• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Masharti ya uingizaji wa mitaji ya kigeni nchini China yaongezeka

    (GMT+08:00) 2015-08-21 13:47:08


    Mwezi Aprili mwaka huu, kampuni kubwa ya kutengeneza ndege ndogo ya Canada, Bombardier inayoshika nafasi ya 3 duniani kwa utengenezaji wa ndege ya abiria hivi karibuni ilifungua kituo cha ukarabati wa ndege ya kibiashara kwenye eneo la biashara huria la Tianjin. Uwekezaji wa jumla uliowekezwa katika mradi huo ni dola za kimarekani milioni 30, na kituo hicho chenye eneo la mita za mraba 9,350, kitatoa huduma za utunzaji, ukarabati, uhifadhi, uuzaji na uagizaji wa vipuri, na usimamizi wa kiufundi wa ndege, pamoja na huduma za maegesho na usafishaji wa ndege.

    Naibu afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Bombardier Michel Ouellette anasema, "Tianjin ina uwezo wa kufanya ukarabati na utunzaji kwa ndege zote za kibiashara."

    Hivi sasa takriban ndege 120 za kibiashara za Bombardier zinatumika hapa China, idadi ambayo ni theluthi moja ya ndege zote za kibiashara nchini. Ilichukua siku moja tu kwa kampuni hiyo kupata leseni ya biashara kwenye eneo la biashara huria la Tianjin. Mbali na utoaji wa haraka wa leseni, baada ya tarehe 8, Mei, uwekezaji wa kigeni umeanza kuruhusiwa kuingia kwa uhuru katika sekta karibu zote kwenye eneo la biashara huria la Tianjin. Naibu mkurugenzi wa kamati ya usimamizi wa eneo hilo Jiang Guangjian anasema, "Kampuni za kigeni zinatakiwa kuandikishwa tu kabla ya kufanya usajili wa biashara, na hatua nyingine zote za utaratibu wa zamani wa uidhinishaji zimefutwa."

    Mwezi Aprili mwaka huu, Baraza la Serikali ya China lilitangaza "kanuni za usimamizi maalumu wa utoaji wa ruhusa ya kuingia kwa uwekezaji wa kigeni kwenye maeneo ya majaribio ya biashara huria" na "mpango wa majaribio wa ukaguzi wa usalama wa taifa kwa wawekezaji wa nje kwenye maeneo ya majaribio ya biashara huria", sera ambazo zitatekelezwa katika maeneo manne ya biashara huria ya Shanghai, Guangdong, Tianjin na Fujian. Kati ya hatua 122 maalumu zilizowekwa kwenye Orodha ya sekta zisizokubalika kwa uwekezaji wa nje (Negative List), 85 ni za vizuizi, na 37 ni za marufuku. Ikilinganishwa na toleo la mwaka jana, orodha ya mwaka huu imepunguza hatua 17 kuliko mwaka jana, na hatua 68 kuliko mwaka juzi, hatua ambacho inalenga kwenda sambamba na kanuni za kimataifa na kufungua zaidi kwa nje.

    Usimamizi kuhusu haki ya kiraia na kanuni hizo kabla ya uwekezaji wa kigeni kuruhusiwa kuingia nchini ni hatua muhimu ya China ya kufungua mlango kwa nje na kuhimiza mageuzi, pia ni uvumbuzi wa kisera wa kuzoea hali mpya ya mfungamano wa uchumi duniani na mabadiliko ya kanuni za uwekezaji wa kimataifa. Kutokana na maeneo ya biashara huria kujaribu kuimarisha sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, China inatarajia kupata uzoefu mwingi zaidi ili kuweka msingi wa kutekeleza sera hizo kote nchini China. Naibu mkurugenzi wa kamati ya usimamizi ya eneo la biashara huria la Shanghai Zhu Ming anasema, "Lengo kuu la utekelezaji wa hatua zilizotolewa katika orodha ya marufuku ni kuhamasisha ipasavyo uhai wa uvumbuzi na ujasiriamali katika masoko yanayoruhusiwa kuwekezwa kwa mujibu wa orodha hiyo, kwani hivi sasa shughuli nyingi za uvumbuzi na ujasiriamali zinafanyika kati ya sekta na viwanda tofauti."

    Baada ya mageuzi kuimarishwa katika maeneo ya biashara huria, kanuni hizo zitarekebishwa na kupunguza idadi ya vipengele, na wakati huohuo maeneo yanayoruhusiwa kuwekezwa pia yataongezeka. Hali halisi ni kuwa, kuhimiza ufunguaji mlango kupitia kuimarisha mageuzi hakutokei tu kwenye maeneo ya biashara huria. Mwezi Aprili, orodha ya mwongozo wa sekta zinazowekezwa na wawekezaji wa nje ya nchi iliyofanyiwa marekebisho ilianza kutekelezwa, na imepanua wigo wa uwekezaji katika sekta ya huduma na utengenezaji wa kawaida. Ikilinganishwa na ya zamani, katika orodha mpya ya mwongozo, vizuizi kwa wafanyabiashara wa kigeni vilipunguzwa hadi 38 kutoka 79, na katika vizuizi kuhusu mgawanyo wa hisa kwa wafanyabiashara wa kigeni, vipengele vya "ubia na ushirikiano" vilipunguzwa hadi 15 kutoka 43, vipengele vya "asilimia kubwa ya hisa inamilikiwa na upanda wa China" vimepunguzwa hadi 35 kutoka 44.

    Sera bora, soko kubwa na huduma zinazozidi kupevuka zimefanya kampuni za kigeni kuwa na matumaini mazuri na uwekezaji wao nchini China. Tokea mwaka huu uanze, kampuni maarufu za kimataifa za Roche, Air Products and Chemicals na Bosch zimeendelea kuongeza uwekezaji wao nchini China. Kwa mujibu wa uchunguzi wa biashara ya China kwa mwaka 2015 uliofanywa na Shirikisho la Wafanyabiashara wa Marekani la Shanghai, asilimia 67 ya kampuni zilizohojiwa zinapanga kuongeza uwekezaji nchini China. Ripoti ya uchunguzi iliyotolewa mwezi Februari mwaka huu na Shirikisho la Wafanyabiashara wa Marekani la China kuhusu mazingira ya kibiashara kwa mwaka 2015 inasema, asilimia 73 ya watu waliohojiwa wanaona kuwa mwaka jana, kampuni zao zilipata faida au faida kubwa, ingawa wana wasiwasi na usimamizi wa idara husika za China na kupanda kwa gharama ya nguvukazi, na asilimia 70 ya watu waliohojiwa bado wana matumaini na faida zinazoweza kupatikana katika soko la China.

    Kampuni ya CITIC iliyoanzishwa mwaka 2011 ni kampuni ya kimataifa inayohusisha mambo ya fedha na sekta ya utengenezaji, na kuanzishwa kwake kulifanywa na kundi la CITIC, kampuni inayomilikiwa na serikali ya China. Ili kuhimiza aina tofauti kwenye muundo wa hisa na mambo ya kimataifa ya kampuni, mwezi Januari mwaka huu, wafanyabiashara wa kigeni waliwekeza kwenye kampuni hiyo, ambapo kampuni ya Chia Tai Guang Ming iliingia ubia na kampuni ya ITOCHU ya Japani na kampuni ya Chia Tai ya Thailand ilitumia dola za kimarekani bilioni 80 kununua asilimia 20 ya hisa ya kampuni ya CITIC. Vyombo vya habari vinasema huu ni uwekezaji mkubwa zaidi uliofanywa na kampuni ya Japani kwa kampuni ya China. Naibu mkuu wa taasisi ya mambo ya fedha ya kimataifa ya Lujiazui kati ya China na Ulaya Liu Shengjun anasema, "CITIC ni mfano unaostahili kufuatiliwa katika mageuzi ya kampuni inayomilikiwa na serikali ya China, ambapo baada ya wawekezaji kutoka nje ya nchi kumiliki asilimia kubwa ya hisa, wanaweza kushiriki kwa kiasi kikubwa katika usimamizi wa kampuni hiyo, na hata kushika nafasi za uongozi, jambo ambalo litachangia zaidi kwenye mabadiliko ya utaratibu wa uendeshaji wa kampuni zinazomilikiwa na serikali ya China. Pia linaweza kusaidia kukomboa mawazo ya kampuni hizo, kwa kuwa mabadiliko ya utaratibu wa kampuni yatapatikana baada ya mgawanyo wa hisa kubadilika kihalisi."

    Uamuzi wa kuimarisha mageuzi kamili uliotangazwa katika mkutano wa tatu wa wajumbe wote wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China umetoa kipaumbele kwa mageuzi kuhusu umiliki wa muungano kwenye kampuni zinazomilikiwa na serikali. Mageuzi kuhusu umiliki wa muungano yanaweza kusaidia China kujenga soko lenye usawa na haki zaidi. Pia kuingiza uwekezaji wa kigeni na mtaji wa sekta binafsi katika kampuni zinazomilikiwa na serikali kunaweza kuongeza nguvu ya ushindani na uvumbuzi kwa kampuni hizo.

    Hivi sasa, uchumi wa China unashuhudia mabadiliko ya ukuaji kutoka kasi kubwa hadi kiwango kinachofaa, na njia ya maendeleo ya uchumi itazingatia zaidi ubora na ufanisi. Muundo wa uchumi utarekebishwa kwa kushughulikia malimbikizo na kuboresha ongezeko la uchumi, na kupata sekta mpya zinazoweza kuleta maendeleo ya uchumi. Naibu katibu mkuu wa Kamati ya Taifa ya Maendeleo na Mageuzi ya China Wang Yiming anasema, "Hatuwezi kupata ongezeko endelevu la uchumi kwa kutegemea mkakati wa zamani wa kupanua ukubwa wa viwanda, na katika siku za baadaye kwa uhakika tutafanya juhudi za kuendeleza mnyororo wa thamani wa viwanda. Ndiyo maana tunavutia uwekezaji wa kigeni huku tukitarajia uwekezaji huo utajikita zaidi katika utafiti, maendeleo na ubunifu, na kampuni za ndani na nje ya China zitaweza kufanya kazi kwa pamoja ili kuinua kiwango cha mageuzi ya sekta ya utengenezaji nchini China."

    Kwa takriban miaka 30, China imefanya juhudi kuvutia uwekezaji kutoka nje, hivi sasa imeingia kwenye kipindi cha kuingiza kwa ufanisi uwekezaji kutoka nje ikiwa sambamba na kutoka nje kwa wingi kwa mitaji ya China. Kampuni za kigeni zinazohusisha utengenezaji wa hali ya chini zimeshindwa kukidhi mahitaji ya maendeleo ya uchumi wa China unaorekebishwa, hivyo njia ya mitaji ya kigeni kuingia China na maeneo yatakayowekezwa pia yanatakiwa kufanyiwa marekebisho kwa mujibu wa hali inavyobadilika nchini China. Naibu spika wa zamani wa Bunge la Umma la China ambaye ni mwanauchumi maarufu nchini China Cheng Siwei anasema, "Hatutavutia uwekezaji wa kigeni kutokana na hitaji la fedha kama ilivyokuwa zamani, hivi sasa tunapaswa kuvutia wawekezaji wengi zaidi kwa mujibu wa mkakati wa taifa letu, yaani ni wawekezaji wanaoweza kutusaidia katika sekta za teknolojia, soko na usimamizi. Pia tunatarajia kuwa watawekeza katika maeneo yetu dhaifu na yale tunayotarajia kuendeleza, kama vile sekta za nishati mpya na huduma za kisasa. Hivi sasa baadhi ya sehemu za magharibi mwa China bado zinahitaji fedha, na kama tatizo linalozikabili ni upungufu wa fedha tu, zinaweza kuomba msaada kutoka serikali, lakini sio kuingiza ovyoovyo uwekezaji wa kigeni, haswa kampuni zile zinazolenga kuhamisha uchafuzi wao hapa China."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako