• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mlango wa China kufunguliwa zaidi kwa magharibi

    (GMT+08:00) 2015-11-25 11:32:26


    Mwezi Septemba na Oktoba mwaka 2013, rais Xi Jinping wa China alitoa mipango ya kujenga "Ukanda wa Uchumi wa Njia Mpya ya Hariri" na "Njia ya Hariri ya Baharini ya Karne ya 21", akitoa wito kwa nchi husika kujenga "jumuiya yenye maslahi ya pamoja" ya kunufaishana na "jumuiya yenye hatma ya pamoja" inayohimiza maendeleo na ustawi wa pamoja. Pendekezo hilo liliungwa mkono na nchi zaidi ya 60 zilizoko katika kanda hiyo, lakini pia lilitiliwa mashaka na baadhi ya vyombo vya habari vya kimagharibi, ambavyo vinaona wasiwasi kuwa mpango wa "Ukanda Mmoja na Njia Moja" wa China ni "mpango wa Marshal" toleo la China, na China inatumia mpango huo kujipatia nafasi ya uongozi katika kanda hiyo.

    Alipokuwa ziarani nchini Uingereza mwezi uliopita, rais Xi Jinping alisema kuwa mpango wa "Ukanda Mmoja na Njia Moja" uko wazi, na ulitolewa kutokana na Njia ya Hariri ya Zamani, lakini hauzihusishi tu nchi zilizopo katika Njia hiyo, bali mpango huo unajumuisha kwa pamoja nchi za mashariki za Asia na Pasifiki, zile za magharibi mwa Ulaya, na pia nchi zilizopo katikati ya Afrika. Alisema nchi zote zenye hamu zinaweza kujiunga na mpango wa "Ukanda Mmoja na Njia Moja", kwani mpango huo si njia nyembamba iliyojengwa kwa ajili ya maslahi ya upande fulani, bali ni njia pana inayowakutanisha watu wote. Akizungumzia mpango huo, meya wa Mji wa London ambao ni eneo la kifedha la mji mkuu huo Bw. Alan Yarrow anasema, "Pendekezo la 'Ukanda Mmoja na Njia Moja' limetumia vizuri wazo la Njia ya Hariri, na litaunganisha tena nchi za mashariki na Ulaya. Baadhi yake inatekelezwa kwenye njia za baharini, na sehemu nyingine ni kupitia nchi kavu. Pendekezo hilo linatupa fursa nzuri za ushirikiano, hasa katika sekta ya miundombinu, na linachangia maendeleo yetu ya pamoja katika siku za baadaye."

    Hivi karibuni, kikao cha 5 cha wajumbe wote wa Kamati Kuu ya 18 ya Chama cha Kikomunisti cha China kiliidhinisha pendekezo la kutunga mpango wa 15 wa miaka mitano kuhusu maendeleo ya uchumi na jamii ya China. Pendekezo hilo limesema China itahimiza ujenzi wa "Ukanda Mmoja na Njia Moja", kusukuma mbele ushirikiano wa kunufaishana na nchi na sehemu husika katika sekta mbalimbali, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa wa kiviwanda na utengenezaji wa mitambo na kujenga muundo mpya unaounganisha nchi za mashariki na magharibi kupitia njia za baharini na nchi kavu. Hii ni mara ya kwanza kwa mpango wa miaka mitano wa China kuhusisha nchi zilizopo katika ukanda huo na njia hiyo, na hii itasaidia China na nchi husika kuimarisha mawasiliano ya kisera, kuunganisha miundombinu, pamoja na kuhimiza maingiliano ya biashara na maelewano kati ya watu. Baada ya sera inayohimiza "uagizaji kutoka nje" kutekelezwa kwa zaidi ya miaka 30, China kwa sasa imeingia katika kipindi kipya cha kuzingatia "uagizaji kutoka nje" na "kutoka nje" kwa pamoja. Naibu mtafiti wa taasisi ya masuala ya kimataifa ya China Su Xiaohui anaona kuwa ukiwa jukwaa jipya la China kufungua mlango kwa nje, mpango wa "Ukanda Mmoja na Njia Moja" unaounganisha mtandao wa kiuchumi wa Asia ya kati na mtandao wa kiuchumi wa Ulaya sio tu utahimiza marekebisho ya muundo wa uchumi wa China, bali pia utatoa fursa mpya za maendeleo kwa nchi husika.Anasema,

    "Pendekezo la 'Ukanda Mmoja na Njia Moja' linazihudumia pande mbili, haswa Ukanda wa Kiuchumi wa Njia ya Hariri, ambao ubunifu wake unalenga kuunganisha mabara ya Asia na Ulaya. Mtandao wa kiuchumi wa Asia mashariki una mustakabali na matumaini mazuri, ni kanda yenye nguvu kubwa ya uhai barani Asia, na kwamba nchi nyingi zinafuatilia kwa karibu maendeleo ya Asia mashariki. Kitu tunachokitaja kama karne ya Asia ni dhana nzuri, nchi nyingi zilizoendelea za Ulaya zina msingi mzuri, kwa hiyo kama pande hizo zinaunganishwa, hakika kutakuwa na mafanikio makubwa."

    Korea Kusini ni nchi muhimu kiuchumi katika kanda ya Asia Mashariki. Mwaka 2013, serikali ya nchi hiyo ilitoa pendekezo la Asia na Ulaya linalohusu diplomasia za kiuchumi. Mwezi Julai mwaka huu, watu 250 kutoka sekta za siasa, elimu, utamaduni na sanaa walipanda treni ya kasi ya urafiki wa Ulaya na Asia kwenda Irkutsk, Russia na Berlin, Ujerumani. Safari hiyo ilianzia Busan, Korea Kusini na kupita kwenye miji zaidi ya 10 ya nchi tano ikiwemo Beijing na Ulan Bator, na Mongolia. Mtaalamu Yoon Myung-chul kutoka Chuo Kikuu cha Dongguk cha Korea Kusini alishiriki safari hizo.

    "Katika safari hizo, tulikutana na kufanya majadiliano na wataalam wa nchi mbalimbali, kutembelea vifaa vya sekta mbalimbali, na pia tumeona kuwa Ulaya na Asia zinaweza kufanya ushirikiano na kuleta maendeleo ya pamoja katika maeneo mengi."

    Profesa Yoon ameeleza kuwa kiini cha pendekezo la Ulaya na Asia la Korea Kusini ni kujenga mtandao wa usafirishaji bidhaa kati ya mabara hayo mawili, na linafanana na "Mpango Mmoja na Njia Moja" ya China, ambayo yote ni kuhimiza Asia kupata soko kubwa zaidi katika nchi za magharibi na kuleta muungano kati ya pande hizo mbili. Hivi sasa idadi ya watu wanaoishi barani Ulaya na Asia inachukua asilimia 75 ya watu wote duniani, pato la jumla pia linachukua asilimia 60 ya pato la dunia, kwa hiyo pande hizo mbili zina masoko makubwa yanayotegemewa. Yoon anasema,

    "Naona tunaweza kutumia mambo sawa yaliyopo katika pendekezo la Ulaya na Asia na 'Ukanda Mmoja na Njia Moja', ili kuleta mafanikio kwa pande zote."

    Kwa upande mwingine wa ukanda wa kiuchumi wa Njia ya Hariri, yaani nchi za Ulaya, pendekezo la kimkakati la "Ukanda Mmoja na Njia Moja" limeanza kujulikana. Balozi wa Ujerumani nchini China Michael Clauss anasema, "Pendekezo la ukanda wa kiuchumi wa Njia ya Hariri limekuwa dhana inayojulikana nchini Ujerumani. Kati ya China na Ujerumani kuna reli moja inayounganisha Chongqing na Duisburg, na alipofanya ziara nchini Ujerumani mwaka 2014, rais Xi Jinping wa China alishuhudua ujio wa treni iliyotoka Chongqing. Naona muungano wa njia za nchi kavu unaweza kuendelea kuhimiza uhusiano wa kibiashara, na ujenzi wa miundombinu ya usafiri kati ya China na Ulaya na kutakuwa na miradi mingi ya miundombinu."

    Balozi wa Italia nchini China Ettore Francesco Sequi pia ameeleza maoni yake akisema, "Italia ina shauku kubwa ya kushiriki kwenye miradi ya ushirikiano inayotokana na 'Ukanda Mmoja na Njia Moja", na sio kushiriki tu, bali inataka kupata nafasi muhimu katika ushirikiano huo, kwani pendekezo hilo lina maana kubwa za kiuchumi na kisiasa, na lilitolewa kwa upeo wa kuona mbali. Njia ya Hariri ipo tangu zamani, na Italia na China zilikuwa mwisho wa pande mbili, ni njia iliyohimiza utamaduni, uchumi na sekta nyingi mbalimbali. Tuna matumaini mazuri na ushirikiano wa 'Ukanda Mmoja na Njia Moja', ambao utahusu reli, bandari, usafiri wa ndege n.k, mambo ambayo baadhi yao tumekuwa na ushirikiano na China, na hivi sasa kuna safari 49 za ndege za moja kwa moja kati ya Italia na China.

    Takwimu zilizotolewa mwanzoni mwezi huu na Wizara ya Biashara ya China zinaonesha kuwa kuanzia mwezi Januari hadi Septemba, thamani ya jumla ya biashara ya pande mbili kati ya China na nchi zilizo katika "Ukanda Mmoja na Njia Moja" ilifikia dola za kimarekani bilioni 742.8, kiasi ambacho kilichukua asilimia 25.6 ya biashara ya China na nchi za nje ya kipindi hicho. Uwekezaji wa moja kwa moja uliofanywa na China kwa nchi 48 zilizopo katika "Ukanda Mmoja na Njia Moja" ulifikia dola za kimarekani bilioni 12.03 na kuongezeka kwa asilimia 66. Wakati huohuo, nchi zilizopo katika "Ukanda Mmoja na Njia Moja" zilianzisha makampuni 1,604 nchini China, fedha za kigeni zilizotumiwa zilikuwa dola za kimarekani bilioni 6.12, kiasi ambacho ni ongezeko la asilimia 18.4 kuliko mwaka jana kipindi kama hicho.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako