• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mradi wa uhamiaji wa Ningxia wasaidia watu wa milimani kuishi katika nyumba mpya

    (GMT+08:00) 2016-01-07 10:44:41



    Mkoa unaojiendesha wa kabila la Wahui wa Ningxia uko kaskazini magharibi mwa China, na unaweza kugawanywa katika sehemu mbili. Sehemu ya kaskazini ya mkoa huo ni tambarare, na Mto Manjano unatiririka kupita kwenye sehemu hiyo, lakini sehemu ya kusini ina milima mingi, ambayo imefunikwa na udongo wa manjano, na inapata milimita 300 za mvua kwa mwaka. Wilaya tatu zilizoko kusini kabisa mwa mkoa huo Xiji, Haiyuan na Guyuan hata zilitajwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO kama moja ya sehemu ambazo hazifai kuishi kwa binadamu.

    Ili kuboresha maisha ya watu wa sehemu ya kusini ya mkoa huo, na kuhifadhi hali ya viumbe ya sehemu ya milimani, mkoa huo ulifanya uhamiaji mkubwa wa watu katika kipindi cha 12 cha maendeleo ya mitaka mitano, ukipanga kuhamisha familia elfu 78.8 zenye watu laki 3.46. Mradi huo wa uhamiaji uliwafanya watu hao wa sehemu ya milimani kuishi katika nyumba mpya, na kubadili kabisa hali ya maisha yao ya taabu. Bw. Zhang Xuanke alihamia katika kijiji kipya cha wahamiaji cha Qingquan wilayani Longde mjini Guyuan mwezi Novemba mwaka 2011 kutoka sehemu ya ndani ya milimani. Alipokumbuka nyumba aliyoishi milimani, Bw. Zhang anasema,

    "Nyumba niliyoishi zamani ilijengwa kwa udongo tu, na ilibomoka kwa urahisi wakati wa mvua kubwa. Hatukuwa na maji ya bomba. Tulikuwa na chemchem ndogo tu, na tulipaswa kuamka mapema kuchota maji. Kama hukuamka mapema, wengine watateka maji yote, basi utakosa maji ya kunywa."

    Licha ya ugumu wa maisha, sura ya ardhi yenye utatanishi ya milimani pia ilizuia maendeleo ya mawasiliano ya barabarani, ambayo ilikuwa vigumu kwa watu wa milimani kujitegemea kubadili hali yao ya maisha. Mkuu wa kijiji cha Fengling cha wilaya ya Longde mjini Guyuan Zhang Huimin anasema,

    "Wakati ule hali ya maisha ilikuwa ngumu sana. Hawakuwa na barabara, wala maji. wakati ule walisafirisha chakula kwa punda, hawakuwa na barabara kama tuliyo hivi sasa."

    Mradi wa uhamiaji wa Ningxia unalenga watu wa milimani wenye taabu maishani. Mradi huo unawahamisha watu kutoka milimani na kuwaweka katika sehemu inayofaa kuishi. Serikali ya sehemu wanayohamia wahamiaji inajenga nyumba yenye mita za mraba 54 kwa kila familia inayokidhi masharti ya kuhamia, na pia inaipa kila familia ua wenye mita za mraba kati ya 2 hadi 6. Nyumba hizo mpya zinafikiwa na maji na umeme, na baadhi ya sehemu pia zinaweka mashine za joto zinazotumia nishati ya jua. Ili kurahisisha maisha ya wahamiaji, kila sehemu ya kupanga wahamiaji inajenga miundo mbinu mbalimbali zikiwemo shule, zahanati, viwanja, supamaketi, kituo cha huduma za kuwatafutia ajira wahamiaji n.k. Serikali pia inachukua urahisi wa maisha kama moja ya sababu muhimu ya kuchagua maeneo mapya ya kuhamia wahamiaji. Mkuu wa idara ya usimamizi wa wahamiaji chini ya ofisi ya kupunguza umaskini ya mkoa unaojiendesha wa Ningxia Bw. Zhang Xiuyan anasema,

    "Tunapochagua mahali pa kuhamia tunazingatia mambo matatu, ukaribu na maji, miji na barabara, ili wahamiaji wasafiri kwa urahisi, kufanya kazi kwa urahisi, kupata ajira, kwenda shule na kushughulikia mambo kwa urahisi."

    Baada ya kuhamia katika nyumba mpya, wahamiaji wanaweza kupanua eneo la nyumba zao katika ua kwa kufuata hali halisi ya familia zao. Katika miaka miwili ya kwanza baada ya wahamiaji kuhamia katika nyumba mpya, kila mwaka serikali inaipa kila familia Yuan 1,000 kama ruzuku ya matumizi ya maji na mfumo wa kupasha joto. Kama wakipatwa na shida katika matumizi ya maji na umeme, serikali itatuma mafundi kuwasaidia. Akizungumzia nyumba mpya anayoishi hivi sasa, Bw. Zhang Xuanke anasema kwa furaha,

    "Nyumba ya sasa kweli ni nzuri. Ni rahisi kwetu kufanya kazi, kwa watoto kwenda shule, na pia ni rahisi kwetu kutumia maji ya bomba. Sasa serikali inaweka majiko ya kupikia na mitambo ya kuchemsha maji inayotumia nishati ya jua. Sasa kila kitu ni rahisi sana."

    Mabadiliko ya maisha sio tu yametokea katika familia ya Bw. Zhang Xuanke tu. Bw. Jin Luren kabla ya kuhamia katika eneo la Taiyangliang katika tarafa ya Qukou wilayani Zhongning alikuwa anaishi katika milima ya ndani wilayani Haiyuan. Alimwambia mwandishi wetu wa habari hisia zake kuhusu kuhama akisema,

    "Hatuthubutu kufikiri maisha ya zamani ikilinganishwa na maisha ya sasa, kweli kuna mabadiliko makubwa sana. Maisha ya sasa ni mazuri sana kuliko ya zamani."

    Bila shaka, sera ya nyumba inayohusiana na wahamiaji wengi namna hii iliwahi kukumbwa na matatizo mengi. Moja ya masuala makubwa zaidi ni eneo la nyumba zilizojengwa na serikali haliwezi kukidhi mahitaji ya familia kubwa yenye watu wengi. Kwa hiyo, serikali ya mkoa unaojiendesha wa Ningxia imechukua hatua mbalimbali za utatuzi, ambazo ni pamoja na kuboresha mpango wa nyumba na kujenga wenyewe kwenye eneo lao. Katika siku za usoni, serikali pia itaendelea kuchukua hatua kutatua kabisa suala hilo na kuboresha mazingira ya nyumba ya wahamiaji. Mkuu wa idara ya usimamizi wa wahamiaji katika ofisi ya kupunguza umaskini ya mkoa unaojiendesha wa Ningxia Bw. Zhang Xiuyan anasema,

    "Kadiri muda wa uhamiaji unavyokwenda, ndivyo idadi ya watoto inavyoongezeka, ndivyo suala hilo linaonekana kidhahiri. Katika kipindi cha 13 cha maendeleo ya miaka mitano, tunataka kufanya uchunguzi ili kujua familia kubwa za wahamiaji katika kipindi cha 12 cha miaka mitano. Kama kweli wanaishi kwa vizazi vitatu au zaidi kwa pamoja, tutawasaidia kutatua suala la nyumba. Tunataka kuwa si kama tu kuwahamishia hapa, bali pia kuwafanya waishi na kujiendeleza kwa masikilizano."

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako