kuendesha gari. Hata hivyo, polisi huyo anasema viti hivyo ni moja kati ya njia kubwa ya kulinda usalama wa watoto katika ajali za barabarani.

    "Wazazi hawatakiwi kujisahau. Haijalishi kama ni safari ya kupitia barabara kuu au safari fupi ndani ya mji. Kwa kuwa umenunua kiti maalum cha mtoto cha kwenye gari, unapaswa kukitumia kikamilifu ili kuhakikisha usalama wa mtoto wako."

    Inaaminika kuwa, ukosefu wa sheria ya usalama wa watoto katika magari ni sababu kubwa ya matumizi haba ya viti hivyo maalum vya watoto kwenye magari. Kwa wakati huu, ni mji wa Shanghai na mkoa wa Shandong ambayo inatekeleza kanuni hizo, na wakati huohuo, ubora wa viti hivyo unafuatiliwa kwa makini na maofisa. Sun Huichuan anafanya kazi kwenye mamlaka ya ukaguzi wa ubora, na anasema kutakuwa na usimamizi mzuri zaidi ili kuhakikisha ubora wa bidhaa ya viti vya usalama vya watoto.

    "Viti vya usalama vinajumuishwa mahsusi katika utaratibu wa ukaguzi wa taifa kwa ubora wa bidhaa mwaka huu. Katika hatua inayofuata, tutaanza ukaguzi wa ghafla wa viti vya usalama kutoka maduka yote, ya kupitia mtandao wa internet nay a kawaida. Kwa upande mmoja, tutautangazia umma chapa ambazo hazina ubora, na kwa upande mwingine, kampuni zinazohusika zitafungwa mpaka zitakapokuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye ubora"

    Kuanzia mwezi Septemba mwaka huu, viti maalum vya watoto vinavyoingia kwenye soko vitatakiwa kuwa na hati maalum ya China, hivyo kuhakikisha zaidi usalama wa watoto katika magari.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako