• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ulaya yakabiliwa na wimbi kubwa zaidi la wakimbizi baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia

    (GMT+08:00) 2015-08-25 10:43:37

    Chansela wa Ujerumani bibi Angela Merkel na rais Francois Hollande wa Ufaransa wamekutana huko Berlin ili kujadili njia za kukabiliana na suala la wakimbizi linalozidi kuwa baya siku hadi siku.

    Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, wakimbizi kutoka nchi za Mashariki ya kati na Afrika ya kaskazini kama vile Syria na Libya wamemiminika kwa wingi barani Ulaya, na kuhamia katika sehemu zilizoendelea za Ulaya kupitia Ugiriki na Italia. Takwimu zimeonesha kuwa, kwa mwezi Julai pekee, wakimbizi zaidi ya laki moja walivuka mpaka na kuingia barani Ulaya, idadi ambayo imevunja rekodi ya historia. Katika sehemu ya Balkan, bado kuna wakimbizi wengi wanaovuka Macedonia na Serbia na kuingia Ulaya ili kutafuta uhifadhi.

    Ili kukabiliana na suala la wakimbizi, Ujerumani na Ufaransa zitakuwa na mzigo mzito, kwani kwa hivi sasa nchi hizo mbili zimepokea wakimbizi wengi zaidi. Mwaka huu Ujerumani huenda itapokea ombi la hifadhi kutoka kwa wakimbizi zaidi ya laki 8. Bibi Merkel aliwahi kuonya kuwa, kumiminikia kwa wahamiaji haramu ni tatizo kubwa linalokabili Umoja wa Ulaya, ambalo ni kubwa zaidi kuliko suala la madeni ya Ugiriki. Kwa mtazamo huo, bibi Merkel ametoa wito kuitaka kamati ya Umoja wa Ulaya ifanye juhudi kubwa zaidi, akisema,

    "Kama tunavyojua, sehemu nyingi za Ulaya zina sera moja ya kushughulikia wakimbizi, lakini utekelezaji katika sehemu mbalimbali ni tofauti. Ujerumani na Ufaransa zinataka nchi wajumbe wote wa Umoja wa Ulaya ziweze kutekeleza kikamilifu sera zilizopo za kushughulikia wakimbizi, zikiwemo utaratibu wa kusajili wakimbizi, kigezo cha msingi kuhusu kambi ya wakimbizi na uhakikisho wa kimsingi wa matibabu na afya. Tunaomba kamati ya Umoja wa Ulaya ifanye kazi kwa ufanisi, na kuhimiza nchi wajumbe wa Umoja huo zitekeleze kigezo kimoja cha kupokea wakimbizi."

    Rais Hollande wa Ufaransa amekubaliana na bibi Merkel, akisisitiza kuwa jambo muhimu kwa sasa ni kwamba nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya hasa Italia na Ugiriki zitekeleze kigezo cha sasa cha kupokea wakimbizi, kugawa kwa mwafaka idadi ya wakimbizi katika nchi wanachama wa Umoja huo na kutekeleza utaratibu wenye ufanisi wa kurudisha wahamiaji haramu. Rais Hollande anasema,

    "Nafafanua mapendekezo ya bibi Merkel kuhusu Ufaransa na Ujerumani kukabiliana na suala la wakimbizi. Kwanza Italia na Ugiriki zianzishe haraka kituo cha kupokea wakimbizi, ili kurahisisha wakimbizi wanaowasili kwa njia ya bahari na ardhi kavu wa Umoja wa Ulaya wasajiliwe hapohapo. Vilevile tunapaswa kutofautisha kwa makini wale wanaotafuta hifadhi na wahamiaji haramu, na hatutapokea wahamiaji haramu."

    Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana, bibi Merkel na rais Hollande pia wamesema, kwenye mkutano wa wakuu wa Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika utakaofanyika wakati wa majira ya mpukutiko mwaka huu, wakuu hao watajadiliana na nchi za Afrika kuhusu makubaliano ya kuwarudisha wakimbizi. Aidha, Umoja wa Ulaya pia utasaidia nchi jirani na Syria kama vile Jordan, Lebanon na Uturuki, kujenga kambi za wakimbizi zenye mazingira mazuri zaidi.

    Licha ya suala la wakimbizi, mgogoro kati ya kundi lenye siasa kali nchini Ujerumani na wakimbizi pia unaongezeka. Mwishoni mwa wiki iliyopita, watu wenye siasa kali wapatao 200 walikusanyika nje ya kambi ya wakimbizi na kufanya vurugu. Bibi Merkel amelaani vurugu hizo na kusema kuwa kitendo hicho hakivumiliwi nchini Ujerumani. Pia amesisitiza kuwa, Ujerumani ni nchi yenye demokrasia na kutawaliwa kisheria, katiba inahakikisha haki za binadamu za watu wote hazikiukwi, wakiwemo wakimbizi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako