• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Smartphone app zatumika kukusanya na kuondoa vijidudu kwenye maziwa ya mama nchini Afrika Kusini

    (GMT+08:00) 2015-08-24 14:47:33

    Sote tunafahamu umuhimu wa kumnyonyesha mtoto mchanga, na kuzingatia ule muda uliopendekezwa wa kunyonyesha. Lakini kuna baadhi ya kina mama kwa sababu moja ama nyingine wanashindwa kunyonyesha watoto wao, labda ni kutokana na maradhi, au wanaweza kuwa na sababu zao binafsi. Kitu kimoja kiko wazi, ni muhimu sana kwa mama kumyonyesha mtoto kwa faida ya mama mwenyewe na pia kwa faida ya mtoto.

    Kunyonyesha ni muhimu. Mama anaponyonyesha mtoto wake, anajenga ukaribu na mtoto huyo, na kuwa na muunganiko ambao hauwezi kamwe kuvunjika. Ni kutokana na kunyonyesha ndipo mtoto anamtambua mama yake, ingawa ni mdogo na hatambui kitu, lakini mara anapokuwa kwenye mikono ya mama yake anajua yuko mahali salama na anaweza kupata mlo wake unaostahili. Kuna baadhi ambao wana matatizo ya kiafya hivyo wamekatazwa na madaktari kunyonyesha watoto, lakini pia kuna wale ambao wanaogopa kunyonyesha watoto wao, kisa tu, matiti yao yatapoteza mvuto wake, sasa hebu tujiulize, kipi bora, matiti kuwa au mvuto na mtoto kuathirika?

    Nchini Afrika Kusini, smartphone app ni njia mpya inayotumika kukusanya, kuondoa vijidudu, na kuuza maziwa halisi ya mama. Njia hiyo inawasaidia watoto wengi zaidi kupata maziwa ya mama na pia kuokoa maisha yao. Katika hospitali ya King Edward wa 8 mjini Durban, Afrika Kusini, muuguzi mmoja anajiandaa kumlisha mtoto maziwa hayo yaliyotolewa msaada mpaka pale mama wa mtoto atakuwa na hali nzuri na kuweza kumlisha mtoto wake mwenyewe.

    "Mtoto huyi mdogo amezaliwa njiti, uzito wake ni gram 980. Watoto njiti wanasumbuliwa sana na ugonjwa unaoitwa kitaalam necrotizing enterocolitis, NEC. Kwa sababu viungo vya watoto hawa bado havijakomaa vizuri, utumbo wao ni dhaifu sana hauwezi kuhimili maziwa ya aina nyingine. Hivyo tunawapa maziwa ya mama kwa kuwa yana virutubisho muhimu. Tatizo kubwa linaloweza kutokea kwa watoto njiti ni NEC na maziwa ya aina nyingine pia yanaweza kutengenezwa katika mazingira ambayo sio masafi, hivyo maziwa ya mama ni bora zaidi. Yanapambana na maambukizi yoyote anayoweza kuwa nayo mtoto, hivyo ni msaada mkubwa sana"

    Katika hospitali ya King Edward wa 8, maziwa ya mama yanakusanywa na kurutubishwa kwa kutumia app moja kwenye simu za kisasa za mkononi, inayoitwa iThemba Lethu Community Milk Bank Project. Hebu tumsikilize meneja wa app hiyo Sandy Reid akieleza jinsi inavyofanya kazi

    "Cha kushangaza kuhusu utaratibu huu ni kwamba, inafanyika kwa kupima joto kwa kutumia kifaa maalum kilichounganishwa kwenye simu yenye app hiyo ambacho kinafuatilia halijoto ya maziwa, na muda gani maziwa hayo yanatakiwa kupoozwa. Na pia tunaweza kuhifadhi taarifa kwenye sehemu inayoweza kusimamiwa katika na sehemu mbalimbali na kupata uhakiki wa ubora wake kupitia njia hiyo"

    Software hiyo inayojulikana kama Foneastra app iliundwa na Mradi wa teknolojia sahihi ya huduma ya afya, kwa kushirikiana na chuo kikuu cha Washington na Chuo kikuu cha Kwazulu Natal. Jo-Anne Breedkamp ni mmoja wa wakina mama wanaotoa maziwa yao kwenye mradi huo unaowanufaisha watoto waliozaliwa na uzito mdogo, watoto ambao wazazi wao wana VVU, na yatima.

    "Kukamua maziwa sio jambo rahisi kabisa duniani, hususan kama una familia, na pia inahitaji watu wote katika familia kuwajibika. Lakini hata kama ukipata milimita 5 au 10 kwa wakati, igandishe, unaweza kufanya tena kesho, na inafurahisha unapoweka maziwa na kuona idadi inaongezeka, na pia kufahamu kuwa sijawahi kukutana na watoto hawa lakini ninawapa mwanzo mzuri. Namshauri mtu yeyote ajaribu na kuleta mabadiliko"

    Ni muhimu sana kwa mama kunyonyesha mtoto wake, kwani maziwa ya mama yana virutubisho ambavyo havipatikani kwenye maziwa ya kopo wala ya ng'ombe. Na pia tukumbuke kuwa, unapomnyonyesha mtoto, hakuna uchafu wowote ambao mtoto anaweza kula kwa sababu maziwa hayo yanatoka moja kwa moja kwa mama, hayapiti sehemu nyingine yoyote.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako