• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Uhusiano wa kibiashara kati ya China na Marekani watarajiwa kukua zaidi kufuatia makampuni mengi ya China kuwa na nia ya kuwekeza nchini Marekani

    (GMT+08:00) 2015-09-29 12:04:35


    Mwaka 2014, China kwa mara ya kwanza ilikuwa nchi iliyowekeza kwa wingi zaidi nje ya nchi kuliko uwekezaji iliovutia kutoka nje. Baada ya kuingia mwaka 2015, mkondo wa makampuni ya China kuwekeza katika nchi za nje unaendelea, na hata katika soko la Marekani linalochukuliwa kuwa na masharti makali zaidi kwa makampuni ya kigeni, makampuni ya China yamepata maendeleo ya kasi kwa miaka mingi mfululizo. Kuhusu njia ya uwekezaji, kuunganisha, kununua na kuanzisha kampuni ya ubia ni mbinu zinazopendekezwa zaidi kati ya makampuni ya China. Kwa ujumla, maendeleo ya makampuni ya China bado yapo katika kipindi cha mwanzo nchini Marekani, na kuna pengo kubwa kati ya ukubwa wa uwekezaji uliofanywa na makampuni ya China na ule kutoka Ulaya, Japan na hata Korea Kusini. Katika siku za baadaye, kama makampuni ya China yanaweza kuungana vizuri na uchumi wa Marekani, na Marekani itaweza kukumbatia zaidi uwekezaji wa China nchini humo, mambo hayo yataamua kama uhusiano wa kibiashara utaweza kuimarishwa zaidi kati ya China na Marekani

    Katika miaka ya karibuni, muundo wa uchumi wa kimataifa umebadilika na raundi mpya ya uhamisho wa kiviwanda imetokea duniani, ambapo makampuni ya China yanatumia nguvu kufanya uwekezaji nje ya nchi. Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Biashara ya China zinaonesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, makampuni elfu tatu ya China yapo nchini Marekani, na kufanya uwekezaji wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 65.22, kati yao uwekezaji wa moja kwa moja ulifikia dola za kimarekani bilioni 38.01, kiasi ambacho kinachukua asilimia 58.3 ya uwekezaji wote. Marekani imekuwa nchi ya tatu duniani iliyowekezwa kwa wingi zaidi na China. Katika miezi minane ya kwanza mwaka huu, uwekezaji wa China nchini Marekani ulifikia dola za kimarekani bilioni 4.43, kiasi ambacho ni ongezeko la asilimia 35.9 kulika mwaka jana kipindi kama hicho. Naibu mjumbe wa mazungumzo ya biashara ya kimataifa katika Wizara ya Biashara ya China Zhang Xiangchen anasema, hivi sasa, uwekezaji wa makampuni ya China nchini Marekani unaongezeka kwa kasi, lakini bado hautoshi na unafanywa katika sekta chache.

    "Mwaka jana, uwekezaji wa moja kwa moja wa China nchini Marekani ulifikia dola za kimarekani bilioni 7.596, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko ule uliovutiwa nchini China kutoka Marekani. Hata hivyo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, uwekezaji uliofanywa na China ulichukua asilimia moja tu ya uwekezaji uliovutiwa nchini Marekani kutoka nje. Pia uwekezaji wa China nchini Marekani unahusu sekta kuu 18, lakini sekta 4 za fedha, utengenezaji, uchimbaji madini na nyumba zinachukua asilimia 80 ya uwekezaji wote."

    Takwimu za kampuni ya ushauri ya Rhodium ya Marekani zinaonesha kuwa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, makampuni ya China yamewekeza moja kwa moja katika maeneo 88 kupitia kununua makampuni ya Marekani na kujenga viwanda vipya. Tukio kubwa lilikuwa ni kwa kampuni ya bima ya AB ya China kununua hoteli ya Waldorf Astoria ya New York. Aidha, uwekezaji uliofanywa na makampuni ya mtandao wa internet ya China yakiwemo Alibaba na Tencent kwa sekta ya teknolojia ya habari ya Marekani pia umefuatiliwa na watu wengi. Ujenzi wa eneo la kwanza la utengenezaji lililojengwa na kampuni ya kutengeneza treni ya CRRC ya China ulizinduliwa tarehe 3, mwezi huu na kuonesha kuwa uhusiano wa kibiashara kati ya China na Marekani uko katika kipindi kipya cha mwanzo. Mkurugenzi wa idara ya utafiti wa uchumi wa dunia ya Taasisi ya Utafiti wa Uhusiano wa Kimataifa wa Kisasa ya China Bibi Chen Fengying anaona kuwa mabadiliko mapya ya kimuundo yametokea katika uwekezaji wa makampuni ya China nchini Marekani, na makampuni ya watu binafsi yamekuwa nguvu ya uwekezaji huo.

    "Makampuni ya China yameanza kuwekeza katika sekta zenye ushindani, na hali halisi ni kuwa uwekezaji huo umeingia katika ushirikiano wa aina mpya yaani ushirikiano wa kiviwanda, kama vile treni ya mwendo kasi. Hivi sasa uwekezaji nchini Marekani haufanywi na kampuni moja moja, ama tuseme makampuni yanayomilikiwa na serikali tu. Tutaona makampuni mengi zaidi ya watu binafsi kama vile Alibaba, Tencent n.k. yanawekeza katika soko la Marekani."

    Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirikisho la Wafanyabiashara Nchini Marekani, ifikapo mwaka 2030, ujenzi wa miundombinu kama vile uchukuzi na nishati utahitaji uwekezaji mpya usiopungua dola za kimarekani bilioni nane, na makampuni ya China yanaweza kushiriki katika miradi ya miundombinu nchini humo kwa njia ya kuwekeza fedha au kutoa bidhaa na huduma. Lakini jinsi ya kuzoea usimamizi, sheria na muundo wa kisiasa wa Marekani ni changamoto kubwa kwa makampuni ya China yanayotaka kuwekeza nchini humo. Wakili wa Mahakama Kuu ya Marekani anayeshughulikia sheria ya kimataifa Zhang Jun anaona kuwa makampuni ya China yanayopenda kuingia kwenye soko la Marekani hayapaswi kutumia uzoefu waliopata katika masoko ya nchi nyingine, na yanatakiwa kutilia mkazo zaidi kutekeleza wajibu wao wa kijamii katika sehemu wanazofanya biashara zao nchini Marekani. Anasema,

    "Wachina wanapaswa kutumia muda kutafiti sheria na kanuni za sehemu mbalimbali za Marekani, kufahamu mila na utamaduni wa Marekani na jinsi ya kuanzisha uhusiano na makampuni ya kienyeji na eneo la makazi la huko, na kama msimamizi wa kampuni akiwa mmarekani, hii itasaidia kampuni ya China kuharakisha mchakato wa muungano wa kitamaduni na jamii ya wenyeji."

    Tarehe 23, mwezi huu, rais Xi Jinping wa China alitembelea kiwanda cha kutengeneza ndege za kibiashara cha kampuni ya Boeing na makao makuu ya Microsoft mjini Seattle na kuhudhuria kongamano kati ya wafanyabiashara wa China na Marekani. Rais Xi alisisitiza kuwa nguvu kubwa zimejificha kwenye ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani, uchumi wa nchi hizo unaweza kusaidiana, na kuna fursa nyingi zilizopo katika ushirikiano wao. Ziara hiyo ya rais Xi Jinping wa China nchini Marekani imeendeleza uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kwa njia mbalimbali ikiwemo mazungumzo kuhusu makubaliano ya uwekezaji ya China na Marekani, na itasaidia makampuni ya China kufanya uwekezaji nchini Marekani. Mkurugenzi wa ofisi ya uhusiano wa kimataifa ya taasisi ya utafiti wa uchumi na nje iliyo chini ya Kamati ya Taifa ya Maendeleo na Mageuzi ya China Zhang Jianping anasema makubaliano ya uwekezaji wa China na Marekani yana maana kubwa kwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili na hata uchumi wa dunia, na pia yatainua ngazi ya uwekezaji wa makampuni ya China nchini Marekani.

    "Kama China na Marekani zikifikia makubaliano ya uwekezaji, zinaweza kusimamia tu sekta zile zisizoruhusiwa kuwekezwa, halafu China itapata uwekezaji zaidi kutoka Marekani, Marekani pia itapata uwekezaji zaidi kutoka China, na uchumi, biashara na uwekezaji kati ya pande hizo mbili vitakuwa na ustawi mzuri zaidi. Kwa dunia nzima, makubaliano hayo pia ni muhimu, iwapo China na Marekani zinatatua suala hilo, basi China na nchi nyingine pia zitaweza kutatua suala kama hilo, na maendeleo ya China yatatoa mchango kwa maendeleo ya dunia. Naona katika mchakato wa siku za baadaye wa marekebisho ya muundo wa uchumi wa China, kwa mfano sekta ya huduma ya China kuwekezaji nchini Marekani kutakuwa na fursa nyingine. Sekta zinazohitaji fedha nyingi na zile zenye teknolojia ya hali ya juu pia zitakuwa na soko nchini Marekani. Naamini kuwa makubaliano ya uwekezaji ya China na Marekani yatahimizi makampuni mengi zaidi ya China kuwekeza nchini Marekani."

    **********************

    Wakati wa ziara ya rais Xi Jinping wa China nchini Marekani, Wizara ya Biashara ya China na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani vilisaini kumbukumbu ya maelewano kuhusu kuendeleza ushirikiano na kujenga utaratibu wa mawasiliano kati ya China na Marekani.

    Kwa muda mrefu, China imekuwa inashikilia sera ya kutoa msaada kwa nje bila ya masharti yoyote ya kisiasa, na pia China inatumia ujenzi wa miradi mbalimbali kama njia muhimu ya kuzisaidia nchi nyingine kuendeleza jamii na uchumi. Katika kuhimiza "Maendeleo kati ya Kusini na Kusini", China imefanya kazi muhimu za kiujenzi.

    Katika miaka hii miwili, chini ya msingi wa kuheshimu hali halisi ya taifa na nia ya nchi zinazopewa msaada, China na Marekani zilifanya ushirikiano katika sekta ya kilimo na utoaji mafunzo nchini Timor Mashariki na Afghanistan, ziliratibu kwa pamoja misaada kwa nchi za Afrika Magharibi katika kupambana na maambukizi ya Ebola, na kufanya ushirikiano wa maendeleo kati ya China na Marekani uwe na msingi wa mwanzo. Mwezi Juni mwaka huu, Wizara ya Biashara ya China na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani zilifanya mkutano wa kwanza wa ngazi ya manaibu waziri wa ushirikiano wa maendeleo kati ya China na Marekani, na kutoa pendekezo la kuanzisha utaratibu wa maendeleo, ushirikiano na mawasiliano. Baadaye, pande hizo mbili zilifanya mazungumzo kadhaa kuhusu kanuni na sekta za ushirikiano kwa lengo la kuinua ngazi ya ushirikiano wa maendeleo na kuingiza mambo mapya katika ushirikiano wa pande mbili kati ya China na Marekani, na mwisho kutia saini kumbukumbu ya maelewano iliyotajwa sasa hivi.

    Akizungumzia kusainiwa kwa kumbukumbu hiyo, mkurugenzi wa idara ya utoaji msaada kwa nje iliyo chini ya Wizara ya Biashara ya China aliyeshiriki maandalizi yake Wang Shengwen anasema,

    "Utiaji saini wa kumbukumbu hiyo umeinua kiwango cha mawasiliano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika maendeleo ya kimataifa. Pili, umeingiza mambo mapya kwa uhusiano wa pande mbili kati ya China na Marekani na kuonesha matarajio ya pamoja ya nchi hizo mbili katika kuhimiza maendeleo ya dunia."

    Hata hivyo, Wang Shengwen amesema, kusainiwa kwa kumbukumbu hiyo hakumaanishi kuwa shughuli zote za kutoa msaada kwa nje za China na Marekani zitalazimika kufanyika kwa pamoja, bali China na Marekani zitajaribu kufanya ushirikiano na nchi ya tatu inayopewa msaada, lakini zinapaswa kufuata kanuni za "nchi inayopewa msaada kutoa pendekezo, kukubali na kuongoza ushirikiano huo".

    Akizungumzia sekta zitakazofanyiwa ushirikiano na China na Marekani katika hatua zijazo, Wang Shengwen anasema,

    "Kumbukumbu hiyo ya maelewano imeanisha sekta tutakazofanya ushirikiano, na miradi muhimu inahusu usalama wa chakula, afya ya umma, msaada wa kibinadamu na utoaji wa mafunzo kwa watu. Aidha, China na Marekani zilisaini kumbukumbu ya maelewano wakati Umoja wa Mataifa ulipotunga ajenda ya maendeleo endelevu ya baada ya mwaka 2030, pande hizo mbili pia zinapenda kufanya juhudi za pamoja za kutokomeza umaskini uliokithiri na kuhimiza maendeleo endelevu ya dunia."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako