• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tamasha kubwa la televisheni la Afrika la DISCOP lafanyika Afrika Kusini

    (GMT+08:00) 2015-11-13 20:15:31

    Tamasha kubwa la televisheni la Afrika la DISCOP limemalizika Jumatano wiki iliyopita mjini Johanesburg Afrika kusini. Katika kipindi cha leo, tutazungumzia tamasha hilo kubwa la televisheni barani Afrika.

    Mashirika zaidi ya 1,700 ya televisheni kutoka nchi na sehemu 90 duniani yameshiriki kwenye tamasha hilo la siku mbili. China ikiwa ni nchi mgeni wa heshima katika tamasha hilo, mashirika zaidi ya 20 kutoka China, yakiwemo kampuni kuu ya televisheni ya kimataifa ya China, Radio China Kimataifa, kampuni ya Star Times na kampuni ya utamaduni, radio, filamu na televisheni ya mji wa Shanghai SMG, yameshiriki kwenye tamasha hilo.

    Kwenye ufunguzi wa tamasha hilo, balozi wa China nchini Afrika Kusini Bw. Tian Xuejun alisema, sekta ya filamu na televisheni ya Afrika inaingia kwenye enzi ya dhahabu, na ushirikiano wa sekta hiyo kati ya China na Afrika ni eneo lenye mustakabali mkubwa. Amesema, kuimarisha ushirikiano wa sekta hiyo kati ya China na Afrika kunaweza kuimarisha melewano na urafiki kati ya watu wa China na Afrika, na kuongeza nguvu ya uhai kwenye mawasiliano ya kiraia kati ya pande hizo mbili. Mbali na hayo, ushirikiano huo pia utaisaidia Afrika kuharakisha mchakato wa kuendeleza mfumo wa utangazaji wa radio na televisheni uwe wa kidijitali.

    Naye Kaimu mkurugenzi mkuu wa ofisi ya habari ya serikali ya Afrika Kusini Donald Liphoko amesema, maswailiano ya filamu na televisheni za Afrika na China ni shughuli ya kunufaishana, ambayo imehimiza kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa kisiasia, kiuchumi na kiutamaduni kati ya watu wa Afrika na China.

    Kwenye tamasha hilo, mashirika 12 ya televisheni ya China na Afrika yamesaini makubaliano 6 kuhusu utangazaji na uendeshaji wa vipindi vya televisheni. Naibu mkurugenzi wa ofisi ya ushirikiano wa kimataifa katika idara kuu ya uchapishaji habari, radio, filamu na televisheni ya China Bw. Ma Li amesema, televishieni ni kama daraja, kupitia daraja hilo, watu wa China na Afrika wanaweza kuzidisha maelewano kati yao. Amesema, China inapenda kushirikiana kwa dhati na nchi mbalimbali za Afrika, kwenda mbele bega kwa bega, na kusukuma mbele ushirikiano wa filamu na televisheni kati ya pande hizo mbili ufikie katika ngazi mpya.

    Imefahamika kuwa mwaka jana China kwa jumla ilitengeneza episodi elfu 16 za tamthilia, dakika laki 1.4 za katuni na filamu 618. China imekuwa soko kubwa la pili la filamu duniani, mwaka jana thamani ya soko la filamu nchini China ilifikia dola za kimarekani bilioni 4.65, ambayo ni ongezeko la asilimia 36 kuliko mwaka 2013.

    Kwa mujibu wa makubaliano ya ushirikiano yaliyosaniwa kwenye tamasha hilo, tamthilia nyingi mpya za kichina zitaoneshwa barani Afrika, ikiwemo tamthilia ya Lang Ya Bang au kwa kingereza Nirvana in Fire, ambayo inaoneshwa sasa nchini China na kupendwa sana na watu wa China.

    Tamthilia hiyo "Nirvana in Fire" inayotokana na riwaya maarufu ya kihistoria kwenye mtandao wa Interent, inazungumzia hadithi kuhusu vita, mapenzi na mapigano ya kisiasa kwenye enzi ya kifalme katika karne ya 4.

    Mpaka sasa kazi ya kutafsri na kuitengeneza Tamthilia hiyo yenye sehemu 55 kuwa ya Kingereza bado inaendelea, lakini inatarajiwa kumalizika hivi karibuni.

    Mbali na tamthilia hiyo, kwenye tamasha hilo mashirika ya China pia yalionesha filamu, tamthilia na katuni nyingi bora zinazoweza kuwakilisha kiwango cha sekta ya filamu na televisheni ya China, kama vile Dokumentari "Mambo ya China usiyoyajua", "Njia ya hariri ya baharini", "Ladha ya China", "Mfereji mkuu wa China" na kadhalika. Kazi hizo zinatarajiwa kuonesha kwa pande zote utamaduni wa China kwa watazamaji wa Afrika, na pia kusaidia kuzidisha maelewano na urafiki kati ya watu wa China na Afrika.

    Mbali na mashirika ya televisheni ya jadi, kampuni nyingi za video kwenye mtandao wa Internet za China, kama vile Tencent, Iqiyi na Youku, pia zimeshiriki kwenye tamasha la televisheni la mwaka huu.

    Kutokana na maendeleo ya kasi ya huduma za mtandao wa Internet kwenye simu za mkononi, tamthilia za China zimeanza kuleta faida katika nchi za nje kupitia biashara ya hakimiliki yake. Kwenye tovuti za Youtube na Facebook, tamthilia nyingi za China zinapatikana, na tamthilia hizo zinaingiza sehemu mpya karibu wakati mmoja na tovuti zile za China.

    Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya filamu na tamthilia za China zilizouzwa nchi za nje imeendelea kuongezeka. Mwaka 2014, filamu na tamthilia za China zenye muda wa saa zaidi ya elfu 10 ziliuzwa katika nchi zaidi ya mia moja katika Asia, Ulaya, Amerika, Afrika na Oceania.

    Habari kutoka idara kuu ya uchapishaji habari, radio, filamu na televisheni ya China, zinasema katika miaka miwili iliyopita, idadi ya tamthilia za China zilizouzwa Afrika, na idadi ya katuni za kichina zilizouzwa katika nchi za kiarabu zote zimefikia kiwango kipya, na kuzifanya Afrika na nchi za kiarabu kuwa soko jipya la filamu na tamthilia za China.

    Katika miaka ya karibuni, mawasiliano na ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta ya radio, filamu na televisheni vimekua kwa kasi. Kwa upande wa ushirikiano wa vipindi, hadi sasa China imesaini makubaliano 76 ya ushirikiano na vyombo vya habari 55 kutoka nchi 44 za Afrika, kila mwaka tamthilia kadhaa za China zinazoonesha hali halisi ya China, maisha ya watu na maadili ya jamii ya China zinatafsiriwa kwa lugha 8 za kienyeji na kuoneshwa kwenye vyombo vikuu vya habari na televisheni barani Afrika. Hivi sasa kwa jumla tamthilia hizo zimeoneshwa kwa muda wa masaa zaidi ya 4500 katika nchi 30 za Afrika, na kutazamwa na watu milioni 600 wa Afrika.

    Kwa upande wa ushirikiano wa teknolojia, kampuni za China zenye teknolojia na sifa bora pia zimepeleka teknolojia, vifaa na uzoefu wa China hadi Afrika. Kwa mfano wa kampuni ya Star Times ya Beijing, kampuni hiyo imetoa mpango wa kuendeleza mfumo wa utangazaji kuwa wa kidigitali kwa nchi 10 za Afrika na kusaini makubaliano.

    Kwa upande wa mawasiliano kati ya wafanya kazi, kuanzia mwaka 2009, mamia ya wafanyakazi wa radio na televisheni wa nchi za Afrika wamekuja China kushiriki kwenye semina, kujadiliana na kufundishana kuhusu uzoefu wa usimamizi wa radio na televisheni.

    Filamu na tamthilia za China zimependwa na watu wa Afrika. Kwa mfano Afrika kusini, mwezi Disemba mwaka jana, filamu moja iitwayo American dreams in China inayozungumzia jinsi vijana kadhaa wa China walivyofanya bidii kuanzisha shughuli zao na hatimaye kupata mafanikio, imevutia watazamaji wengi nchini Afrika Kusini. Baada ya kutazama filamu hiyo, wanasema, si kama tu wameelewa hadithi inayoelezwa kwenye filamu hiyo, na kuelewa hisia za watu wa China, bali pia wamepata mafunzo kutoka kwenye filamu hiyo.

    Tamthilia nyingine inayopendwa sana na watu wa Afrika inaitwa "Doudou na mama wakwe zake", tamthilia hiyo inazungumzia uhusiano kati ya mke na mama mkwe, kupitia hadithi za mhusika mkuu Doudou, watazamaji wanaweza kufikiria maisha yao yenyewe, kwani haijalishi ni wachina au waafrika, kwa upande huu, maisha hufanana kabisa.

    Tamthilia hiyo ilitafsiriwa kwa lugha mbili za kiingereza na kiswahili. Idhaa yetu ya Kiswahili ya Radio China kimataifa ndiyo iliyotafsiri na kutengeneza toleo ya lugha ya kiswahili ya tamthilia hiyo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako