• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ndoto ya China iliyoko mjini Beijing

    (GMT+08:00) 2015-09-23 18:54:32


    Katika zama za leo zinazotilia maanani uvumbuzi na ujasirimali, watu wengi nchini China wamepata fursa za kutimiza ndoto zao kupitia kufanya uvumbuzi na kujiajiri. Vijana wana matumaini ya kufungua maduka ya maua au mgahawa, ambako marafiki zao wanapiga stori wakinywa kahawa, jambo litakaloleta furaha kwa watu hata kufikiria tu. Kijana Zhao Tianwei mwenye umri wa miaka 33 ni mwenyeji wa Beijing, na yeye pia ana matarajio yake na fursa hii.

    "Kwanza napenda kunywa kahawa, pia napenda kupika. Nilifikiria mambo haya kabla sijafungua mgahawa wangu. Marafiki zangu pia wanapenda mahali kama hapa, naona hili ni jambo ninalopenda kufanya, na pia marafiki zangu wanapata sehemu ya kupumzika. Ni jambo lenye maana."

    Kabla ya kuamua kufungua mgahawa, Zhao Tianwei alikuwa mhariri wa redio, na ili kufanya kitu anachokipenda kwa moyo, alijiuzulu kazi ambayo ameifanya kwa miaka saba. Katika mtazamo wa wengine, uamuzi wa Zhao Tianwei ni wa kijasiri, lakini sio wa busara. Zhao amesema anapenda kufanya kazi kwenye tasnia ya habari, na pia alisita sana kabla ya kuacha kazi. Lakini kama alivyosema, maisha yanasonga mbele, ni wakati kuyafanyia mabadiliko. Zhao Tianwei anaona kuwa anapaswa kufanya jambo analotaka kufanya wakati bado akiwa kijana, na hakujutia uamuzi wake wa kuacha kazi.

    "Sina majuto. Nilifanya uamuzi huu nilipokuwa na umri wa miaka 30, niliona kuwa maisha ya miaka ile yalihitaji mabadiliko, na hayakuniridhisha, na nilitakiwa kujaribu jambo wakati bado kijana, ni wakati uliofaa kwa kufanya mabadiliko."

    Akiwa na matarajio mazuri ya siku za baadaye na kutobadili uamuzi wa kujiajiri, Zhao alifungua mgahawa huo uitwao "Nevertheless" ulioko kando ya ziwa Houhai hapa mjini Beijing. Kwenye mgahawa huo, wakati wa adhuhuri katika majira ya kiangazi, upepo mzuri unavuma, kivuli cha miti kinaonekana dirishani, na kuwafanya wateja wengi kujisikia utulivu. Hata hivyo, nyuma ya uzuri huo, ni taabu alizozipata katika ujasilimali, na mpaka sasa bado anakumbuka siku ambayo alitafuta mahali pa kufungua mgahawa wake.

    "Bado nakumbuka majira ya kiangazi ya mwaka 2012, joto lilikuwa kali sana. Tuliposikia kuna mgahawa uliofunga biashara yake na kuacha mahali, tulienda kuangalia. Ilichukua miezi mitatu hadi minne hivi, na hatimaye tukapata mahali hapa, na baadaye tulianza kuyafanyia usanifu na kupamba, kazi ambazo zilichukua muda mwingi na mawazo mengi."

    Kila mjasiriamali hukumbwa na taabu tofauti. Zhao Tianwei amekiri kuwa akiwa mgeni katika utengenezaji wa kahawa, jinsi ya kutengeneza vizuri kahawa na kuwaridhisha wateja ili waweze kuja tena ni jambo alilotakiwa kufikiri kila siku. Alishindwa kuajiri mtengenezaji kahawa na mhudumu wa baa, na ili kubana matumizi, ilimbidi ajifunze kutengeneza kahawa na kuchanganya vinywaji. Kila siku kabla ya kufungua mlango, Zhao alijifunza jinsi ya kutengeneza kahawa, na alikunywa kahawa alizotengeneza kwani alisita kutupa. Na ili kutengeneza kahawa nzuri, Zhao Tianwei aliwahi kunywa vikombe kumi vya kahawa kwa siku.

    "Nilikuwa nikiendelea kujaribu, kiasi cha buni, maziwa, kubadili muundo na viungo, ili nijue jinsi ya kuvichanganya nipate kahawa nzuri zaidi. Naona kwanza ni lazima niridhike halafu nitaweza kuwauzia wateja. Kama nisiporidhika, siwezi kuwauzia marafiki na wateja wangu."

    Upungufu wa fedha huwa ni tatizo linalowakabili wajasiriamali wote ikiwa ni pamoja na Zhao Tianwei, ikizingatiwa kuwa mgahawa wake uko katika ziwa Houhai, ambako bei ya pango ni kubwa mno. Katika hatua ya mwanzo, pesa zote zilitakiwa kutumiwa ipasavyo. Akikumbuka wakati mgumu zaidi, Zhao Tianwei anasema katika majira ya baridi wakati mgahawa wake ulipofunguliwa upya, upepo mkali ulivuma na theluji kubwa ilianguka, biashara haikuwa nzuri, na alikuwa peke yake kwenye mgahawa, na hisia ya upweke anaikumbuka vizuri hadi leo. Lakini Zhao Tianwei aliona kuwa anatakiwa kufanya juhudi zaidi kutimiza chaguo lake.

    "Kazi yoyote si rahisi kufanywa, mwanzo huwa ni mgumu, na nilijiandaa vya kutosha. Kwa hiyo ingawa kuna matatizo mengi, lakini ilinibidi niyakabili, kwani hili ni chaguo langu."

    Ili kubana matumizi, ni Zhao Tianwei peke yake alifanya kazi zote za mgahawani. Mbali na kutengeneza kahawa na pombe, kila siku pia anafanya usafi. Anasema hakuwahi kuosha vyombo nyumbani kwao, lakini ilimbidi kuosha vyombo kwenye mgahawa wake, na hata kufanya usafi chooni.

    Katika miaka mitatu iliyopita tangu kufunguliwa kwa mgahawa wake, Zhao Tianwei amekuwa rafiki wa wateja wengi, ambao wanapenda kwenda kwenye mgahawa wake, ambapo wanapiga stori, wakizungumzia maisha na ndoto zao. Akizungumzia mambo hayo, tabasamu ya kuridhika inaonekana usoni mwake. Kulikuwa na wasichana kadhaa ambao walikuja kwa mgahawa huo kabla ya kuondoka Beijing baada ya kuhitimu masomo yao chuoni, na walisema mgahawa huo ni sehemu ya kumbukumbu yao hapa Beijing. Bibi Chen mwenye umri wa miaka 69 ni mteja wa mara kwa mara, anapenda kahawa safi ya mgahawa huo pamoja na mapambo yenye ladha ya kitamaduni. Ukuta wa rangi safi, meza za mbao, vitu vya sanaa vimesambaa sehemu mbalimbali ndani ya mgahawa huo, na picha za mmiliki wa mgahawa huo zilizotundikwa kwenye ukingo wa meza, keki na ice cream zenye rangi mbalimbali zilizochorwa kwenye ubao wa matangazo, hayo yote yameonesha jinsi Zhao anavyotumia akili zake. Bibi Chen anasema,

    "Naona yeye si mtu anayefanya biashara kwa ajili ya kuchuma pesa tu, na anafanya mgahawa huo uwe na tamaduni nyingi. Pia yeye ni mtu mwema, hana tabia mbaya walizo nazo wafanyabiashara, anawatendea wengine kwa utulivu na kuwaheshimu."

    Kwa Zhao Tianwei, mgahawa huo si kazi tu, bali pia ni furaha zinazotoka kwa marafiki zake. Anasema kama marafiki zake wana huzuni, anaweza kuwapa sehemu nzuri kama familia, kunywa kahawa au pombe, jambo hilo linamridhisha.

    "Ingawa sasa bado mgahawa ni mdogo, lakini nina matarajio ambayo labda hayawezi kutimizwa daima, yaani ninaweza kuwa na mgahawa wangu wa pili na hata wa tatu, na kuwawezesha watu wengi zaidi wapate mahali pa kukaa wanapoona upweke au furaha, hii itaniridhisha."

    Mvumilivu hula mbivu. Hivi sasa pato la mgahawa huo kwa mwezi linaridhisha ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita. Lakini Zhao Tianwei anasema ndoto yake bado haijatimizwa, na kuna mambo mengi yanahitaji juhudi na marekebisho. Anasema kwake yeye, ujasiriamali haulengi faida, bali ni ndoto yake ya siku zote, na ni muhimu kuanza safari tofauti maishani.

    "Naona juhudi na umakini ni muhimu. Ninachohitaji kwa sasa ni kufanya mgahawa uwe mzuri zaidi katika sekta mbalimbali. Natarajia naweza kudumisha jitihada zangu kwani hii haimaanishi kazi tu kwangu, bali ni ndoto, hivyo nataka kuitekeleza."

    ************************

    Katika mji wa ujasiriamali wa Shenzhen, China, kuna wafanya biashara milioni 1.885, hivyo katika mji huo wenye wakazi milioni 15, katika kila watu wanane, mmoja ana biashara yake.

    Ning Ji mwenye umri wa miaka 25 ndiye mmoja kati yao. Yeye ni mwanzilishi wa kampuni ya roboti mjini Shenzhen. Tangu akiwa masomoni katika chuo kikuu, alibuni bidhaa zenye teknolojia ya hali ya juu ikiwemo roboti. Alipoanza biashara mwishoni mwa mwaka 2012, yuan elfu moja hadi mbili kwa mwezi ya kupanga nyumba katika maeneo ya ujasiriamali mjini Shenzhen ilikuwa ni gharama kubwa kwake. Hata hivyo, Ning Ji anaona kuwa hivi sasa fursa zimeongezeka baada ya serikali kutoa sera ya kuunga mkono ujasiriamali na uvumbuzi wa umma.

    "Ujasiriamali kwa sasa ni tofauti na zamani. Nilipoanza kufanya biashara mwishoni mwa mwaka 2012, nilitakiwa kulipa kodi ya pango, sikuthubutu kuchelewa kulipa. Sio tu tulitakiwa kulipa kodi, na pia kujikimu kimaisha, na kuendelea na shughuli zetu, siku hizo hazikuwa rahisi. Lakini sasa hali imebadilika. Wajasiriamali wanaheshimika sana hapa. Kwa mfano tunapewa ruzuku kama tukipangisha nyumba kwa wengine, pia wanatoa jukwaa ili tuoneshe bidhaa zetu. Jukwaa hilo halikuwepo zamani, lakini baada ya waziri mkuu wa China Li Keqiang kutilia maanani ujasiriamali, eneo la Qianhai lilianza kufuatiliwa."

    Kiwanda cha ndoto cha vijana wa bandari ya kina kilichopo katika eneo la Qianhai mjini Shenzhen katika eneo la biashara huria la mkoa wa Guangdong ndicho kilichomridhisha Ning Ji. Kiwanda hicho sio tu kimempatia sehemu ya kufanyia kazi, bali pia kimesaidia maendeleo ya kampuni yake kutoka yeye peke yake hadi timu ya sasa yenye watu kumi. Vijana hao wamebuni roboti kamili yenye mfumo mzuri wa uwiano, na pia wameanzisha mfumo wa ukaguzi wenye teknolojia ya kisasa unaoweza kutumiwa katika treni ya mwendo kasi. Lakini wastani wa umri wa vijana hao ni miaka 23 tu!

    Msemaji wa idara ya utawala ya Qianhai ya Shenzhen Wang Jinxia amesema tangu kiwanda hicho kianzishwe tarehe 7, Disemba mwaka jana, kimevutia timu 92 za vijana wajasiriamali kufanya biashara zao katika eneo hilo. Ili kuunga mkono vijana hao, eneo la biashara huria la Qianhai limetoa sera nafuu ikiwemo kupunguza au kusamehe kodi ya kupanga nyumba. Anasema,

    "Kwa timu za wajasiriamali, katika mwaka wa kwanza hatuwatozi kodi ya pango, mwaka wa pili tunawatoza nusu, na mwaka wa tatu ni kuwatoza kodi ya kawaida sokoni. Pia tumewekeza mfuko wenye Yuan milioni 250 ili kutoa jukwaa kwa vijana hao."

    Eneo la biashara huria la Qianhai pia limetoa ruzuku kwa kodi ya mapato ili kuwavutia watu wengi zaidi wenye ujuzi kuja kufanya ujasiriamali.

    Xu Lei na Yang Yang ni wajasiriamali wawili waliowahi kusoma katika nchi za Ulaya. Miaka miwili iliyopita, walitumia dola za kimarekani laki 3.3 walizokusanya kwenye tovuti za nchi za nje kubuni kipimajoto kinachoweza kupima joto kutoka 40 digrii sentigredi hadi 125 digrii sentigredi, na kufanikiwa kujipatia chungu yao ya kwanza ya fedha. Wakitambua nguvu kubwa zilizopo katika soko la ndani la China na nguvu bora ya Shenzhen katika utengenezaji wa vifaa vya teknolojia ya hali ya juu, walirudi nchini wakiwa na bidhaa walizobuni, na wanatarajia kujenga jukwaa katika mtandao wa internet linaloweza kutoa taarifa kuhusu halijoto. Xu Lei anasema,

    "Tunafanya ushirikiano na Taasisi ya Sayansi ya China. Mara kwa mara taasisi hiyo inajulisha kwatu wawekezaji na raslimali tunazohitaji. Tutabuni na kutengeneza bidhaa ya kizazi cha pili hivi karibuni, mabadiliko makubwa ni kujumuisha uwezo mwingi zaidi, kwani tumegundua kuwa mahitaji katika soko la ndani ya China ni tofauti, kama tunataka soko la ndani, tunapaswa kufanya marekebisho kwa mujibu wa hali ya soko hilo."

    Sera nzuri, soko kubwa na mitaji mingi vimewahamaisha vijana wengi kufanya ujasiriamali. Hamu kubwa ya ujasiriamali mjini Shenzhen ni ,mfano mmoja tu wa mkondo wa kufanya ujasirimali nchini China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako