• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tule kwa Afya- Juisi za matunda asilia na faida zake mwilini

    (GMT+08:00) 2015-09-28 08:58:08

    Tungependa kuwauliza maswali kadhaa wasikilizaji wetu kabla ya kuendelea na utengenezaji wa juisi, mswali yenyewe ni kwamba je unajua kuwa unaweza kuondoa sumu mwilini, kupunguza mafuta mwilini, kupunguza uzito wa mwili na shinikizo la damu kwa kunywa juisi ya matunda asilia iliyotokana na siki ya apple, limao, mdalasini uliosagwa, asali mbichi pamoja na maji? Juisi yenye mchanganyiko huu wa matunda, mdalasini na asali ni kinywaji asilia chenye faida nyingi kiafya. Kwa hiyo tungewashauri wasikilizaji wetu kujenga afya za mwili wao kwa kunywa juisi yenye mchanganyiko huu mara kwa mara.

    Kuuliza maswali mawili matatu na kutoa ushauri wa kunywa juisi ya matunda asilia kila mara, tuangalie vitu tunavyohitaji katika kutengeneza juisi ya matunda asilia. Kwanza unatakiwa uwe na glasi moja ya maji., kama tunavyofahamu maji yana faida kubwa sana mwilini. Pia unatakiwa uwe na vijiko viwili vya siki ya apple. Vijiko viwili vya juisi ya limao. Kijiko kimoja cha unga wa mdalasini na Kijiko kimoja cha asali mbichi. Baada ya kuandaa mahitaji yote yanayohitajika kutengenezea juisi. Weka juisi ya limao, asali, siki ya apple na unga wa mdalasini katika chombo kisafi kwa kuzingatia kila kimoja kiwe katika kiwango kinachotakiwa. Ongeza maji (250 ml) na koroga vizuri kuhakikisha juisi imechanganyika vizuri. Baada ya kuichanganya vizuri hapo juisi yako itakuwa tayari kwa kunywa.

    Kama ulivyosikia ni rahisi sana kutengeneza juisi hii ambayo ina kazi kubwa sana mwilini. Lakini mbali na juisi hiyo pia leo tutatengeneza juisi ya karoti na apple, kwanza chukua kiasi cha karoti na apple kinachotosha kutengeneza juisi kwa kiasi ulichokusudia. Usikose kipande cha limao kiasi cha nusu. Anza kuandaa juisi yako kwa kuosha na kumenya karoti na apple kisha katakata katika vipande vidogo vinavyoweza kusagika kirahisi kwenye blenda. Saga mchanganyiko wako ili upate juisi. Baada ya kupata mchanganyiko wa juisi yako kamulia limao kwa ajili ya kuongeza ladha. Unaweza kuiweka kwenye friji ili ipate baridi kidogo na tayari kwa kuinywa. Siyo lazima kuongeza sukari kwenye juisi kwani matunda yana sukari asilia na kama unapenda utamu zaidi unaweza kutumia asali.

    Sasa basi hebu tuangalie manufaa yake mwilini tukianza na juisi ya karoti na apple ina uwezo wa kutunza ngozi kwani tunda la apple linaondoa uchafu kwenye ngozi na karoti nayo kwa kutumia kirutubisho cha beta-karotini chenye uwezo wa kutengeneza Vitamin A hulinda na kurejesha uhai katika ngozi ambapo inaifanya ionekane nyororo. Pia juisi hii husafisha tumbo na kuondoa uchafu tumboni. Aidha juisi hii inafanya ini lifanye kazi yake vizuri kwa kulainisha nyongo na kusaidia kuondoa uchafu.

    Kwa upande wa juisi tuliyotengeneza awali husaidia kupunguza mafuta na uzito wa mwili. Huweka sawa sukari (blood sugar) na hivyo kupambana na maradhi ya kisukari. Mbali na hapo pia huondoa sumu mwilini. Na kwa ujumla tunawashauri wasikilizaji wetu wapendelee kunywa juisi zaidi hususan wale waliopo kwenye mpango wa kupunguza uzito wa mwili, kwani kuna baadhi ya watu huwa wanahangaika kwa muda mrefu kupunguza unene bila mafanikio na kuishia kusema "unene ni asili yangu" hakuna mtu mnene duniani, ila unakuja kutokana na mlo tunaokula na tabia ya kujibweteka yaani kutoushughulisha mwili kimazoezi.

    Ni kweli kwani wengine pia huwa hawaridhiki kama hawajatia sukari kwenye kila kitu, wanasahau kuwa sukari ni muuaji mkubwa wa kisirisiri wa afya za watu. Sasa tuangalie manufaa ya kiuongo kimojakimoja kilichotumika kwenye juisi hii. Siki ya apple. Siki ya apple ina enzymes na vitamin C ambazo husaidia kupambana na bakteria waletao magonjwa. Vilevile apple lina tindikaliambayo imedhihirika kiafya kuweza kushusha shinikizo la damu kwa kiwango cha mpaka asilimia sita. Pia juisi ya limao, husaidia kupunguza mafuta mwilini, licha ya limao kuwa na vitamin C juisi yake inasaidia pia katika kuweka sawa kiwango cha sukari na hivyo kusaidia utendaji kazi mzuri wa mwili hasa katika shughuli zinazohusiana na mzunguko wa damu.

    Katika juisi yetu pia tulitumia mdalasini . Mdalasini una madini muhimu yanayohitajika mwilini kama calcium, iron na manganese kwaajili ya uimarishaji, uboreshaji na utendaji kazi wa viungo mbalimbali vya mwili. Na unafahamu kuwa mdalasini husaidia kuzuia vidonda vya tumbo. Tafiti mbalimbali zimedhibitisha mdalasini kuwa kinga ya vidonda vya tumbo kwa kuzuia bakteria wasababishao ulcers wasilete madhara au kuathiri kuta za tumbo.

    Baada ya kuangalia mahitaji ya juisi sasa tuiangalie asali mbichi ambayo ina faida kubwa sana mwilini, na vyema wale wapenda vyakula vitamu kutumia zaidi asali kuliko sukari. Asali imetengenezwa na vitu vingi asilia, hivyo asali imekuwa ni chakula dawa. Kwa karne nyingi asali imekuwa ikitumika kama tiba. Asali inasaidia kutibu vidonda na kuongeza kinga ya mwili kwa kuepusha maradhi mbalimbali kama ya ngozi, moyo n.k. Asali ni kimiminika chenye ladha tamu ya sukari, chenye kunata na rangi ya manjano. Asali kama chakula na dawa ni dhana kongwe katika historia ya mwanadamu. Kwa mfano miaka 4,000 iliyopita madaktari wa tiba wa Kimisri na wale wa Sumarani waliitumia asali kutibu magonjwa mbalimbali kama vile vidonda vya tumbo na vile vya kawaida, magonjwa ya macho, ngozi na yale ya tumbo.

    Kama tulivyosema asali ina faida nyingi mwilini. Kwanza hutumika kama chakula hivyo huongeza nguvu mwilini. Ni kiongezeo katika vyakula kama mkate, karanga na nafaka nyingine. Hutibu vidonda mbalimbali. Kwa kunywa mchanganyiko wa asali, siki na maji katika vipimo sawa ni tiba kwani huaminika kuua vijidudu visababishavyo magonjwa. Pia hufanya ngozi yako kuwa nyororo na katika hali nzuri isiyo ya ukavu wakati wote. Paka asali kwenye ngozi na acha kwa dakika 30 kisha jisafishe. Fanya hivyo mara kwa mara na utaona mabadiliko katika ngozi yako.

    Mbali na kuila asali pia hutumika kama njia moja ya urembo kwani huboresha na kuweka nywele katika hali nzuri wakati wote inapotumiwa kama. Jinsi ya kutengeneza ni kwamba changanya kijiko kimoja cha asali na shampoo kisha tia mchanganyiko huo kwenye nywele zako kwa dakika 20, osha na kausha nywele zako vizuri. Na kama ukitaka kuondoa chunusi na kuboresha ngozi yako. Paka asali sehemu yenye chunusi kwa dakika 30 kisha osha ngozi yako kwa maji ya vuguvugu. Fanya hivyo kwa siku kadhaa utaona mabadiliko.

    Sehemu nyingi duniani watu wanatumia asali kutibu magonjwa mbalimbali. Licha ya kuwa asali huongeza kinga ya mwili, sayansi ya tiba imebaini asali bora ina wingi wa sukari (76g/ml), tindikali (acidity, Ph = 3.6-4.2) na baadhi ya kemikali ambazo zinatokana na viumbe hai (organic compounds) vyote kwa pamoja ni sababu za asali kuwa ni dawa.

    Virutubisho vya kiafya katika asali ni pamoja na kuwa chanzo cha sukari hivyo mwili hupata nguvu na nishati. Asali ina mchanganyiko wa virutubisho na kemikali za aina mbali mbali. Baadhi ya vitu hivyo ni sukari, vitamini, amino acids (vitu vinavyotengeneza protini), vimeng'enyo (enzymes) Kwa hayo machache kuhusu asali na matumizi yake naamini utakuwa umefaidika kwa kujua mambo kadha wa kadha kuhusu asali. Tumia asali kama kinga na tiba ya mwili wako.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako