• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mikopo ta riba nafuu yawanufaisha wanawake wa vijijini nchini China

    (GMT+08:00) 2015-11-09 07:52:27

    Kipindi cha leo tunaelekea huko Guizhou, kusini magharibi mwa China, ambako baada ya mvua ndogo kunyesha, hali ya hewa mlimani inakuwa baridi kidogo. Sasa Pili, huko Guizhou, kuna msemo usemao "hali ya hewa nzuri haizidi siku tatu, eneo la tambarare halitazidi kilomita 1.5, na Guizhou ikinyesha mvua ni kama katika majira ya baridi".

    Na ndio tumeanza hayo majira ya baridi. Sasa kaskazini mashariki mwa mkoa wa Guizhou, kuna mji uitwao Tongren. Katika mji huo, tunakutana na Bibi Yang Li akiwa anatoka kiwanda cha uchapishaji, baada ya kumaliza kutengeneza hagtag, akaenda nyumbani kwa bibi Nie Shuzhen, mwanakijiji wa kijiji cha Heping.

    Lengo la safari ya bibi Yang Li ni kutaka kuajiri wanawake kadhaa wanaojua kutarizi, na kuwauliza kama wanaweza kufanya kazi hiyo wakiwa majumbani kwao au kama wako tayari kwenda kiwandani baada ya kupata mafunzo, kwani kampuni yake inataka kutumia chapa ya "Tarizi ya Qian" aliyoomba na kupitishwa hivi karibuni, na inatarajiwa kuanza uzalishaji rasmi mwaka kesho. Bi Nie Shuzhen ana miaka 40, na anamiliki shamba lenye zaidi ya hekta 23, hivyo anaweza kutatua suala la kazi za wanawake zaidi ya 60 wakati wa msimu wa kazi nyingi, kwa hiyo serikali ya kijiji hicho inaweka "nyumba ya wanawake" nyumbani mwake.

    Katika mji wa Tongren, maliasili mbalimbali za kimaumbile na utalii wa kitamaduni pamoja na sanaa za mikono zenye umaalum wa makabila ya huko, ikiwemo utarizi wa makabila ya Miao na Tujia umewavutia zaidi ya watalii milioni 20 kila mwaka kutoka ndani na nje ya nchi. Bibi Yang Li alizaliwa katika familia ya kawaida ya kijijini mjini Tongren, na alikwenda kufanya kazi mjini Chongqing, magharibi mwa China baada ya kuhitimu chuo kikuu. Mwaka 2009, mtoto wake mchanga alipata matatizo ya kiafya, hivyo bibi Yang Li aliacha kazi yake chuoni na kurudi maskani yake.

    Ili kupungua mzigo wa kiuchumi kwa familia kutokana na gharama kubwa ya matibabu ya mtoto, Yang Li alianza kufanya biashara. Lakini kutokana na sababu mbalimbali, mwaka 2010 biashara yake ilianza kukwama, akapoteza pesa zote alizopata kwa miaka kadhaa, kutokana na hayo yote, alikata tamaa ya maisha, na hata kufikiria kujiua. Akikumbuka jinsi biashara yake ilivyoanguka miaka mitano iliyopita, bibi Yang anashukuru kuwa alivumilia na kuendela nayo. Anasema,

    "Kuanzisha biashara kwa wanawake ni ngumu zaidi kuliko kwa wanaume, tena wanatakiwa kutunza watoto, hivyo baadhi ya mambo huwezi kuepuka, wala hakuna njia ya kuleta uwiano, hivyo unapaswa kujifunza kuvumilia na kuwa imara. Baadhi ya wakati mlango mmoja unafungwa, lakini hakika dirisha moja linafunguliwa, hivyo unapaswa kuwa na matumaini na imani nzuri, ndipo unaweza kuwa mzuri siku hadi siku. Kama unaona umeshindwa, basi hakika umeshindwa, lakini kama unaona bado una nguvu ya hai, na kusema "siogopi", basi hakika una mustakabali."

    Kutokana na kupewa moyo na msaada wa marafiki na walimu wake, Yang Li alianza tena kujiamini. Tangu akiwa mdogo, Yang alilelewa na bibi yake aliyejua sana utarizi wa kabila la Wamiao. Kwa kutumia ujuzi huo, pamoja na taaluma ya ubunifu wa mitindo aliyosomea, bibi Yang, kwa msaada wa wataalam, alibuni njia ya kutarizi kwenye majani yaliyokaushwa, na aliwahi kupata tuzo ya juu katika mashindano ya ubunifu wa bidhaa za kitalii mkoani Guizhou mwaka 2011 kutokana na njia hiyo maalum ya "utarizi kwenye jani". Sasa ushindi huo ulimfanya bibi Yang atake kuanzisha biashara tena, lakini fedha lilikuwa suala gumu kwake. Baada ya kufahamu sera ya mikopo midogo ya nchi na Tongren kwa wanawake, akatafuta msaada kutoka shirikisho la wanawake la huko. Bibi Yang anasema,

    "Shirikisho la wanawake ni kama nyumba ya mama, linaweza kutusaidia kutoa mwito, pia linatufahamisha sera nyingi. Shirikisho hilo linaweza kutoa misaada mingi ikiwemo kutoa mafunzo kuhusu kuanzisha biashara, na kufahamisha sera ya nchi ya mikopo yenye riba nafuu, tunapaswa kujua vizuri sera, kwani inaweza kusaidia kuanzisha biashara."

    Baada ya kupendekezwa na shirikisho la wanawake la mji wa Tongren, bibi Yang Li alipata mkopo mdogo wa kwanza wa Yuan elfu 60 wenye riba nafuu, na alitumia fedha hiyo kufungua duka dogo la ufundi, lakini wateja walikuwa kidogo sana. Ili kuongeza utengenezaji, mwaka 2012 shirikisho hilo lilimpendekeza tena, na hiyo bibi Yang kupitia kampuni yake, aliomba na kupata mkopo wa riba nafuu wa Yuan laki 2, ambao ulitatua suala lake la fedha. Bibi Yang alisema,

    "Mkopo huo wa Yuan laki 2 ulisaidia sana, na shirikisho la wanawake pia lilisaidia kutoa mafunzo ya kutafuta wafanyakazi. Meya wa zamani aliitisha mkutano maalum kwa ajili ya kampuni yetu ndogo, ambao uliongozwa na shirikisho la wanawake na kuzitaka idara mbalimbali zitusaidie"

    Kuanzia mwaka 2010 hadi mwezi Juni mwaka huu, mkoa wa Guizhou umetoa mikopo midogo ya dhamana inayofikia dola za kimarekani bilioni 1.195 hivi, na wanawake karibu laki 2 wa mijini na vijijini wamepata mikopo hiyo, ambayo imeunga mkono kifedha kwa wanawake kuanzisha biashara na kupata ajira. Bibi Zhou Peizhi ni naibu mwenyekiti wa shirikisho la wanawake la mkoa wa Guizhou.

    "Wanawake wanapoanzisha shughuli, matatizo makubwa zaidi ni fedha na miradi. Kuhusu mambo ya fedha, kazi kubwa ya shirikisho la wanawake ni kuwaelimisha kuhusu sera na kuhamasisha wanawake, baada ya kufanya hilo, shirikisho linasaidia idara ya mambo ya fedha kutathmini, kuidhinisha, na kupendekeza kwa idara ya mambo ya fedha na idara inayoshughulikia raslimali za nguvukazi watu wanaofaa kunufaishwa na sera hiyo, ambayo ni kuwasaidia watu maskini na wale wadhaifu, pia litaangalia kama ana miradi mizuri, tena kutathmini kama mtu huyu ana akili ya kutumia fedha hizo vizuri."

    Wakati huohuo, majadiliano kati ya bibi Yang Li na bibi Nie Shuzhen bado yanaendelea.

    Bibi Nie Shuzhen ana miaka 41 pia ananufaishwa na sera ya mkopo mdogo. Katika miaka kadhaa iliyopita, bibi Nie alitegemea shamba la hekta 0.13 tu kutunza familia ya watu 6, hivyo maisha yalikuwa magumu sana. Bibi Nie anasema,

    "Mwanzoni nilikuwa na shamba lenye hekta 0.13 tu, tulikuwa maskini sana, hata hatukuweza kula chakula cha kutosha."

    Mwaka 2011 kufuatia uhamasishaji wa sera za huko za kuendeleza kilimo cha mashamba makubwa, bibi Nie akaomba mkopo kutokana na ujuzi wake kuhusu masuala ya kilimo, na kuanza kilimo cha mboga. Alitumia miaka michache tu kuongeza ukubwa wa shamba lake dogo hadi kuwa shamba kubwa la sasa lenye hekta 23. Wakati ule, ili kutatua suala la fedha la bibi Nie, ofisa mhusika wa shirikisho la wanawake la kijiji cha Heping bibi Wang Huiying alikuwa anakwenda na kurudi kati ya bibi Nie na idara husika. Bibi Wang anasema,

    "Katika kijiji, kama akikosa fedha, mwenye ardhi anaweza kuweka ardhi yake kama dhamana na kuomba mkopo benki, pia anaweza kuomba msaada au mkopo wa riba nafuu kutoka idara inayosaidia wamaskini, vilevile tuna mkopo wa "Fuhuijiahe", na wanawake wanaweza kupata mkopo kuanzia Yuan elfu 80 hadi laki moja."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako