• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mkutano wa kilele wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika watarajiwa kutoa hatua mpya za ushirikiano

    (GMT+08:00) 2015-11-26 18:09:10

    Mkutano wa kilele wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika unatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Disemba huko Jahannesburg nchini Afrika Kusini, na hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika barani Afrika, ambapo rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Afrika Kusini Jacob Zuma wataendesha mkutano kwa pamoja, na kutangaza hatua mpya za ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

    Huu ni mwaka wa 15 tangu Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika lianzishwe. Baraza hilo lilianzishwa mwaka 2000. Kwenye mkutano wa 5 wa mawaziri wa baraza hilo uliofanyika mwaka 2012, China ilitangaza kuunga mkono maendeleo ya Afrika katika sekta tano, na kusukuma mbele maendeleo ya uhusiano mpya wa wenzi wa kimkakati kati ya pande hizo mbili.

    Naibu waziri wa biashara wa China Bw. Qian Keming leo amesema, katika miaka mitatu iliyopita, China imetimiza lengo la kutoa mkopo dola za kimarekani bilioni 20 kwa nchi za Afrika, kutekeleza miradi 900 ya misaada na kuandaa wataalamu zaidi ya elfu 30 kwa nchi hizo. Mbali na hayo, China pia ilijenga miradi mikubwa ya reli kama vile reli za kutoka Addis Ababa hadi Djibouti, na kutoka Nairobi hadi Mombasa.

    Bw. Qian Keming amesema, kwa mtizamo wa kufundishana na kunufaishana, China imetoa misaada kwa Afrika kulingana na uwezo wake. Akizungumzia hali ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika, Bw. Qian ametoa takwimu mbalimbali akisema.

    "China imekuwa mwenzi mkubwa wa kibiashara kwa Afrika kwa miaka 6 mfululizo. Mwaka 2014, thamani ya biashara kati ya China na Afrika ilifikia dola za kimarekani bilioni 222, ikiwa ni ongezeko la mara 20 kuliko lile la wakati Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika lilipoanzishwa; Afrika imekuwa soko kubwa la pili la miradi ya kandarasi kwa kampuni za China na inapokea uwekezaji kwa wingi kutoka China. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, uwekezaji wa moja kwa moja wa China barani Afrika umefikia dola za kimarekani bilioni 32.4, na umedumisha ongezeko la asilimia 30 kila mwaka katika miaka 15 iliyopita. Ushirikiano kati ya China na Afrika umeendelea kupanuliwa kwenye sekta za kilimo, utengenezaji, fedha, utalii, safari za ndege, mawasiliano ya habari, radio na televisheni, afya na matibabu na usambazaji bidhaa na kadhalika."

    Kuanzia mwaka huu, kutokana na kupungua kwa ukuaji wa uchumi wa dunia, biashara kati ya China na Afrika pia imekabiliwa na shinikizo kubwa la kushuka. Kuhusu hali hiyo, Bw. Qian Keming amesema, kupungua kwa biashara kati ya China na Afrika kunatokana na kushuka kwa kiwango cha bei ya bidhaa duniani, lakini uagizaji bidhaa wa China kutoka Afrika haujapungua.

    Bw. Qian Keming amedokeza baadhi ya hatua mpya za ushirikiano zitakazotangazwa kwenye mkutano huo wa Johannesburg.

    "Hivi sasa Afrika imeweka ruwaza ya 2063, ambayo inaweka mpango halisi kuhusu maendeleo ya viwanda na utandawazi barani Afrika. China itaangalia mahitaji ya Afrika na kuanzisha ushirikiano wa viwanda, ili kuisaidia Afrika iendeleze sekta yake ya viwanda. Jambo lingine muhimu ni kilimo cha kisasa, China itatoa kipaumbele katika kuisaidia Afrika kuhakikisha usalama wa chakula. Tatu ni uwekezaji katika miundombinu, haswa katika miradi ya umeme, reli, barabara na viwanja vya ndege, ambayo itatangazwa rasmi na rais Xi Jinping kwenye mkutano huo."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako