• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wanawake wasio na waume wapigwa marufuku kugandisha mayai yao ya uzazi

    (GMT+08:00) 2015-11-23 07:56:49

    Tungependa kuwafahamisha wasikilizaji wetu kuwa hapa China wanawake wasio na waume hawaruhusiwi kabisa kuhifadhi au kugandisha mayai yao, ambayo wataweza kuyatumia baadaye wanapohitaji kufanya hivyo, na kwa sasa hapa hapa nchini China suala hili limekuwa likijadiliwa sana kuwa ni kiini cha suala la haki ya uzazi ya mwanamke asiye na mume. Katika nchi zetu za Afrika hususan Tanzania suala hili la kugandisha au kuhifadhi mayai ya uzazi halitekelezwi sana na wanawake, wengi wao wakishaolewa huwa wanatamani kupata mtoto. Na kwa wale ambao hawako kwenye ndoa huwa hata hawafikirii kabisa kugandisha kwani wengi hujitahidi kupata mume ili apate mtoto kabla umri haujampita.

    Kutokana na hilo wasomi na wanawake mbalimbali hapa China wamekuwa wakitoa maoni na kuwatetea wanawake wasio na waume nao wapewe fursa ya kugandisha mayai yao ya uzazi. Miongoni mwa wasomi wanaotetea wanawake hao ni profesa maarufu sana wa sosholojia wa Chuo Kikuu cha Peking Bi Li Yinhe. Bi Li anasema bila kujali kama wanawake wameolewa au la, wote wanapaswa kutendewa kwa usawa, na hususan linapokuja suala la kupata watoto. Hivyo anashauri warejeshewe haki yao ya kuzaa.

    Hivi karibuni kuna mwigizaji mmoja wa kike aitwaye Xu Jinglei ambaye ni mashuhuri sana hapa China, yeye alisema amegandisha mayai yake, na anaona hii ndiyo "dawa pekee ya kuondoa majuto" duniani. Akiwa na maana hatakuwa na majuto hapo baadaye kwani atakapotaka kuzaa anaweza kutumia mayai yake ya uzazi aliyoyagandisha na kupata mtoto. Baada ya kutangaza hilo, mada kuhusu "kugandisha mayai ya uzazi ya wanawake" imekuwa ikifuatiliwa tena na jamii nchini China.

    Wanawake wasio na waume wamekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu haki zao za uzazi, na kwa mujibu wa mwanasosholojia Li suala hilo linapaswa kushughulikiwa haraka na pia amesisitiza kuwa sheria inapaswa kubadilishwa kwa mujibu wa hali ya mabadiliko ya jamii. Kutokana na sera ya uzazi wa mpango na maendeleo ya uchumi wa kijamii, mtazamo wa Wachina kuhusu uzazi umebadilika pia. Ndio maana wale wasio na waume wanadai kupatiwa haki yao ya kugandisha mayai ya uzazi.

    Teknolojia ya kugandisha mayai ya wanawake imekuwa ikiendelea kwa miaka 30 hivi, na hapa China mtoto mchanga wa kwanza aliye zaliwa kwa njia ya teknolojia hiyo katika test-tube ilikuwa ni mwaka 2004. Miaka ya karibuni, hapa China kadiri wanawake wengi zaidi wanao olewa na kuzaa watoto wakiwa na umri mkubwa zaidi, ndivyo mama wengi zaidi siku hadi siku wanaamua kugandisha mayai yao. Wasiwasi wao mkubwa ni kwamba, muda ukipita uwezo wao wa kuzaa unaweza kupungua, hivyo wanataka kugandisha mayai yao wakiwa na umri mdogo, ili kuhakikisha wanazaa watoto wenye afya njema katika siku za baadaye. Na hapa hebu tusikilize maoni mbalimbali kuhusu suala hili la kugandisha mayai ya uzazi ya wanawake

    "Nimekuwa na umri mkubwa, nitaenda kugandisha mayai yangu? Naweza kusema itakuwa maumivu."

    "Kutokana na sababu za kazi na mambo mengine, wanawake wengi wanaahirisha kuzaa, hivyo mayai ya wanawake yanaweza kugandishwa kwa kupitia teknolojia hiyo."

    "Haya ni manufaa yanayotokana na teknolojia kwa baadhi ya wanawake wenye kazi kwa sasa."

    "Unaweza kugandisha mayai yako ukiwa na hali nzuri zaidi hadi utakapotaka kuzaa mtoto, ni kama bima, ni salama sana."

    Naye mkuu wa hospitali ya tatu ya Chuo Kikuu cha Beijing Bibi Qiao Jie anasema, hivi sasa kiwango cha kesi za kugandisha mayai ya uzazi ya wanawake zilizofanikiwa ni chini ya asilimia 30, na mazingira ndani ya tumbo la mama pia yanaathirika.

    "Kama mafanikio yatapatikana au la kunategemea na ubora wa yai, kwa hivyo mama mwenye umri mdogo zaidi ni bora zaidi. Kuna tofauti kubwa baina ya mama wenye umri wa miaka 30, 35 na 40 kugandisha mayai yao. Teknolojia ya kugandisha mayai inatakiwa kufanyiwa utafiti zaidi, kwa sababu mayai yenyewe yanaweza kuathiriwa kwa urahisi, yana maji mengi ndani yake, hivyo yanaweza kuwa na barafu, na kuharibika. Kwa hivyo teknolojia hiyo ina taabu, lakini pia inahitajika."

    Hata hivyo kumekuwa na mswali mengi watu wanayojiuliza kwamba watoto waliozaliwa kwa njia ya kugandisha mayai, afya zao zitaathirika au la? Takwimu zilizotolewa na hospital ya tatu ya Chuo Kikuu cha Beijing zinaonesha kuwa, kwa nyakati tofauti miongoni mwa watoto 936 na 200, hakuna tofauti kubwa kati ya watoto hao na wale waliozaliwa kwa njia ya kawaida, kikilinganishwa kiwango chao cha kasoro na kiwango cha watoto wachanga wenye uzito mdogo. Lakini hivi sasa kwa hapa China mtoto mwenye umri mkubwa zaidi aliyezaliwa kwa njia hiyo ana miaka 12 tu, huku duniani akiwa na umri wa miaka 29. Hivyo tunaweza kusema kuwa takwimu kuhusu hali ya afya ya mwili na akili za watoto kama hao wakiwa na umri wa makamo na uzee bado hazitoshi.

    Lakini hata baadhi ya wataalamu wa magonjwa ya wanawake wanasema njia hiyo mpya sio nzuri sana kama baadhi ya watu walivyotarajia. Qiao Jie ni mkuu wa hospitali ya tatu ya chuo kikuu cha Peking ambacho kinafanya utafiti wa kugandisha mayai ya uzazi hapa nchini China. Na hapa anafafanua zaidi

    "Hakuna takwimu rasmi juu ya kwamba kuna watoto wangapi wanaozaliwa kila mwaka kupitia njia hii hapa China, lakini idadi inaongezeka kidogo kidogo. Tunafanya upasuaji zaidi kila mwaka kuliko hapo zamani na idadi ya jumla hospitalini haizidi 300."

    Teknolojia hiyo ilijipatia umarufu zaidi baada ya muigizaji niliyemtaja awali Xu Jinglei kutangaza kugandisha mayai yake. Lakini wakati Bi Xu Jinglei akifikiria hilo, njia hiyo bado inawafanya wanawake wengine wa China wawe na wasiwasi nayo. Na hapa wanaeleza wasiwasi wao

    "Naweza kuamua kutumia njia hiyo kama nikilazimika. Ubora wa mayai huwa unapungua kadiri mtu aanavyozeeka. Hivyo nitafanya upasuaji kwa ajili ya afya ya mtoto wangu."

    "Sidhani kama ni njia ya kuaminika. Hakuna shaka kwamba njia ya kawaida ni nzuri zaidi."

    Hata hivyo hivi sasa kuna uvumi ulioenea hapa China kuwa kuzaa kwa njia hiyo, kunaweza kusababisha kusita mapema kupata hedhi. Daktari wa magonjwa ya wanawake Qiao Jie anasema hakuna ukweli wowote kuhusu uvumi huo. Hata hivyo, amesisitiza kuwa kiwango cha mafanikio ya njia hiyo ni chini ya asilimia 30. Pia amesema wanawake wanaotaka kugandisha mayai wanapaswa kufanya mapema kadiri iwezekanavyo.

    "Kiwango cha mafanikio kinategemea sana na ubora wa yai. Ubora wa mayai unatofautiana sana kulingana na umri wa mtu. Kwa ujumla, kadiri mwanawake anavyokuwa na umri mdogo ndio vizuri zaidi'.

    Lakini pia kuna maswali kuhusu uwezekano wa hatari za kiafya kwa mtoto anayezaliwa kwa njia hiyo. Dokta Qiao anasema kwa sasa bado hawajapata ushahidi wowote kwamba njia hiyo inaweza kusababisha hatari za kiafya kwa mtoto. Hata hivyo amesisitiza kuwa njia hiyo bado ipo kwenye hatua za mwanzo kwa hapa China

    "Kwa sasa inaonekana ni salama. Lakini teknolojia hiyo bado ni changa na imetumika kwa watu wachache tu. Tunahitaji muda zaidi kuchunguza hatari za njia hiyo"

    Tangu ianzishwe miaka 30 iliyopita, karibu watoto 2,400 wamezaliwa duniani kupitia njia hii. Mtoto wa kwanza kuzaliwa kwa njia ya kugandisha mayai hapa China ilikuwa ni miaka 11 iliyopita. Chini ya sheria ya sasa ya China, wanawake wote wenye waume na wasio nao wanaweza kugandisha mayai yao. Hata hivyo, ni wanawake walioolewa na wakiwa na vyeti halali vya ndoa tu ndio wanaoruhusiwa kutumia mayai yao.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako