• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Pikipiki za kubebea wagonjwa zapunguza kiwango cha vifo vya mama wajawazito

    (GMT+08:00) 2015-08-10 14:42:56

    Vifo vya uzazi ni moja ya tishio kubwa sana la afya. Kila saa 24, takriban wanawake 800 wanafariki kutokana na matatizo ambayo mara nyingi yanaweza kutibika yanayohusiana na ujauzito na kujifungua. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, asilimia 99 ya vifo vya uzazi vinatokea katika nchi zinazoendelea, hususan zile zilizoko kusini mwa Sahara na Asia Kusini. Ndio maana mashirika mbalimbali ya kimataifa, taasisi za afya za kitaifa, na mamlaka za afya zinaungana pamoja kupambana na vifo vya uzazi katika sehemu zinazoathirika zaidi na matatizo hayo. Katika juhudi hizo za kutafuta ufumbuzi wa tatizo la vifo vya uzazi ambalo pia husababishwa na kuchelewa kufika hospitali kwa wajawazito, njia nyepesi ya usafiri ikagunduliwa.

    Kuanzishwa kwa pikipiki za kubebea wagonjwa katika maeneo ya vijijini nchini Uganda kumesaidia sana kuokoa mamia ya akina mama wajawazito pamoja na watoto ambao hawajazaliwa ambapo vinginevyo wangeweza kupoteza maisha kama sio huduma hiyo. Katika kipindi cha mwaka mmoja tu tangu huduma hii ianzishwe na kuchukua nafasi ya magari ya kubebea wagonjwa katika wilaya ya Mbale nchini Uganda, kiwango cha vifo vya uzazi kimepungua kwa kiasi kikubwa.

    Mlima Elgon upo mashariki mwa Uganda. Ingawa mlima huu ni mzuri sana na wa kuvutia, lakini mteremko wake unasababisha changamoto kubwa kwa watu wanaojaribu kwenda kupata huduma za afya. Maeneo haya mengi hayawezi kufikiwa kwa magari, hivyo wagonjwa wanalazimika kutembea umbali mrefu sana kuweza kufika kwenye vituo vya wajawazito pamoja na hospitali. Na wale wanaoathirika zaidi ni mama wajawazito pamoja na watoto. Katika kesi za dharura za kujifungua, mama mara nyingi anakuwa kwenye hatari ya kupoteza mtoto au hata maisha yake.

    Kama ulivyosema Pili waathirika wakubwa ni wajawazito na watoto, lakini kwa sasa, tatizo hilo linaonekana kupungua, kwani ukimpiga simu tu dereva wa pikipiki ya wagonjwa anakuja kukusaidia kubeba na kukufikisha mahali ambapo magari ya kawaida ya kubebea wagonjwa hayawezi kufika. Na pia hakuna tena haja ya kusumbuka kutembea kwa masafa marefu. Dereva mmoja wa pikipiki hizo aitwaye Lameck Manuali anapokea simu na hapohapo kupandia pikipiki yake kwa haraka. Pikipiki yake yenye uwezo kupita kwenye ardhi ya aina mbalimbali pembeni ina kigari kidogo chenye kitanda. Pikipiki hizi zimetengenezwa kwaajili ya watu waishio maeneo ya milimani, na njia zisizopitika Akielezea kuhusu idadi ya vifo tangu pikipiki hizi zianzishwe Bwana Lameck anasema.

    "Tangu pikipiki za wagonjwa zianze kutumika hadi sasa ni mgonjwa mmoja tu aliyefariki dunia ambaye ni mzee, lakini wagonjwa wote tunaowabeba wako hai, kwa hiyo siku hizi mtu yeyote anayeumwa huwa napigiwa simu tu, nakwenda."

    Pikipiki hizi za kubebea wagonjwa zinalazwa kwenye vituo vya afya wilayani hapo, na wafanyakazi wa afya au watu wa jamii ya huko wanafunzwa namna ya kuziendesha na kuzitunza. Zinafaa zaidi kuendesha kwenye njia mbovu na za vilimani kuliko magari ya kawaida ya kubebea wagonjwa, hususana katika msimu wa mvua, lakini kwa mujibu wa Bwana Lameck, pikipiki hizi pia nazo zina kikomo chake.

    "Changamoto kubwa ninayokumbana nayo ni kwamba barabara ni mbaya sana, na baadhi ya wakati huwa hazipitiki kabisa, na hususan pale inaponyesha mvua wakati mwingine unapigiwa simu na bahati mbaya huwezi kupatikana, hadi mtu aje kwa miguu kuniita halafu ndio nakwenda".

    Sasa pikipiki hizi za kubebea wagonjwa zimeanzishwa na wilaya ya Mbale ikiwa ni kama sehemu ya mradi wa serikali ya wilaya uitwao Umoja wa Mbale Dhidi ya Umasikini. Na kwa sasa umeenea hadi kwenye wilaya nyingine tatu za jirani. Afisa wa afya wa wilaya John Baptist Waniaye anasema mradi huo umekuwa na ufanisi mkubwa katika kupunguza idadi ya vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua.

    "Tulikuwa na kiwango kikubwa sana cha vifo vya wajawazito kuliko kile cha wastani cha taifa, kwa hiyo suala hili lilikuwa linatishia sana na tukiwa kama watu wa afya tulikuwa tunasema kwamba tunachoweza kufanya ni kubadili hali, kwa hiyo kuja kwa hizi pikipiki ilikuwa ni njia mojawapo ya kubadili hali, ambayo tunaona itabadili kiini cha hali ya afya ya wazazi na huduma za afya za watoto wilayani".

    I Idadi ya vifo vya uzazi nchini Uganda katika mwaka 2013 ilikuwa 435 kati ya laki moja, ambapo katika wilaya ya Mbale idadi hiyo ilikuwa iko juu zaidi ambayo ni vifo 680. Lakini Bw. Waniaye anasema idadi hiyo imepungua sana tu tangu kuanzishwa kwa pikipiki za kubebea wagonjwa. Na mbali na hapo pia anasema maendeleo hayo ya kupatikana kwa pikipiki za kubebea wagonjwa yamepelekea wanawake wengi kujifungulia kwenye vituo vya huduma ya afya. Kwani anasema kabla ya kuanzishwa kwa huduma hii, akina mama wajawazito wa maeneo ya vijijini walikuwa wakijifungulia nyumbani kwa msaada wa wanawake wazee au wakunga wa jadi.

    "Pikipiki iliyoletwa katika Kaunti ndogo ya Wanale ilikuwa ni ya kwanza kabisa kuletwa na hilo ni eneo ambalo ni la mlimani kabisa na ni vigumu kufikika, ambapo kama unataka kwenda kumchukua mama mwenye uchungu wa kujifungua unalazimika kupata wanaume labda kumi hivi wenye nguvu wa kumbeba na kuendelea kubadilishana wakati wakimbeba huyo mama kwenye kitanda na kumpeleka Hospitali ya Mbale ili apatiwe huduma ya dharura ya afya."

    Lakini pikipiki hizo zina faida moja kubwa ambayo ni gharama nafuu. Pikipiki za kubebea wagonjwa ni rahisi mara nne zikilinganishwa na magari ya kubebea wagonjwa.

    "Magari mengi ya kubebea wagonjwa ni kwa ajili ya vituo vya afya, katika wilaya nyingi, utayaona yameegeshwa tu, unajua kwanini yameegeshwa tu? kwasababu ya tatizo la milima na ukosefu wa mafuta ya kwenda kuwachukua wagonjwa na kuwapeleka hospitali. Sasa kwa uvumbuzi huu, kwa vile zipo katika muundo wa pikipiki, unajua kuwa pikipiki zinatumia mafuta kidogo kuliko magari, kwa hiyo unaweza kujaza lita moja tu ya mafuta na inaweza kumpeleka na kumrejesha mgonjwa hospitali, kwa hiyo kimsingi hiyo ndio tofauti yao."

    Mbali na nchini Uganda pikipiki hizi za kubebea wagonjwa pia zinasaidia katika nchi mbalimbali za Afrika. Nchini Sudan Kusini pikipiki hizi zimenunuliwa na kusambazwa katika vituo vya afya katika majimbo matano ya nchi hiyo. Lakini mbali na hapo madereva wa pikipiki hizo pia wamepatiwa mafunzo juu ya mambo ya msingi ya huduma za afya za wajawazito na watoto. Hadi kufikia mwaka 2013 pikipiki hizi zimebeba wajawazito wapatao 272 na kuwafikisha salama hospitali ili waweze kujifungua na kupata huduma nzuri.

    Hapa msikilizaji tuna mfano mzuri wa mama mmoja aitwaye Martha Ajak, mama huyu ana watoto watatu na anatokea katika kijiji cha Karic. Anasema pikipiki hizi zimeokoa maisha yake na kwamba hivi sasa asingekuwepo hapa kama sio msaada wa pikipiki hizo. Martha alipelekwa hospitali kutokana na matatizo wakati wa kujifungua na anashukuru sana kwa kuwepo usafiri huo wakati ambao alikuwa akiuhitaji. Bibi Martha anataraji kuwa pikipiki hizi zitaongezwa zaidi kwasababu kituo cha afya kinahudumia wilaya nne hivyo kuwepo kwa pikipiki hizi kutaweza kusaidia na kina mama wa maeneo mengine.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako