• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Utenzi wa mfalme Gesar, ensaiklopidia ya utamaduni wa Tibet

    (GMT+08:00) 2015-09-11 09:10:09

    Utenzi wa mfalme Gesar ni shairi la kughani linalojumuisha historia, mashairi, mithiolojia, methali na hekaya za Tibet ya kale. Kutokana na kufariki kwa waimbaji wazee, usanii wa kughani shairi hilo unakaribia kutoweka. Bw. Buqiong ni mmoja wa wasanii wachache vijana wanaoweza kughani shairi hilo. Katika kipindi cha leo, tutazungumzia hadithi za mwimbaji huyo Buqiong pamoja na utenzi wa Gesar.

    Kama vijana wengine wa kawaida wa Tibet, Buqiong mwenye umri wa miaka 33 aliyevaa miwani na nguo ya michezo yenye mtindo wa kisasa, haonekani kabisa kueandana na shughuli ya kughani shairi la kale. Lakini wakati anapoanza kusoma utenzi wa mfalme Gesar, kijana huyo mwenye haya huonesha usoni moyo wa umakini na kujiamini akighani bila kusita shairi hilo la kumsifu shujaa huyo wa kale wa Tibet.

    Shairi hilo linasomwa kwa lugha ya Kitibet, Bw. Buqiong anatuelezea hadithi aliyoisoma .

    "Shairi nililoghani sasa hivi linaelezea jinsi Gesar alivyonyakua ufalme wake kupitia mashindano ya farasi. Kwa ufupi, mfalme Gesar akiwa utotoni alifukuzwa na kwenda kuishi kwenye bonde la mlima katika nchi yake ya Ling, mpaka alipofikia umri wa miaka 13, wakati huo mungu alitoa ishara ya kumtaka ashiriki kwenye mashindano ya farasi yaliyolenga na kumchagua mfalme wa nchi yake, hatimaye akanyakua ufalme wa nchi ya Ling baada ya kushinda kwenye mashindano hayo."

    Inasemekana kwamba, mfalme Gesar aliyezaliwa katika karne ya 11 ni shujaa mwenye damu ya mungu. Kutokana na ujasiri na uhodari wake katika mapambano dhidi ya shetani na majambazi, Gesar alipendwa na kuungwa mkono sana na watu wa Tibet. Utenzi wa mfalme Gesar unaosifiwa kuwa ni "Utenzi wa Homer" wa mashariki ndio shairi maarufu linaloelezea hadithi kuhusu maisha yake ya kishujaa. Utenzi huo ukiwa ni mrefu zaidi duniani, una mistari zaidi ya milioni 10 yenye maneno zaidi ya milioni 20, kwa enzi na dahari umeendelea kughaniwa na wasanii wa Tibet kizazi baada ya kizazi. Mwaka 2009, utenzi wa mfalme Gesar uliorodheshwa kuwa Urithi wa kiutamaduni wa dunia na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa.

    Tofauti na usanii wowote wa uimbaji unaofundishwa na walimu kwa wanafunzi, Buqiong alikuwa na uzoefu wa ajabu wa kujifunza utenzi wa mfalme Gesar. Buqiong aliyezaliwa eneo la mbuga la Nagqu anasema, wasanii wengi wa huko walikuwa na uzoefu kama yeye, yaani baada ya kupona ugonjwa mkubwa, au kuamka kutoka ndotoni, ghalfa waliweza kukumbuka hadithi zote za kishujaa za mfalme Gesar.

    "Nilipokuwa utotoni, wakati watoto wa rika langu wote walipoanza kuongea, mimi nikawa bado siwezi kuongea. Siku moja nilienda kuabudu budhaa kwenye hekalu la Xiaoding kwenye eneo la Nagqu, ghalfa nikaweza kuongea. Wakati nilipotimiza umri wa miaka 11, siku moja nililala mlimani nilipokuwa nikichunga mifugo, niliota ndoto kwamba watawa wawili ambao mmoja alivaa nguo nyeupe na mwengine akivaa nguo nyekundu, walikuja mbele yangu wakishika misahafu mkononi. Mtawa aliyevaa nguo nyekundu alipokuwa akinipatia misahafu, ghalfa akaja mbwa mmoja na kuniamsha kutoka kwenye ndoto. Baada ya kuamka, nikaona mtu mmoja aliyevaa nguo nyekundu na kupanda farasi halafu aliniambia nienzi hadithi ya mfalme Gesar. Wakati huo ingawa nilikuwa nazifahamu hadithi zake, lakini sikuweza kuzieleza vizuri, nilikuwa naongea ovyoovyo. Kutokana na desturi ya sehemu za kaskazini ya Tibet, hali kama yangu inaweza kuondolewa tu baada ya mtawa mkuu kuniwezesha. Baada ya hapo, nikaweza kukumbuka waziwazi utezdi huo mzima."

    Tokea mfalme Gesar azaliwe hadi aanze vita, Buqiong anaweza kughani utenzi huo bila kusita kwa siku zaidi ya kumi mfululizo, mpaka huwa anajisahau nafsi yake.

    "Kila mara niliposoma utenzi wa m

    falme Gesar, kwanza hueleza hadithi, halafu naanza kughani na siwezi kusita. Nikiwa kwenye kughani huwa najisikia vizuri sana, nahisi kama nimeingia kwenye ulimwengu mwingine. Hasa ninapoendelea kueleza na kuimba kwa muda mrefu, hadithi za mfalme Gesar huwa naziona moja kwa moja machoni mwangu kama jinsi ninavyotazama televisheni, wakati huo huwa najisikia vizuri, raha sana."

    Bw. Buqiong amesema, kueleza hadithi za kishujaa za mfalme Gesar ni utegemezi usiobadilika katika moyo wake. Alipokuwa na umri wa miaka 17, alianza kughani kwenye jukwaa kubwa. Baada ya miaka mitano na kupata umaarufu zaidi, yeye pamoja na wasomaji wengine wakaanza kufanya maonesho kwenye majumba ya sanaa, miaka 11 hadi leo.

    "Naghani kila siku, katika jumba letu kuna wasomaji watatu, wawili wanaghani kwa masaa mawili halafu huwa naendelea mimi. Zamani tulikuwa tunaishi kwenye eneo moja mbugani, sasa tumekusanyika mjini na shughuli zetu zinaendelea kukua. Tunaamua wenyewe hadithi gani tutakazoghani, lakini kama watazamaji wanafahamu sana utenzi wa mfalme Gesar, pia wanaweza kuchagua sehemu wanazopenda kusikiliza."

    Katika miaka zaidi ya kumi iliyopita, Buqiong ameghani utenzi kwenye maeneo yote ya Nagqu.

    "Usanii wa kughani unapendwa sana na watu wa Tibet. Niliwahi kughani kwenye kaunti ya Sog halafu Nyima, sasa nimekuja kaunti ya Xainza. Watu wa hapa wanapenda sana namna ninavyoghani, kwa kuwa kwenye maskani yetu ya mbugani, sote tulikuwa tukisikiliza hadithi za mfalme Gesar tangu tulipokuwa utotoni."

    Utenzi wa mfalme wa Gesar unajumuisha historia, mashairi, mithiolojia, methali na hekaya za Tibet ya kale, tunaweza kusema utenzi huo ni kama ensaiklopidia kuhusu utamaduni wa Tibet. Lakini kutokana na wengi wazee wanaoghani kufariki dunia , shairi hilo linalosomwa kwa kukariri linakabiliwa na hatari ya kutoweka. Tokea miaka 80 ya karne iliyopita hadi leo, serikali ya mkoa wa Tibet imechukua hatua mbalimbali kuokoa shairi hilo la kale, na kuanza kurekodi kwa njia ya maandishi au video mali hii ya kiroho inayorithiwa na wasanii kizazi baada ya kizazi. Serikali pia inawahamasisha wasomaji vijana wa mashairi waenzi utenzi huo wa kale.

    Buqiong akionesha kwa fahari kipande cha jina kifuani kwake kilichoandikwa "Mrithi wa Urithi wa utamaduni wa dunia eneo la Nagqu", amesema ana imani kubwa kuhusu mustakbali wake.

    "Zamani sikuwa na cheti cha utambulisho kilichotolewa na serikali. Mwaka jana serikali ya mkoa unaojiendesha wa Tibet imenichagua kuwa mrithi wa usanii huo. Baada ya hapo, kuighani utenzi wa mfalme Gesar kumekuwa ustadi wangu maalumu na sehemu muhimu ya maisha yangu. Baadae, nitaandika vitabu na kutoa albamu, na kufanya maonesho kwenye sehemu nyingi zaidi. Nina imani juu ya mustakbali wangu wa siku za baadae."

    Kila siku Buqiong anaendelea kughani kwa moyo wote hadithi za kishujaa za mfalme Gesar kwenye jumba la sanaa, huku akiwa amevalia vazi la kijadi la Tibet la jenerali wa enzi za kale. Buqiong amesema hana wasiwasi kwamba watazamaji wake watapungua kutokana na mabadiliko ya maisha. Ataendelea kughani kwa kuwa popote pale walipo watibet, wako wasanii wanaoghani utenzi wa mfalme Gesar.

    "Hakuna jambo lolote linalonifurahisha zaidi kuliko kughani utenzi wa mfalme Gesar. Kila ninapokuwa na mambo ya kusumbua, nikipanda jukwaani na kuanza kughani, wasiwasi wote huwa unaniondoka kabisa."

    Mwaka 2014, eneo la Nagqu likiwa ni eneo lenye waghani wengi zaidi wa utenzi wa mfalme Gesar mkoani Tibet, lilianzisha kituo cha usanii wa kughani utenzi huo. katika matamasha mbalimbali ya kushindana farasi yanayofanyika kila mwaka kwenye eneo hilo, maonesho ya kusoma utenzi wa mfalme Gesar ambaye ni hodari katika kupanda farasi, huwa ni sehemu muhimu ya matamasha hayo. Ni kutokana na juhudi za bila kusita zilizofanywa na warithi kama kijana Buqiong, katika mitaa au majumba, watu wa Tibet bado wanaweza kusikiliza hadithi za kishujaa zinazotoka enzi na dahari za kumsifu mfalme Gesar.

    Mbali na juhudi za wasanii, kazi ya kuhifadhi na kuenzi utenzi wa mfalme Gesar pia imetiliwa mkazo na idara ya utamaduni katika serikali ya Tibet.

    Naibu mkurugenzi wa idara ya uhusiano mwema ya Kamati ya chama cha kikomunisti cha eneo la Nagqu Bw. Li Hongwei alipofahamisha kuhusu hali ya wasomaji wa utenzi huo, amesema kuna wasomaji wengi wanaoweza kughani utenzi huo, lakini wanaotambuliwa na kuandikishwa na serikali ni wasomaji 71.

    "Wasanii hao wote hawakuwahi kwenda shule, wote hawajui kusoma wala kuandika, lakini wanaweza kusoma utenzi wa mfalme Gasar. Tunasema kila msanii ana toleo lake tofauti la utenzi huo, ingawa hawana elimu, lakini wanaweza kusoma utenzi huo. Mkoani Tibet hasa kwenye eneo la Nagqu, wasomaji hao wanaamini kuwa wanachaguliwa na mungu. Kwa kawaida, walipokuwa na umri wa miaka 10 na zaidi, walipata ghalfa uwezo wa kukumbuka utenzi huo baada ya kupona ugonjwa, kuwa na ndoto au kuwa na uzoefu maalumu, Jambo ambalo huwezi kusema ni la kishirikina, lakini pia hakuna maelezo sahihi ya kisayansi."

    Inasemekana kuwa kuna njia mbalimbali za kupata ustadi wa kughani utenzi wa mfalme Gesar, kwa mfano kuchimbua vitu vya kale vilivyofichwa ardhini au mlimani. Lakini njia ya kawaida zaidi ni kupata uwezo huo kupitia ndoto, wale waliopata ustadi kwa njia ya ndoto huaminiwa kuwa wanachaguliwa na mungu.

    Bw. Li Hongwei anasema, serikali ya eneo la Nagqu inatilia maanani sana kazi ya kuhifadhi na kurithi usanii wa Gesar, na wataalamu wa usanii wa Gesar na mashairi ya kughaniwa kutoka Taasisi ya sayansi ya kijamii ya mkoa wa Tibet wametumwa kwenda kuwatambua na kuwaandikisha wasomaji wa utenzi huo. Akizungumzia vigezo vya kuandikisha wasomaji hao, Bw. Li Hongwei anasema:

    "Kwanza wanapaswa kutambuliwa na umma, kama hawakubaliwi na umma, basi wataalamu pia hawatawakubali. Pili ni muda wa kughani, ukiweza kughani kwa masaa mawili matatu mfululizo, pia haikubaliki. Kuna kigezo cha muda wa kughani, yaani masaa zaidi ya 20 mfululizo. Halafu ni sauti ya kughani, kama sauti yako ya kughani inafanana sana na ya wengine, basi inawezekana kwamba umewaiga wengine. Wasomaji wa utenzi lazima wawe na mitindo yao maalumu, kwa upande wa maudhui yanayosomwa, haifai kurudia rudia maneno yanayoghaniwa na wengine, wala haifai kwenda kinyume sana na msingi wake. Huwezi kuimba ovyoovyo tu, kwa kuwa hadithi za mfalme Gesar zina mfumo wake, lakini zinakubaliwa kuwa na mambo tofauti madogomadogo."

    Wasomaji wote walikuwa ni wafugaji na hawana mapato yoyote. Hivi sasa waisomaji 71 wametambuliwa rasmi na serikali ya Nagqu, 7 kati yao ni wa ngazi ya mkoa na wawili ngazi ya taifa, ambao wanapewa ruzuku ya yuan 3000 na 5000 kila mwaka. Bw. Li Hongwei amesema, serikali za mitaa pia zimejitahidi kutoa ruzuku kwa wasomaji hao wa utenzi ili kuboresha maisha yao.

    "Serikali na kamati ya chama ya hapa zimefanya juhudi nyingi kwa ajili ya kuenzi na kuhifadhi utamaduni wa kijadi wa Gasar. Utamduni huo si kama tu ni sehemu ya utamaduni wa eneo la Nagqu au mkoa wa Tibet, naona ni sehemu ya utamaduni wa taifa la China."

    Ingawa maendeleo yamepatikana, lakini kazi ya kueneza usanii wa kughani utenzi huo bado inakabiliwa na changamoto kadha wa kadha. Bw. Li Hongwei anasema, wafugaji hao walipata ustadi wa kusoma utenzi huo kwa njia mbalimbali, hivyo ni vigumu kuwafanya waghani utenzi huo kwa lugha ya kichina, hivi sasa serikali ya Nagqu inashirikiana na maktaba ya mkoa wa Tibet, kurekodi video au sauti za maonesho ya kughani ya wasanii hao, halafu kuyahifadhi kwa njia ya maandishi na kuyatafsiri kwa lugha ya kichina.

    Alai, ambaye ni mwandishi wa kitabu cha Mfalme Gesar kutoka Tibet, aliwahi kusema, lengo la kuandika kitabu hicho ni kuionesha dunia Tibet ilivyo, kuongeza uelewa wa watu kwamba Tibet ni zaidi ya mlima wa theluji, uwanda wa juu na Kasri la Potala, na kuwawezesha watu waelewe moyo wa watibet. Ni sawasawa kwamba kuenzi usanii wa kughani utenzi wa mfalme Gesar pia kunaweza kuwafanya watu wengi zaidi waifahamu Tibet kwa undani zaidi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako